Na John Gagarini, Msoga
MKOA wa Pwani unatarajiwa kuwa na uwanja wa kisasa ambao utasaidia kukuza soka la vijana na kuinua michezo kwenye mkoa huo ambao umepania kuwa moja ya mikoa itakayolea vipaji.
Uwanja huo unatarajiwa kujengwa kwenye Kijiji cha Msoga kata ya Msoga Halmashauri ya Chalinze wilayani Bagamoyo na serikali ya watu wa China lengo likiwa ni kukuza sekta ya michezo kwa vijana kwenye mkoa na nchi kwa ujumla.
Akizungumza katika hafla maalumu iliyoandaliwa kwa ajili ya kwenda kutembelea eneo ambalo litajengwa uwanja huo Dk Kikwete alisema kwamba uwanja huo wa wa mpira wa miguu utajengwa kwa ufadhili wa serikali ya watu wa china na kuongeza kuwa utakuwa ni mkombozi mkubwa katika kukuza na kuinua vipaji kwa vijana wadogo.
“Tumehamasisha wadau wa michezo kujenga uwanja lengo lake kubwa ni kuhakikisha kwamba Tanzania katika siku za usoni inakuwa ni wachezaji wengi wenye vipaji ambao wataweza kuunda timu nzuri ya Taifa ambayo itaweza kufanya vizuri katika mashindano mbali mbali ya Kimataifa,” alisema Dk Kikwete.
“Uwanja huu wa mpira wa miguu pindi utakapokamilika utaweza kuwa ni mkombozi mkubwa wa vijana wadogo hususan wale wa shule, hivyo nimeshazungumza na rafiki zetu wa serikali ya china na wamekubali kutujengea kwa hivyo ni jambo la msingi sana katika kuendeleza sekta ya michezo kwa watoto wetu hawa mbao wataweza kuleta mafanikio makubwa katika siku zijazo,”allisema Kikwete.
Dk Kikwete alisema kuwa anaipongeza serikali ya china kwa kuona umuhimu wa kusaidia kujenga kiwanja hicho, na kuongeza kuwa pindi kitakapokamilika kitakuwa na michezo mingine ambayo itakuwa ikifanyika mbali na mchezo huo wa soka lengo ikiwa ni kuwapa fursa vijana kuweza kuonyesha vipaji walivyonavyo.
Naye Mwakilishi wa balozi wa China nchini Tanzania Yang Tong aliahidi kuendelea kutoa ushirikiano wa dhati katika kukuza sekta ya michezo hususani kwa vijana wadogo ikiwa ni sambamba na kujenga viwanja ili watoto wasiweze kucheza katika viwanja vya vumbi.
Naye Mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete alisema kwamba lengo lake kubwa ni kuhakikisha anakuza michezo wa vijana wadogo katika jimbo lake hivyo kukamilika kwa ujenzi wa uwanja huo kutaweza kuwasaidia vijana kukuza vipaji vyao.
Nao baadhi ya wadau wa mchezo wa soka katika kijiji hicho cha Msoga akiwemo Michael James pamoja na Mohamed Halfan wamempongeza Rais mstaafu Dk Jakaya Kikwete kwa ubunifu wa ujenzi huo wa uwanja kwa ajili ya vijana wadogo kwani kutaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa kuleta mabadiliko chanya katika michezo ukiwemo wa soka.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment