Friday, October 2, 2015

ADHA YA MAJI KIJIJI CHA GONGO KATA YA MKANGE JIMBO LA CHALINZE WILAYA YA BAGAMOYO PWANI





Na John Gagarini, Mkange
WANANCHI wa Kijiji cha Gongo kata ya Mkange wilayani Bagamoyo wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa maji ambapo huweka foleni ya kuchota maji kwenye kisima kilichopo kijijini hapo baada ya wiki mbili.
Kutokana na usosefu huo wa maji wananchi hao wamekuwa wakinunua maji ya bomba ndoo ya lita 20 kati ya shilingi 1,000 na shilingi 1,500 maji ambayo huuzwa kwenye magari au pikipiki hivyo kuwafanya wajikute hawapati maendeleo kutokana na gharama kubwa kuzitumia kununulia maji.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya mkutano wa kampeni wa mgombea Ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ridhiwani Kikwete, kwenye kata ya Mkange mwananchi wa Kijiji hicho Hungilo Nyoka alisema kuwa maji yamewafanya washindwe kupata maendeleo.
Nyoka alisema kila kaya inatakiwa ichote madumu manne ili angalau kila mmoja apate baada ya hapo maji hukatika ambapo inatakiwa mtu asubirie tena na mzunguko huo hufanya foleni ya mtu mmoja kufikiwa tena baada ya wiki mbili kwani hapa kuna wananchi 1,690.
Alisema changamoto kubwa kwao ni maji ambayo yamekuwa yakiwafanya washindwe kufanya shughuli za maendeleo ipasavyo kwani hata wakipata fedha kutokana na shughuli zao fedha zote huishia kununulia maji.
“Tunawaomba wahusika kutuangalia kwa jicho la huruma maji kwetu ni kikwazo cha kupata maendeleo kwani hata ukipata fedha kiasi gani zote zinaishia kwenye maji hivyo tunaomba tuchimbiwe kisima kwani kilichopo maji ni kidogo sana yanatoka kila baada ya saa moja yanakatika,” alisema Nyoka.
Aidha alisema kuwa maji wanayokunywa ni ya bomba lakini yanatoka vijiji jirani vya Matipwili ambako kuna umbali wa kilomita 11 na kijiji cha Mkange kilomita tisa na alisema kuwa chanzo cha maji ya kisima kutotoka ipasavyo ni kwamba waliochimba kisima hawakuchimba hadi kuuukuta mwamba ambapo chini ya mwamba ndiyo kuna maji mengi.
“Tunaomba wadau wa masula ya maendeleo kutusaidia kuweza kupata maji kwani tunashindwa hata kujiletea maendeleo kutokana ukosefu wa maji na wkati mwingine watoto hushindwa kwenda shule endapo maji yanakuwa ya shida kwani hawawezi kwenda wachafua kwani mimi kwa siku hutumia madumu matatu hadi matano kwa siku,” alisema Nyoka.
Kwa upande wake mgombea udiwani kupitia CCM Injinia Juma Mgweno alisema kuwa tatizo hilo ni kubwa sana lakini atahakikisha maji yanapatikana kwa kuita wadau mbalimbali ili waweze kuwachimbia kisima.
Naye mgombea wa Ubunge kupitia CCM Ridhiwani Kikwete alisema kuwa visima viwili vilivypo kijiji hapo havitoi maji ambapo kimoja kinahitaji pampu ambayo imeharibika atahakikisha inapatikana mpya ili kuwaondolea kero wananchi wa kijiji hicho.
Ridhiwani alisema kuwa mbali ya kuhakikisha pampu mpya inapatikana pia kuna mradi mwingine wa mjai toka Matipwili na ule wa Wami Chalinze atahakikisha maji yanafika kwani mradi huo utavifikia vijiji na vitongoji ambavyo havikupata maji katika awamu mbili zilizopita vitafikiwa na awamu hii.
Mwisho.










MGOMBEA UDIWANI AHAIDI KUTOA ASILIMIA 50 YA POSHO KUCHANGIA SHUGHULI ZA MAENDELEO

Na Mwandishi Wetu, Kibaha
MGOMBEA Udiwani wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kata ya Kawawa Jimbo la Kibaha Vijijini Otto Kanyonyi amesema kuwa endapo atafanikiwa kuchaguliwa kwenye nafasi hiyo atatoa asilimia 50 ya posho zake atakazokuwa anapata kwenye vikao vya madiwani  kwa ajili ya kuchangia shughuli za maendeleo kwenye kata hiyo.
Kanyonyi aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari huko Mlandizi Kibaha juu ya mikakati yake ya kuwaletea maendeleo wakazi wa kata hiyo endapo atashinda kwenye nafasi ya udiwani kwenye uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 25 mwaka huu.
Alisema kuwa moja ya mkakati wake ambao ataupa kipaumbele ni ujenzi wa zahanati katika kata hiyo ili kuwapatia huduma wananchi badala ya kupata huduma hizo kwenye kata za jirani.
“Endapo nitafanikiwa kuwa diwnai wa kata yetu ya Kawawa nitahakikisha natoa asilimia 50 ya posho nitakayokuwa npata naitoa kwa ajili ya shughuli za maendeleo hasa zile huduma za jamii ikiwa ni pamoja na afya, elimu na maji,” alisema Kanyonyi.
Aidha alisema kuwa ameamua kujitolea posho hizo kutokana na kuwa na uchungu wa maendeleo na kuona kuwa moja ya njia za kuleta maendeleo ni kuchagia kwa hali na mali.
“Fedha hizo nataka zilete maendeleo katika kata yangu kwani ili kufanikisha mambo kiongozi lazima uonyeshe njia kwa wale unaowangoza hivyo na mimi nataka niwe kiongozi wa mfano ili niache kumbukumbu kuwa nilihamasisha maendeleo,” alisema Kanyonyi.
Alibainisha kuwa wananchi wanakabiliwa na changamoto nyingi hivyo moja ya njia za kuwahamasisha kujiletea maendeleo ni pamoja na kuchangia shughuli za maendeleo.
Mwisho.
Na John Gagarini, Chalinze
UMOJA wa Wanawake Tanzania (UWT) wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani umetoa salamu za rambirambi kufuatia kifo cha mwenyekiti wa tawi la Ubena Zomozi Kido Antoni (65) kufariki dunia wakati wa mkutano wa kampeni wa diwani wa kata ya Ubena Jimbo la Chalinze.
Mwenyekiti huyo wa tawi alifariki Septemba 30 majira ya saa 7 mchana wakati wakiwa kwenye shamrashamra ya kuwahamasisha wananchi kujiandaa kwa kucheza huku wakimsubiri mgombea udiwani wa kata hiyo kupitia CCM Nicholaus Muyuwa kwa ajili ya mkutano wa kampeni.
Akitoa salamu za pole katibu wa UWT wilaya ya Bagamoyo Mwatabu Hussein alisema kuwa wameupokea msiba huo kwa masikitiko makubwa kwani marehemu alikuwa kwenye harakati za kukipigania chama wakati huu wa kampeni kuelekea uchaguzi mkuu.
Hussein alisema kuwa familia pamoja na chama vimepata pigo kubwa la kuondokewa na kiongozi wao na kumwomba Mungu aipe nguvu katika kipindi hichi bkigumu cha majonzi.
“Tunawapa pole familia pamoja na chama kwa kuondokewa na mpendwa wao kwani alikuwa kwenye harakati za kuhakikisha chama kinapata ushindi kwenye uchaaguzi wa wagombea wa chama kuanzia Rais, Mbunge na Diwani,” alisema Hussein.
Kwa upande wake mgombea huyo wa udiwani Muyuwa alisema kuwa kifo amekipokea kwa masikitiko makubwa kwani marehemu alikuwa mtu muhimu sana ndani ya chama na amekufa wakati akipambana kuhakikisha ushindi unapatikana.
Muyuwa alisema kuwa marehemu alikuwa mzima kabisa na alikuwa kifurahi na wenzake na kutoa hamasa kwa wananchama  na wasio wanachama juu ya kukipigia kura ili kiweze kushinda kwenye uchaguzi m kuu ujao.
Alisema kuwa marehemu alianguka ghafla wakati wakimsubiri yeye aweze kufika kwa ajili ya kuhutubia kwenye mkutano wa kampeni na baada ya kuanguka walimpeleka kwenye zahanati ya Ubena Estate na alifariki wakatia kipatiwa matibabu.
Naye mgombea Ubunge kwenye Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete alifika nyumbani kwa marehemu na kutoa salamu za pole kwani wakati tukio hilo linatokea mgombea huyo alikuwa kwenye mkutano wa kampeni katika kata hiyo kwenye Kijiji cha Mdaula.
Taarifa toka kwa daktari mfawidhi wa zahanati hiyo zilisema kuwa alikufa kutokana na presha na upungufu wa damu, marehemu alizikwa juzi kwenye makaburi ya Ubena na ameacha watoto watano.
Mwisho.
Na John Gagarini, Bagamoyo
MGOMBEA ubunge jimbo la Bagamoyo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM),Dk Shukuru Kawambwa, amesema endapo atachaguliwa kuongoza Jimbo hilo atahakikisha zahanati ya Yombo inapandishwa hadhi na kuwa kituo cha afya ili kupanua huduma za kiafya.
Sambamba na kupandishwa hadhi kwa zahanati hiyo pia Dk Kawambwa  atahakikisha kunakuwa na gari la kubeba wagonjwa wanaopata rufaa kwenda hospitali kubwa  tofauti na ilivyo sasa.
Dk Kawambwa aliyasema hayo kwenye Kijiji cha Yombo wakati wa mkutano wa kampeni na kusema kuwa vipaumbele vyake ni kuhakikisha huduma muhimu za jamii zinapatikana kwa uhakika.
“Mara zahanati hii ikipandishwa hadhi na kuwa kituo cha afya huduma zitaboreka ikiwa ni pamoja na kuwa na wataalamu wa kutosha na huduma nyingi zitatolewa hapa hivyo itapunguza kutumia muda mwingi kufuata huduma mbali,” alisema Dk Kawambwa.
Aidha alisema kuwa pia kipaumbele kingine ni kuhakikisha anasimamia utekelezaji wa ujenzi wa barabara kutoka Makofia-Yombo hadi Mlandizi-Mzenga kwa kiwango cha lami Dk ambapo kwa sasa upembuzi yakinifu umeshafanyika na kilichobakia ni tathmini ya watakaolipwa fidia ambako itapita barabara pamoja na hatua nyingine ili kupisha mpango huo.
“Utekelezaji wa ujenzi wa barabara hiyo kuwa kwa kiwango cha lami upo katika ilani ya Chama Cha Mapinduzi 2015-2020 na ukamilikaji wake utafungua fursa nyingi za kiuchumi hivyo kuleta maendeleo na kuinua uchumi wa wananchi,” alisema Dk Kawambwa.
Katika hatua nyingine alisema kuwa atahakikisha wakazi wa kata ya Yombo na maeneo ambayo hayajafikiwa umeme kuwa atashirikiana na tanesco kupitia mradi wa wakala wa umeme vijijini (REA) kuondoa tatizo hilo ndani ya miaka mitano ijayo.
"Nitahakikisha nasimamia mipango yote,na ilani ya chama changu ili niweze kupunguza makali ya kero zinazowakabili wana Bagamoyo ikiwemo kwenye afya,maji,nishati ya umeme ,elimu na miundombinu"alisema Dk.Kawambwa.
Kwa upande wake mgombea udiwani kata ya Yombo jimbo la Bagamoyo, kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mohamed Usinga,aliwaahidi wakazi wanaoishi katika vijiji vinavyounda kata hiyo kuwa atahakikisha anamalizia kazi ya kusambaza maji, umeme na kituo cha afya kilichopo katani humo.
Alieleza kuwa pindi wakazi hao wakimpatia ridhaa ya kushika nafasi hiyo atapambana ili kumalizia kazi ambayo ilikuwa imeanzwa na mtangulizi wake Ubwa Idd Mazongera ambaye kwa sasa ametangulia mbele za haki.
Awali akiwanadi wagombea hao,meneja kampeni jimbo la Bagamoyo,AbdulSharif alisema wananchi jimboni hapo wasifanye makosa kuchagua wapinzani bali wawachague wagombea kupitia CCM.

Mwisho

Saturday, September 26, 2015

KAMPENI CHALINZE





Na John Gagarini, Chalinze
HALMASHAURI ya wilaya ya Bagamoyo imeshauriwa kuisitisha mikata ya umiliki wa ardhi iliyochukuliwa na wawawkezaji ambao hawajaiendeleza ardhi hiyo kwa kipindi cha zaidi ya miaka 15 wairejeshe kwenye serikali za vijiji kwa ajili ya matumizi ya umma.
Hayo yalisemwa na mgombea Ubunge Jimbo la Chalinze kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ridhiwani Kikwete wakati wa mikutano ya hadhara ya kampeni kwenye Vijiji vya Makombe na Kinzagu kwenye kata ya Lugoba na kusema kuwa wamiliki hao kama wameshindwa kuiendeleza ardhi hiyo ni vema wakairudisha kwa wananchi.
Ridhiwani alisema kuwa inashangaza kuona kuwa wananchi kwenye vijiji hivyo wamekuwa wakihangaika kutafuta ardhi kwa ajili ya kilimo pamoja na matumizi mengine lakini wanakosa maeneo ambayo yamehodhiwa na watu wachache.
“Kwa sasa ni vema halmashauri zikasitisha mikata ya umiliki wa ardhi hiyo kutokana na kushindwa kuiendeleza kwa kipindi cha miaka zaidi yha 10 ambapo sheria inataka mwekezaji kuiendeleza ardhi ndani ya kipindi cha miezi 32 na endapo atashindwa kuiendeleza anaweza kufutiwa umiliki,” alisema Ridhiwani.
Alisema kuwa haipendezi kuona wananchi wanahangaika kutafuta maeneo huku baadhi ya watu wakiwa wamehodhi maeneo bila ya kuyaendeleza na kuacha yakiwa mapori ambayo yanahatarisha usalama wao.
“Ni vema maeneo hayo yakarejeshwa kwenye serikali za vijiji ili yaweze kugawiwa kwa wananchi kwa ajili ya kilimo kwani itakuwa ni sehemu ya kutoa ajira kwa wananchi hususani vijana,” alisema Ridhiwani.
Kwa upande wake diwani wa kata hiyo ya Lugoba ambaye amepita bila ya kupingwa Rehema Mwene alisema kuwa ni kweli maeneo hayo yalichukuliwa na wawekezaji muda mrefu lakini hayajaendelezwa.
Mwene alisema wananchi wa maeneo hayo hususani vijana hawana ajira lakini endapo ardhi hiyo itarejeshwa itasadia kujiajiri kupitia kilimo ambacho ni ajira ya uhakika lakini wanashindwa kujiajiri kupitia kilimo kutokana na kukosa maeneo kwa ajili ya kulima.
Mwisho.
Na John Gagarini, Chalinze
WANANCHI wa Kijiji cha Makombe wameomba uwekwe utaratibu wa malori yanayobeba kokoto kutoka kwenye machimbo ya kokoto yapimwe uzito ili yabebe uzito kutokana na uwezo wa barabara.
Sambamba na hilo wameomba kuwe na utaratibu wa magari hayo kutoa fedha kwa ajili ya ukarabati wa barabara ambazo zimekuwa zikiharibika vibaya kutokana na kupitishwa malori hayo ambayo yana  uzito mkubwa.
Ombi hilo lilitolewa na Rehema John alipozungumza na waandishi wa habari mara baada ya mkutano wa kampeni wa mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ridhiwani Kikwete.
John alisema kuwa barabara hizo zimeharibika vibaya kutokana na magari ya kubebea kokoto ambayo ni mazito na hakuna utaratibu wa kuyapima uzito hali inayosababisha barabara kuharibika.
“Tunaiomba serikali kuweka utaratibu mzuri wa malori hayo yanayobeba kokoto kutoka kwenye machimbo  na kusababisha uharibifu wa barabara inayoelekea kwenye machimbo hayo na kutoka huko kwenda barabara kubwa ya lami,” alisema John.
Alisema kuwa kwa sasa barabara hizo zinazoelekea kwenye machimbo hayo ya kokoto zimeharibika vbaya kutokana na uzito kuwa mkubwa hivyo kushindwa kuhimili uzito.
Kwa upande wake diwani wa kata ya Lugoba ambaye amepita bila ya kupingwa Rehema Mwene alisema kuwa atahakikisha maombi hayo anayapeleka sehemu husika ili hatua ziweze kuchukuliwa kwani uharibifu ni mkubwa sana.
Mwene alisema kuwa barabara zinazoelekea kwenye machimbo hayo zote ni mbaya kutokana na kutofanyiwa ukarabati ambapo licha ya halmashauri kuzifanyia matengenezo lakini zinaharibika haraka kutokana na uzito mkubwa wa malori hayo.
Kwa upande wake mgombea Ubunge wa CCM Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete alisema kuwa kuna haja ya wanaotumia barabara hizo hasa wale wenye magari yanayobeba kukoto pamoja na wawekezaji kwenye machimbo hayo kufanya ukarabati wa barabara hizo.
Ridhiwani alisema kuwa wawekezaji wanapaswa kuboresha huduma mbalimbali ndani ya kijiji ili wananchi waweze kunufaika na uwekezaji wao na hivyo ni vema wakazikarabati barabara hizo.
Mwisho.
Na John Gagarini, Chalinze
WANANCHI wakiwemo wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliojiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura wilayani Bagamoyo hususani wanawake wametakiwa wasikubali kurubuniwa na baadhi ya watu na kuuza shahada zao kwa matapeli kwa madai ya kuipunguzia kura kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba 25 mwaka huu.
Akizungumza kwenye mkutano wa kampeni wa mgombea wa CCM Ridhiwani Kikwete kwenye kijiji cha Lunga kata ya Lugoba wilayani humo katibu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Mwatabu Husein alisema kuwa wapinzani wao wameanza kununua kadi za wapiga kura ili kukipunguzia kura.
Hussein alisema kuwa kuna watu wanapita na kuwarubuni wananchi na wanachama wa CCM ili wawauzie kadi za mpiga kura ili kupunguza idadi ya wapiga kura kwani endapo mtu atakuwa hana kadi ya mpiga kura hatakuwa na haki ya kupiga kura kwenye uchaguzi huo.
“Nawashauri wananchi na wana CCM kuwa makini na watu hao kwani wamekuwa wakitumia njia hiyo ya kuzinunua kadi hizo ili kutuathiri kupata ushindi wa kishindo hivyo mnapaswa kuwa macho hasa wakinamama msikubali kuyumbishwa,” alisema Hussein.
Alisema kuwa tayari wamewashika pabaya wapinzani wao ambao sasa wamenza kuweweseka na kufanya vitendo vinavyoashiria kushindwa na kuanza kutapatapa.
“Wapinzani wetu hawatuwezi wamenza kununua kadi za wapiga kura ili kutupunguzia ushindi wa kishindo lakini tayari wameshachelewa tutawashinda kwa kishindo kikubwa na mwisho wao utakuwa Oktoba 25 mwaka huu,”a lisema Hussein.
Aidha alisema kuwa wapinzani hali yao imekuwa mbaya kwani hawana uwezo wa kuishinda CCM ambayo imejipanga vizuri kwa mikakati yake ya ushindi na washindani wao tayari wameshakubali kushindwa sasa wanatafuta sababu ya kushindwa hata kabla uchaguzi haujafanyika.
Mwisho.








Wednesday, September 23, 2015

WALILIA KISIMA CHA MAJI KILICHOPO HUTOA MAJI KILA BAADA YA MASAA MANNE

Na John Gagarini, Mkange
WANANCHI wa Kijiji cha Gongo kata ya Mkange wilayani Bagamoyo wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa maji ambapo huweka foleni ya kuchota maji kwenye kisima kilichopo kijijini hapo baada ya wiki mbili.
Kutokana na usosefu huo wa maji wananchi hao wamekuwa wakinunua maji ya bomba ndoo ya lita 20 kati ya shilingi 1,000 na shilingi 1,500 maji ambayo huuzwa kwenye magari au pikipiki hivyo kuwafanya wajikute hawapati maendeleo kutokana na gharama kubwa kuzitumia kununulia maji.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya mkutano wa kampeni wa mgombea Ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ridhiwani Kikwete, kwenye kata ya Mkange mwananchi wa Kijiji hicho Hungilo Nyoka alisema kuwa maji yamewafanya washindwe kupata maendeleo.
Nyoka alisema kila kaya inatakiwa ichote madumu manne ili angalau kila mmoja apate baada ya hapo maji hukatika ambapo inatakiwa mtu asubirie tena na mzunguko huo hufanya foleni ya mtu mmoja kufikiwa tena baada ya wiki mbili kwani hapa kuna wananchi 1,690.
Alisema changamoto kubwa kwao ni maji ambayo yamekuwa yakiwafanya washindwe kufanya shughuli za maendeleo ipasavyo kwani hata wakipata fedha kutokana na shughuli zao fedha zote huishia kununulia maji.
“Tunawaomba wahusika kutuangalia kwa jicho la huruma maji kwetu ni kikwazo cha kupata maendeleo kwani hata ukipata fedha kiasi gani zote zinaishia kwenye maji hivyo tunaomba tuchimbiwe kisima kwani kilichopo maji ni kidogo sana yanatoka kila baada ya saa moja yanakatika,” alisema Nyoka.
Aidha alisema kuwa maji wanayokunywa ni ya bomba lakini yanatoka vijiji jirani vya Matipwili ambako kuna umbali wa kilomita 11 na kijiji cha Mkange kilomita tisa na alisema kuwa chanzo cha maji ya kisima kutotoka ipasavyo ni kwamba waliochimba kisima hawakuchimba hadi kuuukuta mwamba ambapo chini ya mwamba ndiyo kuna maji mengi.
“Tunaomba wadau wa masula ya maendeleo kutusaidia kuweza kupata maji kwani tunashindwa hata kujiletea maendeleo kutokana ukosefu wa maji na wkati mwingine watoto hushindwa kwenda shule endapo maji yanakuwa ya shida kwani hawawezi kwenda wachafua kwani mimi kwa siku hutumia madumu matatu hadi matano kwa siku,” alisema Nyoka.
Kwa upande wake mgombea udiwani kupitia CCM Injinia Juma Mgweno alisema kuwa tatizo hilo ni kubwa sana lakini atahakikisha maji yanapatikana kwa kuita wadau mbalimbali ili waweze kuwachimbia kisima.
Naye mgombea wa Ubunge kupitia CCM Ridhiwani Kikwete alisema kuwa visima viwili vilivypo kijiji hapo havitoi maji ambapo kimoja kinahitaji pampu ambayo imeharibika atahakikisha inapatikana mpya ili kuwaondolea kero wananchi wa kijiji hicho.
Ridhiwani alisema kuwa mbali ya kuhakikisha pampu mpya inapatikana pia kuna mradi mwingine wa mjai toka Matipwili na ule wa Wami Chalinze atahakikisha maji yanafika kwani mradi huo utavifikia vijiji na vitongoji ambavyo havikupata maji katika awamu mbili zilizopita vitafikiwa na awamu hii.
Mwisho.
Na John Gagarini, Mkange
KIJIJI cha Gongo kata ya Mkange wilaya ya bagamoyo mkoa wa Pwani kinakabiliwa na ukosefu wa mizani ya kuwapimia watoto wenye umri chini ya miaka mitano hali inayowafanya akinamama kuwapimia watoto wao mzani wa kijiji cha jirani cha Matipwili.
Akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea kijiji hicho wakati wa mikutano ya kampeni ya CCM ya kuwania Ubunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwnai Kikwete, moja ya akinamama Mwajuma Juma alisema kuwa hutugemea mizani ya majirani zao ili kupata huduma hiyo.
Juma alisema kuwa kama ujuavyo kiafya watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano hubidi wahudhurie kliniki kila baada ya mwezi ambapo huchunguzwa afya yake na moja ya jambo muhimu ni kupima uzito kwenye zahanati ya kijiji.
“Tatizo lililopo kwenye zahanati yetu ni ukosefu wa mizani ambapo hutubidi tukaazime kwa majirani zetu kijiji cha jirani hivyo kusababisha msongamano mkubwa inapofikia siku ya kwenda kliniki tunaomba tusaidiwe upatikanaji wa mizani kwa ajili ya kurahisisha huduma hiyo ambayo ni muhimu kwa watoto,” alisema Juma.
Alisema kuwa kijiji kinalazimika kutoa kisia cha shilingi 10,000 kwa jili ya kumlipa mhudumu wa afya wa Kijiji hicho cha Matipwili ambaye ndiyo hutoa huduma hiyo ya kuwapima uzito watoto hao wanapokwenda kliniki.
“Tunaomba tusaidiwe kifaa hicho kwani akinamama wanajitihada kubwa ya kuwapeleka watoto wao kliniki lakini changamoto kubwa ni ukosefu wa mizani ya kuwapimia ambapo siku unapokuja siku hiyo inabidi kazi nyingine zisifanyike kwa ajili ya kusubiria foleni kwa ajili ya kuwapima watoto uzito,” alisema Juma.
Kwa upande wake mgombea Udiwani kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi CCM, Injinia Juma Mgweno alisma kipaumbele chake cha kwanza endapo atachaguliwa ni kuhakikisha huduma za afya hasa za mama na mtoto zsinaboreshwa.
Mgweno alisema kuwa akichaguliwa atahakikisha kuwa huduma bora zinapatikana ili akinamama na watoto waweze kuwa na afya bora kwa kupata huduma muhimu za kiafya kwani bila ya afya bora mama hatoweza kuihudumia familia yake.
Naye Mgombe Ubunge wa CCM Ridhiwani Kikwete alisema kuwa chnagamoto ya vifaa tiba pamoja na wahudumu katika zahanati ya kijiji iliyojengwa na Mkapa Foundation anaijua lakini mkakati wake ni kuhakikisha kuwa wahudumu wa afya wanakuwepo pamoja na mganga ili huduma bora ziwepo.
Ridhiwani alisema kuwa atahakikisha wagnga watatu wanaletwa kwenye zahanati hiyo ili kukabiliana na upungufu wa wahudumu wa afya katika zahanati hiyo ambayo inakabiliwa na changamoto mbalimbali.
Mwisho.
Na John Gagarini, Mkange
MGOMBEA Ubunge kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi( CCM) Ridhiwani Kikwete amesema kuwa endapo atachaguliwa kuwa mbunge wa Jimbo hilo atahakikisha ujenzi wa shule ya Msingi Kwamakulu unakamilika ili kuwaondolea adha wanafunzi kusoma shule ya kitongoji jirani cha Manda.
Aliyasema hayo jana kwenye Kitongoji  cha Kwamakulu kata ya Mkange wilayani Bagamoyo wakati wa mkutano wake wa kampeni kuomba ridhaa ya kuliongoza jimbo hilo kwa kipindi cha miaka mitano ijayo kwenye uchaguzi utakaofanyika Oktoba 25 mwaka huu.
Ridhiwani alisema kuwa atahakikisha ujenzi huo unafanyika ambapo kwa sasa wanafunzi wanaotoka kitongoji hicho husomea shule ya Msingi Manda kwenye kitongoji cha jirani kwa kutembea muda wa masaa mawili hadi kufika shuleni hali inayosababisha wengine kushindwa kusoma kutokana na umbali.
“Namshukuru Mungu kunijalia mimi nimesoma kiasi fulani lakini hali kama hii ya kitongoji kukosa shule ya msingi ni jambo ambalo halinifurahishi hata kidogo lakini naomba mnipe ridhaa ya kuwa kiongozi wenu ili niweze kufanya kazi hii ya kuhakikisha shule ya msingi inapatikana hapa ili watoto wafaidi shule,” alisema Ridhiwani.
Alisema kuwa elimu ni haki ya msingi ya mtoto lakini pia anapaswa aipate katika mazingira mazuri siyo kugeuka tena mateso kwani umbali wa masaa mawili kwa mwanafunzi wa shule ya msingi ni tatizo kubwa.
“Tumeanza na ujenzi wa darasa la awali ambapo nilitoa mifuko 100 ya simenti nashukuru naona angalau kimepatikana chumba kimoja cha darasa na choo pamoja na nyumba ya mwalimu nitahakikisha ujenzi huu unakamilika na baadaye tutaendelea na ujenzi wa madarasa mengine ili kupata shule hapa badala kwenda Manda,” alisema Ridhiwani.
Kwa upande wake mgombea udiwani wa CCM Injinia Juma Mgweno alisema kuwa kwa kutumia elimu yake akishirikiana na mgombea ubunge watahakikisha kwa pamoja shule inajengwa na inakamilika ili watoto waondokane na adha ya kusoma mbali.
Mgweno alisema kata hiyo inakabiliwa na baadhi ya changamoto ikiwa ni pamoja na ukosefu wa shule kutokana na baadhi ya vitongoji kujigawa kutoka kwenye vijiji hivyo atahakikisha ujenzi wa shule na nyumba za walimu inakuwa kipaumbele chake.
Naye mwananchi wa Kijiji hicho Siyawezi Juma alisema kuwa ujenzi wa shule ya Msingi utasaidia kuwapunguzia adha watoto wao kwenda kusoma umbali mrefu ambapo husababisha wengine kukata tama na kuacha shule kutokana na umbali.
Juma alisema kujengwa kwa shule kitongojini hapo itakuwa ni mkombozi wa watoto wao katika suala la elimu ambayo ni muhimu kwa watoto kwani endapo wataikosa itawasababishia kuwa nyuma kielimu na kuhsindwa kujiendeleza kimaisha.

Mwisho.     

Tuesday, September 22, 2015

KAMPENI ZAENDELEA JIMBO LA CHALINZE

Na John Gagarini, Mandela
MGOMBEA Ubunge Jimbo la Chalinze kupitia Chama Cha Mapinduzi Ridhiwani Kikwete amesema kuwa endapo atafanikiwa kuchaguliwa kwenye nafasi hiyo atahakikisha zahanati inajengwa kwenye Kijiji cha Kibaoni ili kuwaondolea adha wananchi wa kijiji hicho.
Aliyasema hayo jana kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika Kijijini hapo kata ya Mandela na kusema kuwa ilani ya chama anasema kila kijiji lazima kiwe na zahanati huku kila kata ikitakiwa kuwa na kituo cha afya ili kurahishisha upatikanaji wa huduma za afya karibu.
Ridhiwani alisema kuwa hicho kitakuwa moja ya vipaumbele vyake ambavyo atahakikisha kuwa katika kipindi cha miaka mitano ujenzi huo unakamilika na wanakijiji wanapata huduma za afya karibu tofauti na sasa ambapo huwalazimu kwenda kijiji jirani cha Mandela.
“Ilani ya chama inasema kuwa kila kijiji lazima kiwe na zahanati hivyo endapo nikichaguliwa kwenye nafasi hii ya ubunge kwa kushirikiana na wananchi hivyo nitahakikisha zahanati inajengwa ili huduma zipatikane karibu,” alisema Ridhiwani.
Alisema kuwa hata kata ya Mandela haina Kituo cha afya ambapo kata hiyo ni mpya ambayo imezaliwa kutoka kata ya Miono na kutaka ujenzi wa kituo hicho cha afya kujengwa kwenye kijiji hicho.
“Katika kipindi cha uongozi wangu wa mwaka mmoja na miezi miwili tumeweza kukarabati zahanati 24 huku nane zikiwa zimejengwa pia tumeweza kufanikisha kujngwa nyumba za waganga pamoja na upatikanaji wa vifaa tiba na dawa,” alisema Ridhiwani.
Aidha alisema kuwa bado kuna changamoto ya baadhi ya vijiji kukosa zahanati hata hivyo mikakati ni kuhakikisha zinajengwa ambapo mipango inaendelea kwa kushirikiana na wananchi.
Kwa upande wake mgombea udiwani wa kata ya Mandela Madaraka Mbode alisema kuwa tayari kata imetenga eneo lenye ukubwa wa hekari 10 kwa ajili ya ujenzi wa zahanati kwenye kijiji cha Kibaoni.
Mbode alisema kuwa ujenzi wa zahanati hiyo utafanikiwa endapo wananchi watawachagua wgombea kutoka CCM lakini endapo wakiwachagua viongozi wa vyama vya upinzani hawataweza kupata maendeleo.
Naye mkazi wa Kibaoni Ally Athuman alisema kuwa changamoto kubwa inayowakumba wananchi kwenye zahanati wanazokwenda kupata matibabu ni ukosefu wa dawa.
Mwisho.
Na John Gagarini, Mandela
MGOMBEA Udiwani kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kata ya Mandela wilaya ya Bagamoyo Madaraka Mbode amemwomba mgombea Ubunge Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete kusimamia ujengwaji wa tenki kubwa la maji ili kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa maji.
Mbode aliyasema hayo kwenye Kijiji cha Lupungwi wakati wa mkutano wa kampeni za Ubunge nakusema kuwa Ridhiwani ndiye aliyeanzisha mchakato wa ujengwaji wa matenki kwenye baadhi ya vijiji.
Alisema kuwa awamu ya pili imevifanya vijiji vingi kwenye Jimbo hilo kuwa na maji lakini baadhi bado havijapata huduma hiyo ambapo awamu ya tatu ya mradi wa maji utavifikia vijiji na vitngoji ambavyo havikubahatika kupata maji.
“Wananchi nawaombeni mchagueni Ridhiwani kwani anauwezo wa kutufanikishia kupata maji ambapo kwa sasa maji yanatoka lakini endapo kunatokea tatizo kwenye mtambo maji hayapatikani ndiyo maana ujenzi wa matenki makubwa unaanza ili kuhakikisha maji yanapatikana muda wote,” alisema Mbode.
Aidha alisema kuwa anaomba na yeye achaguliwe kwenye nafasi ya udiwani ili ashirikiane na mbunge huyo kuwaletea maendeleo ambapo kwa sasa kijiji hicho kimewekewa nguzo kwa ajili ya kuwasambaziwa umeme.
Naye Ridhiwani Kikwete alisema kuwa tayari tathmini imeshaanza kufanywa ambapo wataalamu wameshachukua udongo kwa ajili ya kupima kabla ya kujenga tenki hilo ambalo litakuwa na uwezo wa kuhifadhi maji mengi.
Ridhiwani alisema kuwa awamu hii ya tatu ya mradi wa maji wa wami chalinze utavifikia vijiji na vitongoji vyote sambamba na ujengaji wa matenki makubwa kwa ajili ya kuhifadhia maji.
Mwisho.
Na John Gagarini, Mandela
BAADHI ya waangalizi wa uchaguzi wamesema kuwa Tanzania imeweka historia kwa kuwa na waangalizi wengi kwenye uchaguzi wa mwaka huu hali ambayo itafanya uchaguzi kuwa huru na wa haki.
Hayo yalisemwa jana na mwangalizi wa ndani kutoka (TEMCO) Renatus Mkinga kwenye kijiji cha Lupungwi kata ya Mandela wilayani Bagamoyo wakati wa mkutano wa kampeni wa mgombea ubunge wa Jimbo la Chalinze kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ridhiwani Kikwete.
Mkinga alisema kuwa kwa waangalizi wa ndani ni zaidi ya 6,000 huku wale wa kutoka nje wakiwa ni 600 ambao ni wengi na haijawahi kutokea katika chaguzi zilizopita.
“Sisi hatuna vyama tunachokifanya ni kuangalia ,mwenendo mzima wa uchaguzi kuanzia hatua ya kampeni hadi utakapofanyika uchaguzi Oktoba 25 mwaka huu,” alisema Mkinga.
Alisema kuwa kazi ya wasimamizi ni kuangalia mienendo ya uchaguzi katika kampeni na anaamini kuwa utakuwa huru na haki kwani hadi sasa kampeni zinaendele vizuri.
“Tunahudhuria kwenye mikutano ya vyama mbalimbali ili kuangalia wanapiga kampeni vipi na kuangalia wananchi wanajitokeza vipi kusikiliza sera za vyama husika,” alisema Mkinga.
Aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kusikiliza sera za vyama mbalimbali ili waweze kuangalia ni mgombea gani ambaye anawafaa ili mwisho wa siku waweze kumchagua kiongozi bora na si bora kiongozi.
Mwisho.
   

        

Monday, September 21, 2015

SITA WAFA WANNE WAJERUHIWA

 Na John Gagarini, Mkuranga
WATU sita wamepoteza maisha na wanne kujeruhiwa baada ya basi dogo la abiria kugongana uso kwa uso na basi kubwa la kampuni ya Ibra.
Ajali hiyo ilitokea jana katika kijiji cha Njopeka wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani.
Kamanda wa polisi mkoa wa Pwani Jafari Ibrahim alithibisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa katika ajali hiyo watu sita amekufa na wanne kujeruhiwa.
Ibrahim alisema basi hilo kubwa  lenye namba za usajili T 195 DCE aina ya YU TONG likiendeshwa na Alex Peter (46) liligongangana na gari ndogo iliyokua ikitokea Jaribu kuelekea Mbagala jijini Dar Es Salam lenye namba za  usajili T 782 DC.
Alisema kuwa chanzo cha ajali hiyo kuwa ni dereva wa Basi la Ibra kuendesha zaidi kulia na hivyo kukutana uso kwa uso na kusababisha ajali hiyo.
Aidha alisema baada ya ajali hiyo wamelazimika kuweka askari katika eneo hilo, huku wakiwataka madereva kuwa makini na sheria za barabarani.
Ibrahim aliwasihi wananchi kutoa taarifa kwa Askari wa Usalama barabarani kwa namba zilizopo kwenye mabasi pindi wanapobaini kukiukwa kwa sheria za barabarani kabla ajali haijatokea.
Mwisho.

WENGI WAMUAGA MTOTO WA ALIKUWA KIONGOZI WA WAFUGAJI, RAIS DK JAKAYA KIKWETE ATUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI

Na John Gagarini, Lugoba
WAGOMBEA wanaowania nafasi za uongozi hapa nchini wametakiwa kukubali matokeo mara uchaguzi utakapofanyika Oktoba 25 mwaka huu kwani kuna maisha mengine baada ya uchaguzi  kuendelea kufanya kampeni zao huku wakiendelea kuhubiri na kulinda amani iliyopo kwani wana nafasi kubwa ya kuwashawishi wafuasi wao wasifanye vurugu au kufanya vitendo vinavyosababisha uvunjifu wa amani.
Pia wagombea watakaoshindwa kwenye uchaguzi mkuu wakubali matokeo kwani kwenye washindani lazima kuwe na washindwa ili kuondoa hali ya mafarakano kwani kwa wale watakaoshindwa wasipokubali matokeo wanaweza kuleta uvunjifu wa amani.
Hayo yalisemwa juzi Kijiji cha Maviayangombe kata ya Lugoba wilayani Bagamoyo mkoani Pwani na Askofu mkuu wa Dayosisi ya Morogoro ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Jacob Mameo Ole Paulo wa Dayosisi ya Morogoro wakati wa mazishi ya mtoto wa aliyekuwa kiongozi wa wafugaji Laban Moreto, Karokya Moreto (33) ambaye alikuwa mwanajeshi wa kikosi cha 04/691 cha Mtwara.
Askofu Ole Paulo alisema kuwa wagombea hao wanauwezo wa kudumisha amani kwa kuhubiri au kuingiza nchi kwenye machafuko endapo watayatumia vibaya majukwaa wakati wa kipindi hichi cha kampeni za uchaguzi.
“Wanapaswa kuhubiri amani na kuacha kutumia maneno yatakayo haribu amani ya nchi iliyopo ambayo imedumu kwa kipindi kirefu tangu nchi ilipopata uhuru miaka zaidi ya 50 hivyo itakuwa ajabu ivunjwe kisa kuwania uongozi tu,” alisema Askofu Ole Paulo.
Aidha alisema kuwa vyama vya siasa vinapaswa kupingana kwa hoja na kwa malumbano ambayo hayana maana bali yanaweza kuleta mitafaruku isiyokuwa ya lazima hasa kwa wale wanaoshindwa kwani wanapaswa kukubali matokeo.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete alisema kuwa amesikitishwa na kifo cha marehemu ambaye alikuwa ni ndugu kwani wamekuwa wakiishi kama familia moja na walikuwa na ushirikiano mkubwa baina ya familia zao.
Ridhiwani alisema kuwa kifo hicho ni pigo kwa familia hiyo pia kwa Taifa kwani alikuwa ni mtumishi wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) na alikuwa mtaalamu wa rada hivyo pengo lake haliwezi kuzibika kikubwa ni kumwombea marehemu.
Kufuatia msiba huo Rais Dk Jakaya Kikwete alituma salamu za pole kwa familia hiyo kupitia kwa Mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete na kusema kuwa anatoa pole na Mungu awape nguvu katika kipindi hichi kigumu cha maombolezo na yuko pamoja nao.
Alisema kuwa Rais alishindwa kuhudhuria msiba huo kwani kwa sasa yuko nje ya nchi lakini pindi atakaporudi ataitembelea familia hiyo kwa ajili ya kuifariji kufuatia kifo cha mtoto wa aliyekuwa kiongozi wa kabila wafugaji
Naye mgombea Ubunge Jimbo la Chalinze kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mathayo Torongei alisema ili amani iendelee kuwepo ni vema dola ikatenda haki badala ya kupendelea upande mmoja.
Marehemu alifariki kwa ajali baada ya gari alilokuwa akiendesha kupasuka tairi la mbele na kusababisha ajali iliyopelekea kifo chake siku ya Septemba 16 mwaka huu  huko Mtwara ameacha mke na watoto watatu.
Mwisho. 







Mgombea Ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Chalinze wilayani Bagamoyo mkoani Pwani Ridhiwani Kikwete kulia akifurahia jambo na mkuu wa wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi Pololet Mgema wakati wa mazishi ya Karokya Moreto (33) mtoto wa alikuwa kiongozi wa wafugaji Laban Moreto huko Kijiji cha Maviyangombe kata ya Lugoba. 

 Baadhi ya Wazee wakiwa wamekaa kwenye msiba huo huko kijiji cha Maviyangombe Lugoba wilayani Bagamoyo. 

Kulia ni Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Morogoro  Jacob mameo Ole Paulo akiwa na mgombea Ubunge jimbo la Chalinze kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ridhiwani Kikwete. 

Kulia Ridhiwani Kikwete mgombea Ubunge Jimbo la Chalinze kupitia CCM akifuatiwa na mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Majid Mwanga, mkuu wa wilaya ya Nachingwea Pololet Mgema na mgombea ubunge Jimbo hilo kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Matayo Torongei wakiwa kwenye msiba huo. 

 Askofu Jacob Mameo Ole Paulo akizungumza wakati wa msiba huo. 

Baadhi ya ndugu wa wakilia kuomboleza kifo cha ndugu yao. 

 baadhi ya ndugu wa wakilia kuomboleza kifo cha ndugu yao.

Akinamama ndugu wa karibu wa marehemu wakilia kuomboleza kifo hicho. 

Baadhi ya askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania JWTZ wakiwa wamebeba jeneza lilokuwa na mwili wa marehemu kuelekea makaburini kwa ajili ya mazishi. 

Baadhi ya waombolezaji wakiaga mwili wa marehemu kabla ya mazishi  

Sehemu ya waombolezaji wa msiba huo.