Na John Gagarini, Kibaha
JUMLA ya wanafunzi 15,528 mkoani Pwani wamefaulu
kwenda shule za sekondari kwa mwaka 2017 baada ya kufanya mtihani wa kumaliza
darasa la saba mwaka huu.
Aidha wanafunzi 9,290 wamefeli sawa na asilimia
37.4 na wanafunzi wote waliofaulu wamechaguliwa kujiunga na elimu ya sekondari
ambapo wamefaulu kwa kupata alama zaidi ya 100 kati yao 288 wamepata daraja la
A.
Hayo yamesemwa mjini Kibaha na Kaimu ofisa elimu
mkoa wa Pwani Modest Tarimo wakati wa uchambuzi wa matokeo ya mtihani wa
kuhitimu eilimu ya msingi mwaka 2016 ya mkoa na kusema kuwa wanafunzi
waliofanya mtihani walikuwa ni 24,818.
Tarimo amesema kuwa wanafunzi 2,636 walipata daraja
B, wanafunzi 12,604 wamepata daraja C na wote waliopata daraja A na C wote
wamechaguliwa kujiunga na sekondari
Amesema kuwa wanafunzi waliokuwa wakitarajiwa
kufanya mtihani walikuwani 24,913 ambapo waliofanya walikuwa ni 24,818 wavulana
wakiwa ni 11,334 na wasichana walikuwa ni 13,484 sawa na asilimia 99.9.
Ameeleza kuwa ufaulu kwa mwaka huu umeshuka kwani
ni asilimia 62.5 ikilinganishwa na mwaka 2015 ambapo ufaulu ulikuwa ni asilimia
63.1 matokeo haya hayaridhishi kwani ufaulu badala ya kupanda lakini umeshuka
kwa asilimia 0.5 na kwa matokeo hayo mkoa umeshika nafasi ya 21 kitaifa.
Amebainisha kuwa watahiniwa 95 hawakufanya mtihani
sawa na asilimia 0.3 kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na utoro,
wanafunzi 75, mimba mwanafunzi mmoja, vifo 11, ugonjwa wawili na sababu nyingine
sita ambapo wadau wanapaswa kupiga vita utoro ambao umepungua 204
ikilinganishwa na mwaka jana.
Kaimu ofisa elimu huyo wa mkoa ambaye ni ofisa
taaluma amesema serikali iliweka wastani wa asilimia 80 ya ufaulu kwa shule za
msingi ikiwa ni mkakati wa kufikia mpango wa matokeo makubwa sasa BRN ambapo
wadau wa elimu wanapaswa kukabiliana na changamoto zinaosababisha ufaulu
kushuka.
Naye Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Pwani Edward
Mwakipesile amesema kuwa wadau wa elimu wanapaswa kushirikiana na idara ya elimu
ya mkoa ili kuhakikisha matokea ya wanafunzi yanakuwa mazuri ambapo kwa mwaka
huu yanaonekana kushuka.
Mwakipesile amesema kuwa mbali ya changamoto ya
matokeo hayo pia changamoto iliyopo ni vyumba vya madarasa ambavyo ni vichache
na kusababisha madawati kukosa sehemu ya kukaa baada ya zoezi la utengenezaji
madawati kufanikiwa.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment