MEYA wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Dk Nicas Mawazo amezindua Darasa Janja (Live Teaching) Shule ya Sekondari Bundikani na kuiomba Serikali kuanzisha madarasa hayo kote nchini ili kukabiliana na upungufu wa walimu
Mawazo alitoa ombi hilo wakati akizindua darasa hilo shuleni hapo ambapo shule hiyo ni Sekondari ya Kata ya Maili Moja Wilayani Kibaha na kuwa darasa janja yatasaidia kuwafanya wanafunzi kuwa na ari ya kusoma.
Amesema kuwa mwalimu mmoja anayefundisha kupitia darasa janja moja anaweza kufundisha shule zote ambazo zitakuwa zimeunganishwa kwenye mfumo huo wa darasa la aina hiyo kote nchini kwa wakati mmoja.
"Mfumo huu wa darasa janja ni mzuri kwa kukabiliana na changamoto ya upungufu wa walimu kwani mwalimu mmoja anauwezo kufundisha shule zote ambazo zimeunganishwa kwenye mfumo huo,"amesema Nicas.
Aidha amesema kuwa pia mbali ya kufundisha wakati mmoja pia yale aliyofundisha mwalimu huyo yanaweza kurekodiwa na kuwafundisha wanafunzi wengine kwa ubora ule ule.
"Jambo zuri ni kuwa walimu wote wanaofundisha kupitia madarasa janja wote ni wale wenye umahiri wa kufundisha hivyo watawajengea wanafunzi uwezo mkubwa wa kujifunza na kupata ujuzi,"amesema Mawazo.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Mrisho Mlela amesema kuwa wataendelea kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa madarasa janja kwenye shule za sekondari.
Mlela amesema kuwa wameendelea kuboresha sekta ya elimu kwa kujenga shule tatu za mfumo wa Kiingereza na shule hizo zote zimejengwa kutokana na fedha za mapato ya ndani na kutengeneza madawati viti na meza 4,000 kwa shule za msingi na sekondari.
Naye Mkuu wa Shule ya Bundikani Bernard Muyenjwa amesema kuwa wanaishukuru Serikali kwa kuwapatia darasa hilo janja kwani litarahisisha katika ufundishaji na kupunguza changamoto ya upungufu wa walimu.
Muyenjwa amesema kuwa kuanzishwa kwa darasa janja hilo shuleni kwao kutasaidia walimu kufundisha bila ya kuchoka wala kutumia nguvu kubwa na kuwapa wanafunzi umahiri na kujua namna ya kutumia teknolojia.
mwisho








