Na John
Gagarini, Kibaha
ZOEZI la
kubomoa soko la Maili Moja wilayani Kibaha pamoja na nyumba za biashara na za
makazi ambavyo vilijengwa kwenye hifadhi ya barabara limefanyika na Wakala wa
Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Pwani chini ya ulinzi mkali wa polisi.
Zoezi hilo
ambalo lilianza jana majira ya asubuhi limefanyika baada ya kushindikana
kufanyika kwa muda mrefu ambapo mara ya mwisho wameliki wa maeneo hayo walipewa
barua na TANROADS miezi sita iliyopita.
Akizungumza
na waandishi wa habari ofisini kwake meneja wa wakala hao mkoa wa Pwani Injinia Yudas
Msangi alisema kuwa lengo kuu la kubomoa ni kuhakikisha kuwa eneo hilo la
hifadhi ya barabara inakuwa wazi.
Msangi alisema
kuwa zoezi hilo limefanikiwa kutokana na kuwajulisha mapema wahusika kuwa
wabomoe wenyewe kabla ya siku ya kubomoa kufanyika jana Januari 23.
“Tunashukuru
kwani hakuna mtu anayelalamika kwa sababu tuliwapa taarifa mapema na wengi
wametii kwa kuvunja wao wenyewe na kutoa vitu vyote vya thamani licha ya
wachache ambao walishindwa kubomoa wao wenyewe,” alisema Msangi.
Alisema kuwa
zoezi hilo kwa Maili Moja ndiyo limehitimisha ubomoaji kwa watu waliojenga
kwenye hifadhi ya barabara katika mkoa huo ambapo mwaka jana walibomoa maeneo
mengine ya wilaya zote za mkoa huo.
“Baada ya
zoezi la kubomoa wananchi hawpaswi kujenga tena kwenye eneo hilo la hifadhi ya
barabara ambalo lina matumizi mbalimbali kwa ajili ya magari na shughuli
nyingine zinazohusu barabara,” alisema Msangi
Aidha alisema
kuwa jana walivunja eneo la umbali wa mita 60 kutoka barabara kuu ya Morogoro
ambazo ziko ndani ya hifadhi ya barabara ambayo ilitengwa kwa ajili ya matumizi
mengine.
Naye mkaguzi
wa barabara Injinia Livingstone Urio alisema kuwa zoezi hilo ni mwendelezo wa
usafishaji wa maeneo ambayo ni hifadhi ya barabara ambapo pia ni usalama kwa
wananchi kwani ni hatari kujenga au kufanya biashara karibu na barabara.
Urio alisema
kuwa eneo hilo lilitengwa kisheria na watu hawakutakiwa kujenga makazi au
vibanda vya biashara na wananchi wengi wao wanajua mmiliki wa eneo hilo.
Kwa upande
wake mfanyabiashara wa soko la Maili Moja Ally Gonzi alisema kuwa wao wamepokea
zoezi hilo kama lilivyo kwani tayari wlaikuwa na taarifa juu ya matumizi ya
eneo hilo.
Gonzi alisema
kuwa kwa kuwa wametengewa eneo la kufanyia biashara hivyo wataenda huko kwa
ajili ya kuendelea na biashara zao licha ya kuwa maandalizi ya soko jipya
wamechelewa.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment