Na John Gagarini, Chalinze
HALMASHAURI ya Chalinze wilayani Bagamoyo mkoani
Pwani imetoa mikopo yenye thamani ya shilingi milioni 79.8 kwa vikundi vya
wajasiriamali 26 vya akinamama na vijana kwenye kata za Halmasahuri hiyo.
Aidha fedha hizo zinatokana na asilimia 10 ya
mapato ya Halmashauri ya robo mwaka ambazo ni kiasi cha shilingi milioni 809
yaliyokusanywa katika kipindi hicho.
Akikabidhi baadhi ya vikundi hivyo vya vijana na
akaimama kwenye kata ya Msoga ambapo kila kundi linapata asilimia tano kutokana
na mapato hayo Mwenyekiti wa Halmashauri Said Zikatimu alisema kuwa fedha hizo
zitakuwa zikitolewa kwa kila robo ya mwaka.
Zikatimu alisema kuwa lengo la kutolewa fedha hizo
kwanza ni kufuata sheria ambayo inataka asilimia tano ya mapato yote ya
Halmashauri wakopeshwe vijana na asilimia tano kwa ajili ya akinamama kupitia
vikundi vya vya uzalishaji mali.
“Tunaomba vikundi vyote ambavyo vinakopeshwa fedha
hizi wazirejeshe kwa wakati ili ziwe na mzunguko kwa watu wengine na vikundi
vihakikishe vinazitumia kwa malengo waliojiwekea na si kuanzisha miradi ambayo
hamjaombea mnaweza kushindwa kurejesha,” alisema Zikatimu.
Alisema kuwa fedha hizo siyo msaada bali ni fedha
kwa ajili ya kuboreshea shughuli za ujasiriamali na wanapaswa kurejesha kwa
wakati ili vikundi vingi viweze kupata fedha hizo ambazo zinatokana na mapato
ya ndani yanayotokana na vyanzo mbalimbali.
“Hizi fedha ni kwa ajili ya wananchi wote na hasa
wale waliojiunga kwenye vikundi hivyo zitumike kama zilivyoombewa na siyo
kununulia nguo au baadhi huzitumia kwa ajili ya kufanyia starehe mkifanya hivyo
mtaharibu maana ya mkopo huu na mtashindwa kurejesha na kujikuta mkishtakiwa,”
alisema Zikatimu.
Aidha aliyatakama makundi mbalimbali ya vijana na
akimama kujiunga na kuanzisha vikundi vingi kwa ajili ya kukopa kwani fedha si
tatizo bali ni wao kujiunga kwa wingi fedha ziko za kutosha.
Kwa upande wake ofisa maendeleo ya jamii na ofisa
vijana wa Halmashauri ya Chalinze Felista Kizito alisema kuwa vikundi hivyo
vilivyopewa fedha hizo vitapewa mwezi mmoja kabla ya kuanza kurejesha marejesho
yao.
Kizito alisema kuwa vikundi hivyo vimegawaanyika
kwenye shughuli mbalimbali kutegemeana na mazingira yao na vimepewa fedha kati
ya shilingi milioni mbili hadi sita kutegemeana na aina ya mradi ambao
waliuanzisha.
Naye diwani wa kata ya Msoga Hassan Mwinyikondo
alisema kuwa Halmashauri hiyo imefanya jambo kubwa kwa kutoa fedha hizo ambazo
zitasaidia kuboresha maisha ya wananchi.
Mwinyikondo alisema kuwa mikopo hiyo ya Hlamashauri
ni nafuu na haina masharti magumu kama ilivyo kwa taasisi za kifedha ambazo
watu wengi wameshindwa kukopa kutokana na masharti kuwa magumu.
Mwisho.
|
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Chalinze wilayani Bagamoyo mkoani Pwani Said Zikatimu katikati akiwakabidhi hundi kikundi cha ujasirimali cha Wanawake cha Nianjema cha ufugaji wa Mbuzi Kijiji cha Kwa Konje kushoto ni mwenyekiti wa Kijiji hicho Omary Mbwana anayefuatia ni diwani wa kata ya Kibindu Ramadhan Mkufya akifuatiwa na Ofisa Maendeleo ya Jamii na Ofisa Vijana Halmashauri ya Chalinze Felista Kizito na mwenyekiti wa kikundi hicho Veronica Chusi |
Kushoto Mwenyekiti wa Halmashauri ya Chalinze Said Zikatimu akiwakabidhi hundi ya fedha wana kikundi wa Muungano Mindukene kata ya Talawanda |
No comments:
Post a Comment