DIWANI wa Kata ya Tangini Antony Milao ametoa pole kwa wananchi waliokumbwa na kadhia ya mvua ikiwemo ya mwanafunzi Morhat Abdala (9) kunusurika kifo baada ya kusombwa na maji akitoka shuleni.
Mvua hiyo iliyonyesha jana jioni ilileta athari kwa baadhi ya wakazi wa Mtaa wa Machinjioni Kata ya Tangini ambapo nyumba mbili na Machinjio ya mbuzi ambapo mapaa yaliezuliwa baada mvua kubwa kunyesha ikiambatana na upepo mkali kwenye Mtaa huo.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutokea matukio hayo Milao amesema kuwa mwanafunzi huyo ambaye amepumzishwa kwenye Kituo cha Afya Mkoani akipatiwa matibabu anaendelea vizuri.
Milao amesema anamshukuru Mungu kumnusuru mtoto huyo ambaye anasoma darasa la nne Shule ya Msingi Maendeleo akiwa anatoka shule akiwa na mwenzake waliteleza wakati wakivuka kalavati na kusombwa na maji kabla ya wasamaria wema kuwaokoa.
"Pia nilimtembelea Mzee Boniface Mpanda ambaye nyumba yake imeezuliwa paa na nyumba ya Jackson Sellu ambaye hakuwepo nitawasiliana naye pamoja na sehemu ya paa la Machinjio jambo la kushukuru hakuna madhara kwa binadamu zaidi ya mapaa kungoka nimewashika mkono wale waliopata athari hizo ili waweze kutengeneza nyumba zao ili waendelee na maisha yao,"amesema Milao.
Mama wa mwanafunzi aliyesombwa na maji Fatuma Juma amesema kuwa alipata taarifa toka kwa wasamaria wema kuwa mwanae yuko Hospitali baada ya kusombwa na maji baada ya mvua kubwa kunyesha.
Juma amesema anamshukuru Mungu kwani mwanae kwa sasa anaendelea vizuri baada ya kupatiwa matibabu na anawashukuru wasamaria wema kumuokoa mwanae na kumuwaisha hospitali.
Naye Mzee Boniface Mpanda ambaye nyumba yake imeezuliwa paa amesema kuwa alikuwa ndani wakati mvua inanyesha mara akashtukia paa linarushwa na upepo mkali na vitu vyake vyote kulowa.
Mpanda anasema majirani walimsaidia kutoa vitu vyake na kuviweka kwenye mazingira salama wanatoa shukrani zao kwa majirani kwa kutoa msaada na diwani jinsi alivyojitoa kuwasaidia.
Kwa upande wake jirani ambapo nyumba hizo mbili zilizoezuliwa paa Remminister Komanga amesema kuwa mvua hiyo ilinyesha na ilikuwa na upepo mkali na kuezua mapaa hayo pamoja na kuangusha sehemu ya ukuta wake uliozungushiwa kwenye nyumba yake.
Komanga amesema upepo huo ulikuwa ni kama kimbunga na ulikuwa ni sehemu hiyo tu kwani maeneo mengine hakukuwa na upepo zaidi ya mvua kuwa tu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Machinjioni Aidan Saimon amesema kuwa baada ya kutokea madhara hayo waliwasiliana na diwani ili waangalie namna ya kuwasaidia wananchi hao.
Simon amesema kuwa alipewa maagizo na diwani kuhakikisha vifaa vyote vya upauaji atakavyovitoa vinatumika kwa haraka ili nyumba ya Mzee Mpanda ipauliwe upya na atawasiliana na Sellu kuona atamsaidiaje ambapo vyumba vyake viwili vimeezuliwa na upepo.

No comments:
Post a Comment