Saturday, December 24, 2016

FAMILIA YA WATU SABA WASIOONA YASAIDIWA

 FAMILIA ya Watu saba wasioona
Na John Gagarini, Kibaha
JUMUIYA ya Maili Moja A ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Maili Moja imetoa misaada ya nguo na vyakula kwa familia yenye wasioona saba inayoishi kwenye Mtaa wa Simbani wilayani Kibaha mkoani Pwani.
Akizungumza na gazeti hili mara baada ya kukabidhi misaada hiyo ambayo ilipelekwa na Jumuiya hiyo mwenyekiti Jacob Samson alisema kuwa waliamua kupeleka misaada hiyo baada ya kupata taarifa za familia hiyo.
Samson alisema kuwa wametoa misaada hiyo pia ni katika kuwafanya nao waweze kusherehekea siku kuu ya X- Mass na wenzao wakiwa na furaha hasa ikizingatiwa wao ni wahitaji na wanahitaji misaada mbalimbali.
“Tunaamini kusaidia jamii zenye mahitaji ni ibaada kamili na inawatia moyo na kujiona kuwa hawako peke yao kwani kuna watu wanawaunga mkono na kushiriki nao kwa pamoja,” alisema Samson.
Alisema kuwa Jumiya yao hufanya ibaada za nyumba kwa nyumba ambapo hutembeleana na kushirikiana kwenye masuala mbalimbali ya kijamii pamoja na ya kiimani.
“Jumuiya yetu iko kwa ajili ya kusaidiana kwenya matatizo na furaha hivyo wanajumuiya walisema kuwa twende kwenye hiyo familia iwe sehemu ya ibaada ya yetu ya kila Jumamosi ili kuwafariji na wamejitolea sana ili kuhakikisha familia ile nayo inafurahia kipindi hichi cha mwisho wa mwaka,” alisema Samson.
Aidha alisema kuwa wanaomba watu wengine nao wajitokeze kuisaidia familia hiyo ambayo ina hitaji misaada mbalimbali kutokana na kuwa kwenye mazingira magumu.
“Kutoa ni moyo na si utajiri kwani watu wenye moyo wanapaswa kwenda kuwasaidia kwa jambo lolote la kijamii hasa ikizingatiwa familia hiyo inasimamiwa na mwanamke ambaye alitengana na mumewe,” alisema Samson.
Kwa upande wake mama wa familia hiyo Mwajuma Maulid alisema kuwa anaishukuru Jumuiya ya maili Moja kwa kuwapatia misaada hiyo ambayo wameitoa kwani wameonyesha moyo wa kipekee.
Maulid alisema kuwa vyakula vilivyotolewa vitawasaidia katika kusherehekea sikukuu ya X-Mass kwa furaha kama wanavyofurahia watu wengine na kuwataka watu wengine waendelee kuwasaidia.
“Tuko kwenye mazingira magumu sana kwani hali yetu si nzuri ambapo tunaishi maisha ya kubahatisha kwa hiyo wanapokuja watu kama hawa na kutupa misaada tunashukuru sana,” alisema Maulid.
Familia hiyo inaishi mtaa wa Simbani kata ya Kibaha ina watu saba ambao hawaoni ambapo wasioona ni mume wake ambaye walitengana,watoto wanne wasioona na  wajukuu wawili wote hawaoni na inaishi kwa kutegemea kuchoma mkaa na kusuka mikeka.

Mwisho.     

zee wa Kanisa kutoka Jumuiya ya Maili Moja A Samwel Luhembe kushoto akikabidhi sabuni iliyotolewa na jumuiya hiyo ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania KKKT usharika wa Maili Moja anayepokea ni mama wa familia ya watu wasioona saba Mwajuma Maulid kulia  
  Mzee wa Kanisa kutoka Jumuiya ya Maili Moja A Samwel Luhembe kushoto akikabidhi unga uliotolewa na jumuiya hiyo ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania KKKT usharika wa Maili Moja anayepokea ni mama wa familia ya watu wasioona saba Mwajuma Maulid kulia 

Mzee wa Kanisa kutoka Jumuiya ya Maili Moja A Samwel Luhembe kushoto akikabidhi nguo zilizotolewa na jumuiya hiyo ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania KKKT usharika wa Maili Moja anayepokea ni mama wa familia ya watu wasioona saba Mwajuma Maulid kulia 


Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maili Moja A ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania KKKT usharika wa Maili Moja Jacob Samson kushoto akimkabidhi moja ya msaada uliotolewa na Jumuiya hiyo kwa familia ya watu saba wasioona anayepokea ni Mwajuma Maulid ambaye ndiye mama anayeihudumia familia hiyo

Wednesday, December 14, 2016

MSOGA KUJENGA UWANJA WA KISASA



Na John Gagarini, Msoga

MKOA wa Pwani unatarajiwa kuwa na uwanja wa kisasa ambao utasaidia kukuza soka la vijana na kuinua michezo kwenye mkoa huo ambao umepania kuwa moja ya mikoa itakayolea vipaji.

Uwanja huo unatarajiwa kujengwa kwenye Kijiji cha Msoga kata ya Msoga Halmashauri ya Chalinze wilayani Bagamoyo na serikali ya watu wa China lengo likiwa ni kukuza sekta ya michezo kwa vijana kwenye mkoa na nchi kwa ujumla.

Akizungumza katika hafla maalumu iliyoandaliwa kwa ajili ya kwenda kutembelea eneo ambalo litajengwa uwanja huo Dk Kikwete alisema kwamba uwanja huo wa wa mpira wa miguu utajengwa  kwa ufadhili wa serikali ya watu wa china na kuongeza kuwa  utakuwa ni mkombozi mkubwa katika kukuza na kuinua vipaji kwa vijana wadogo.

“Tumehamasisha wadau wa michezo kujenga uwanja lengo lake kubwa ni kuhakikisha kwamba Tanzania katika siku za usoni inakuwa ni wachezaji wengi wenye vipaji ambao wataweza kuunda timu nzuri ya Taifa ambayo itaweza kufanya vizuri katika mashindano mbali mbali ya Kimataifa,” alisema Dk Kikwete.

“Uwanja huu wa mpira wa miguu pindi utakapokamilika utaweza kuwa ni mkombozi mkubwa wa vijana wadogo hususan wale wa shule, hivyo nimeshazungumza na rafiki zetu wa serikali ya china na wamekubali kutujengea kwa hivyo ni jambo la msingi sana katika kuendeleza sekta ya michezo kwa watoto wetu hawa mbao wataweza kuleta mafanikio makubwa katika siku zijazo,”allisema Kikwete.

Dk Kikwete alisema kuwa anaipongeza serikali ya china kwa kuona umuhimu wa kusaidia kujenga kiwanja hicho, na kuongeza kuwa pindi kitakapokamilika kitakuwa na michezo mingine ambayo itakuwa ikifanyika mbali na mchezo huo wa soka lengo ikiwa ni kuwapa fursa vijana kuweza kuonyesha vipaji walivyonavyo.

Naye Mwakilishi wa balozi wa China nchini Tanzania Yang Tong aliahidi kuendelea kutoa ushirikiano wa dhati katika kukuza sekta ya michezo hususani kwa  vijana wadogo ikiwa ni sambamba  na kujenga viwanja ili watoto wasiweze kucheza katika viwanja vya vumbi.

Naye Mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete alisema kwamba lengo lake kubwa ni kuhakikisha anakuza michezo wa vijana wadogo katika jimbo lake hivyo kukamilika kwa ujenzi wa uwanja huo kutaweza kuwasaidia vijana  kukuza vipaji vyao.

Nao baadhi ya wadau wa mchezo wa soka katika kijiji hicho cha Msoga akiwemo Michael James pamoja na Mohamed Halfan wamempongeza Rais mstaafu Dk Jakaya Kikwete kwa ubunifu wa ujenzi huo wa uwanja kwa ajili ya vijana wadogo kwani kutaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa kuleta mabadiliko chanya katika michezo ukiwemo wa soka.

Mwisho.

CCM WAANZA MCHAKATO WA KUMPATA MGOMBEA UDIWANI MISUGUSUGU

Na John Gagarini, Kibaha

RAMADHAN Bogas ameshinda kura za maoni za kumpata mgombea udiwani kata ya Misugusugu kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) baada ya kupata kura 43 huku aliyeshinda udiwani kabla ya mahakama kutengua matokeo Addhu Mkomambo akiambulia kura mbili.

Uchaguzi huo ambao ulifanyika Misugusugu ulisimamiwa na Yusuph Mbonde, Selina Wilson na Mohamed Mpaki ambao ni wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM wilaya, ulihusisha wagombea saba.

Akizungumza na waandishi wa habari katibu wa CCM Kibaha Mjini Abdala Mdimu alisema kuwa kura zilizopigwa zilikuwa 115 na hakuna kura iliyoharibika.
Mdimu akitaja matokeo alisema kuwa mshindi wa pili alikuwa Eliasi Masenga aliyepata kura 37, Ramadhan Mataula aliyepata kura 15 huku Salumu Mkali akipata kura 14, huku watano akiwa Mkomambo aliyepata kura mbili, Francis Alinamiswe alipata kura mbili na Laurence Likuda naye kura mbili.

Alisema kuwa bado vikao mapendekezo vinaendelea kukaa ambapo jana kilitarajiwa kukaa kikao cha kamati ya siasa ya kata ambapo leo kikao cha kamati ya Usalama na maadili wilaya kinakaa.

“Desemba 16 kamati ya siasa ya wilaya itakaa na baadaye vitaendelea vikao vya mkoa na Desemba 19 Halmashauri Kuu ya mkoa itafanya uteuzi wa mwisho wa mgombea atakayekiwakilisha chama kwenye uchaguzi huo,”alisema Mdimu.

Uchaguzi huo mdogo wa udiwani unarudiwa baada ya mahakama ya mkoa kutengua matokeo kutokana na malalamiko yaliyotolewa na diwani wa Chadema ambapo mgombea wa CCM Addhu Mkomambo alikuwa ameshinda.

Mwisho.