Thursday, July 27, 2017

AKIMAMA WAFANYABIASHARA WALALAMIKA KUNYANYASWA


                                    Na John Gagarini, Kibaha

MTAA wa Maili Moja umesema utawafuatialia na kuwachukulia hatua mgambo ambao waliwadhalilisha akina mama wafanyabiashara ndogo ndogo kwa kuwadai rushwa ya ngono kwa madai kufanyabiashara kwenye eneo ambalo haliruhusiwi.

Akizungumza kwenye mkutano wa mtaa mwenyekiti wa Mtaa wa maili Moja Athuma Mkongota alisema kuwa baadhi ya akinamama walilalamika ofisini kwake kuwa walitakiwa watoe penzi ili wasitozwe faini kwa kudaiwa kufanya biashara kwenye maeneo yaliyokatazwa.

Mkongota alisema kuwa jambo la kushangaza akinamama hao waliokuwa wakifanyabiashara nje ya eneo la Hifadhi ya Barabara ambapo waliondolewa kufuatia kubomolewa soko la zamani la Maili Moja.

“Hawa mgambo walifanya makosa kuwanyanyasa akinamama hawa hata kama walikuwa na makosa taratibu za wanaokiuka sheria sizipo kwanini wadai mapenzi pia walikuwa hawafanyibiashara kwenye eneo lililokatazwa hivyo tutawatafuta na kuwapeleka kwenye vyombo vya sheria ili wachukuliwe hatua,” alisema Mkongota.

Mkongota alisema kuwa baada ya wakinamama hao kuondolewa eneo lililokatazwa la hifadhi ya barabara ambalo liko jirani na stendi walienda kwenye barabara za mitaa na kuendelea kufanyabiashara lakini mgambo hao waliwafuata na kuwakamata huku wakimwaga vyakula na matunda waliyokuwa wakiyauza.

“Baadhi ya akinamama walifika ofisini na kudai kuwa baadhia ya mgambo walikuwa wakiwataka kimapenzi ili wasiwapige faini wakidai kuwa wanachafua mazingira jambo hili halikubaliki kwani tutawatafuta na wakibainika watepelekwa sehemu husika kwnai kuna baadhi wanajifanya mabwana afya,” alisema Mkongota.

Kwa upande wake Mwanahamisi Shomary ambaye ni muuzaji wa samaki alisema kuwa tangu waondolewe kwenye eneo la stendi na kuhamia kwenye barabara za mitaa wamekuwa wakisumbuliwa na mgambo hao.

Shomary alisema kuwa mgambo hao wamekuwa kero kubwa kwani wanatunyanyasa sana huku wakichukua bidhaa zetu na kuziharibu ambapo inabidi tujitafutie ili tuweze kurejesha mikopo tuliyokopa.


Mwisho.   

WAASWA KUTUMIA VITUO VYA MAFUNZO

                                      Na John Gagarini, Kibaha

WALIMU wakuu wa shule za msingi, sekondari na vyuo nchini wameshauriwa kuwapeleka wanafunzi wao kwenye vituo vya mafunzo badala ya kuwapeleka kwenye sehemu za starehe.

Ushauri huo umetolewa na makamu mwenyekiti wa wataalamu wasaidizi wa mifugo nchini Tavepa Ephrahim Masawe alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.

Masawe ambaye pia ni mkurugenzi wa shamba darasa Kibaha akizungumzia juu ya kilimo cha kisasa alisema kuwa ziara za safari ni vema zikawa za kujifunza kuliko kujifurahisha.

“Kwenye mafunzo hujifunza mambo mengi kuliko kwenda kwenye sehemu ambazao hazina faida kwani ujuzi unaweza kumsaidia mtu kuliko kufanya vitu visivyo na faida,” alisema Masawe.

Naye moja ya wanafunzi kwenye shamba darasa mkazi wa Mbweni Jijini Dar es Salaam Hilda Ngowi akiezea kilicho msukuma kwenda hapo kujifunza ni kutaka kupata ujuzi wa ufugaji wa kuku.

Ngowi alisema ushauri juu ya shule na vyuo kuwapeleka wanafunzi kwenye sehemu za mafunzo kama hayo alisema kuwa sehemu za mafunzo ni muhimu kwa vijana.

Mwisho.

DEREVA AFA AJALINI

                                 Na John Gagarini, Kibaha

DEREVA wa gari la mizigo ambaye jina lake halikuweza kufahamika mara moja amekufa baada ya gari alilokuwa akiliendesha kugongwa na gari lingine kwenye ajali iliyosababisha magari matatu kugongana.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa mjini Kibaha kwa vyombo vya habari na kamanda wa polisi mkoani Pwani Jonathan Shana ilisema kuwa katika tukio hilo mtu mmoja alijeruhiwa.

Kamanda Shana alisema kuwa tukio hilo lilitokea Julai 20 majira ya saa 4:20 usiku barabara kuu ya Dar es Salaam Morogoro eneo la Picha ya Ndege wilayani Kibaha.

Shana alisema kuwa gari aina ya Scania lenye namba za usajili T 774 BBU likiendeshwa na dereva asiyefahamika liligonga gari lililokuwa likiendeshwa na dereva asiyefahamika lenye namba za usajili T 678 BRD lenye tela namba T 293 BVA na Scania T 188 AVN likiendeshwa na Hashimu Mhina (36) wa Dar es Salaam.

“Chanzo cha ajali hii ni dereva wa gari la kwanza kuyapita magari mengine bila ya kuchukua tahadhari ambapo alikimbia mara baada ya ajali hiyo na tunamtafuta tumempa siku tatu ajitokeze na asipojitokeza tutamtafuta ili afikishwe kwenye vyombo vya sheria,” alisema Shana

Mwisho

Na John Gagarini, Kibaha

JESHI la Polisi mkoani Pwani linawashikilia wahamiaji 44 kutoka nchi ya Ethiopia kwa tuhuma za kuingia nchini bila ya kibali.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Kibaha kamanda wa Polisi mkoani Pwani Jonathan Shana alisema kuwa wahamiaji hao haramu walikamatiwa wilayani Bagamoyo.

Kamanda Shana alisema kuwa wahamiaji hao haramu walikamatwa eneo la Razaba kata ya Makurunge Tarafa ya Mwambao wilayani humo wakiwa wametelekezwa kwenye ufukwe wa Bahari ya Hindi.

Alisema kuwa  kufuati tukio hilo jeshi lake linaendelea na uchunguzi kujua watu waliohusika na tukio la kuwasafirisha wahamiaji hao haramu kisha kuwatelekeza.

“Tunafuatilia kujua vitu vingi ikiwa ni pamoja na wanaowafadhili wahamiaji hao haramu kwani kumekuwa na baadhi ya watu wanaowasafirisha wahamiaji hao ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yao,” alisema Shana.


Mwisho

SAMATTA ASAIDIA JEZI CHAMA CHA SOKA KIBITI


                                     Na John Gagarini, Kibaha

CHAMA Cha Soka wilaya ya Kibiti (KFA) mkoa wa Pwani kimemshukuru mwanasoka anayecheza soka la kulipwa kwenye timu ya KRC Genk ya Ubelgiji Mbwana Samatta kwa kuwapatia jozi za jezi kwa ajili ya washindi wa ligi daraja la nne.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi katibu wa chama hicho Rashid Mkinga alisema kuwa wanashukuru msaada huo utakaozisaidia timu zitakazoshinda na kuwakilisha wilaya hiyo kwenye mashindano ya mkoa.

Mkinga alisema kuwa waliandika barua kwa Samata kwa ajili ya kuomba vifaa mbalimbali vya michezo ambapo aliwajibu na kusema kuwa atawapatia.

“Samatta kwa kupitia mwakilishi wake Said Ngulupi alitupatia jozi ya seti tatu ambazo tutawakabidhi washindi watatu wa juu ambao ni wawakilishi wa wilaya yetu,” alisema Mkinga.

Alisema kuwa hawana cha kusema zaidi ya kushukuru kwa msaada huo mkubwa aliowapatia licha ya yeye kuwa mbali lakini anathamini vijana wenzake ambao wanacheza soka hapa nchini.

“Tunamshukuru Samatta kwa mchango wake kwani awali tulikuwa hatuna zawadi za kuwapa washindi zaidi ya kombe kwa ajili ya mshindi wa kwanza kwani ametukomboa kwa kutupa msaada huo,” alisema Mkinga.

Aidha alisema kuwa mpira unachezwa kama kawaida na kuna amani kubwa siyo kama watu wanavyofikiria kwani ulinzi uko wa kutosha na hadi sasa hakuna tukio lolote la kutishia lililotokea.

“Kupitia michezo amani imetawala na hakuna vurugu zozote au tishio lolote la kutishia amani hivyo watu wasiwe na wasiwasi kwenye wilaya yetu ambayo ilikumbwa na mauaji na kuwafanya watu kuwa na hofu,” alisema Mkinga.

Alibainisha kuwa ligi ya Kibiti ndiyo yenye timu nyingi ndani ya mkoa wa Pwani ambapo kwenye ligi daraja la nne jumla ya timu 19 zinachuana na timu zilizosajiliwa ni 31 na bado kuna zingine zinahitaji usajili.


Mwisho.  

MJI KIBAHA KUJENGA STENDI YA KISASA KWA MABILIONI

Na John Gagarini, Kibaha

HATIMAYE Halmashauri ya Mji Kibaha mkoani Pwani imeanza mradi wa ujenzi wa stendi ya kisasa wenye thamani ya shilingi billion 3.4.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Kibaha ofisa habari wa Halmashauri hiyo Innocent Byarugaba amesema kuwa stendi hiyo itaondoa tatizo la mji huo kutokuwa na stendi ya uhakika kwa kipindi cha takribani miaka 40.

Byarugaba alisema kuwa stendi ambayo inatumika kwa sasa ni ndogo na imejengwa kwenye hifadhi ya barabara na ambapo iko ndani ya mita 60 ikitakiwa kuondolewa na ina hudumia mabasi ya mikoa 24.

“Stendi mpya mara itakapokamilika inatarajiwa kuwa na uwezo wa kuhudumia mabasi 60 kwa wakati mmoja na itajengwa kipindi cha miezi sita na kukamilika mwishoni mwa mwaka huu au Januari mwakani,” alisema Byarugaba.

Alisema kuwa fedha zinazotumika kwenye ujenzi huo ni ufadhili kutoka benki ya dunia kupitia benki kuu ya Tanzania kwenye mradi wa uendelezaji wa Miji (ULGSP) unaoendeshwa kwenye miji 18 hapa nchini.

“Stendi itakuwa na miundombinu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kituo cha polisi, ofisi za mabasi, sehemu ya texi, Bajaji, pikipiki, huduma ya vyoo, vibanda vya kupumzikia abiria, Atm, kituo cha mafuta,gereji, hoteli na kizimba cha kuhifadhia takataka na huduma nyingine muhimu,” alisema Byarugaba.

Aliwataka watu wenye viwanja vinavyozunguka stendi hiyo kujenga ambapo ramani iliyopitishwa ni kuanzia ghorofa moja na kuendelea pamoja na wale walioko kwenye eneo la kitovu cha mji kufanya ujenzi kama sheria zinavyowataka.

Aidha alisema kuwa ujenzi huo unafanywa na kampuni ya Group Six International Ltd ambayo ilijenga stendi ya kisasa ya Msamvu mkoani Morogoro chini ya wataalamu washauri Ace Consult, Lupta Consult na Mhandisi.


Mwisho.

WATAKIWA KUEPUKA NYAMA ZA MITAANI

Na John Gagarini, Kibaha

WANANCHI wa kata ya Picha ya Ndege wilayani Kibaha mkoani Pwani wametakiwa kuacha kununua nyama zinazouzwa mitaani kwa bei nafuu kwani ni hatari kwa maisha yao.

Hayo yalisemwa na diwani wa kata hiyo Robert Machumbe alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kufuatia kuenea kwa taarifa kuwa kuna watu wanauza nyama mitaani zikiwa zimewekwa kwenye ndoo.

Machumbe alisema kuwa watu hao wamekuwa wakichukua ngombe ambao wamekufa maeneo mbalimbali kisha kuwauzia wanachi nyama hiyo kwa baei nafuu ya shilingi 2,000.

“Wananchi nawaomba mjihadhari na nyama hizi zinazouzwa mitaani ni hatari kwa afya zenu kwani hamjui nyama hizo zinatoka wapi kwani hazijapimwa na daktari hali ambayo ni hatari,” alisema Machumbe.

Alisema kuwa wananchi wasipende kununua nyama hizo bali wanunue sehemu maalumu ambako ni kwenye mabucha ya kuuzia nyama ili wale nyama ambayo imepimwa na ni salama kwa afya zao.

Kwa upande wake ofisa mifugo wa kata ya Picha ya Ndege Mlaki alisema kuwa alipata taarifa wiki iliyopita kuwa kuna ngombe walikufa kwa moja ya wafugaji wa Lulanzi na watu hao waliichukua nyama hiyo na kuiuza mtaani.

Mlaki alisema kuwa kuna athari ningi zinazotokana na watu kula nyama ambazo hazijapimwa kwani wanaweza kuambukizwa magonjwa mbalimbali kama vile tb, tumbo, kuharisha na magonjwa mengine.   

Mwisho.

AOMBA WALIMU WA SEKONDARI HURIA WAPEWE MOTISHA

Na John Gagarini, Kibaha

SERIKALI imeombwa kuwalipa walimu wanaofundisha vituo vya shule huria ambazo ziko chini ya Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima ili kuwapa motisha walimu hao.

Hayo yalisemwa na meneja wa shule ya Pangani Remedial Open School iliyopo wilayani Kibaha Ally Mohamed na kusema kuwa kuwalipa walimu hao itakuwa moja ya motisha kuwafanya wafundishe kwa moyo.

Mohamed alisema kuwa shule hizo zimekuwa mkombozi kwa wanafunzi ambao wamekosa nafasi za kwenda shule za sekondari na watu wazima waliokosa nafasi hiyo.

“Shule hizi ambazo zamani zilikuwa ni kwa ajili ya watu wazima kwa sasa zimeboreshwa na zinatoa elimu ya sekondari kama kawaida na wanapofaulu mitihani ya kidato cha nne wanakwenda kidtao cha tano kama wale walio kwenye mfumo rasmi hivyo kuna haja ya walimu wake kulipwa kama walimu wenzao wa shule za serikali,” alisema Mohamed.

Alisema kuwa walimu hao kwa sasa wanalipwa na shule hizo lakini kwa kiasi kikubwa wamekuwa wakijitolea kwani uwezo wa kuwalipa mishahara hawana ambapo Taasisi hiyo imekuwa ikisimamia mitihani ya Kujipima huku ile ya kidato cha pili na ile ya kidato cha nne ikisimamiwa na Baraza la Mitihani la Taifa (NACTE).

“Shule hizi kwa sasa zimekuwa mkombozi kwa wanafunzi hao ambao zamani walikuwa hawana pa kwenda hivyo tunaomba serikali kuliangalia suala la kuwalipa walimu hao ili kuwapa hamasa ya kufundisha ili kuongeza ufaulu kwa wanafunzi wa shule hizo,” alisema Mohamed.

Alisema kuwa mfumo huo uliboreshwa mwaka 2014 ambapo ulisajili vituo hivyo ambavyo vinachukua wanafunzi ambao walishindwa kuendelea na masomo kama vile ukosefu wa ada, mimba, mazingira magumu, yatima na watu wazima waweze kujiendeleza.

Aidha alisema kuwa kwa sasa zinachukua wanafunzi wenye umri kati ya miaka 12 hadi 24 ambao wanasoma kwa miaka minne huku wale wenye kuanzia miaka 25 husoma kwa miaka miwili,shule hiyo ilianza mwaka 1997 na ina wanafunzi 100.

Mwisho.


GARI LATUMBUKIA MTO WAMI WAWILI WAFA

                                   
                                         Na John Gagarini,Kibaha

MADEREVA wawili wamekufa baada ya gari walilopanda kugonga kingo za daraja la mto wa wami na kuangukia mtoni

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na kamanda wa polisi mkoa wa Pwani Jonathan Shana amesema kuwa gari lililopata ajali ni mali ya kampuni ya Usangu Logistics.

Shana amesema kuwa ajali hiyo ilitokea majira ya saa saba usiku na kulihusisha gari lenye usajili namba T 857 ARP aina ya Scania likiendeshwa na Yahaya Karimu miaka kati ya (30)  na (35) akiwa na dereva mwenzake ambaye jina lake halikuweza kufahamika mara moja likitokea Dar es Salaam kwenda Arusha.

Amesema kuwa chanzo cha ajali hiyo ni breki za gari hilo kukatika na kugonga kingo za daraja hilo kisha kuanguka mtoni 

Na John Gagarini, Kibaha

MTU mmoja aliyetambulika kwa jina la Mwesigwa Mberwa (23) amekutwa amekufa kwenye nyumba ya kulala wageni ya Msukuma iliyopo Mlandizi wilayani Kibaha.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari mjini Kibaha na kamanda wa Polisi mkoani Pwani Jonathan Shana zimesema kuwa marehemu alikuwa amelala chumba namba 38.

Shana amesema kuwa tukio hilo lilitokea Julai 22 majira ya saa 12 jioni eneo la kitongoji cha Usalama wilaya ya Kipolisi Mlandizi ambapo marehemu alipanga kwenye nyumba hiyo tangu Julai 19.

Amebainisha kuwa muhudumu Kulekwa Kulwa ndiye aliyegundua kufa kwa marehemu baada ya kutia mashaka kutokana na kutomwona kutoka nje mteja wake tangu alipoingia na kwenda kutoa taarifa polisi.

Amesema kuwa polisi walipofika kwenye chumba hicho iliwabidi kuvunja mlango na kuukuta mwili wa marehemu ukiwa hauna jeraha lolote mwilini mwake na kupelekwa hospitali Teule ya Rufaa ya mkoa ya Tumbi na ulifanyiwa uchunguzi na utakabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya mazishi.

Mwisho.

Na John Gagarini, Kibaha

ABIRIA waliokuwa wakisafiri na basi la kampuni ya Tashirifu waliokuwa wakisafiri kutokea Dar es Salaam kwenda mkoani Tanga wamenusurika kifo baada ya basi hilo kuwaka moto.

Kwa mujibu wa taarifa ya kamanda wa polisi mkoani Pwani kwa vyombo vya habari Jonathan Shana imesema kuwa basi hilo liliteketea lote na moto huo haukuleta madhara yoyote kwa binadamu na kusababisha hasara ikiwemo mizigo ya abiria.

Kamanda Shana amesema kuwa ajali hiyo ilitokea Julai 22 majira ya usiku eneo la Kwa Zoka kata ya Vigwaza wilaya ya Kipolisi Chalinze barabara kuu ya Dar es Salaam Morogoro.

Amesema kuwa basi hilo lenye namaba za usajili T 681 DFX aina ya Yutong lilikuwa likiendeshwa na dereva aitwaye Salum Issa (42) liliwaka moto hata hivyo chanzo cha moto huo hakikuweza kufahamika mara moja na polisi wanaendelea na uchunguzi kujua chanzo cha moto huo.

Mwisho.

Na John Gagarini, Kibaha

JESHI la Polisi mkoani Pwani linawashikilia watu sita kwa tuhuma za kuchoma moto nyumba za watu watatu na kusababisha hasara ikiwa ni pamoja na pikipiki mbili zenye thamani ya shilingi milioni 3.8

Kamanda wa polisi mkoani humo Jonathan Shana amesema kuwa mbali ya kuchoma nyumba hizo pia waliingia kwenye mazizi na kuchinja ngombe ambao idadi yao haijajulika kisha kuondoka na nyama na kubakiza utumbo.

Shana amesema kuwa tukio hilo lilitokea Kijiji cha Vikumburu kata ya Vikumburu Tarafa ya Chole wilaya ya Kisarawe ambapo hata hivyo haikuweza kufahamika chanzo cha uhabifu huo wa mali ambao thamani yake haijajulikana.

Amewataja watu waliochomewa nyumba zao kuwa ni Joseph Simboyi (55), Rebeka Yona (23) na Selina Simon (28).

Aidha amewataja watuhumiwa wa tukio hilo kuwa ni Abdala Shomary (53), Omary Athuman (42) Seifu Shomary (38), Uzalimata Selasela (36) Salum Shomary (40) na Jumanne Omary (49) wote wakazi wa Vikumburu.


Mwisho. 

AUWAWA NA WANANCHI HASIRA KWA TUHUMA WIZI WA BODABODA

                                   
                                      Na John Gagarini,Kibaha

MTU mmoja anayedhaniwa kuwa ni jambazi mmoja ameuwawa na wananchi wenye hasira kali kwa kupigwa kisha kuchomwa moto kwa tuhuma za kupora pikipiki.

Kamanda wa Polisi mkoani Pwani Jonathan Shana alisema kuwa kuwa tukio hilo lilitokea Julai 23 majira ya saa 1:45 usiku kitongoji cha Amani kata ya Kerege tarafa ya Yombo wilaya ya Bagamoyo.

Kamanda Shana alisema kuwa marehemu akiwa na wenzake watatu wakiwa na silaha inayodhaniwa kuwa ni bastola walimvamia mwendesha pikpiki aitwaye Mbaraka Joel (25) mkazi wa Amani walimpora pikipiki yake yenye namba za usajili T 852 BRA aina ya Sanlg.

“Watu hyao kabla ya kufanya uporaji walimsimamisha wakijifanya kuwa ni abiria lakini ghafla walimbadilikia kwa kufayatua risasi mbili hewani na kumtaka awape pikipiki ambayo aliiachia na kutoweka nayo kusikojulikana,” alisema Shana.

Alisema baada ya taarifa kulifikia jeshi la polisi wilaya ya Bagamoyo waliendesha msako mkali kwa kushirikiana na wananchi kupitia vikundi vyao vya ulinzi shirikishi kwenye maeneo mbalimbali likiwemo eneo la Mtambani.

“Wananchi hao waliweza kuwakurupusha watu hao wakiwa wanapanga mipango ya kwenda kufanya uhalifu sehemu nyingine na kutokana na idadi ya wananchi kuwa kubwa watu hao walikimbia na kutelekeza pikipiki mbili moja walioipora kwa Joel na nyingine yenye namba za usajili T MC 972 AJM aina ya Boxer,” alisema Shana.

Aidha alisema kuwa wananchi hao waliendelea kuwakimbiza na kufanikiwa kumkamata marehemu ambapo walimpiga kwa mawe na marungu kisha kumchoma moto na kupoteza maisha papo hapo.

“Wananchi hawapaswi kujichukulia sheria mikononi kwa kuwaua wahalifu wanapaswa kuwakabidhi polisi kwa ajili ya hatua za kisheria pia wataweza kubaini mtandao wa wizi kuliko kuwaua,” alisema Shana.

Mwisho.


MWANAMKE AUWAWA KINYAMA

                                      
                                         Na John Gagarini, Kibaha

MWANAMKE mmoja ambaye ni mfanyabiashara Mariamu Omary (31) mkazi wa Mtaa wa Muharakani wilayani Kibaha mkoani Pwani ameuwawa kwa kupigwa na kitu kizito kichwani.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa kwa vyombo vya habari mjini Kibaha na Blasius Chatanda kwa niaba ya kamanda wa polisi mkoani Pwani alisema kuwa marehemu aliuwawa na watu wasiofahamika.

Kamanda Chatanda alisema kuwa tukio hilo lilitokea eneo la Kwa Mathias majira ya saa 7 usiku umbali wa mita 40 toka kwenye nyumba aliyokuwa akiishi.

“Marehemu alikutwa asubuhi huku akiwa amevuja damu nyingi sehemu za usoni na kichwani na alikutwa na jeraha kubwa kichwani upande wa kushoto,” alisema Chatanda.

Kwa upande wake mwenyekiti wa mtaa wa Muharakani Hamis Mwarizo alisema kuwa marehemu alipigiwa simu usiku na mtu ambaye jina lake linaonekana kwenye simu ya marehemu.

Mwarizo alisema kuwa waliingia kwenye chumba cha marehemu na kuzikuta simu zake mbili na moja inaonyesha ilipigwa usiku huo na inaonekana baada ya kupigiwa ndipo alipotoka ndipo alipokutwa na umauti.

Naye mama mwenyenyumba Miriamu John alisema kuwa marehemu alikuwa ni mgeni kwenye nyumba yake akiwa na miezi akiwa na miezi miwili tu na siku ya tukio hawakuweza kusikia kitu chochote.

Mwisho.


MBUNGE ATOA MAGARI MAWILI YA KUBEBA WAGONJWA

Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini Hamoud Jumaa kulia akimkabidhi kaimu mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Kibaha Beda Mmbaga funguo za magari mawili ya kubebea wagonjwa na moja liliotolewa na Rais Dk John Magufuli kwa vituo vya afya vya Halmashauri hiyokulia ni mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Mansour Kisebengo.
 
Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Ummy Mwalimu akiwasha gari lililotolewa na Rais Dk John Magufuli kwa ajili ya kituo cha Afya cha Mlandizi wilayani Kibaha mkoani Pwani wanaoshuhudia ni Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini Hamoud Jumaa kaimu mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Kibaha na mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya Mansour Kisebengo.
Vitanda vitatu vya kuzalishia wanawake wajawazito vilivyotolewa na Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini Hamoud Jumaa kwa ajili ya vituo vya afya vya Jimbo hilo. 

POLISI PWANI WAKAMATA VIFAA VYA UVUVI HARAMU




                          Na John Gagarini, Kibaha

JESHI la Polisi mkoani Pwani linawashikilia Makamba Sixbert (32) na Doto Mwinyi (45) wakazi wa Mlingotini wilayani Bagamoyo kwa tuhuma za kukutwa na vifaa vya uvuvi haramu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari mjini Kibaha na kamanda wa Polisi mkoani Pwani Jonathan Shana alisema kuwa watu hao walikamatwa kwenye msako.

Shana alisema kuwa mtuhumiwa Sixbert  na Mwinyi walikamatwa Julai 25 majira ya saa 8 usiku maeneo ya Mlingotini kata ya Zinga baada ya msako maalumu wa makosa mbalimbali ukihusisha askari wa Jeshi la polisi wilaya ya Bagamoyo, Polisi Makao makuu, Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) na maofisa uvuvi na mifugo wa wilaya hiyo.

“Mtuhumiwa huyo wa kwanza alikutwa na Scoopy Net moja, vioo vya kuogelea vitatu, mitarimbo mitatu, bunduki moja ya kuulia samaki, mikuki ya kuulia samaki mitatu na viatu vya kuogelea (Slipers) pea tatu huku mtuhumiwa wa pili akishikwa na Cylinder Gas walivyokuwa wakivitumia kwenye uvuvi haramu,” alisema Shana.

Kwenye tukio lingine madereva wawili wa pikpiki Juma Ally (37) na Mduga Agustino (25) kwa tuhuma za kupatikana na mitambo mitano ya kutengenezea pombe ya Moshi maarufu kama Gongo.

Kamanda Shana alisema kuwa tukio hilo limetokea Julai 25  majira ya saa tano asubuhi maeneo ya Lugoba kata ya Lugoba wilaya ya Kipolisi Chalinze wilayani Bagamoyo.

“Madereva hao wa pikipiki pia walikutwa na pombe ya Moshi lita 40 na lita 60 za Molasesi wakiwa wamezipakiza kwenye pikipiki yenye namba za usajili T 399 BHS aina ya Sanlg,” alisema Shana.

Aidha walifanikiwa kuwakamata Ahmada Hassan (45) mkazi wa Gogoni na wenzake watano kwa tuhuma za wizi wakiwa na Sabufa aina ya Kodec inayodhaniwa kuwa ni ya wizi.

Shana alisema watu hao walikamatwa maeneo ya Dunda kata ya Dunda Tarafa ya Mwambao wakituhumiwa kujihusisha na matukio ya uhalifu ikiwa ni pamoja na uporaji nyakati za usiku kwenye maeneo mbalimbali wilayani

“Misako wanayoifanya ni endelevu na askari shupavu wametawanywa kila kona kuhakikisha hali ya amani inakuwepo kwenye makazi ya wananchi na sehemu za biashara,” alisema Shana.

Aliwataka watu wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu kuacha mara moja kwa kutafuta shughuli nyingine za kufanya za kuwaingizia kipato halali kwani hawatasita kuwachukulia hatua kali za kisheria.

Mwisho