MWENYEKITI wa Mtaa wa Mwendapole B Manispaa ya Kibaha Abubakar Matumla ameendelea na ziara ya kutafutia majawabu changamoto zinazowakabili wananchi wa Mtaa huo.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Matumla amesema ziara hiyo inaifanya kwa kutembelea Balozi zote zilizopo kwenye Mtaa huo ili kubaini changamoto ili kupeleka sehemu husika kwa utatuzi.
Changamoto ambazo zimekuwa zikijirudia ni pamoja na miundombinu ya barabara, uhalifu, uvutaji wa bhangi, maji, elimu ya msingi.
Matumla amesema kuwa kutokana na changamoto hizo watawasiliana na mamlaka husika ili wazifanyie kazi changamoto hizo ili ziweze kupatiwa majawabu.
Akizingumzia uhalifu amesema kuwa tayari baadhi ya maeneo yameainishwa kuwa ni kitovu cha uhalifu pamoja na matumizi ya dawa za kulevya aina ya bhangi.
"Tayari tumeshaweka mikakati ya kudhibiti uhalifu kwa kushirikiana na Polisi Kata ili kuwakama wahalifu hao pia ni kufanya doria za kushtukiza ambapo baadhi ya wahalifu wanajificha kwenye Bodaboda ambapo tayari mipango ya kuwatambua inafanyika,"amesema Matumla.
Amesema baadhi ya maeneo kuna changamoto ya upatikanaji wa maji, miundombinu ya barabara imeharibika lakini hata hivyo Mtaa huo umepata barabara moja ambayo itajengwa lami.
"Kwa upande wa elimu ya Msingi changamoto kubwa ni uhaba wa madawati na vyumba vya madarasa ambapo Manispaa ya Kibaha imetoa madawati 20 ambayo yatasaidia kukabiliana na changamoto ya upungufu wa madawati,"amesema Matumla.



No comments:
Post a Comment