Sunday, October 19, 2014

GOMBO GAMBUSI




 Mtumishi wa Mungu wa kituo cha maombezi cha Gombo Gambusi kilichopo Kibamba kwa Waitara Mwalimu Allister Albano akiwa anahubiri kituoni hapo Jumapili hii. 

 Mtumishi wa Mungu Mwalimu Allister Albano kushoto akiwa na mkewe wakifanya maombi kwa waumini kituoni hapo Jumapili hii

 Mtumishi wa Mungu Mwalimu Allister Albano kushoto akimwombea mgonjwa wakati wa ibada iliyofanyika kituoni hapo Jumapili hii 

 Baadhi ya waumini wakiwa kwenye maombi kwenye ibaada iliyofanyika Jumapili hii 

 Baadhi ya waumini wakiwa wanafanyiwa maombi na mtumishi wa Mungu Mwalimu Allister Albano 

 Mmoja ya waumini akiwa ameanguka chini baada ya kufanyiwa maombi kwenye ibaada ya Jumapili iliyofanyika kituoni hapo 

 Waumini wa kituo hicho wakiwa wanamsikiliza Mwalimu Allister Albano wa kituo hicho hayupo pichani alipokuwa akihubiri Jumapili hii 

 Waumini wakiwa wanaomba wakati wa ibaada hiyo Jumapili hii.

WACHINA WAVUTIWA BAGAMOYO

Na John Gagarini, Bagamoyo
JIMBO la Jilin nchini China limekubali kuwekeza hapa nchini kwenye eneo la Uwekezaji la (EPZ) la Kamal lililopo Kijiji cha Kerege kwa Kiwete wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.
Uwekezaji huo utafanyika baada ya ujio wa baadhi ya viongozi wa Jimbo hilo kutembelea maeneo mbalimbali ya uwekezaji wilayani humo na kuonekana kuvutiwa na sehemu hiyo.
Akizungumza jana mara baada ya kutembelea maeneo kadhaa akiongozana na mkuu wa mkoa wa Pwani Mwantumu Mahiza na sekretarieti ya mkoa wa Pwani na kuvutiwa na eneo hilo la uwekezaji la EPZ, Naibu Gavana wa Jimbo hilo Zhoncheng Sui alisema ameridhika na eneo hilo.
Sui alisema kuwa kutokana na urafiki wa kihistoria uliyopo kati ya Tanzania na China toka enzi za viongozi wa mataifa hayo Mwalimu Julius Nyerere na Mao Tse Sung kumekuwa na ushirikiano ambao ni wa damu hivyo lazima udumishwe kwa ushirikiano wa kimaendeleo.
“Tumeona mambo mengi ambayo tunaweza kushirikiana ambapo moja ni pale kwenye eneo la uwekezaji ambapo tutakuja kuwekeza hapo kwani kuna miuondombinu mizuri ya barabara, maji na umeme pia waiteni na wenzetu waliopo hapa Tanzania ili nao waje wajionee na kuangalia namna wanavyoweka kuwekeza kwenye mkoa huu wa Pwani,” alisema Sui.
Awali akimkaribisha naibu gavana wa Jimbo hilo la Jilin mkuu wa mkoa wa Pwani Mwantumu Mahiza alisema kuwa mkoa wa Pwani una mambo mengi ambayo wawekezaji wanaweza kuwekeza ikiwa ni pamoja na kwenye kilimo, uvuvi, utalii na mifugo.
“Fursa zipo nyingi ndani ya mkoa wetu na hata miundombinu ya barabara, anga, bandari, uememe na reli viko vizuri kwa ajili ya kufanikisha uwekezaji ambao una hitaji uwepo wa mawasiliano mazuri,” alisema Mahiza.
Ujumbe huo ulikuwa na ziara ya siku moja wilayani Bagamoyo kutembelea  maeneo ya uwekezaji kwenye ujenzi wa soko la kimataifa la samaki, eneo itakapojengwa bandari na eneo la uwekezaji la Kamal.

Mwisho.
 Mkuu wa mkoa wa Pwani Mwantumu Mahiza katikati mwenye kilemba akiwa na ugeni toka nchini China wakiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi wa wilaya ya Bagamoyo mara baada ya kumaliza mkutano wa pamoja uliofanyika kwenye hoteli ya Oceanic bay Hotel $ Resort  

 Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mwantumu Mahiza kulia akiteta jambo na kiongozi wa ujumbe  kutoka Jimbo la Jilin nchini China Zhongcheng Sui wali[potembelea wilaya Bagamoyo kuangalia maeneo ya uwekezaji 



 Mkuu wa mkoa katikati na ugeni kutoka nchini China wakiangalia bomba ambalo limetoboka na maji kumwagika, kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Ahmed Kipozi

Monday, October 13, 2014

WAIMBAJI NA KWAYA ZA INJILI ZIJIUNGE NA BASATA

Na John Gagarini, Kibaha

KWAYA na Waimbaji wa nyimbo za Injili nchini wameshauriwa kujisajili Baraza la Sanaa ili watambulike kisheria kwa lengo la kuepuka kudhulumiwa haki za kazi zao.

Hayo yalisemwa mjini Kibaha mwishoni mwa wiki na Naibu Waziri wa Sheria na Katiba Angella Kairuki wakati alipokuwa mgeni rasmi katika hafla ya kuchangia fedha za kununulia vifaa vya mawasiliano na kurekodi albamu ya video ya kwaya ya kanisa la Sabato la Maili Moja Kibaha mkoani Pwani.

Waziri Kairuki alisema kuwa baadhi ya kwenye makanisa ya na waimbaji mbalimbali hawajaona umuhimu wa kujisajili ili ziweze kutambulika na kunufaika kama zilivyo kazi nyingine za sanaa.

“Kwaya na waimbaji wa nyimbo za injili nazo zinawajibu wa kujisajili katika baraza hilo ili ziweze kupata haki zao pamoja fursa mbalimbali pia kukabiliana na baadhi ya watu wanaotumia kazi zao kujinufaisha binafsi huku walengwa wakiwa hawaambulii kitu hivyo sio vyema kukaa bila kujisajili rasmi,” alisema Waziri Kairuki.

Alisema ameona ni vyema akawahimiza kwani  jambo hilo lina manufaa kwa waimbaji na kwaya za makanisa ili waweze kupiga hatua kama ilivyo kwa baadhi ya wasanii wengine wa nyimbo za injili ambao tayari wamepiga hatua.

Alibainisha kuwa muziki unachangia amani,upendo na mshikamano hivyo wajitahidi pia kuimba nyimbo za kuiombea nchi yetu kwa masuala hayo muhimu pamoja na kumtukuza mungu.

“Nawaomba wanakwaya wa nyimbo na waimbaji wa nyimbo za injili kutengeneza albamu za video zenye maadili kwa michezo na mazingira yake pasipo kwenda kinyume na maadili ya kidini na kugeuza injili kuwa biashara, kwani zipo baadhi ya kanda za wasanii wengine ambazo hazionyeshi maadili mazuri,” alisema Waziri Kairuki.

Waziri Kairuki alisema serikali ipo pamoja na wasanii wa aina zote na inatambua kazi za sanaa ,tasnia ya wasanii na ndio maana katika katiba inayopendekezwa walihakikisha wanatambua kazi za wasanii, katika hafla hiyo kulipatikana zaidi ya sh m 22 ambapo ahadi zilizotolewa ni zaidi ya Mil 19.

Mwisho



WLAC YAPONGEZWA KUSAIDIA WANANCHI MASUALA YA SHERIA BURE

Na Mwandishi Wetu, Kibaha
MKUU wa wilaya ya Kibaha mkoani Pwani Halima Kihemba amekipongeza kituo cha Msaada wa Kisheria  kwa Wanawake (WLAC) kwa kujitolea kutoa huduma za kisheria bure kwa wananchi wasio na uwezo wa kumudu gharama za kuwalipa wanasheria.
Aliyasema hayo mjini Kibaha wakati akifunga mafunzo ya wasaidizi wa Kisheria wilayani humo ya siku 25 yaliyoandaliwa na Kituo cha Msaada wa Kisheria kwa Wanawake (WLAC).
Kihemba alisema kuwa kituo hicho kimeonyesha umuhimu wa kutoa msaada wa kisheria ni muhimu kwa watu hususani wanawake na watoto ambao wamekuwa wakipoteza haki zao kutokana na baadhi ya watu kutumia unyonge wao wakutokuwa na sauti ndani ya jamii kuwadhulumu haki zao.
“Huduma ya kisehria ni muhimu ndani ya jamii lakini watu wengi wamekuwa wakishindwa kumudu gharama hizo hivyo kushindwa kupata haki zao hivyo mashirika kama haya ni ya kuigwa,” alisema Kihemba.
Aidha alisema kuwa makundi hayo mawili ndiyo yamekuwa yakidhulumiwa haki zao kwa kiasi kikubwa hivyo mashirika kama WLAC yanayojitolea lazima yaungwe mkono na wadau mbalimbali ikiwemo serikali.
Awali akimkaribisha mkuu wa wilaya mkuu wa idara ya Mafunzo ya WLAC Magdalena Mlolere alisema kuwa lengo la kituo hicho ni kuhakikisha kuwa watu wanapata haki zao ambazo ni za msingi na ziko kikatiba.
Mlolere alisema kuwa lengo la kutoa mafunzo hayo kwa wasaidizi wa kiseheria wa vituo vya KPC na KPP ni ili waweze kusaidia wananchi kutatua migogoro inayojitokeza kabla ya kufika kwenye vyombo vya kisheria ikiwemo mahakama na polisi.
“Mafunzo hayo pia yatasaidia kupunguza kesi zinazopelekwa mahakamani ambazo nyingine zimekuwa zikitumia muda mrefu kuamuliwa na kuwafanya wahusika kutumia muda mwingi kwenda mahakamani huku wakishindwa kufanya shughuli zao za maendeleo,” alisema Mlolere.
Akisoma hotuba mbele ya mgeni rasmi moja ya wahitimu wa mafunzo hayo kwa niaba ya wahitimu John Gagarini alisema kuwa changamoto zinavyovikabli vituo hivyo ni baadhi ya wanajamii kutokuwa wawazi katika kuyapeleka mashauri hayo kwenye vituo hivyo pia ni ukosefu wa usafiri wa kuweza kufika kwenye maeneo hasa yale ya vijijini, jumla ya wahitimu 32 walihitimu mafunzo hayo na kukabidhiwa vyeti na mkuu huyo wa wilaya ya Kibaha Halima Kihemba.
Mwisho.
  


WAZIRI KAIRUKI ALITAKA KANISA KUOMBEA AMANI YA NCHI


Na John Gagarini, Kibaha

NAIBU Waziri wa Sheria na Katiba Angella Kairuki amewataka waumini wa Kanisa la Sabato Maili Moja Kibaha mkoani Pwani na wananchi kuendelea kuiombea nchi isiingie kwenye machafuko .

Waziri Kairuki aliyasema hayo mjini Kibaha katika kanisa hilo alipokuwa mgeni rasmi kwenye hafla ya kuchangia fedha za kununulia vifaa vya mawasiliano na kurekodia vya kwaya ya kanisa hilo na kusema kuwa wasikubali kutumiwa na baadhi ya watu kwa mambo ambayo ni kinyume na sheria za nchi.

Alisema nchi imekuwa na amani kwa miaka mingi sasa ikiwa ni mfano wa kuigwa na nchi nyingine hivyo haina budi kila mmoja akasali kuliombea taifa ambalo pia likielekea kwenye chaguzi mbalimbali.

“Msiwakubali watu ambao wamekuwa wakitumia wananchi ili kuvuruga amani ya nchi na wamekuwa wakitaka kuungwa mkono lakini wanaokuja kupata matatizo ni wananchi na siyo wao hivyo msikubali kufuata mkumbo,” alisema Waziri Kairuki.
Aidha Waziri Kairuki alisema hakuna haja ya kuendelezwa kwa mijadala ya katiba inayopendekezwa ama kuibua hoja zisizo na tija kwa maslahi ya taifa kwani muda wake umekamilika na hatua inayosubiriwa ni tamko kutoka kwa Mh Rais litakaloeleza wakati wa kupiga kura ya maoni kwa wananchi.

Kwa upande wake Mchungaji wa Kanisa la Sabato Maili Moja Eliasi Timasi alimshukuru Waziri Kairuki kwa nasaha zake na kusema wataendelea kuhimiza amani kwa kufanya mawasiliano ya karibu na serikali pamoja na kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazowakabili waumini wa kanisa hilo.

Katika shughuli hiyo ya kuchangia vifaa vya mawasiliano ya kanisa na kurekodia  kwaya kulipatikana zaidi ya sh m 22 ambapo ahadi zilizotolewa ni zaidi ya m 19.

Mwisho.

Thursday, October 2, 2014

WANAFUNZI WAASWA KUHUSU TEKNOLOJIA

Na John Gagarini, Kibaha
WAZAZI wilayani Kibaha mkoani Pwani wametakiwa kuwalinda watoto wao waepukane na matumizi mabaya ya Teknolojia ya mawasiliano ili wasifuate tamaduni mbaya za nchi za Magharibi ambazo zimewaharibu vijana Tanzania.
Hayo yalisemwa mjini Kibaha na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha,  Jenifa Omollo wakati wa mahafali ya tisa ya darasa la saba ya shule ya awali na Msingi ya Kibaha Independent (KIPS).
Omollo alisema kuwa teknolojia ya mawasiliano ni nzuri endapo inatumiwa vizuri lakini ina athari endapo itatumiwa vibaya hasa kwa vijana kuiga tamaduni za nje zinazohamasisha vitendo viovu.
“Tuko kwenye utandawazi ambao unatumia teknolojia ya mawasiliano na kuifanya dunia kuwa Kijiji na kumekuwa na muingiliano mkubwa wa tamaduni ambazo nyingine ni mbaya zinazokinzana na maadili ya kitanzania ikiwa ni pamoja na mavazi, ngono, matumizi ya dawa za kulevya na matumizi mabaya ya mitandao ya kuangalia picha za ngono,” alisema Omollo.
Alisema kuwa kundi la vijana limeathiriwa kwa kiasi kikubwa na tamaduni hizo mbaya ambapo vijana hao wanafikiri ndiyo kwenda na wakati kumbe wanajiharibia maisha yao ya baadaye.
“Kwa sasa kuna matumizi mabaya ya teknolojia kupitia njia za simu, kompyuta na televisheni hivyo lazima wazazi wawaelekeze matumizi sahihi ya vifaa hivyo ambavyo endapo vitatumiwa vizuri vinaweza kuwa na manufaa mazuri kwa watumiaji,” alisema Omollo.
Awali akimkaribisha mgeni rasmi mkurugenzi wa shule hiyo Said Mfinanga alisema kuwa shule yao moja ya vitu inavyozingatia ni maadili mazuri ya Kitanzania ili wanafunzi wanapotoka hapo wawe na tabia njema.
Mfinanga alisema kuwa licha ya shule kufundisha masomo ya mawasiliano ya Kompyuta lakini wanazingatia maadili ili kuepuka na matumizi mabaya ya Teknolojia na kuzingatia kutoa elimu bora.
Shule hiyo ni ya kutwa na bweni ilianzishwa mwaka 2002 na ina jumla ya wanafunzi 480 na ni miongoni mwa shule zinazofanya vizuri kwenye wilaya hiyo pamoja na mkoa ambapo mwaka huu jumla ya wahitimu 39 walipewa vyeti vya kuhitimu darasa la saba.

Mwisho.