Saturday, December 24, 2016

FAMILIA YA WATU SABA WASIOONA YASAIDIWA

 FAMILIA ya Watu saba wasioona
Na John Gagarini, Kibaha
JUMUIYA ya Maili Moja A ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Maili Moja imetoa misaada ya nguo na vyakula kwa familia yenye wasioona saba inayoishi kwenye Mtaa wa Simbani wilayani Kibaha mkoani Pwani.
Akizungumza na gazeti hili mara baada ya kukabidhi misaada hiyo ambayo ilipelekwa na Jumuiya hiyo mwenyekiti Jacob Samson alisema kuwa waliamua kupeleka misaada hiyo baada ya kupata taarifa za familia hiyo.
Samson alisema kuwa wametoa misaada hiyo pia ni katika kuwafanya nao waweze kusherehekea siku kuu ya X- Mass na wenzao wakiwa na furaha hasa ikizingatiwa wao ni wahitaji na wanahitaji misaada mbalimbali.
“Tunaamini kusaidia jamii zenye mahitaji ni ibaada kamili na inawatia moyo na kujiona kuwa hawako peke yao kwani kuna watu wanawaunga mkono na kushiriki nao kwa pamoja,” alisema Samson.
Alisema kuwa Jumiya yao hufanya ibaada za nyumba kwa nyumba ambapo hutembeleana na kushirikiana kwenye masuala mbalimbali ya kijamii pamoja na ya kiimani.
“Jumuiya yetu iko kwa ajili ya kusaidiana kwenya matatizo na furaha hivyo wanajumuiya walisema kuwa twende kwenye hiyo familia iwe sehemu ya ibaada ya yetu ya kila Jumamosi ili kuwafariji na wamejitolea sana ili kuhakikisha familia ile nayo inafurahia kipindi hichi cha mwisho wa mwaka,” alisema Samson.
Aidha alisema kuwa wanaomba watu wengine nao wajitokeze kuisaidia familia hiyo ambayo ina hitaji misaada mbalimbali kutokana na kuwa kwenye mazingira magumu.
“Kutoa ni moyo na si utajiri kwani watu wenye moyo wanapaswa kwenda kuwasaidia kwa jambo lolote la kijamii hasa ikizingatiwa familia hiyo inasimamiwa na mwanamke ambaye alitengana na mumewe,” alisema Samson.
Kwa upande wake mama wa familia hiyo Mwajuma Maulid alisema kuwa anaishukuru Jumuiya ya maili Moja kwa kuwapatia misaada hiyo ambayo wameitoa kwani wameonyesha moyo wa kipekee.
Maulid alisema kuwa vyakula vilivyotolewa vitawasaidia katika kusherehekea sikukuu ya X-Mass kwa furaha kama wanavyofurahia watu wengine na kuwataka watu wengine waendelee kuwasaidia.
“Tuko kwenye mazingira magumu sana kwani hali yetu si nzuri ambapo tunaishi maisha ya kubahatisha kwa hiyo wanapokuja watu kama hawa na kutupa misaada tunashukuru sana,” alisema Maulid.
Familia hiyo inaishi mtaa wa Simbani kata ya Kibaha ina watu saba ambao hawaoni ambapo wasioona ni mume wake ambaye walitengana,watoto wanne wasioona na  wajukuu wawili wote hawaoni na inaishi kwa kutegemea kuchoma mkaa na kusuka mikeka.

Mwisho.     

zee wa Kanisa kutoka Jumuiya ya Maili Moja A Samwel Luhembe kushoto akikabidhi sabuni iliyotolewa na jumuiya hiyo ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania KKKT usharika wa Maili Moja anayepokea ni mama wa familia ya watu wasioona saba Mwajuma Maulid kulia  
  Mzee wa Kanisa kutoka Jumuiya ya Maili Moja A Samwel Luhembe kushoto akikabidhi unga uliotolewa na jumuiya hiyo ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania KKKT usharika wa Maili Moja anayepokea ni mama wa familia ya watu wasioona saba Mwajuma Maulid kulia 

Mzee wa Kanisa kutoka Jumuiya ya Maili Moja A Samwel Luhembe kushoto akikabidhi nguo zilizotolewa na jumuiya hiyo ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania KKKT usharika wa Maili Moja anayepokea ni mama wa familia ya watu wasioona saba Mwajuma Maulid kulia 


Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maili Moja A ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania KKKT usharika wa Maili Moja Jacob Samson kushoto akimkabidhi moja ya msaada uliotolewa na Jumuiya hiyo kwa familia ya watu saba wasioona anayepokea ni Mwajuma Maulid ambaye ndiye mama anayeihudumia familia hiyo

No comments:

Post a Comment