Monday, December 5, 2016

HALMASHAURI YA CHALINZE YAANZA KUMWAGA FEDHA KWA WAJASIRIAMALI


Na John Gagarini, Chalinze

HALMASHAURI ya Chalinze wilayani Bagamoyo mkoani Pwani imetoa mikopo yenye thamani ya shilingi milioni 79.8 kwa vikundi vya wajasiriamali 26 vya akinamama na vijana kwenye kata za Halmasahuri hiyo.

Aidha fedha hizo zinatokana na asilimia 10 ya mapato ya Halmashauri ya robo mwaka ambazo ni kiasi cha shilingi milioni 809 yaliyokusanywa katika kipindi hicho.

Akikabidhi baadhi ya vikundi hivyo vya vijana na akaimama kwenye kata ya Msoga ambapo kila kundi linapata asilimia tano kutokana na mapato hayo Mwenyekiti wa Halmashauri Said Zikatimu alisema kuwa fedha hizo zitakuwa zikitolewa kwa kila robo ya mwaka.

Zikatimu alisema kuwa lengo la kutolewa fedha hizo kwanza ni kufuata sheria ambayo inataka asilimia tano ya mapato yote ya Halmashauri wakopeshwe vijana na asilimia tano kwa ajili ya akinamama kupitia vikundi vya vya uzalishaji mali.

“Tunaomba vikundi vyote ambavyo vinakopeshwa fedha hizi wazirejeshe kwa wakati ili ziwe na mzunguko kwa watu wengine na vikundi vihakikishe vinazitumia kwa malengo waliojiwekea na si kuanzisha miradi ambayo hamjaombea mnaweza kushindwa kurejesha,” alisema Zikatimu.

Alisema kuwa fedha hizo siyo msaada bali ni fedha kwa ajili ya kuboreshea shughuli za ujasiriamali na wanapaswa kurejesha kwa wakati ili vikundi vingi viweze kupata fedha hizo ambazo zinatokana na mapato ya ndani yanayotokana na vyanzo mbalimbali.

“Hizi fedha ni kwa ajili ya wananchi wote na hasa wale waliojiunga kwenye vikundi hivyo zitumike kama zilivyoombewa na siyo kununulia nguo au baadhi huzitumia kwa ajili ya kufanyia starehe mkifanya hivyo mtaharibu maana ya mkopo huu na mtashindwa kurejesha na kujikuta mkishtakiwa,” alisema Zikatimu.

Aidha aliyatakama makundi mbalimbali ya vijana na akimama kujiunga na kuanzisha vikundi vingi kwa ajili ya kukopa kwani fedha si tatizo bali ni wao kujiunga kwa wingi fedha ziko za kutosha.

Kwa upande wake ofisa maendeleo ya jamii na ofisa vijana wa Halmashauri ya Chalinze Felista Kizito alisema kuwa vikundi hivyo vilivyopewa fedha hizo vitapewa mwezi mmoja kabla ya kuanza kurejesha marejesho yao.

Kizito alisema kuwa vikundi hivyo vimegawaanyika kwenye shughuli mbalimbali kutegemeana na mazingira yao na vimepewa fedha kati ya shilingi milioni mbili hadi sita kutegemeana na aina ya mradi ambao waliuanzisha.

Naye diwani wa kata ya Msoga Hassan Mwinyikondo alisema kuwa Halmashauri hiyo imefanya jambo kubwa kwa kutoa fedha hizo ambazo zitasaidia kuboresha maisha ya wananchi.

Mwinyikondo alisema kuwa mikopo hiyo ya Hlamashauri ni nafuu na haina masharti magumu kama ilivyo kwa taasisi za kifedha ambazo watu wengi wameshindwa kukopa kutokana na masharti kuwa magumu.

Mwisho.


 Mwenyekiti wa Halmashauri ya Chalinze wilayani Bagamoyo mkoani Pwani Said Zikatimu katikati akiwakabidhi hundi kikundi cha ujasirimali cha Wanawake cha Nianjema cha ufugaji wa Mbuzi Kijiji cha Kwa Konje kushoto ni mwenyekiti wa Kijiji hicho Omary Mbwana anayefuatia ni  diwani wa kata ya Kibindu Ramadhan Mkufya akifuatiwa na Ofisa Maendeleo ya Jamii na Ofisa Vijana Halmashauri ya Chalinze Felista Kizito na mwenyekiti wa kikundi hicho Veronica Chusi

 Kushoto Mwenyekiti wa Halmashauri ya Chalinze Said Zikatimu akiwakabidhi hundi ya fedha wana kikundi wa Muungano Mindukene kata ya Talawanda 

Friday, October 21, 2016

WALIBYA WASAIDIA MRADI WA MAJI MKURANGA


Na John Gagarini, Mkuranga

WANANCHI wametakiwa kuwa na utamaduni wa kulipa kodi mbalimbali za serikali ili ziweze kutumika kwa ajili ya maendeleo kama wanavyofanya wananchi wa Libya.

Hayo yalisemwa wilayani Mkuranga na mkurugenzi wa Taasisi ya World Islamic Call Society iliyopo chini ya ubalozi wa Libya hapa nchini Ammara Zaiyani wakati akikabidhi mradi wa kisima cha maji kwenye Kijiji cha Binga–Kisiju.

Zaiyani alisema kuwa fedha ambazo zimesaidia ujenzi wa kisima hicho cha maji ya kunywa chenye thamani ya shilingi milioni 18 zimetokana na kodi za wananchi wa Libya kwa ajili ya kusaidia watu wenye changamoto mbalimbali za kimaendeleo.

“Wananchi wa Libya wanajitolea kuwasaidia wenzao hivyo na nyie mnapaswa kuwa na utamaduni wa kuwasaidia wengine kupitia kwenye malipo mbalimbali ya serikali yenu ambayo ina sema hapa Kazi Tu,” alisema Zaiyani.

Naye mwakilishi wa Ubalozi wa Libya hapa nchini Mohamed Atoumi alisema kuwa serikali ya Libya kupitia taasisi hiyo imekuwa ikipokea maombi mbalimbali na imekuwa ikisaidia kadiri ya uwezo unapokuwepo.

Atoumi alisema kuwa wamekuwa wakisaidia kwenye sekta mbalimbali ikiwa ni pamoja kwenye huduma za afya, maji na shughuli nyingine za maendeleo lengo likiwa ni kudumisha ushirikiano uliopo na Tanzania.

Kwa upande wake kadhi mkuu wa mkoa wa Pwani Sheikh Hamis Mtupa alisema kuwa wanashukuru kwa msaada huo kwani umesaidia kuwaondolea adha wananchi wa Kijiji hicho ambao walikuwa wakishinda wakitafuta maji ambayo siyo safi wala salama.

Mtupa alisema kuwa wananchi wanapaswa kulinda miundombinu ya kisima hicho ili isiharibike kwani maji hayo ni kwa wananchi wote bila ya kujali dini ya mtu na ni huduma muhimu kwa binadamu.

Naye mkazi wa kijiji hicho Mwanahawa Maulid alisema kuwa wamekuwa wakihangaika kutafuta maji ambayo yanapatikana mbali na wamekuwa wakitumia muda mwingi kusubiria maji.

Maulid alisema kuwa maji waliyokuwa wakiyatumia ni ya kuchimba chini ambayo si salama kiafya na yamekuwa wakiwasababishia magonjwa mbalimbali kama vile kuhara na UTI.

Mwisho.





Mkurugenzi wa Taasisi ya World Islamic Call Society ya Libya tawi la Tanzania Ammara Zaiyani kulia aliyeshika ndoo ya maji baada ya kumtwisha ndoo ya maji Saida Ally mkazi wa Kijiji cha Binga-Kisiju kata ya Dondo wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani, kushoto kadhi mkuu wa mkoa wa Pwani Sheikh Hamis Mtupa (Picha na John Gagarini)
Mkurugenzi wa Taasisi ya World Islamic Call Society ya Libya tawi la Tanzania Ammara Zaiyani katikati akielezea jambo kulia ni kadhi mkuu wa mkoa wa Pwani Sheikh Hamis Mtupa na kushoto ni mwakililishi wa balozi wa Libya Mohamed Atoumi wakati wa uzinduzi wa mradi wa maji kwenye Kijiji cha Binga Kisiju- kata ya Dondo wilaya ya Mkuranga mkoa wa Pwani Picha na (John Gagarini)

Mkurugenzi wa Taasisi ya World Islamic Call Society ya Libya tawi la Tanzania Ammara Zaiyani akifungua bomba la maji baada ya uzinduzi wa kisima cha maji kwenye Kijiji cha Binga-Kisiju wilayani Mkuranga mkoani Pwani kushoto kwake ni mwakililishi wa balozi wa Libya Mohamed Atoumi (Picha na John Gagarini)  

      

Monday, October 3, 2016

MWANAMKE ATUMIKA WIZI CWT WALINZI WAWILI WASHIKILIWA

Na John Gagarini, Kibaha

JESHI la la polisi mkoani Pwani linawashikilia walinzi wawili wa jengo la ofisi ya Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) mkoa baada ya watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi kuvunja na kuiba fedha kiasi ambacho bado hakijajulikana na computer za ofisi hizo.

Akizungumzia na waandishi wa habari mjini Kibaha kuhusiana na tukio hilo katibu wa (CWT) Nehemiah Joseph amesema kuwa tukio limetokea usiku wa octoba mosi kuamkia octoba 2 mwaka huu.

Joseph amewataja walinzi hao kutoka kampuni ya Noble security Tanzania Ltd ya Kibaha kuwa ni Hamad Kisoki (32) mkazi wa Maili Moja na Said Mohammed (39) mkazi wa Mwanalugali.

Amesema siku ya tukio walinzi waliotakiwa kuingia zamu walikuwa ni wawili lakini Said Mohammed pekee ndiye aliyefika kazini na mwenzake Hamad Kisoki haikuweza kufahamika mara moja ni kwa sababu gani hakuingia kazini.

Aidha amesema kuwa Said Mohamed alipokuwa kwenye lindo lake anadaiwa kupatiwa chips na juisi vinavyosemekana kuwa na madawa ya kulevya kutoka kwa mwanamke asiyefahamika.

Katibu huyo wa CWT mkoa wa Pwani ameeleza kuwa baada ya kupatiwa chakula hicho mlinzi alipoteza fahamu na hivyo kutoa mwanya kwa watu hao kuvunja milango ya ofisi hizo na kuingia na kuiba vitu hivyo ambavyo thamani yake bado haijafahamika.

Ametaja ofisi zilizopo kwenye jengo hilo ambazo zimeibiwa ni pamoja na CWT mkoa ,CWT wilaya,beem financial services (BFS) ,Chodawu,Tuico na TCCIA ambapo kwasasa wameshafikisha taarifa hizo polisi kwa hatua zaidi na ofisi ya chama hicho imeshakaa na taasisi zote zilizopanga jengo hilo kufanya tathmini.

hata hivyo amesikitishwa sana kutokea kwa wizi huo na kushangazwa na mlinzi huyo kula ama kununua vyakula kwa watu wasiowajua kwani kwa kufanya hivyo kumesababisha kuwapa wahalifu urahisi kutekeleza tukio hilo ambalo limesababisha hasara kwa wamiliki wa ofisi hizo.

Kwa upande wake kamanda wa polisi mkoani Pwani,Bonaventure Mushongi ,amekiri kutokea kwa tukio hilo ambapo amesema taarifa ya tukio hilo ilitolewa  saa 5 asubuhi kutoka kwa Elizabeth Thomas ambae ni katibu wa chama CWT wilaya ya Kibaha huko mkoani A ,kata ya Tumbi.

Mushongi amesema kuwa baada ya kufanya wizi huo watu hao walitokomea kusikojulikana na jeshi hilo bado linawatafuta,huku akiomba ushirikiano kwa wananchi kuwafichua watu wanaowadhania kuhusika na wizi huo na kwasasa wanawashikilia walinzi hao kwa ajili ya uchunguzi juu ya tukio hilo.

Mwisho













      

Monday, September 26, 2016

MAJALIWA AWASIMAMISHA MAOFISA MISITU RUFIJI

Na John Gagarini,Rufiji
WAZIRI mkuu Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi Meneja wa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) wilaya ya Rufiji mkoani Pwani Suleiman Bulenga kwa kushindwa kudhibiti na kusimamia mapato yatokanayo na shughuli za misitu hivyo kuikosesha mapato Serikali.
Mbali ya meneja huyo maafisa misitu watatu nao wamesimamishwa kutokana na kushindwa kudhibiti na kusimamia shughuli za uvunaji misitu na kusababisha wilaya kukosa mapato .
Maofisa misitu waliosimamishwa ni pamoja na Ofisa maliasili na mazingira wa wilaya Dk Paul Ligonja,Ofisa misitu Gaudence Tarimo na Jonas Nambua ambao watsimamishwa hadi hapo uchunguzi utakapokamilika.
Majaliwa alichukua hatua hiyo wilayani Rufiji wakati akizungumza na watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Rufiji na wananchi wa wilaya hiyo  na kusema kuwa sekta ya misitu ni tatizo kwa kila wilaya na Rufiji ni moja ya wilaya hizo .
“Magogo yanasafirishwa bila utaratibu,na ndio wanakata miti kwenye misitu ya Utete na kupiga nyundo maeneo ya Kilwa,” alisema Majaliwa.
Alisema kuwa hakuna manufaa na TFS hivyo ameamua kusimamisha shughuli zote za uvunaji,katika wilaya hiyo na watumishi hao hadi wizara itakapotoa maelekezo mengine.
“Wilaya ya Rufiji inaongoza katika suala la utoroshaji wa misitu na kuruhusu uvunaji holela suala ambalo halikubaliki na nataka uwajibikaji na uadilifu katika maeneo ya kazi na watumishi wanapaswa wabadilike na waache kufanya kazi kwa mazoea,” alisema Majaliwa. 
Aidha Majaliwa alikemea utozwaji wa ushuru kwa watu wanaochoma mkaa unaofanywa na halmashauri ya Rufiji kwani kwa kufanya hivyo ni kuruhusu ukataji ovyo wa miti.
“Mkuu wa wilaya na mkurugenzi wa halamshauri ya Rufiji mnapaswa kusimamia mapato na matumizi ya fedha ili kuongeza mapato ya halmashauri iweze kupiga hatua ya kimaendeleo,”alisema Majaliwa.
Naye mbunge wa Rufiji,Mohammed Mchengelwa alisema kuwa nidhamu kwa watumishi inaonekana kupungua kwa baadhi ya watumishi kwenye halmashauri hiyo.

Mwisho




Friday, September 23, 2016

WAWILI WAFA AJALINI MMOJA ACHOMWA MOTO

Na John Gagarini, Kibaha

WATU wawili wamefariki dunia na wengine 11 kujeruhiwa mkoani Pwani kufuatia ajali iliyohusisha mabasi madogo mawili ya abiria kugongana uso kwa uso huko Kiparanganda wilayani Mkuranga.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari mjini Kibaha na Kamanda wa Polisi mkoani humo Bonaventura Mushongi alisema kuwa watu hao walifariki papo hapo.

Mushongi alisema kuwa ajali hiyo ilitokea Septemba 21 mwaka huu majira ya saa 10:30 jioni T363 DCV likiendeshwa na Zidadu Mohamed (25) mkazi wa Dar es Salaam akielekea Kimazinchana liligongana na T363DHD yote aina ya Toyota Hiace likiendeshwa na Miraji Mlonga (22) akielekea Dar es Salaam.

Aliwataja waliokufa kuwa ni Zuhura Haji (21) na Neema Julius (25) wote wakazi wa Kimazinchana wilaya ya Mkuranga ambapo miili yao imehifadhiwa kwenye Hopsitali ya Wilaya ya Mkuranga kusubiri ndugu kwa ajili ya mazishi.

Aidha aliwataja watu waliojeruhiwa kuwa ni Majeruhi ni Mariamu Aloyce (46) wa Kimazinchana Mariamu Sultan (60) mkzai wa Chanika, Yusufu Maziku (33) mkazi wa Kimazinchana,Kulwa Abdala (30) makzi wa Mbagala,Ibrahim Hamis (3) mkazi wa Mbagala na Fatma Abdul (25) mkazi wa Chanika.

Wengine ni Salum Mohamed (54) mkazi wa Mwalusembe, Litus Mwarami (26) mkazi wa Kimazinchana Kidawa Abdala (30) mkazi wa Mbagala, Issa Hemed (2) mkazi wa Kimazinchana na Greyson Ernest (23) mkazi wa Kimazinchana.

“Tuna washikilia madereva wote waili kutokana na kusababisha ajali hiyo na watafikishwa mahakamani mara upelelezi wa kesi hiyo utakapokamilika ili kujibu tuhuma hizo zinazowakabili,” alisema Mushongi.

Kwenye tukio lingine mkazi wa Kwa Mathias Hamis Tenende (38) aliuwawa kwa kupigwa kisha kuchomwa moto na wananchi wenye hasira kali kwa madai ya kutaka kuiba pikipiki eneo la Umwelani.

Mwisho.
 








Monday, September 12, 2016

WAPONGEZA IDD EL HAJI KUFANYIKA KWA PAMOJA


Na John Gagarini, Kibaha

KUFUATIA sherehe ya Idd el Haji ambayo inahusisha na uchinjaji kufanyika jana ambapo waumini wa dini ya Kiislamu walisherehekea kwa pamoja tofauti na miaka mingine ambapo kila dhehebu lilikuwa likifanya siku tofauti safari hii wamefurahi kufanya kwa pamoja.

Wakizungumza na waandishi wa habari mjini Kibaha baadhi ya waumini wa Kiislamu wamesema kuwa utaratibu wa kusherehekea kwa pamoja ni mzuri kwani unaonyesha umoja na ni vema ukaendelea hata kwa siku zijazo.

Mrisho Halfan “Swagala”  alisema kuwa hakuna sababu wao kama waumini wa imani moja kufanya sherehe kwa wakati tofauti na kufanya kama ni imani tofauti.

“Tunaomba viongozi wa taasisi hizi za dini yetu wakae kwa pamoja na kufanya vitu kwa pamoja kwani kama mwaka huu sikukuu imependeza kwani wote tumejumuika na hali hii imeondoa tofauti na kutufanya kitu kimoja,” alisema Swagala.

Alisema kuwa kuna haja ya kuunganisha umoja wa waislamu kama hivi kwa kiufanya sherehe hiyo ambayo ni kubwa kwa Waislamu kote duniani kukumbuka yale yaliyofanywa na mtume ikiwa ni kufanya mambo yanayompendeza Mungu.

Kwa upande wake Abubakari Lipambila kutoka Masjidi Hazarajii Maili Moja Kibaha alisema kuwa sikukuu hiyo ni kwa ajili ya kurejesha furaha kwa watu wote.

Lipambila alisema kuwa waumini wa dini ya kiislamu wanapaswa kujihadhari na shetani katika kipindi hichi cha sherehe kwani naye yuko kazini kwa kuwapotosha watu ili waende kinyume na imani kwa kujiingiza kwenye vitendo viovu.

Mwisho.

Wednesday, September 7, 2016

BINTI AZAA MTOTO AMTUPA

Na John Gagarini, Kibaha

BINTI aliyetambulika kwa jina la Judith Paulo anayekadiriwa kuwa na umri katia ya miaka (18) na (22) anatuhumiwa kuzaa mtoto wa jinsia ya kike kisha kumtupa mwanae jirani na jalala.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu mwenyekiti wa Kitongoji cha Pera kata ya Pera Chalinze Mjini Hussein Mramba alisema kuwa tukio hilo lilitokea Septemba 7 majira ya saa 12 asubuhi eneo la Kwa Mwarabu.

Mramba alisema kuwa kichanga hicho chenye uzito wa kilogramu 3.2 kiliokotwa baada ya watoto waliokuwa wakiokota vitu mbalimbali jirani na jalala huku kikiwa kimewekwa kwenye mfuko wa Rambo.

“Watoto hao ndiyo waliogundua na ndipo walipotoa taarifa kwa watu wazima na kwenda kumchukua ambapo walimkuta mtoto huyo akiwa na afya njema huku akiwa hajavalishwa nguo yoyote mwilini mwake na jambo la kumshukuru Mungu kuwa mtoto huyo hakupata madhara yoyote,” alisema Mramba.

Alisema kuwa baada ya hapo ilibidi wasamaria wema wampeleke Hospitali ili kuangalia namna ya kumsaidia mtoto huyo ambaye kwa sasa yuko kwa mama mmoja ambaye amejitolea kukaa naye wakati taratibu nyingine zinafanyika ili apelekwe sehemu stahiki.

“Kwa maelezo tuliyopata baada ya kwenda Kituo cha Afya cha Chalinze ili kujua kama alijifungua hapo ilibainika kuwa binti huyo alijifungua kituoni hapo juzi majira ya saa 4 baada ya kufika hapo majira ya saa 3 usiku akiwa na uchungu wa kujifungua huku akiwa hajaongozana na mtu yoyote,” alisema Mramba.

Mramba ambaye pia ni mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Mdogo wa Chalinze alisema kuwa baada ya kujifungua alikaa kama masaa mawili kisha kuomba kuondoka baada ya kujifungua salama na alimwomba muuguzi aondoke kwani alikuwa hajafunga mlango wa nyumba anayoishi hivyo ana hofu ya kuibiwa vitu vyake.

“Kutokana na utetezi wake huo ilibidi baadhi ya wazazi wamsaidia fedha kwa ajili ya kulipia teksi baada ya kumuonea huruma ambapo yeye alifika hapo kituoni kwa kutumia bodaboda,” alisema Mramba.

Aidha alisema kuwa binti huyo alionekana kuwa na wasiwasi alipofika kituoni hapo lakini hata hivyo baadhi ya wazazi waliokuwa hapo walijaribu kumweka sawa ili aone jambo la uzazi ni la kawaida.

Alisema kuwa taarifa hizo wamezitoa sehemu mbalimbali ikiw ani pamoja na polisi kwa ajili ya kusaidia kupatikana kwa binti huyo ambapo mita kama 100 aliposhushwa na teksi wamejaribu kuulizia lakini inavyoonekana kuwa hakuwa anakaa maeneo hayo kwani jina hilo hakuna mtu anayelifahamu.


Mwisho.