JAMII imetakiwa kuheshimu ajira ya wafanyakazi wa majumbani kwani nitaaluma kama zilivyo taaluma zingine kwa kuifanya kuwa yenye staha kwani ni sehemu ya ustawi wa jamii na ukuzaji wa uchumi.
Hayo yalisemwa Jijini Dar es Salaam kwenye ukumbi wa Confucius wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Rashid Ally Salim Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kazi na Uwekezaji Zanzibar wakati akifungua mkutano wa mradi wa Urasimishaji wa kitaaluma kwa wafanyakazi wa majumbani Tanzania.
Salim alisema kuwa jamii inapaswa kuona kazi za nyumbani ni taaluma kwa kuzingatia maslahi na haki za msingi za mfanyakazi kwani anaiendeleza jamii.
"Hawa ni watu muhimu sana kwani wanatunza familia zetu pale tunapokuwa kazini au kwenye majukumu mengine ya kimaendeleo hivyo tuwape heshima yao,"alisema Salim.
Alisema kupatiwa mafunzo ya ujuzi kupitia vituo vya VETA ni moja ya vitu vitavyoweza kuwasaidia katika maisha yao kwani ujuzi huo utakuwa ni mkombozi kwao na utawasaidia kujitambua na kujiamini.
Naye mwakilishi kutoka Veta Abdala Ulomi alisema kuwa tayari wametoa mafunzo ya ujuzi kwa wafanyakazi wa majumbani 1,280 kwenye vyuo sita vya Bara na vitatu vya Zanzibar na mtaala wao tayari umeshaandaliwa.
Ulomi alisema kuwa wanarasimisha mafunzo kwa wafanyakazi wa majumbani kwani mahitaji yao ni makubwa ndani na nje ya nchi na hiyo itakuwa taaluma kama taaluma zingine.
Kwa upande wake Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Profesa Rose Upor alisema kuwa asilimia 95 ya wafanyakazi wa majumbani ni wanawake ambapo kuna umuhimu wa kuboresha mazingira ya hali za kijinsia.
Upor alisema kuwa suluhisho ni kukuza utu na mazingira bora ya kazi ambapo kuna haja ya kushughulikia tafiti zinazofanywa ili kuleta usawa na kuepukana na vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Mkurugenzi wa Shirika la CVM Tanzania Magesa Nathaniel alisema kuwa wamekuwa wakitekeleza mradi wa miaka mitatu ambao umefika mwisho wa kukuza kazi za staha na haki kwa wafanyakazi kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na wadau mbalimbali wa ndani na nje.
Nathaniel alisema kuwa baadhi ya kazi walizokuwa wakifanya ni kuwajengea uelewa na kuwajengea uwezo kuwaunganisha na chama cha wafanyakazi wa majumbani CHODAWU katika utetezi wa haki zao.
Asteria Gerald mwakilishi wa CHODAWU alisema kuwa kutambuliwa kwa kazi zao kutasababisha kupata heshima ulinzi na stahiki nyingine kwani bado wananyanyaswa wanafanyiwa ukatili na wanafanya kazi kwa muda mrefu.
Gerald alisema kuwa wanaomba kuridhiwa kwa mkataba namba 189 wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) ambayo inalinda haki hadhi usalama wa wafanyakazi wa majumbani.
Mkurugenzi wa Taasisi za Taaluma za Kijinsia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Dk Sara Kisanga alisema kuwa wafanyakazi wa nyumbani wanapaswa kutambuliwa na kulindwa na kuendelezwa kiujuzi.
Kisanga alisema kuwa wataalamu wanaotoka chuoni hapo wanawezesha jamii ili kuleta mabadiliko chanya ili kuwa kazi ambazo zina staha na kuzingatia haki za binadamu.

No comments:
Post a Comment