Tuesday, June 23, 2026

PWANI YAKUSANYA BILIONI 266

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Pwani imefanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 266 katika kipindi cha miaka 10 iliyopita na kuvuka malengo yaliyowekwa ya kukusanya shilingi bilioni 235 katika kipindi hicho.

 

Akizungumza kwenye Kongamano la Mamlaka hiyo ya kutimiza miaka 30 tangu kuanzishwa kwake Meneja wa TRA Mkoa wa Pwani Peter Jackson alisema kuwa mafanikio hayo ni ongezeko la asilimia 113 ya makusanyo kwa kipindi hicho.

 

Jackson alisema kuwa mafanikio hayo yametokana na ushirikiano ulioonyeshwa na wafanyabiashara na wadau wote wa kodi ambapo katika kipindi hicho malaengo ya makusanyo yalikuwa ni bilioni 23 lakini zilikusanywa kiasi cha shilingi bilioni 27.

 

“Kwa wastani makusanyo kwa kipindi cha miaka 10 ni ongezeko la asilimia 10 ambapo yamekuwa yakiongezeka hadi kufikia kiasi hicho na kuonyesha jinsi gani mamlaka hiyo inavyopiga hatua katika kuleta maendeleo ya nchi,”alisema Jackson.

 

Alisema kuwa makusanyo yana faida kubwa kwani yanatumika kwa ajili ya kufanya shughuli za kimaendeleo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa miundombinu ikiwemo ya barabara ujenzi wa reli ya kisasa SGR huduma za afya, huduma za elimu na masuala mbalimbali.

 

Aidha alisema kuwa ukusanyaji wa mapato makubwa ndiyo njia ya kukuza uchumi wa nchi ambapo walipa kodi wanapaswa kulipa kwa hiyari na kwa wakati ili kuondoa changamoto za kupewa adhabu ambayo inawarudisha nyuma.

 

“Kwa sasa tumeweka mifumo madhubuti ya ukusanyaji na namna ya kuwafikia kwa urahisi walipa kodi na kuwaondolea usumbufu wa kufika ofisini badala yake wanauwezo wa kulipa au kufanya shughuli zote wakiwa maeneo yao jambo ambalo limerahisisha utendaji kazi,”alisema Jackson.

 

Akizungumzia kuhusu changamoto alisema kuwa ukuaji wa uchumi usio rasmi umekuwa ni tatizo kwani unakuwa nje ya mfumo rasmi hivyo kusababisha kukosekana kwa mapato kutokana na kukwepa au kupunguza kodi kuongezeka kwa biashara mtandaoni biashara haramu na za magendo ambazo huathiri ushindani wa kibiashara..

 

Kwa upande wake mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT) Mkoa wa Pwani Abdala Ndauka alisema kuwa baadhi ya wafanyabiashara hawana uelewa juu ya masuala ya ulipaji kodi hivyo kuna haja ya kutolewa elimu ya kutosha.

 

Ndauka alisema kuwa ulipaji kodi unapaswa kuwa rafiki na si kama adhabu bali uwe rafiki hata hivyo malalamiko kwa sasa yamepungua kwani kwa sasa kumekuwa na majadiliano juu ya changamoto zinazowakumba walipa kodi na watengeneze walipa kodi wapya.

 

Mwenyekiti wa Chemba ya wafanyabiashara Mkoa wa Pwani Said Mfinanga alisema kuwa matumizi ya teknolojia yamesaidia kuwapunguzia muda walipa kodi kwenda ofisini ili kufanya kufanya taratibu mbalimbali juu ya masuala ya ya biashara zao.

 

Mfinanga alisema kuwa mfumo wa teknolojia pia utumike kutoa elimu juu ya masuala ya ulipaji kodi na taratibu zote zihusikanazo na masula ya kodi ili kujenga uelewa wa pamoja kwa walipa kodi na mamlaka hiyo ambayo inajuhusisha na ukusanyaji wa mapato ya serikali.   

 

Naye mwenyekiti wa Shirikisho la Umoja wa Machinga (SHIUMA) Mkoa wa Pwani Philemon Maliga alisema kuwa ili kuboresha ukusanyaji wa mapato Mamlaka inapaswa kuwa na mahusiano bora na mazuri na walipakodi kwnai kundi lao ni kubwa na lina uwezo wa kuchangia pato la serikali.

 

Maliga alisema kuwa TRA iatoe limu kuanzia mashuleni na sehemu mbalimbali ili kuwajengea walipa kodi utamaduni wa kulipa mapato ili kuonyesha uzalendo wa nchi yao kwani kodi ndiyo msingi mkubwa wa maendeleo.

 

Monday, June 15, 2026

TAARIFA KWA UMMA


Ofisi ya Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, inapinga na kukanusha vikali taarifa ya uongo na upotoshaji inayosambaa mitandaoni, ikidai kuwa Dkt. Kikwete anahusishwa na mradi unaodaiwa kuwa wa uwekezaji unaowaahidi Watanzania kipato cha uhakika kupitia jukwaa la kifedha linalotumia teknolojia ya akili mnemba

Taarifa hiyo inadai kuwa maelfu ya Watanzania tayari wamenufaika na mradi huo baada ya kuwekeza kiasi cha shilingi 653,000, huku wakiahidiwa kupata zaidi ya shilingi 9,200,000 kwa mwezi. Madai hayo si ya kweli hata kidogo.

Ofisi ya Rais Mstaafu inapenda kuweka wazi kwamba Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete hajawahi kushiriki, kuidhinisha, kutangaza, kuunga mkono, wala kuhusika kwa namna yoyote ile na mpango huo wa kifedha. 

Ofisi yake haijawahi kuruhusu matumizi ya jina, picha, au heshima yake kuhusishwa na mradi huo unaodaiwa, na haitajihusisha na shughuli za aina hiyo.

Wananchi wanashauriwa kupuuza taarifa hiyo ya uongo na kuwa makini dhidi ya miradi ya kitapeli na vitendo haramu vya aina hiyo. 

Mtu yeyote atakayekutana na taarifa kama hizo za upotoshaji anapaswa kuzichukulia kama habari za uongo, kuepuka kuzisambaza, kujisajili, au kutuma fedha kwa mtu au jukwaa lolote linalohusishwa nazo.

Sunday, June 14, 2026

PWANI YAENDELEA KUHAMASISHA UCHANGIAJI DAMU KUOKOA MAISHA YA WATU

MKOA wa Pwani umekusanya jumla ya chupa za damu 1,129 kwa ajili ya Hospitali na Vituo vya Afya.

Hayo yamesemwa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani Kusirye Ukio wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Mchangiaji Damu wa Dunia kimkoa ambapo maadhimisho hayo yamefanyika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani Tumbi.

Kwa upande wake Msimamizi wa Huduma kwa Mteja na Wachangiaji Damu Salama Makao Makuu Kaito Tamba amesema kuwa kwa sasa mpango ni kukusanya chupa 600,000 kwa mwaka 

Akisoma risala ya siku hiyo Mkuu wa Idara ya Maabara Hospitali ya Tumbi Simon Lupatu amesema kuwa kauli mbiu ya mwaka huu inasema "Changia Damu Okoa Maisha" ambapo wanahitaji mashine kwa ajili ya uzalishaji mazao ya damu.

Naye Mkuu wa Idara ya Kinamama na Uzazi wa Hospitali ya Tumbi Dk Alfonce Moyo amesema kuwa takwimu zinaonyesha vifo vilivyotokea kwa mwezi Januari hadi Juni mwaka huu asilimia 80 vilitokana na kupoteza damu nyingi.

Saturday, June 13, 2026

*SERIKALI YADHAMIRIA KUWAENDELEZA WACHIMBAJI WADOGO NCHINI*

▪️Taarifa ya mapendekezo ya kuwaendeleza Wachimbaji wadogo yawasilishwa

▪️Prof Mkumbo aeleza umuhimu wa sekta ya madini kufikia Dira 2050

Lengo ni Kuongeza Ajira, Kupunguza Umaskini na Kukuza Uchumi

▪️Mfuko wa Dhamana  kutatua changamoto ya mitaji kwa wachimbaji

▪️Serikali yaanzisha mfuko wa Madini kwa ajili ya Utafiti wa Madini

📍 Dar Es Salaam

Serikali imesisitiza kufanyia kazi kwa haraka Mapendekezo yaliyotolewa na Timu ya Wataalamu iliyoundwa Kuishauri Wizara ya Madini kuhusu namna ya Kuwaendeleza Wachimbaji Wadogo Kiuchumi na kueleza kuwa, utatuzi wa changamoto za Mitaji, Teknolojia na upatikanaji wa taarifa sahihi za Kijiolojia kwa Wachimbaji Wadogo wa Madini ni hatua muhimu ya kuongeza ajira kwa watanzania, kupunguza umaskini na kukuza uchumi wa Taifa kuelekea Dira 2050.

Hayo yamebainishwa Juni 13, 2026 jijini Dar Es Salaam  na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, wakati wa hafla ya Kupokea Mapendekezo ya Kuwaendeleza Wachimbaji Wadogo Nchini na kusisitiza kwamba, maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha mipango ya maendeleo inajibu changamoto tatu kuu za taifa ambazo ni kuongeza mitaji kwa wananchi, kuzalisha ajira na kupunguza umaskini.

Amesema kuwawezesha wachimbaji wadogo kupata mitaji na teknolojia, kunafungua fursa za kuongeza uzalishaji, ajira na kipato cha wananchi na kuongeza kuwa hiyo ndiyo njia mojawapo ya kupambana na umaskini.

‘’Kazi kubwa ya Waziri ni kutoa mwelekeo wa kisera wa taasisi au wizara anayoiongoza. Kwa muda niliokaa kwenye Wizara yangu, Mhe. Mavunde amekua akijua kipaumbele anachokitaka na jinsi ya kukipata,’’amesisitiza Prof. Mkumbo.

Ameongeza kwamba, hali ya umaskini nchini  bado ipo kwa kiwango cha juu na kutolea mfano wa Mkoa wa Geita ambao unaoongoza kwa shughuli za uchimbaji madini ya dhahabu nchini ambapo  hali ya umaskini inafikia asilimia 38 na kusisitiza kwamba, wachimbaji wadogo wanapowezeshwa wanasaida kutatua changamoto kama hizo na kuongeza kuwa, Sekta ya Madini imewekwa kama moja ya sekta muhimu za kimageuzi  inayotarajiwa kuchangia kwenye ukuaji wa uchumi na ajira ambapo awali haikuwa ikibeba watu wengi.

Naye, Waziri wa Madini Anthony Mavunde akizungumza katika halfa hiyo, amesema Serikali iliamua kuunda kamati hiyo kutokana na mchango mkubwa unaotolewa na wachimbaji wadogo katika Sekta ya Madini, licha ya kukabiliwa na changamoto za mitaji, teknolojia na upatikanaji wa huduma za kifedha , hivi sasa wanachangia asilimia 40 ya makusnyo ya maduhuli ya Serikali.

Ameongeza kwamba, kuwa mafanikio makubwa yaliyopatikana katika Sekta ya Madini ndani ya miaka ya hivi karibuni yanaonyesha umuhimu wa kuwawezesha zaidi wachimbaji wadogo ili waongeze mchango wao katika uchumi wa taifa.

Kwa mujibu wa Waziri Mavunde, Mwaka wa Fedha  2015/16 Sekta ya Madini katika mwaka mmoja iliingiza shilingi bilioni 161 pekee katika Mfuko Mkuu wa Serikali. 

Hata hivyo, kufuatia mageuzi mbalimbali yaliyofanyika ikiwemo mabadiliko ya sheria, kuanzishwa kwa masoko ya madini na udhibiti wa biashara haramu ya madini, makusanyo yameongezeka kwa kiwango kikubwa kufikia Shilingi trilioni 1.107 mwaka 204/25 na mpaka kufikia  tarehe 13, Juni, tayari Serikali imekusanya shilingi trilioni 1.3.

Amesisitiza kuwa jukumu la Serikali yoyote duniani ni kuwawezesha wananchi wake kufanya shughuli za uzalishaji kwa tija zaidi sababu ambayo ilipelekea  Serikali kuweka mkakati maalum wa kuwawezesha wachimbaji wadogo ili waweze kukua na kuwa wachimbaji wa kati na baadaye wakubwa.

Kuhusu changamoto ya mitaji, Waziri Mavunde  amesema Serikali imeanza utekelezaji wa Kampuni ya dhamana ya mikopo (Credit Guarantee Corporation) itakayosaidia  wachimbaji kupata mikopo kutoka taasisi za fedha mbalimbali.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati hiyo  Dkt. Victor Tesha  amesema suluhu ya changamoto hizo ni kujenga mfumo jumuishi wa kuwawezesha wachimbaji wadogo kupitia upatikanaji wa mitaji, teknolojia za kisasa, taarifa za kijiolojia na uratibu wa taasisi zinazohusika na sekta hiyo huku akipendekeza kuanzishwa kwa Mfuko wa Madini Tanzania utakaowezesha miradi yenye sifa kupata fedha za kuendeleza uzalishaji, kununua mitambo na kuboresha shughuli za uchimbaji, na kuongeza kwamba, mfuko huo utasaidia kugharamia tafiti na taarifa za kijiolojia kwa wachimbaji.

Ameongeza kuwa, baada ya mfuko huo kukua na kuimarika, hatua itakayofuata itakuwa ni kuanzisha Benki ya Wachimbaji itakayotoa huduma maalumu za kifedha kwa sekta ya madini kwa masharti yanayoendana na mazingira ya wachimbaji.

‘’Kamati pia imependekeza mikopo ielekezwe zaidi katika ununuzi wa mitambo na teknolojia badala ya fedha taslimu pekee, ili kuongeza tija, uzalishaji na usalama katika shughuli za uchimbaji,’’ amesema Tesha.


 Naye, rais wa Shirikisho la Vyama Vya Wachimbaji Wadogo John Bina, ameipongeza Serikali kwa ripoti hiyo na kueleza imetokana  na Serikali kusikiliza na kuyafanyia kazi maoni na changamoto za wachimbaji wadogo, pamoja na kuipongeza kwa kutenga asilimia 10 ya mapato yanayotokana na shughuli za madini kwa ajili ya utafiti.

Wednesday, June 10, 2026

HALMASHAURI YA MANISPAA YA KIBAHA YATOA MIKOPO YA SHILINGI MILIONI 991.5 KWA VIKUNDI

HALMASHAURI ya Manispaa ya Kibaha Mkoani Pwani imetoa mikopo ya jumla ya shilingi milioni 991.5 kwa vikundi 51 vya ujasiriamali.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Dk Rogers Shemwelekwa wakati wa hafla ya utoaji mikopo ya robo ya tatu.

Shemwelekwa amesema kuwa fedha hizo kiasi cha shilingi milioni 359 ni kwa vikundi 17 vya wanawake shilingi milioni 557 kwa vikundi 25 vya Vijana.

"Kiasi cha shilingi milioni 75.5 kilitolewa kwa watu wenye ulemavu 17 ambapo fedha hizo zimetokana na asilimia 10 ya mapato ya Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha,"amesema Shemwelekwa.

Amesema kuwa miradi iliyokopeshwa kwa vikundi hivyo ni pamoja na mradi wa usafirishaji ambapo pikipiki 25 zimetolewa na TOYO moja, Bajaji nne, pia miradi ya ufugaji kuku, uchomeleaji ,ushonaji na hardware.

"Viwanda vidogo vya utengenezaji batiki, sabuni, kilimo cha umwagiliaji, kiwanda na stationery miradi hiyo yote inatokana na vikundi hivyo ambavyo ni vya wajasiriamali,"amesema Shemwelekwa.

Aidha amesema kuwa kwa mwaka wa fedha wa 2024/25 ambapo mikopo ilianza kutolewa mwezi Disemba 2024 kwa kanuni mpya hali ya urejeshaji kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu imefikia asilimia 52. 

"Pia mikopo ya mwaka huu wa 2025/26 ambayo imetolewa kuanzia mwezi Novemba 2025 marejesho yamefikia asilimia 26 ambapo inaashiria marejesho yapo vizuri,"amesema Shemwelekwa.

Kwa upande wake Mgeni rasmi Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka amesema kuwa kutolewa mikopo hiyo ni jitihada kubwa zinazofanywa katika ukusanyaji wa mapato.

Koka amesema kuwa Halmashauri imeendelea kuimarika kwenye upande wa mapato hali ambayo inaongeza utoaji wa mikopo kutokana na asilimia 10 ya mapato.

Naye Mwenyekiti wa Kikundi cha Lulu ya Wajane Kanyenda Mweri alisema kuwa fedha hizo zitawasaidia wao kama wajane kukuza mtaji wao wa ufugaji wa kuku.

Mweri alisema wanaishukuru Halmashauri na Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa kurejesha mikopo hiyo ya asilimia 10 baada ya kusitishwa  kwa muda na kuwekwa utaratibu mpya.

Tuesday, June 9, 2026

LULU YA WAJANE KUANZISHA MRADI WA MINOFU YA KUKU

KIKUNDI cha Lulu ya Wajane kilichopo Kongowe Wilayani Kibaha Mkoani Pwani kinatarajia kuanzisha mradi wa uuzaji wa minofu ya kuku.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa kikundi hicho Kanyenda Mweri wakati akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea kikundi hicho ambacho kinajihusisha na ufugaji wa kuku.

Mweri amesema kuwa kikundi chao kinaundwa na wanachama watano kiliwezeshwa na Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha mkopo wa asilimia 10 kiasi cha shilingi milioni 46 ambapo tayari wameshazirejesha.

"Tumeomba mkopo mwingine wa fedha nyingi kidogo ambapo tutanunua mashine ya kuchakata minofu, mashine ya kunyonyolea kuku, mashine ya kutotolesha na kuuza vifaranga, mashine ya kusaga vyakula vya kuku na kufufua mashine ya kusaga unga,"amesema Mweri.

Amesema kuwa tayari wameshafanya utafiti juu ya soko la minofu ambapo mbali ya minofu watauza kuku na viungo vyake ikiwemo miguu, vichwa na vyote vitokanavyo na kuku.

"Uwezo wa kurejesha mkopo tutakaokopeshwa tunao kwani mkopo uliopita tulikopeshwa milioni 46 tukazirejesha mapema kabla ya muda kwani tulipewa miaka mitatu kurejesha lakini tulirejesha kwa miezi 11 tu na kupewa cheti cha wajasiriamali bora,"amesema Mweri.

Aidha amesema kuwa kutokana na mradi wa ufugaji kuku unaoendelea kila mwezi wanajilipa kiasi cha shilingi  100,000 pia wameweza kuwaajiri mabinti wa wawili ambao ni wahitimu wa vyuo wakiwa na diploma ya mifugo ambao ndiyo wanafanya shughuli za kitaalamu na kijana mmoja wa kiume.

"Tunamshukuru Mungu kwani ameweza kutuunganisha na kutupa mshikamano ambao ndiyo siri ya mafanikio yetu na ushirikiano tunaoupata kutoka kwa wataalamu wa Halmashauri na Mkurugenzi,"amesema Mweri..

Amesema kuwa walianzisha kikundi hicho kwa malengo ya kusaidiana kutatua changamoto na kutafuta fursa mbalimbali za ujasiriamali na kûwa na miradi ya kiuchumi endelevu kwani wanawake wanapofiwa na waume zao ndugu huwanyanyasa naa kuwanyanganya mali. 

"Matarajio yetu ni kuwa kikundi imara na hodari ambapo kwa sasa tayari wameanzisha kikundi cha vijana wanawake wanaojulikana kama Lulu Nazi wanaozalisha bidhaa zitokanazo na nazi,"amesema Mweri.

Ameongeza kuwa wanaiomba Halmashauri wawapatie mikopo kutokana na maombi kwani malengo wanakuwa wameshayaweka hivyo kuwakopesha chini ya walichoomba husababisha kufanya malengo yasifikiwe ya kile walichokiombea.

"Pia watoe mikopo kwa muda uliopangwa ambapo wao wanasubiri awamu ya pili tangu Desemba mwaka jana hadi leo bado hawajapata mkopo waliouomba ambapo gharama zinaongezeka za mahitaji mfano chakula cha kuku bei imeongezeka na mkopo hesabu zilizopigwa tayari zinakuwa chini,"amesema Mweri.

Amewataka wanawake wajane kutokata tamaa katika kupambania maisha yafamilia zao kwani wao ndiyo walezi wa familia na kulinda maadili ya watoto wao na kikundi hicho kilianzishwa mwaka 2022 na kimesajiliwa.

mwisho.







 



 

POLISI PWANI KUFANYA UCHUNGUZI KISAYANSI KUCHUNGUZA MADAI MZAZI KUBADILISHIWA MTOTO

JESHI la Polisi Mkoa wa Pwani linafanya uchunguzi wa kitaalamu na kisayansi ili kubaini ukweli juu ya lalamiko la mwanamke aitwaye Filomena Mataris (36) Mkazi wa Gongo la Mboto Dar es Salaam kudai kubadilishiwa mtoto baada ya kujifungua katika Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo.

Uchunguzi huo unafanyika baada ya mlalamikaji kudai kuambiwa mtoto wake aliyejifungua amefariki na kuzikwa pasipo yeye na mume wake kushiriki mazishi ya mtoto wake ambapo alizikwa na ndugu zake.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani Salim Morcase alisema kuwa Juni 5 mwaka huu Filomena Mataris akiwa na mume wake Caros Kapata walifika kituo cha Polisi Bagamoyo wakilalamika kubadilishiwa mtoto kwenye Hospitali ya Bagamoyo. 

Morcase alisema kuwa walipofika polisi walieleza kuwa Aprili 14 mwaka huu Filomena Mataris alihamia Kerege Wilayani Bagamoyo kwa mtoto wa dada yake aitwaye Avetha Mabadiliko kwa ajili ya uangalizi wa karibu akitokea Gongo la Mboto Dar es Salaam.

"Mnamo Mei 17 mwaka huu majira ya saa 3:000 asubuhi Mataris alipata uchungu wa kujifungua hivyo aliongozana na ndugu yake huyo Mabadiliko kwenda Hospitali ya Kerege kwa ajili ya kujifungua,"alisema Morcase.

Alisema kuwa baada ya kufika hospitalini hapo na kufanyiwa vipimo daktari alibaini Mataris ana dalili ya uzazi pingamizi hivyo alielekeza apelekwe Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji.

"Iipofika Mei 18 mwaka huu majira ya saa 8:00 usiku Mataris alihamishiwa Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo ambapo saa 8:30 usiku alijifungua mtoto wa kiume kwa njia ya upasuaji na alieleza kuwa alimuona mtoto wake na kumbeba akiwa mzima wa afya,"alisema Morcase.

Aidha alisema Mataris alisema kuwa baada ya kupewa huduma na kwenda wodini alioneshwa picha za mtoto kwenye simu ya daktari na kuambiwa ndiye mtoto wake na ameshafariki. 

"Mtoto aliyeonyeshwa kwenye picha alikuwa na changamoto kama vile kichwa kubonyea na kuwa na uvimbe kifuani tofauti na mtoto wake aliyembeba baada ya kujifungua,"alisema Morcase.

Aliongeza kuwa baada ya kuonyeshwa picha hizo aliambiwa na daktari kuwa mwili umekabidhiwa kwa ndugu zake ambao ni Mabadiliko na shangazi
yake aitwaye Adora Mathias kwa ajili ya mazishi. 

"Mtoto huyo alizikwa bila uwepo wa Mataris ambaye ni mama wa mtoto wala baba wa
mtoto hakufahamishwa kuhusu mazishi hayo na mara baada ya kupata taarifa hiyo kutoka kwa familia hiyo Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani lilifungua jalada la uchunguzi lenye
namba BAG/PE/33/2026,"alisema Morcase.

Aliongeza kuwa Polisi walianza ufuatiliaji ulianza ambapo walimhoji Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo Dk. Mariam Ngwele aliyeeleza kuwa baada ya kumpokea Mataris.

Alisema kuwa Dk Ngwele alieleza kuwa Mataris  alijifungua kwa njia ya upasuaji lakini mtoto hakuwa wa kawaida kwani alikuwa na kichwa kilichobonyea na uvimbe sehemu ya kifuani na changamoto ya upumuaji hivyo alifariki muda mfupi baada ya kuzaliwa.

Kamanda Morcase alisema kuwa kutokana na changamoto hiyo Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani linaendelea na uchunguzi zaidi wa kitaalamu
na kisayansi ili kubaini ukweli wa taarifa hiyo.