Thursday, July 31, 2014

KAMATI ZA MADIWANI SARAKASI TUPU NA DIWANI CHADEMA AONDOLEWA KIKAONI

 Baadhi ya madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha mkoani Pwani wakiwa kwenye kikao cha baraza hilo kilichofanyika leo mjini Kibaha
 Na John Gagarini, Kibaha
ZOEZI la kuchagua kamati mbalimbali za baraza la madiwani wa
halmashauri ya Mji wa Kibaha wilayani humo mkoani Pwani limekumbwa na
mtafaruku baada ya baadhi ya madiwani kupinga taratibu za kuwachagua
viongozi na wajumbe wa kamati hizo.
Mtafaruku huo ulitokea baada ya baadhi ya madiwani kulalamika kuwa
wengi wao walipewa kamati nzuri kwa upendeleo na kuwaweka madiwani
wengine kwenye kamati ambazo si nzuri.
Sakata hilo lilitokea jana wakati wa kikao cha baraza la madiwani wa
Halmashauri ya Mji huo lililofanyika mjini Kibaha ambapo madiwani hao
walidai kulikuwa na upendeleo wakati wa kuchagua wajumbe na wenyeviti
wa kamati hizo.
Walisema kuwa uchaguzi huo uliambatana na upendeleo mkubwa ambapo
baadhi ya madiwani wamekuwa wakichaguliwa kwenye moja hasa ile ya
Mipango Miji na Mazingira ambapo wako kwenye kamati hiyo kwa vipindi
vinne mfululizo ambapo wao walitaka wabadilishwe na kuwekwa kwenye
kamati zingine.
“Baadhi ya madiwani wamechaguliwa kutokana na urafiki baadhi
tunateuliwa kwenye kamati ambazo si nzuri inasikitisha sana lazima
kuwe na mabadiliko kama vipi sisi wengine tutajitoa kwenye kamati na
kubaki na udiwani pekee,” walisema madiwani hao.
Hata hivyo hali ilikuwa mbaya zaidi ambapo baadhi walidai kuwa wengine
walichaguliwa kwenye kamati hiyo ya mipango miji kama kulipa fadhila
baada ya kumpa mmoja wa viongozi kwenye uchaguzi wa chama.
“Watu walihongwa fedha ili wamchague mtu ushahidi upo sisi hatukubali
tunaona kuwa baada ya uchaguzi ule leo jana wanalipana fedhila
hatutaweza kufanikiwa tunachotakiwa ni kuwahudumia wananchi,” walisema
madiwani hao.
Kwa upande wake mwenyekiti wa halmashauri Addhu Mkomambo alisema kuwa
uchaguzi huo haukuwa na upendeleo na kama kuna tatizo wanapaswa
kupeleka ofisini kwake na si kuunda vikundi.
Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Abdala Mdimu alisema kuwa
amesikitishwa na madiwani hao kufikia hatua ya kusema mambo ambayo
hayakupaswa kusemwa hapo badala yake yangepelekwa kwenye chama kwa
hataua.
Mdimu alisema kuwa atakaa na madiwani hao ili kuzungumzia masuala hayo
ambayo yalionekana kumsononesha na kusema kuwa hali hiyo imemsikitisha
sana.
Mwisho.

 Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha Addhu Mkomambo kulia akihutubia kwenye kikao hicho kushoto ni mkurugenzi wa halmashuri hiyo Jenifa Omolo
Na John Gagarini, Kibaha
DIWANI wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Kata ya  Tumbi
Mbena  Makala jana aliondolewa kwenye kikao cha madiwani wa baraza la
madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha wilayani Kibaha mkoani Pwani
kutokana na utovu wa nidhamu.
Kikao hicho cha kawaida cha robo tatu ya mwaka ambacho kilifanyika
jana ilimbidi mwenyekiti wa Halmashauri Addhu Mkomambo kumtoa nje ya
ukumbi baada ya kumtaka diwani huyo kukaa chini baada ya hoja yake
kutakiwa kupatiwa ufumbuzi wakati mwingine na si kwenye kaikao hicho.
Diwani huyo alitoa hoja ambapo alisema kuwa wananchi wake walikuwa
wakihitaji eneo kwa ajili ya kufanya soko huku eneo hilo likitakiwa
kufanyiwa jambo jingine na si soko na watafute sehemu nyingine na hapo
patawekwa kitega uchumi kingine.
“Wananchi walikubaliana eneo hilo la (Community Centre) lijengwe soko
kutokana na kata hiyo kutokuwa na soko ambapo wananchi mbali ya
kuliandaa pia walichanga fedha kwa ajili ya kulirekebisha kwa ajili ya
shughuli hiyo,” alisema Makala.
Makala alisema kuwa wananchi walishakubaliana juu ya eneo hilo
kufanywa ujenzi wa soko lakini cha kushangaza Halmashauri inakataa na
kuwataka watafute sehemu nyingine.
Akijibu hoja hiyo Mwenyekiti Mkomambo alisema kuwa eneo hilo haliwezi
kuwekwa soko na badala yake kiwekwe kitega uchumi kingine hivyo
watafute eneo mbadala kwa ajili ya shughuli hiyo ya soko na nyumba
zilizopo hapo zibomolewe.
Kutokana na majibu hayo ndipo diwani huyo alipoamka na kusema kuwa
miezi michache iliyopita Mwenyekiti alikuwa kwenye ziara na kusema
kuwa soko litajengwa iweje leo anakana kauli yake hivyo hawezi
kukubaliana na maelezo hayo.
Mwenyekiti huyo baada ya maelezo kutoafikiwa na diwani huyo alimwambia
kuwa suala hilo alipeleke kwenye kamati ya mipango miji na mazingira
ili lipatiwe majibu na majibu hayataweza kutolewa hapo.
“Ni kweli nilikuja kwenye kata yako lakini masuala haya itabidi
uyapeleke kwenye kamati ya mipango miji naamini utapata majibu pia
sasa imepita miezi saba tangu nilipotembelea kwanini hukuleta hoja
hizo mapema leo ndiyo unataka majibu hapa ili upate majibu ya uhakika
fuata hizo taratibu nilizokuambia,” alisema Mkomambo.
Kutokana na majibu hayo diwani huyo aliendelea kutoa maneno na
kutakiwa akae lakini alikataa na ndipo mwenyekiti alipomwamuru atoke
nje hadi pale atakapojirekebisha jambo ambalo lilimfanya diwani huyo
atoke nje na kuondoka kabisa eneo la viwanja vya halmashauri.
Mwisho.

Wednesday, July 30, 2014

COPA COCA COLA KUCHUJANA AGOSTI 16



Na John Gagarini, Kibaha
CHAMA cha soka Kibaha Vijijini wilayani Kibaha mkoani Pwani (KIVIFA) kinatarajia kuchagua timu ya vijana wenye umri wa miaka 15 ya Copa Coca Cola Agosti 16 mwaka huu.
Kwa mujibu wa mwenyekiti wa wa mashinadano wa (KIVIFA) Mohamed Msamati amesema kuwa tayari wameshakaa na vilabu 11ili kuwaelekeza namna ya kufanya mashindano hayo.
Msamati amesema mashindano hayo yatafanyika ili kutekeleza agizo la Chama Cha Soka Mkoa wa Pwani (COREFA), kila wilaya kuhakikisha inapata timu ya vijana kwa ajili ya mashindano ya mkoa.
Amesema kuwa kuwa kwa sasa wako kwenye maandalizi ya michuano hiyo ambayo itashirikisha timu zote za Kibaha Vijijini na kuzitaka timu kujiandaa na mashindano.
Aidha amesema kuwa Kila timu inapaswa kuandaa wachezaji wake kwa kufanya mazoezi ya kutosha ili kuhakikisha wilaya inapata wachezaji wazuri watakaowakilisha kwenye mashindano ya mkoa.
Amebainisha kuwa watahakikisha mashindano hayo yanatumia wachezaji ambao wana umri unaopaswa na kuepukana na kutumia wachezaji ambao wana umri mkubwa maarufu kama vijeba.
Kwa upande wake mwenyekiti wa KIVIFA Meja Mstaafu Deus Makwaya amesema wamejipanga vizuri katika kuhakikisha mashindano hayo yanafanikiwa na kupata timu bora.
Meja Makwaya amesema kuwa tayari wameteua viongozi kwa ajili ya kusimamia mashindano hayo ya Copa Cola Cola ambao ni Dk Musa Sama ambaye ni mwenyekiti, Juma Likali katibu na God Mwafulilwa meneja.
Amewataja wajumbe kuwa ni Hija Matitu, Juma Kisebengo, Said Kidile huku walimu wakiwa ni Said Shaban na Mtoso ambao ni timu ya ushindi ya kuandaa vijana hao.
Mwisho.

Monday, July 28, 2014

AMWUA MKEWE KWA WIVU WA MAPENZI



KIJANA aliyetambuliwa kwa jina la Omary Molel mkazi wa Kijiji cha Mwanabwito kata ya Ruvu wilayani Kibaha mkoani Pwani anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka (25) anatuhumiwa kumwua mchumba wake Sina Hamis (21) kwa kumchoma kisu kutokana na wivu wa mapenzi.

Mtuhumiwa huyo ambaye alikuwa akifanya kazi ya kusimamia shamba la mtu pamoja na kufanya kazi ya bodaboda anatuhumiwa kufanya mauaji hayo nyumbani kwa wakwe zake baada ya kuona kuwa mkewe amegoma kwenda kwake kutokana na ugomvi uliokuwepo baina yao.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu mwenyekiti wa Kijiji cha Boko Mnemela Hassan Mohamed amesema kuwa tukio hilo limetokea Julai 27 majira ya saa mbili asubuhi.

Mohamed amesema kuwa siku moja kabla ya tukio hilo Julai 26 mtuhumiwa huyo akiwa na amesindikizwa na mtu mmoja ambaye jina lake bado halijapatikana walikuwa na kikao cha kusuluhishwa baada ya kuhitilafiana  na kikao hicho kilifanyika nyumbani kwa wazazi wa marehemu.

Amesema kuwa Kwa mujibu wa watu waliohudhuria kikao hicho wamesema kuwa kikao hicho kilifanyika kuanzia majira ya saa 2 usiku hadi saa 5 usiku ambapo hata hivyo mwafaka haukuweza kufikiwa kwani marehemu alikataa kwenda kwa mume wake.

Aidha amessema kuwa siku iliyofuata watu waliokuwa wakihusika kusuluhisha waliondoka na yeye pamoja na mtu aliyeambatana naye waliondoka lakini ghafla alirudi akidai kuwa anafuata betri ya simu aliyoisahau nyumbani kwao na marehemu.

Alimkuta mkewe akipepeta mchele jikoni na kuanza kumbembeleza lakini inaonekana aligoma kabisa kurudi kwa mumewe hali ambayo ili mkasirisha mumewe na kuanza kumchoma kwa kutumia kisu huko jikoni kisha wakatoana nje huku marehemu akipiga kelele.

Ameongeza kuwa Mtuhumiwa alimchoma marehemu kwenye ziwa la upande wa kulia na kwenye uti wa mgongo karibu na bega la upande wa kushoto na alimchoma kisu mbele ya bibi yake mama yake wa kufikia na mdogo wake ambao walipiga kelele na kushindwa kumsaidia ambapo mtuhumiwa huyo alikimbia maporini.

Mwenyekiti huyo alipoulizwa juu ya chanzo cha mauaji hayo amesema kuwa kwa mujibu wa watu waliokuwa wakijua ugomvi wao walisema kuwa mtuhumiwa alikerwa na tabia ya mkewe kurudishiwa zaidi chenchi anapokwenda kwenye duka lililopo kijijini hapo.

Ameongeza kuwa Marehemu alikuwa akimjulisha mumewe juu ya hali hiyo ambapo inasemekana aligoma kurudi kutokana na kuambulia vipigo na kutishiwa kuuwawa na mwanaume huyo na kupelekea kufanyika kikao cha usuluhishi na muuza duka kifanyika ili kupata mwafaka lakini ikashindikana na kutokea mauaji hayo ya kusikitisha.

Kwa upande wa kamanda wa Polisi mkoani Pwani Kamishna Msaidizi Mwanadamizi wa Polisi (SACP) Ulrich Matei amekiri kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa mtuhumiwa huyo anatafutwa ambapo jitihada hizo bado hazijazaa matunda.

 

  

Sunday, July 27, 2014

ATUHUMIWA KUMWUA MKEWE KWA KUMCHOMA KISU KUTOKANA NA WIVU WA KIMAPENZI



Na John Gagarini, Kibaha
KIJANA aliyetambuliwa kwa jina la Omary Iddi mkazi wa Kijiji cha Mwanabwito kata ya Ruvu wilayani Kibaha mkoani Pwani anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka (25) anatuhumiwa kumwua mkewe kwa kumchoma kisu kutokana na wivu wa mapenzi.
Mtuhumiwa huyo ambaye alikuwa akifanya ya kusimamia shamba la mtu pamoja na kufanya kazi ya bodaboda anatuhumiwa kufanya mauaji hayo nyumbani kwa wakwe zake baada ya kuona kuwa mkewe amegoma kwenda kwake kutokana na ugomvi uliokuwepo baina yao.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu mwenyekiti wa Kijiji cha Boko Mnemela Hassan Mohamed alisema kuwa tukio hilo limetokea Julai 27 majira ya saa mbili asubuhi.
Mohamed alisema kuwa siku moja kabla ya tukio hilo Julai 26 mtuhumiwa huyo akiwa na amesindikizwa na mtu mmoja ambaye jina lake bado halijapatikana walikuwa na kikao cha kusuluhishwa baada ya kuhitilafiana  na kikoa hicho kilifanyika nyumbani kwa wazazi wa marehemu.
“Kwa mujibu wa watu waliohudhuria kikao hicho walisema kuwa kikao hicho kilifanyika kuanzia majira ya saa 2 usiku hadi saa 5 usiku ambapo hata hivyo mwafaka haukuweza kufikiwa kwani marehemu alikataa kwenda kwa mume wake,” alisema Mohamed.
Alisema kuwa siku iliyofuata watu waliokuwa wakihusika kusuluhisha waliondoka na yeye pamoja na mtu aliyeambatana naye waliondoka lakini ghafla alirudi akidai kuwa anafuata betri ya simu aliyoisahau nyumbani kwao na marehemu.
“Alimkuta mkewe akipepeta mchele jikoni na kuanza kumbembeleza lakini inaonekana aligoma kabisa kurudi kwa mumewe hali ambayo ili mkasirisha mumewe na kuanza kumchoma kwa kutumia kisu huko jikoni kisha wakatoana nje huku marehemu akipiga kelele,” alisema Mohamed.
“Mtuhumiwa alimchoma marehemu kwenye ziwa la upande wa kulia na kwenye uti wa mgongo karibu na bega la upande wa kushoto na alimchoma kisu mbele ya bibi yake mama yake wa kufikia na mdogo wake ambao walipiga kelele na kushindwa kumsaidia ambapo mtuhumiwa huyo alikimbia maporini,” alisema Mohamed.
Mwenyekiti huyo alipoulizwa juu ya chanzo cha mauaji hayo alisema kuwa kwa mujibu wa watu waliokuwa wakijua ugomvi wao walisema kuwa mtuhumiwa alikerwa na tabia ya mkewe kurudishiwa zaidi chenchi anapokwenda kwenye duka lililopo kijijini hapo.
“Marehemu alikuwa akimjulisha mumewe juu ya hali hiyo ambapo inasemekana aligoma kurudi kutokana na kuambulia vipigo na kutishiwa kuuwawa na mwanaume huyo na kupelekea kufanyika kikao cha usuluhishi na muuza duka kifanyike ili kupata mwafaka lakini ikashindikana na kutokea mauaji hayo ya kusikitisha,” alisema Mohamed.
Jitihada za kumpata kamanda wa Polisi mkoani Pwani Kamishna Msaidizi Mwanadamizi wa Polisi Ulrch Matei hazikuweza kuzaa matunda ili aweze kuzungumzia tukio hilo.
Mwisho.

JESHI LA POLISI PWANI LAJIPANGA SIKUKUU YA IDDI




Na John Gagarini, Kibaha
JESHI la Polisi mkoani Pwani limewataka madereva kuwa makini waendeshapo magari na kuacha matumizi ya vilevi ili kuepukana na ajalizisizo za lazima ambazo zinaweza zikajitokeza wakati wa kipindi cha sikukuu ya Eid el Fitr inayofanyika leo duniani kote.
Pia limewataka wanafamilia kutotoka wote majumbani bila ya kuacha watu au kutoa taarifa kwa majirani ili kuepuka wizi na uhalifu unaoweza kujitokeza wakati wa sikukuu.
Kwa mujibu wa kamanda wa polisi mkoani humo Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi (SACP) Ulrich Matei alisema kuwa baadhi ya madereva wamekuwa wakitumia vilevi wakati wa kiendesha magari jambo ambalo ni hatari kwa watumiaji wa vyombo vya usafiri na watembea kwa miguu.
“Jeshi la polisi liko makini katika kipindi hichi cha sikukuu ili kuhakikisha wananchi wanasherehekea sikukuu bila ya matatizo na linawaomba madereva kuachana na tabia ya kutumia vilevi ili kuepuka ajali wakati huu,” alisema Kamanda Matei.
Aidha alisema kuwa kikosi cha usalama barabarani kitahakikisha madereva wanafuata sheria za usalama barabarani ili kuepusha ajali ambazo zianweza kutokea na kuleta madhara kwa watu.
“Tunasisitiza madereva kuachana na ulevi wakati wa kuendesha kwani uzoefu unaonyesha ajali nyingi zimekuwa zikitokana na matumizi ya ulevi hivyo waache matumizi hayo na endapo watabainika watachukuliwa hatua kali za kisheria,” alisema Kamanda Matei.
Kwa upande wa wananchi aliwataka kutumia ulinzi jirani kwa kuacha mtu au watu badala ya kuondoka wote na kuacha nyumba peke yake jambo ambalo linaweza likasababisha wizi majumbani.
“Wezi wamekuwa wakitumia mwanya wa kuiba kwenye nyumba ambazo hazina watu hivyo hata kama nyumba nzima imetoka ni vyema wakatoa taarifa kwa majirani ili wawalindie nyumba zao,” alisema Kamanda Matei.
Aliwataka wamiliki wa kumbi za starehe kutojaza watu kupita kiasi ili kuepuka athari ambazo zinaweza kujitokeza endepo watakuwa wamejaza watu wengi kwenye kumbi zao.
“Kuna hatari nyingi zinazotokana na kumbi kujaa kupita kiasi mfano watu kukosa hewa na kusababisha vifo au bahati mbaya shoti ya umeme endapo itatokea hivyo lazima wazingatie masharti ya leseni zao zinavyowataka ili kuepusha athari kama hizo,” alisema Kamanda Matei.
Alibainisha kuwa jeshi lake limejipanga kuhakikisha kuwa sherehe hizo zinafanyika kwa amani na utulivu kwa kuweka ulinzi kwenye maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufanya doria mitaani.
Mwisho.

MAGUFULI ATOA UFAFANUZI WA FIDIA BARABARA NDUNDU SOMANGA



Na John Gagarini, Rufiji
Serikali kupitia wizara ya Ujenzi imetoa ufafanuzi juu ya suala la fidia kwa wakazi wanaopitiwa na mradi wa ujenzi wa barabara ya Ndundu-Somanga iliyopo kati ya Mikoa ya Pwani na Lindi.
Waziri wa ujenzi Pombe Magufuli akizungumzia suala hilo kwa wananchi wakati akikagua barabara hiyo huku akiwa ameambatana na viongozi mbalimbali wa Serikali,wakala wa Tanroads katika Mikoa ya Lindi na Pwani alisema wale waliojenga nyumba zao ndani ya mita 22.5 hawatolipwa fidia kutokana na kuvunja sheria.
Alieleza kuwa mbali ya kutolipwa fidia pia watu hao watatakiwa kulipia gharama za mafuta ya greda ambalo litafanya kazi ya ubomoaji.
Magufuli Alielezea wale walio nje ya mita 22.5 na ambao makazi yao yamejengwa nyuma ya mwaka 2007 ambapo watawekewa alama ya X kwa rangi ya kijani ikiashiria hao ndio watalipwa fidia .
Aidha Waziri huyo wa Ujenzi alikemea tabia ya kuiba mafuta inayofanywa na baadhi ya watumishi wa mkandarasi huyo sanjali na baadhi ya wananchi kwani kwa kufanya hivyo ni kukwamisha kasi ya ujenzi wa barabara hiyo.
Alitoa rai hiyo baada ya kufikishiwa malalamiko hayo na baadhi ya wananchi wa kijiji cha Manzese kilicho mpakani mwa mikoa ya Lindi na Pwani kuwa kuna tabia ya kuibiwa mafuta jambo ambalo linasababisha ujenzi kusuasua.
Magufuli pia alimtaka mkandarasi wa barabara hiyo M.A Kharafi $ Sons Ltd kuwalipa fedha nzuri wafanyakazi wake  ili waweze kuondokana na tamaa za kuiba mafuta na vifaa vingine.
Mwishoni mwa wiki Magufuli alitoa siku 60 kwa Mkandarasi wa barabara ya Ndundu-Somanga iliyopo kati ya Mikoa ya lindi na Pwani M.A Kharafi $Sons Ltd kuhakikisha anamaliza ujenzi wa barabara hiyo .
Agizo hilo ni kuanzia sasa hadi mwezi wa 9 mwaka huu awe ameshamaliza kazi hiyo na kama akizembea serikali itamchukulia hatua zaidi kwani imeshamlipa kwa awamu nyingine Bil 8.91 hivyo hakuna kisingizio kingine.

Waziri Magufuli alisema mkandarasi huyo amekiuka mkataba hivyo serikali imechoshwa na usumbufu na visingizio vyake  .
Alisema Mkataba wake ulikuwa ukionyesha kuanza ujenzi mwaka 2009 na kukamilika 2011 kwa kujenga km 56.318 kwa kiwango cha lami lakini hadi sasa km 10 bado hajazikamilika.
Sambamba na agizo hilo aliwaagiza mameneja wa wakala wa barabara Tanroads ,Mikoa ya Lindi na Pwani kumbana Mkandarasi huyo ili kuhakikisha hazembei kumaliza kazi hiyo kwa muda aliopewa.
Aidha alisema tayari kwasasa wizara imechukua hatua ya kumfukuza kazi Mhandisi Msimamizi ushauri wa awali wa ujezi wa barabara hiyo Engineering System Group –KSCC toka juni 8 mwaka huu .
Ambapo kwasasa barabara hiyo itasimamiwa na Wakala wa barabara –Tanroads-yenyewe kupitia kitengo cha usimamizi wa kazi ndani ya wakala huo kwa mujibu wa sheria namba 16 ya mwaka 1997.

"Wasimamiazi hao wamsimamie mkandarasi hadi atoke makamasi ,na ni lazima kuanzia sasa afanye kazi usiku na mchana,jumatatu hadi jumapili ili amalize ujenzi kwa muda wa miezi hii miwili pekee”alisema Magufuli.

Alieleza kuwa ifikie hatua ya kusema basi kulea wakandarasi wasumbufu ili kuondoa changamoto zinazowakabili wananchi ikiwemo vumbi na kukwama kwa magari kutokana na uzembe wa mkandarasi husika.

Nae Mtendaji Mkuu wa wakala wa barabara Tanroads nchini ,Mhandisi Patrick Mfugale alieleza mbali ya changamoto hiyo pia mkandarasi huyo alishindwa kuendesha mradi kwa fedha zake mwenyewe hadi serikali ilipomwezesha.
Sababu nyingine ni kucheleweshwa kwa fedha kutoka kwa wachangiaji wa fedha wengine katika mradi huo ikiwemo OPEC na Quwait fund .
Barabara ya Ndundu-Somanga  ina urefu wa km 56.318 ,zilizokamilika ni km 42 huku km 10 zikiwa bado hazijakamilika,na hadi kukamilika kwa ujenzi itagharimu kiasi cha sh. Bil 58.813 ambapo hadi sasa umegharimu sh.Bil 49.
Katika gharama hizo serikali itachangia asilimia 55,OPEC 14 na Quwait Fund asilimia 31.

Mwisho