Saturday, March 7, 2026

WANANCHI WAMIMINIKA KLINIKI YA ARDHI KIBAHA WAOMBA SIKU ZIONGEZWE

 

WANANCHI wa Manispaa ya Kibaha wameendelea kujitokeza kwa wingi kupata huduma katika Kliniki ya Ardhi ijulikanayo kama Samia Ardhi Kliniki, huku baadhi yao wakiomba muda wa utoaji wa huduma hizo uongezwe kutokana na umuhimu wake.

Wananchi hao pia wameishukuru Serikali kwa kusogeza huduma hizo karibu yao na kueleza kuridhishwa na namna wanavyohudumiwa katika kliniki hiyo.

Maoni hayo yametolewa Machi 4, 2026, wakati kambi maalum ya kushughulikia masuala ya ardhi ikiendelea kwa siku ya tatu katika viwanja vya Maili Moja, Stendi ya Zamani, Manispaa ya Kibaha, ambapo wananchi wengi wameendelea kumiminika kupata huduma mbalimbali.

Mkazi wa Kibaha, Ester Joel, aliyefika katika kliniki hiyo kupata huduma ya hati, amesema ameridhishwa na huduma aliyoipata na kuomba muda wa kliniki hiyo uongezwe ili wananchi wengi zaidi wapate fursa ya kuhudumiwa.

“Nimeridhika na huduma niliyoipata hapa. Kwanza nimepokelewa vizuri na nimeelekezwa namna ya kutatua changamoto yangu. Hata hivyo, kutokana na umuhimu wa huduma hii, ningependa siku ziongezwe hata kufikia wiki mbili,” amesema Ester Joel.

Kwa upande wake Coletha Nombo, ambaye pia alifika kupata huduma ya hati, amepongeza juhudi za Serikali kwa kuwaletea wananchi huduma hiyo karibu na maeneo yao.

Naye Ruth Kadema, mkazi wa Pangani, amesema ameridhishwa na huduma aliyoipata na kueleza kuwa amepewa maelekezo ya kufika tena siku ya Jumamosi kwa ajili ya kukamilisha taratibu za kupata hati yake.

“Huduma hii ni nzuri sana. Nimeridhika na nimeambiwa nije Jumamosi kuchukua hati yangu baada ya kuwasilisha taarifa zangu leo,” amefafanua Ruth.

Kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambayo huadhimishwa Machi 8 kila mwaka, Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeandaa kambi hiyo maalum ya huduma za ardhi kwa lengo la kusikiliza na kutatua kero mbalimbali za wananchi zinazohusu masuala ya ardhi, hususan umilikishwaji wa ardhi na upatikanaji wa hati.

Kambi hiyo maalum ya siku sita ijulikanayo kama Samia Ardhi Kliniki ilianza rasmi Machi 2 na inatarajiwa kuhitimishwa Machi 7, 2026.

Friday, March 6, 2026

UMILIKI RASILIMALI KWA WANAWAKE WAPUNGUZA VITENDO VYA UKATILI

SERIKALI imeweka mazingira wezeshi ikiwa ni pamoja na umiliki rasilimali ili kupunguza vitendo vya ukatili kwa wanawake kuelekea Dira ya Maendeleo ya mwaka 2050.

Akizungumza wakati wa sherehe za Siku ya Wanawake Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Pwani Hawa Mchafu amesema uwepo wa mazingira hayo unaondoa ukatili wa kijinsia.

Mchafu amesema kuwa uwepo wa usawa na kulinda kulinda haki za wanawake kuna mchango mkubwa katika suala la maendeleo.

"Usawa wezeshi hiyo ni nyenzo muhimu ili kuketa utandaji wa pamoja wa kufikia malengo ya dira ya maendeleo na kuongeza ushiriki wanawake kwenye masuala muhimu yakiwemo ya uongozi,"amesema Mchafu.

Amesema kuwa dhumuni la kuwarudisha wasichana waliopata mimba wakiwa shuleni ni kutimiza ndoto zao kwani siyo wote waliopata ujauzito kwa kupenda au tamaa bali ni kutokana na mazingira wanayoishi na wengine wamepewa na ndugu.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Dk Rogers Shemwelekwa aesma kuwa asilimia 70 ya watumishi ni wanawake menejimenti idara tano zinaongozwa na wanawake ambapo wanafanya kazi nzuri ikiwemo kwenye zoezi la ukusanyaji mapato.

Shemwelekwa amesema kuwa wamewawezesha wanawake wenye biashara ndogo ndogo kuunda vikundi ambapo walikuwa hawakopesheki lakini sasa wamekopeshwa bilioni 2 na wanarejesha vizuri.

Naye Mkuu wa Divisheni ya Maendeleo ya Jamii Leah Lwanji amesema kuwa vikundi 275 vya wanawake vimekopeshwa zaidi ya bilioni 1 ikiwa ni asilimia 94. 

Lwanji amesema kuwa majukwaa yamehamasishwa kuanzishwa miradi ya kiuchumi ili waweze kujikwamua na mpaka sasa zimekopeshwa milioni 70 kwa akinamama wa majukwaa.

Moja ya kikundi ambacho ni cha mfano cha Lulu ya Wajane mwaka jana kilipata mkopo wa shilingi milioni 46 ambapo walipaswa kurejesha mkopo huo kwa miaka mitatu lakini kimeweza kurejesha ndani ya miezi 11.

Kiongozi wa kikundi hicho Kanyenda Mweri amesema kuwa fedha hizo za mikopo isiyokuwa na riba zimewasaidia kuwakwamua kiuchumi na kuweza kutoa ajira kwa wanawake wenzao.

Thursday, March 5, 2026

MAOFISA USAFIRISHAJI WATAKIWA KUUNDA VIKUNDI WAKOPE HALMASHAURI





MAOFISA Usafirishaji maarufu kama Bodaboda kwenye Mtaa wa Mwendapole B wametakiwa kuunda vikundi ili waweze kukopa vyombo vya usafiri vinavyotolewa na Halmashauri kuachana na mikopo ya taasisi za watu binafsi ambazo zina gharama kubwa.

Aidha alisema kuwa gharama za mikopo ya Halmashauri ni ndogo na marejesho yake ni madogo tofauti na mikopo ya vyombo hivyo kwenye taasisi au watu binafsi.

Hayo yalisemwa na Mwenyekiti wa Mtaa huo Abubakar Matumla wakati wa kikao na waendesha pikipiki wa Mtaa huo na kuwa wanashindwa kufanikiwa kwa kukopa pikipiki kwa riba kubwa.

Matumla alisema kuwa gharama za kukopa pikipiki kwa watu binafsi imekuwa ikiwafanya wasifanikiwe kutokana na gharama kuwa kubwa za mikopo hiyo hivyo hujikuta wanashindwa kujiongezea kipato.

"Serikali imewawekea mazingira mazuri ya mikopo yake kwani mnauwezo wa kukopa pikipiki, bajaji na Toyo kwa gharama nafuu na unarejesha kiasi kilekile ulichokopa na hakuna riba ya mkopo unaokopa hivyo ni wakati wenu wa kujiunga na kuwa na vikundi na mtumie fursa ya mikopo pale Halmashauri fedha zipo za kutosha na vyombo vya moto vipo,"alisema Matumla.

Alisema kuwa yuko tayari kuwasimamia kuhakikisha wanapata mikopo hiyo kwani hapendi kuona waendesha pikipiki wakitaabika ili hali kuna sehemu wanaweza kukopa bila ya kuwa na marejesho makubwa pia aliwataka kutoa taarifa kwa wale wanaojihusisha na vitendo vya kiuhalifu.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa waendesha pikipiki hao Abdulatif Mbonganga alisema kuwa tayari wameshaanzisha kikundi kimoja na tayari kimeshasajiliwa kikiwa kinasubiri wakati ukifika waende kukopa.

Mboganga alisema kuwa changamoto kubwa kwao ni kukosa vyombo vya usafiri hali inayowabidi kukopa vyombo hivyo kwenye taasisi za watu binafsi ambazo zinagharama kubwa na kujikuta wakitumia nguvu kubwa kwenye marejesho.

Moja ya maofisa usafirishaji Salum Msaku alisema kuwa changamoto ya uhalifu inatokana na baadhi yao kuwapa ma "day worker" hasa nyakati za usiku ambapo wanawaletea sifa mbaya.

Msaku alisema kuwa ili kudhibiti hali hiyo kila mwendesha pikpiki aendeshe pikipiki yake na siyo kumpa mtu mwingine pia wahakikishe wanavaa riflector ambazo zitawatambua kwa namba zinazoandikwa mgongoni inakuwa rahisi katika ufuatiliaji.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtaa wa Miembe Saba B Nuru Awadh alisema kuwa wanapaswa kuwa na ushirikiano na kuunda vikundi vya bodaboda ili wapate mikopo nafauu.

Awadh aliwataka wajiheshimu na wasijiunge na makundi mabaya kwani Rais amewapa kipaumbele vijana katika uongozi na sehemu mbalimbali ili wawe vinara kwa utendaji kazi.

Tuesday, March 3, 2026

KAMBI SAMIA ARDHI KLINIKI YAANZA PWANI

HALMASHAURI ya Manispaa Kibaha kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeweka kambi ya Samia Ardhi Kliniki ikiwa ni maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani.

Akizungumza kuhusu huduma zinazotolewa katika kambi hiyo ya siku sita, Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Pwani Rugambwa Banyika alisema kuwa kliniki hiyo inalenga kutoa ushauri wa kisheria kuhusu masuala ya ardhi.

Banyika alisema kuwa shughuli nyingine zitakuwa ni kufanya makadirio ya pango la ardhi, kuandaa nyaraka za umiliki, kujibu changamoto za upimaji, urasimishaji, upangaji miji na michoro pamoja na kutoa hati za umiliki.

"Wananchi wote wanakaribishwa ili kupata huduma zote zihusiananazo na masuala ya ardhi ambapo huduma zimesogezwa ili kila mwananchi apate fursa katika kipindi hichi kuanzia Machi 2 hadi 7 kuelekea kilele cha siku ya Wanawake Duniani Machi 8,"alisema Banyika. 

Alisema kuwa kambi hiyo maalum ina lengo la kushughulikia changamoto mbalimbali za ardhi kwa wananchi hususan wanawake na wasichana katika masuala yanayohusiana na ardhi.

Baadhi ya wananchi Mariam Juma na Ahmed Abdala wameishukuru Serikali kwa kusogeza huduma hizo karibu yao na kueleza kuridhishwa na namna wanavyohudumiwa na wataalamu wa ardhi kwani wanatoa elimu ya kujitosheleza.

Kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kimkoa kinatarajiwa kufanyika Machi 8 2026 katika Uwanja wa Ujamaa Kata ya Umwe Tarafa ya Ikwiriri Halmashauri ya Mji wa Rufiji ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge.

Sunday, March 1, 2026

PWANI YAANZA MAANDALIZI MAADHIMISHO SIKU YA WANAWAKE DUNIANI

MKOA wa Pwani umeanza maandalizi ya Siku ya Wanawake Duniani ambapo kilele cha maadhimisho kimkoa yatafanyika Machi 8, 2026 katika Uwanja wa Ujamaa, Kata ya Umwe, Tarafa ya Ikwiriri, Halmashauri ya Mji Rufiji. 

Mratibu wa maadhimisho hayo, Roseline Kimaro, amesema mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakar Kunenge.

Akizungumza kuhusu maandalizi, Kimaro amesema maadhimisho ya mwaka huu yanaongozwa na kaulimbiu isemayo, “Haki kwa Wanawake na Wasichana: Msingi wa Maendeleo Jumuishi Dira 2050,” ikisisitiza umuhimu wa usawa wa kijinsia na haki kama nguzo ya maendeleo endelevu. 

Amesema lengo ni kutambua na kuenzi mchango wa wanawake katika nyanja za kijamii, kisiasa na kiuchumi, sambamba na kuimarisha mapambano dhidi ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia.

Amebainisha kuwa kuanzia Machi 1 hadi 7 kutafanyika shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo utoaji wa elimu kwa umma na kampeni za uhamasishaji kuhusu usawa wa kijinsia,  kilele cha maadhimisho Machi 8. 

Ameongeza kuwa maandalizi yanaendelea vizuri na kutoa wito kwa wananchi na wadau wa maendeleo kujitokeza kwa wingi kushiriki na kuunga mkono jitihada za kulinda na kuimarisha haki za wanawake na wasichana.

Friday, February 27, 2026

TRA PWANI KUBADILI UTARATIBU UKUSANYAJI KODI BANDARI YA BAGAMOYO

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Pwani kuanza utaratibu mpya ukusanyaji mapato Bandari ya Bagamoyo Machi Mosi mwaka huu.

Akizungumza na wafanyabiashara wa mafuta ya kula kwenye Bandari hiyo Meneja wa TRA Mkoa huo Masawa Masawa alisema kuwa changamoto iliyopo ni malalamiko ya wafanyabiashara kulalamikia bei ya kodi ya mafuta yanayotoka Zanzibar.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Shaibu Ndemanga alisema kuwa wananchi wengi wanategemea biashara ya mafuta na kuna wadau wengi wanategemea shughuli zinazohusiana na biashara ya mafuta.

Naye Diwani wa Kata ya Dunda Amiry Mpwimbwi alisema kuwa eneo hilo la Bandari linatoa ajira zaidi ya 8,000 hivyo kutokana na shughuli kutofanyika kumesababisha serikali kukosa mapato.

Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa Mafuta kwenye Bandari hiyo Shaban Hamsini alisema kuwa hali imeshakuwa mbaya kwani wanategemea shughuli hizo kuendeshea maisha yao.

Saturday, February 21, 2026

MATUMLA AWATAKA WANANCHI KUSHIRIKIANA NA SERIKALI ILI KUTATUA CHANGAMOTO


MWENYEKITI wa Mtaa wa Mwendapole B Manispaa ya Kibaha Abubakar Matumla ameendelea na ziara ya kutafutia majawabu changamoto zinazowakabili wananchi wa Mtaa huo.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Matumla amesema ziara hiyo inaifanya kwa kutembelea Balozi zote zilizopo kwenye Mtaa huo ili kubaini changamoto ili kupeleka sehemu husika kwa utatuzi.

Changamoto ambazo zimekuwa zikijirudia ni pamoja na miundombinu ya barabara, uhalifu, uvutaji wa bhangi, maji, elimu ya msingi.

Matumla amesema kuwa kutokana na changamoto hizo watawasiliana na mamlaka husika ili wazifanyie kazi changamoto hizo ili ziweze kupatiwa majawabu.

Akizingumzia uhalifu amesema kuwa tayari baadhi ya maeneo yameainishwa kuwa ni kitovu cha uhalifu pamoja na matumizi ya dawa za kulevya aina ya bhangi.

"Tayari tumeshaweka mikakati ya kudhibiti uhalifu kwa kushirikiana na Polisi Kata ili kuwakama wahalifu hao pia ni kufanya doria za kushtukiza ambapo baadhi ya wahalifu wanajificha kwenye Bodaboda ambapo tayari mipango ya kuwatambua inafanyika,"amesema Matumla.

Amesema baadhi ya maeneo kuna changamoto ya upatikanaji wa maji, miundombinu ya barabara imeharibika lakini hata hivyo Mtaa huo umepata barabara moja ambayo itajengwa lami.

"Kwa upande wa elimu ya Msingi changamoto kubwa ni uhaba wa madawati na vyumba vya madarasa ambapo Manispaa ya Kibaha imetoa madawati 20 ambayo yatasaidia kukabiliana na changamoto ya upungufu wa madawati,"amesema Matumla.