Friday, January 13, 2017

MATUKIO YA UHALIFU YALIYOTIKISA PWANI 2016


Kamanda wa Polisi mkoa wa Pwani Bonaventura Mushongi akiwaonyesha waandishi wa habari hawapo pichani silaha aina ya SMG no 01304 ikiwa na risasi 30 ya Askari Jackson Shirima  wa Saadani National Park ambaye aliporwa na mtuhumiwa Swalehe Mangupili na kufichwa kichakani huko Kijiji cha Gama wilaya ya Bagamoyo

Na John Gagarini, Kibaha

JUMLA ya makosa makubwa ya uhalifu 4,208 yameripotiwa kwenye vituo vya polisi mkoani Pwani kwa mwaka 2016 ambapo kumekuwa na ongezeko la makosa 419 ikilinganishwa na mwaka 2015 ambao ulikuwa na makosa 3,784.
Aidha makosa madogo 16,332 yaliripotiwa katika kipindi hicho cha mwaka 2016 ambapo kuna ongezeko la makosa 2,396 ikilinganishwa na mwaka 2015 ambapo kulikuwa na makosa 13,936.
Hayo yalisemwa mjini Kibaha na kamanda wa polisi mkoani Pwani Bonaventura Mushongi wakati akitoa taarifa ya mwaka mmoja uliopita na kusema kuwa watu waliohusika na matukio hayo walifikishwa mahakamani.
Mushongi alisema kuwa ongezeko la makosa hayo kumetokana na misako iliyofanywa, doria na oparesheni kwenye maeneo mbalimbali sambamba na ushirikishwaji wa jamii kwenye kufichua uhalifu.
“Tunawashukuru wananachi kwa kuendelea kutupa taarifa mbalimbali ambazo zimesaidia kukabiliana na uhalifu na tunaomba ubia uendelee kwani uwiano wa askari na raia bado hautoshi kwani askari mmoja anahudumia raia zaidi 1,000 hivyo ulinzi shirikishi ni muhimu,” alisema Mushongi.
Alisema kuwa katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita walifikisha mahakamani makosa 1,439 na makosa 159 watuhumiwa walikutwa na hatia na kuhukumiwa kifungo wakati makosa 29 watuhumiwa walishindwa kutiwa hatiani na kuachiwa huru  na makosa mengine kesi bado zinaendelea kwenye mahakama mbalimbali.
“Tumejiwekea mikakati mbalimbali ya kukabiliana na uhalifu kwa kuimarisha vikosi mbalimbali vilivyopo ndani ya mkoa, kuzuia na kutanzua matukio hayo kabla hayajatokea au baada ya kutokea, kuimarisha doria za miguu katika maeneo tete kila wilaya kwa ushirikiano na wananchi,” alisema Mushongi.
Aidha alisema kuwa wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni upungufu wa vitendea kazi ikiwa ni pamoja na uchache wa magari,Jografia ya mkoa kwwenye mipango miji ni ngumu katika kumpata mhalifu kwa haraka pindi uhalifu unapotokea.
“Mwaingiliano na mkoa wa Dar es Salaam unafanya wahalifu kuweza kuingia kirahisi na kufanya makosa,kutokuwa na mpango bora wa matumizi ya ardhi hivyo kusababisha migogoro ya ardhi katika jamii, uwepo wa ukanda wa mkubwa katika bahari unaosababisha kuwepo kwa bandari bubu nyingi za kupitisha wahamiaji haramu na biashara za magendo,” alisema Mushongi.
Alibainisha kuwa mwaka uliopita kulikuwa na matukio makubwa ambayo yaliyovuta hisia za watu ikiwa ni pamoja na kupatikana maiti saba wilaya ya Bagamoyo na mauaji ya viongozi wa serikali za vijiji kwa wilaya za Mkuranga, Rufiji na Kibiti ambapo katika matukio hayo watu 11 walikamatwa  na kufikishwa mahakamani.
Mwisho.


      




No comments:

Post a Comment