Tuesday, January 13, 2015

VIONGOZI WA SERIKALI ZA MITAA NA VIJIJI WAASWA NA WANANCHI WAHAKIKISHIWA KUPATA UMEME


 Na John Gagarini, Bagamoyo
VIONGOZI wa serikali za mitaa na vijiji wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani waliochaguliwa hivi karibuni wametakiwa kusoma mapato na matumizi ili kuepuka kuenguliwa kwenye nafasi zao kama baadhi yao waliopita kukataliwa na wananchi.
Moja ya changamoto zilizosababisha viongozi hao waliopita baadhi yao walienguliwa na wananchi huku wengine wakishindwa kurudishwa kwenye kura za kuteuliwa kuwani uongozi kwenye uchaguzi uliofanyika mwishoni mwa mwaka jana.
Hayo yalisemwa Bagamoyo na katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kombo Kamoto alipozungumza na wananchi wakati wa ziara ya Mbunge wa Jimbo la Chalinze wilayani Bagamoyo Ridhiwani Kikwete kwenye  vijiji vya kata za Kibindu, Mbwewe, Mdaula, Bwiringu, Fukayosi, Miono na Kiwangwa.
Kamote alisema kuwa viongozi hao waliochaguliwa na wananchi hasa wale wanaotoka chama hicho kwani hawana budi kuwatumikia wananchi ipasavyo kwa lengo la kuwatatulia changamoto ambazo zinawakabili katika nyanja mbalimbali kwenye huduma za kijamii.
“Mmechaguliwa na wananchi kwa heshima ya chama chetu, hususani kusoma mapato na matumizi hivyo niwasihi mchape kazi kama sheria na taratibu zinavyowaongoza, sitopenda kusikia wananchi wakilalamikia kuhusu utendaji wenu, mtambue mwaka huu mmeapishwa na mahakimu tofauti na miaka yote, hivyo yeyote atayekiuka kiapo hicho ataondolewa kwenye nafasi yake,” alisema Kamote.
Alisema kuwa viongozi hao watatakiwa kuitisha mikutano na kusoma mapato na matumizi kwa wananchi ili waweze kujua yanayofanyika kwenye maeneo yao.
Viongozi hao pia waliaswa kutokuwa madalali wa kuuza ardhi kiholela na kuwakandamiza wananchi ambao wakati mwingine hawajui haki zao za msingi.
“Baadhi waliondolewa kutokana na kushindwa kuitisha mikutano ikiwa ni pamoja na kushindwa kusoma mapato na matumizi hali iliyowafanya waondolewa madarakani au kushindwa kwenye uteuzi wa kuwania nafasi hizo, alisema Kamote.
Aidha alisema kuwa inashangaza kuona baadhi ya viongozi wanakuwa vinara wa kuuza maeneo na kama yupo kiongozi aliyekuwa anafanya hivyo wanapaswa kuacha na kuwa waadilifu ili kulinda nafasi walizopata.
“Viongozi huu si muda wa kuanza majigambo ama kujivunia nafasi mlizoshika  bali mnatakiwa kutimiza wajibu wenu kwa kusimamia ilani ya chama cha mapinduzi ili kuleta maendeleo kwa wananchi,” alisema Kamote.
Kwa upande wake Ridhiwani Kikwete aliwaomba viongozi hao kufanya kazi kwa bidii ili chama kiendelee kuaminika na kushika dola .
“Fanyeni kazi bila kubagua watu ,watumikieni pasipo kujali itikadi za kisiasa na hiyo ndio sifa pekee ya kiongozi wa sasa asiyejali udini,ukabila wala chama alichopo,”alisema Ridhiwani.
Ridhiwani alisema kuwa yeye akiwa mbunge ataendelea kuwatumika ipasavyo katika kuwaondolea changamoto zinazowakabili.
mwisho.
Na John Gagarini,Chalinze
KILIO cha baadhi ya wananchi wa Jimbo la Chalinze kukosa umeme huenda kikaisha baada ya kuhakikishiwa kuwa watapata huduma hiyo kuanzia m,waka huu kupitia miradi ya umeme vijijini kupitia wakala wa umeme Vijijini (REA).
Changamoto hiyo itapungua kwenye maeneo mbalimbali ya Jimbo hilo katika vijiji ambavyo vipo kwenye awamu ya awamu ya tatu inayotarajiwa kuanza mwezi Juni mwaka huu kupitia miradi hiyo ya REA.
Akiwahutubia wananchi wa vijiji vya Kibindu, Mbwewe, Mdaula, Bwilingu, Fukayosi, Kiwangwa na Chalinze mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete alisema kuwa serikali ya CCM imejipanga kuikabilia changamoto hiyo.
“Kila maeneo niliyopita nimekutana na malalamiko  kutoka kwa wananchi juu ya kukosa umeme wakati vijiji vingine vya kata hizo vikiwa vimepata umeme na kuhoji huku wao wakiona kwa macho umeme umepita juu na kwenda maeneo jirani,” alisema Ridhiwani.
Ridhiwani alise kuwa anatambua umuhimu wa umeme hivyo amekuwa akifanya jitihada za kufuatilia na ndio maana amelazimika kufuatana na meneja wa miradi ya umemem mkoani Pwani Leo Mwakatobe ambaye anatolea ufafanuzi suala hilo.
“Mfano eneo la Kiwangwa halikuwepo katika umeme unaosambazwa na REA lakini baada ya kufanya juhudi hizo fedha zimepatikana hivyo utakuwa wa REA ambapo tanesco imetoa sh.milioni 420 na REA sh.milioni 800,” alisema Ridhiwani.
Aidha alisema kuwa fedha hizo tayari ziko na kazi ya kuanza kusambaza umeme itaanza wakati wowote, kwani anajua umuhimu wa umeme lakini wananchi na kuwaomba wananchi wafahamu juhudi za serikali.
Kwa upande wake  mhandisi wa Tanesco mkoa wa Pwani, Mhandisi Leo Mwakatobe, alisema wanaendelea kumalizia utekelezaji wa awamu ya pili wa mradi wa REA na kazi iliyobaki ni mkandarasi kuanza kazi wakati wowote kuanzia mwezi huu.
Mwakatobe fedha kwa ajili ya mradi wa kusambaza umeme zimepatikana, hivyo wananchi wenye kuhitaji waanze kuchukua fomu.kinachotakiwa wawe na picha mbili na kitambulisho cha aina yoyote.
Mwisho




Monday, January 12, 2015

CHALIWASA YAKANUSHA MASHINE KUUZWA KENYA NA MAGAREZA YAPONGEZWA

Na John Gagarini, Wami
MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Chalinze (CHALIWASA) imekanusha uvumi kuwa mashine za uzalishaji wa maji zimeuzwa nchini Kenya hali ambayo imesababisha maji kukatika mwezi mzima.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake    Meneja wa mamlaka hiyo Injinia Christer Mchomba alisema kuwa uvumi huo si wa kweli kwani mashine zote zipo na zinatumika kama kawaida.
Injinia Mchomba alisema kuwa uvumi huo umekuja kutokana na maji kutokutoka kwa sababu ya mashine hizo kuvuta uchafu ambao umesababisha kuziba na kushindwa kupitisha maji.
“Tatizo la maji kushindwa kutoka hakutokani na mashine kuuzwa bali ni kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha kwenye mkoa wa Morogoro ambapo ndiyo chanzo cha mto Wami na kusababisha uchafu kuwa mwingi na mashine kuziba na kuharibika hivyo maji kushindwa kutoka,” alisema Injinia Mchomba.
Alisema kuwa tatizo ni tekeo ambapo kwa sasa linawekwa ambalo likikamilika litasaidia kuchuja uchafu tofauti na ilivyokuwa mwanzo kwani maji zamani yalikuwa masafi na yalikuwa hayana uchafu.
“Uchafu huo unatokana na uharibifu mkubwa wa mazingira unaofanywa na watu wanaojihusisha na uchimbaji wa madini, kuingiza mifugo kwenye vyanzo vya maji na uchafuzi wa mazingira hivyo kusababisha uchafu mwingi kuja na maji,” alisema Injinia Mchomba.
Alisema kuwa ukarabati wa mashine hizo unaendelea ambapo umefikia asilimia 85 na baada ya miezi miwili au mitatu tatizo la ukosefu wa maji Chalinze litakuwa ni historia
“Tuna mitambo 30 na mingine mipya hata hatujaifungua iweje watu waseme kuwa imeuzwa wakitaka ukweli waje hapa ili waione kuliko kusema tu bila ya kujua ukweli na waache kuvumisha vitu ambavyo havina ukweli,” alisema Injinia Mchomba.
Aidha alisema kuwa kwa sasa kuna mradi unaotekelezwa ambao utavifikia vitongoji vyote vya Jimbo la Chalinze ambapo awamu ya tatu utatumia bilioni 60 hadi kukamilika.
Mwisho.   
Na John Gagarini, Ubena
MBUNGE wa Jimbo la Chalinze wilayani Bagamoyo mkoani Pwani Ridhiwani Kikwete amelipongeza Jeshi la Magereza mkoani Pwani kwa ujenzi wa madarasa mawili ya shule ya Sekondari ya Bwawani kwa gharama nafuu.
Aliyasema hayo wakati akizindua madarasa hayo kwa ajili ya wanafunzi wa kutwa wa shule hiyo ambayo inamilikiwa na Jeshi hilo la Magereza eno la Ubena.
Ridhiwani alisema kuwa Jeshi hilo limeonyesha uzalendo wa hali ya juu na kutumia vizuri rasilimali fedha kwa kujenga madarasa hayo yenye mawili thamani ya shilingi milioni 31.8.
“Haya ndiyo mambo tunayoyataka kwa kufanya ujenzi wa vitu vya umma kwa matumizi mazuri ya fedha na ujenzi bora hivyo taasisi nyingine za serikali zinapaswa kuzingatia ujenzi kama huu,” alisema Ridhiwani.
Alisema baadhi ya taasisi za umma zimekuwa zikifanya ujenzi wa kawaida kwa gharama kubwa huku ukiwa haujazingatia ubora wa ujenzi wa majengo ambayo hutumiwa kwa muda mrefu.
Aidha alizitaka halmashauri kuwatumia wataalamu wa Magereza katika ujenzi wa majengo mbalimbali ambapo ujenzi wao unazingatia ubora matumizi bora ya rasilimali fedha.
Awali akimkaribisha mbunge huyo mkuu wa Magereza mkoa wa Morogoro  Kato Lugainunula ambaye alimwakilisha mkuu wa Magereza nchini John Minja, alisema kuwa lengo la Magereza ni kuihudumia jamii katika nyanja mbalimbali ikiwa ni pamoja na utoaji wa elimu.
Lugainunula alisema kuwa awali shule hiyo ilitumika kutoa elimu ya sekondari kwa watumishi wa Magereza ambao walikuwa hawajapata elimu ya sekondari lakini waliondoa utaratibu huo na kutoa elimu kwa wanafunzi kutoka sehemu mbalimbali.
Naye kaimu mkuu wa shule hiyo ya Bwawani Emanuel Lwinga alisema kuwa madarasa hayo ni kwa ajili ya wanafunzi wa kutwa ujenzi wake ulitumia muda wa miezi mitano hadi kukamilika kwake.
Lwainga alisema kuwa kila darasa lina uwezo wa kuchukua wanafunzi kati ya 40 na 45 ambapo shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 396 wakiwemo wale wa kidato cha tano na shule hiyo ni moja ya shule zinazofanya vizuri kwenye matokeo ya kidato cha nne kimkoa.

  Mwisho.

Thursday, January 8, 2015

CHANGAMOTO YA MAJI NA VIONGOZI WAUZA KIJIJI

Na John Gagarini, Chalinze
UONGOZI wa Mradi wa maji wa Wami Chalinze wilayani Bagamoyo umetakiwa kutoa taarifa juu ya ukosefu wa maji ambao kwa sasa umedumu takribani mwezi mzima ambapo baadhi ya wanasiasa wa vyama vya upinzani wapotosha ukweli kuhusu tatizo hilo.
Hayo yalisemwa na diwani wa kata ya Bwilingu Nassa Karama katika viwanja vya Masoko wakati mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete alipokwenda kusikiliza kero za wananchi wa kata hiyo.
Karama alisema kuwa maji kwa sasa ni kilio kikubwa kwa wakazi wa mjin huo  huku wao wakiwa hawana utaalamu wa kujua tatizo la ukosefu wa maji linatokana na nini hivyo kushindwa kuwapa majibu sahihi wananchi ambapo hali hiyo imesababishwa ndoo kuuzwa kwa shilingi 700 kutoka shilingi 200.
“Suala la kutotoka kwa maji ni la kitaalamu na wahusika wa mradi wa maji wa Wami Chalinze wanapaswa kutoa taarifa juu ya changamoto zinazosababisha ukosefu wa maji ili majibu yasitolewe na wanasissa ambao wanatumia fursa hiyo kupotosha ukweli wa tatazi hilo,” alisema Karama.
Alisema kuwa wananchi wanapata usumbufu mkubwa kwani kwa sasa wananunua maji kwa baadhi ya watu wenye magari ya kuuza maji ambapo kabla ya tatizo hilo walikuwa walikuwa wakinunua kwa sh.200 na sasa ni sh.700 hali inayosababisha kuwapa wakati mgumu baadhi ya wananchi  ambao baadhi yao kipato chao ni cha chini.
“Baadhi ya wanasiasa hao wanapotosha kwa wananchi kuwa kuna mashine mbalimbali za kukamilisha mradi huo zimeuzwa Nairobi nchini Kenya jambo ambalo linachanganya wananchi na kuleta tafsiri tofauti  kutokana na tatizo hilo,” alisema Karama.
Aliutaka uongozi wa maradi kuo kutoa taarifa juu ya ukosefu wa maji ili kutowapa mwanya wanasiasa  wenye nia ya kutumia jambo hilo kama mtaji wao wa kisiasa.
Naye Mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete akijibu kuhusiana na maswali hayo alisema anafanya taratibu ya kumpeleka waziri wa maji ili aweze kwenda kutembelea maeneo yenye kero kubwa jimboni humo kujionea hali halisi ya ukosefu wa maji.
Ridhiwani alisema kuwa tatizo kubwa la ukosefu wa maji linatokana na tope linaloingia katika mitambo hali inayosababisha maji kushindwa kutokana ambapo kwa sasa wamenunua chujio kwa ajili ya kuchuja uchafu ambao umekuwa ukiziba na maji kushindwa kutoka.
Aliwataka wanasiasa kuacha kupotosha ukweli kwani si jambo zuri kupotosha wananchi  na kuwataka wataalamu kujenga tabia ya kutoa taarifa ya vikwazo vilivyopo ili wananchi wajue.
Mwisho.
Na John Gagarini, Fukayosi
BAADHI ya  viongozi wa Kijiji cha Kidomole wilayani Bagamoyo mkoani Pwani waliohusika kuuza ardhi ya Kijiji hicho kinyume cha sheria wametakiwa kujiandaa kusimama kwenye vyombo vya sheria kujibu tuhuma hizo.
Viongozi hao kwa wameuza eneo kubwa la Kijiji ambapo wananchi wa maeneo hayo wanatakiwa kuondoka na kumpisha mununzi huyo ambaye amechukua eneo kubwa la kijiji.
Akizungumza na wananchi wa Kijiji hicho Mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete, wakati wa ziara ya kutembelea na kukagua shughuli za maendeleo alisema viongozi hao lazima wachukuliwe hatua za kisheria kwa ukiukaji wa maadili ya uongozi.
“Inashangaza kuona mtu anakuja na risiti na kusema kuwa kanunua eneo lote la Kijiji na wananchi wanatakiwa kuondoka kumpisha eti mwekezaji jambo kama hili haliwezekani kwani taratibu haziruhusu na viongozi waliofanya hivi wajiandae kwa kukimbilia tutapambana nao ili haki ya wananchi ipatikane,” alisema Ridhiwani.

Alisema kuwa hatakuwa tayari kuona wananchi hao wanaondolewa kwani sheria za ardhi haziruhusu kuuza eneo la Kijiji zaidi ya hekari 50 zaidi ya hapo lazima suala hilo lipelekwe kwa kamishana wa ardhi.

“Inashangaza kusikia kiongozi kauza hekari zaidi ya 100 kwa mwekezaji sheria haisemi hivyo hata hizo hekari 50 lazima wanakijiji waridhie kwa kufanya mkutano mkuu ili kumpitisha muombaji lakini siyo watu wawili au watatu wanakaa huko ofisini na kuuuziana eneo kinyemela utaratibu huu haupo kisheria,” alisema Ridhiwani.

Akizungumzia kuhusiana na baadhi ya maeneo ya Kijiji kuwemo kwenye eneo la ranchi ya Taifa (NARCO) alisema kuwa uongozi wa halmashauri unapaswa kuonyesha mipaka kwani wananchi walioko kwenye eneo hilo walianza kuishi kabla ya ranchi hiyo.

Aidha alisema maeneo yote yanayomilikiwa na ranchi ya Taifa yaliwekewa mipaka na inajulikana rasmi kisheria tofauti na hapo ambapo ranchi hiyo ndo inaanza kuonyesha mipaka huku kukiwa hakuna alama yoyote na kuutaka uongozi wa ranchi kushirikiana na wananchi hao ili kuondoa malalamiko kwani wanapaswa kuondolewa kwenye maeneo hayo.
Mwisho.



Wednesday, January 7, 2015

WAKAZI CHALINZE WALALAMIKA UKOSEFU WA DAWA KITUO CHA AFYA

Na John Gagarini, Chalinze
WAKAZI wa Chalinze Mjini wameiomba Wizara ya Afya kuangalia upya mgawanyo wa dawa kwenye kituo cha Afya cha Chalinze kwani dawa zinazopelekwa kituoni hapo hazikidhi mahitaji.
Wagonjwa wengi wanaokwenda kuhudumiwa kituoni hapo licha ya kuandikiwa dawa hazipatikani na hutakiwa kununua kwenye maduka ya dawa.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara mbele ya Mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete ambaye yuko kwenye ziara ya kukagua masuala ya maendeleo, moja ya wakazi wa Chalinze kitongoji cha Bwiringu aliyejitambulisha kwa jina la Athuman Rashid alisema huduma ya dawa hakuna kabisa.
“Kila ukienda kupata huduma kwenye kituo cha afya Chalinze utahudumiwa vizuri lakini dawa ni mtihani kwani utaambiwa dawa hakuna nenda kanunue kwenye maduka ya dawa,” alisema Rashid.
Rashid alisema kuwa mgawanyo wa dawa kwenye kituo hicho ni mdogo licha ya kuwa kituo hicho kinahudumia wagonjwa wengi lakini kinakuwa na upungufu mkubwa wa dawa.
“Ombi letu sisi kwa Wizara ya Afya ni kuangalia namna gani ya kukiwezesha kituo hichi kuwa na mgao mkubwa wa dawa kwani suala la dawa ni tataizo kubwa sana na linatuathiri kwani maduka ya madawa yanauza kwa bei za juu,” alisema Rashid.
Naye Mbunge wa Chalinze Ridhiwani Kikwete alisema kuwa ni kweli changamoto hiyo ni kubwa sana kwenye kituo hicho na ni vema kituo hicho kikaangaliwa upya.
“Wagonjwa wamekuwa wakilalamika sana juu ya upatikanaji wa dawa kwani kituo hichi kinapewa dawa sawa na vituo vingine vya afya ambavyo havina wagonjwa wengi,” alisema Ridhiwani.
Ridhiwani alisema tayari wameshaongea na Wizara hiyo na stoo ya madawa MSD juu ya kuomba kuongezewa mgao wa dawa kutokana na ukubwa wa kituo kwani mahitaji ni makubwa sana.

Mwisho.    w

Tuesday, January 6, 2015

MBUNGE WA JIMBO LA CHALINZE RIDHIWANI KIKWETE AENDELEA NA ZIARA JIMBONI

Mbunge wa Jimbo la Chalinze wilayani Bagamoyo Ridhiwani Kikwete akiwahutubia wakazi wa Kijiji cha Pera kweny kata ya Kibindu wilayani Bagamoyo mkoani Pwani wakati wa ziara ya kutembela shughuli za maendeleo

 Ridhiwani Kikwete Mbunge wa Jimbo la Chalinze akikabidhi mpira kwa moja ya Wazee kwenye Kijiji cha Pera Kata Kibindu wakati wa zaiara yake kwenye jimbo hilo

 Hili ni darasa la shule ya msingi ya Kibindu ambayo iliezuliwa paa baada ya kutokea mvua kubwa iliyonyesha mwishoni mwa mwaka jana

 Diwani wa Kata ya Kibindu Mawazo Mkufya akiongea na Mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete mwenye kofia alipotembelea shule hiyo kuangalia uharibifu uliotokana na mvua kubw ailiyonyesha na kuharibu baadhi ya madarasa na ofisi ya mwalimu mkuu wa shule hiyo

 Moja ya Madarasa ya shule ya Msingi Kibindu yaliyoharibiwa na mvua kubw ailiyonyesha mwaishoni mwa mwaka jana 

 Mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete kulia akiongea na waandishi wa habari hawapo kushoto ni diwani wa kata ya Kibindu Mawazo Mkufya. 

 Baadhi ya akinamama wa Kijiji cha Kibindu wakimsikiliza Mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete hayupo pichani wakati wa ziara yake kwenye jimbo hilo

 Choo cha shule ya Msingi Maluiwi kikiwa kimebomoka hali ambayo inawafanya wanafunzi wa shule hiyo kujisaidia porini kwa zaidi ya miaka miwili sasa.

 Hichi ni choo cha nyasi ambacho kinatumiwa na walimu wa shule ya Msingi Maluiwi

 Mbunge wa Chalinze Ridhiwani Kikwete akiongea na wananchi wa Kitongoji cha Mdaula alipotembelea kwenye ziara yake ya kuangalia shughuli za maendeleo kwenye jimbo hilo.

Monday, January 5, 2015

MCHAKATO WA MAMLAKA YA MJI MDOGO CHALINZE CHANGAMOTO KUBWA, MAJAMBAZI WATUMIA MSITU WA MWIDU

Na John Gagarini, Ubena
MCHAKATO wa kuifanya Chalinze kuwa mamlaka ya Mji Mdogo umekumbwa na changamoto kubwa baada ya makundi mawili ya wakulima na wafugaji kupinga mpango huo.
Makundi hayo ambayo ndiyo makubwa katika Jimbo la Chalinze yameonekana kutoupokea mpango huo kwa madai kuwa utawasababisha kushindwa kufanya shughuli za ambazo ndizo zinazowafanya waweze kuishi.
Changamoto za kupinga mchakato huo zimebainika wakati wa ziara ya Mbunge wa Jimbo hilo Ridhiwani Kikwete kutembelea shughuli za maendeleo.
Akizungumzia changamoto hizo Ridhiwani alisema Jimbo hilo lilitenga maeneo kwa ajili ya wafugaji na wakulima katika mpango bora wa matumizi ya ardhi ambapo kila kundi linakaa kwenye eneo lake.
“Changamoto hizi zinakuja kutokana na hali halisi kuwa endapo mamlaka hiyo itakubalika ina maana kutakuwa na sheria ya kuzuia ufugaji wa mifugo pamoja na kuzuia kilimo huku makundi hayo yakitegemea shughuli hizo kuendeshea maisha yao,” alisema Ridhiwani.
Ridhiwani alitoa mfano kwenye maeneo ya wafugaji ya Vijiji vya Chamakweza ambao wana mifugo zaidi ya 18,000, Lukenge wana mifugo zaidi ya 10,000 na Matuli mifugo zaidi ya 8,000.
“Wafugaji wamesema kuwa endapo Mamlaka hiyo itapitishwa mifugo yao wataipeleka wapi na wao ufugaji ndiyo maisha yao kwa ajili ya chakula pamoja na uchumi,” alisema Ridhiwani.
Alisema pia kwa wakulima nao hawataruhusiwa kulima je wataishije wakati kilimo ndiyo shughuli yao ya kuendeshea maisha yao ikiwa ni pamoja na uchumi wao na hawana kitu kingine wanachoweza kukifanya.
“Changamoto hizi katika kueleka Mji Mdogo zimekuwa ni kubwa na ukiangalia zina uzito hivyo mchakato huu umesitishwa huku serikali ikiwa inaangalia namna bora ya kufanya ili kutoathiri maisha ya wananchi,” alisema Ridhiwani.
Aliongeza hata hivyo wananchi wanapaswa kujiandaa na mabadiliko kwani kila jambo lina wakati wake ambapo mipango kama hiyo ina lengo la kuwasogezea huduma karibu wananchi.
Mwisho.
Na John Gagarini, Ubena
WANANCHI wa Kata ya Ubena Jimbo la Chalinze wilayani Bagamoyo Mkoani Pwani wameuomba uongozi wa Gereza la Ubena kuwaruhusu kulitumia eneo la pori la Mwidu kwenye barabara ya Morogoro Chalinze ambalo limekuwa likitumiwa na majambazi kujificha kwa ajili ya kuteka magari nyakati za usiku.
Ombi hilo lilitolewa na diwani wa kata hiyo Mrisho Choka mbele ya Mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete ambaye yuko kwenye ziara kutembelea Jimbo hilo kukagua shughuli za maendeleo.
Choka alisema kuwa kuwa pori hilo limekuwa likitumiwa na majambazi ambao hujificha kisha kutega magogo barabarani na kusababisha ajali kisha kufanya uhalifu kwa kutumia silaha mbalimbali.
“Eneo hili limekuwa hatarishi kwa magari hasa nyakati za usiku ambapo kumekuwa na matukio mengi ya utekwaji wa magari ambayo kabla ya kutekwa husababishiwa ajali kwa kuwekewa magogo hivyo tunauomba uongozi wa gereza kuturuhusu tutumie eneo hilo ili kuzuia vitendo hivyo,” alisema Choka.
Alisema kuwa endapo wananchi watalitumia eneo hilo itasaidia kupunguza vitendo hivyo kwani kwa ambapo kwa sasa majambazi hao wanafanya wanavyotaka kutokana na eneo hilo kuwa pori.
Aidha alisema kuwa wiki iliyopita magari manne yalitekwa na katika kukabiliana na uhalifu katika eneo hilo wamekuwa wakifanya doria na askari polisi lakini hata hivyo majambazi hao wamekuwa wakiwategea na kutekeleza uhalifu.
Kwa upande wake Ridhiwani Kikwete alisema kuwa ombi lao atalipeleka kwenye vyombo husika ili lifanyiwe kazi ili kuondokana na vitendo hivyo ambavyo vimekithiri katika eneo hilo.

Mwisho.