Wednesday, January 25, 2017

WAFANYABIASHARA MAILIMOJA WAHUKUMIWA KIFUNGO CHA NJE.

Na John Gagarini, Kibaha
WAFANYABIASHARA 62 wa lililokuwa soko la Maili Moja wilayani Kibaha mkoani Pwani waliofanya mkusanyiko usio halali na kutaka kumwona Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Seleman Jaffo wamehukumiwa kifungo cha nje cha miezi sita.
Hukumu hiyo ilitolewa kwenye mahakama ya hakimu mkazi wa mahakama ya wilaya ya Kibaha Aziza Mbadjo chini ya mwendesha mashtaka mwanasheria wa serikali Auleria Makundi na mkaguzi wa Polisi Rashid Chamwi.
Mahakama ilielezwa kuwa wafanyabiashara hao bila ya kibali walifanya mkusanyiko huo huku wakiwa na mabango yenye jumbe mbalimbali na kutaka kumwona Waziri Jaffo.
Na walifanya mkusanyiko huo wakitaka kutoa malalamiko yao juu zoezi zima la uhamishwaji wao kutoka soko la Maili Moja ambalo limebomolewa hivi karibuni kwenda soko jipya la Mnarani au Sagulasagula maarufu kama Loliondo.
Ikaelezwa kuwa washtakiwa kwa pamoja walitenda kosa hilo Januari 6 mwaka huu majira ya saa 4 asubuhi eneo la Shirika la Elimu Kibaha (KEC) Tumbi walifanya mkusanyiko bila ya kibali toka Polisi wilaya.
Pia walikuwa na mabango hayo jambo ambalo ni kinyume cha sheria jambo ambalo lilionyesha kuleta usumbufu kutokana na kukosa uhalali wa kufanya hivyo.
Baada ya kusomewa shitaka hilo ambalo ni kinyume cha sheria namba 74 (1-2) na 75 kifungu kidogo cha kanuni ya adhabu kilichofanyiwa mapitio mwaka 2002 walikiri kutenda kosa hilo na walijitetea kwa kusema kuwa walifanya kosa hilo bila ya kujua na wanamajukumu mengi ya kifamilia hivyo kuiomba mahakama iwapunguzie adhabu.
Kutokana na utetezi huo hakimu Mbadjo alisema kuwa kutojua sheria siyo sababu ya kuvunja sheria hivyo mahakama imewakuta na hatia hivyo wanahukumiwa kifungo cha nje ambapo wataitumikia jamii na hawapaswi kufanya kosa katika muda huo.
Mwisho.  


No comments:

Post a Comment