Friday, July 7, 2023

SENYAMULE AAGIZA WAZEMBE KUCHUKULIWA HATUA ZA KISHERIA


MKUU wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule ametaka hatua kali za kisheria zichukuliwe kwa watumishi wote ambao wamebainika kuhusika na vitendo vya ubadhirifu wa rasilimali au fedha za umma na kusababisha hoja za ukaguzi kwa uzembe.

 Akizungumza katika Kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino Senyamule amekemea vikali tabia ya baadhi ya watumishi kutotimiza majukumu na wajibu wao wa msingi kwa makusudi hali inayopelekea kukithiri kwa hoja za ukaguzi zisizokuwa na majibu.

 "Kila mmoja atimize wajibu wake, hoja nyingi hapa zinatokana na uzembe wa baadhi ya watumishi kutotimiza majukumu yao kwa mujibu wa Sheria, wanashindwa kuambatisha nyaraka za msingi zinazohitajika hali inayopelekea kukithiri wa hoja za ukaguzi. Senyamule ameonya.

Amesema ili Halmashauri hiyo kuondokana na hoja nyingi ni lazima Kamati ya Fedha kukutana kila mwezi na kuwa na agenda ya kudumu ya kujadili mwenendo wa namna ya kujibu hoja za Mkaguzi wa ndani na zile za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na kuchukua hatua stahiki pale inapobainika uzembe wa aina yoyote.

Senyamule pia, ametoa rai kwa madiwani hao kuhakikisha kuwa fedha zinapelekwa kutekeleza miradi ya maendeleo kwa kuzingatia mgawanyo wa asilimia 40 na asilimia 10 kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kwa mujibu wa Sheria. Pia amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Chamwino Dkt. Semistatus Mashimba kuhakikisha mapato ya Serikali yanakusanywa kikamilifu na kudhibiti upotevu.

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mapendekezo ya mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha 2021/2022  kwa Halmashauri ya Chamwino, Bw. Chambi Ngelela Mkaguzi Mkuu wa Nje amesema Halmashauri hiyo ilipata hati inayoridhisha. 

"Halmashauri  ya Wilaya ya Chamwino ilikuwa na hoja 61 ambapo hoja 13 zimeweza kufungwa na kusalia na hoja 48 ambazo utekelezaji wake unaendelea." Amesema Bw. Ngelela.

Aidha Senyamule katika hatua nyingine amewataka Viongozi hao wa ngazi ya Wilaya kuendelea kutunza Mazingira na kuanza maandalizi ya kuoteshea vitalu vya miche ya miti kwa ajili ya  kupanda wakati wa msimu wa mvua unapokaribia ili kuwe na miche ya kutosha kwa kila Halmashauri kupanda miti milioni moja na laki tano kwa mwaka kwa mujibu wa maelekezo ya Serikali.

"Katika kuendelea kukijanisha Mkoa wetu na kutunza Mazingira tuanze mapema maandalizi ya kuandaa vitalu vya miche na kila wilaya iwe na Miche ya kutosha isiyopungua milioni moja na laki tano,"amesema Senyamule 

"Hapa nisisitize kuwa katika kila wilaya nitakayofanya ziara kuanzia mwezi wa nane nitakagua vitalu hivyo vilevile hakikisheni mnatenga maeneo kwa ajili ya kunufaika na biashara ya hewa Ukaa na kila Wilaya angalau iwe na maeneo matatu kama tulivyokubaliana hapo awali". Amesisitiza  Senyamule

Thursday, July 6, 2023

"ELIMISHENI WANAWAKE JUU YA FURSA ZA MIKOPO YA HALMASHAURI" MHE. MASANJA

Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mwanza na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary  Masanja amewataka wana Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Mkoani Mwanza kuelimisha wanawake na vijana kuhusu fursa za mikopo ya Halmashauri ili waweze kujiinua kiuchumi. 

Mhe. Masanja ameyasema hayo jana katika Kikao cha Baraza la UWT Wilaya ya Nyamagana kilichofanyika katika Ofisi za CCM jijini Mwanza.

"Niwaombe wakinamama turudi chini tuwaelimishe wanawake wengine kuhusu mikopo hii ya Halmashauri na kuwasimamia kutekeleza miradi yao ili wajiinue kiuchumi" Mhe. Masanja alisisitiza. 

Aidha, Mhe. Masanja amewataka wakinamama wa UWT  kuhakikisha wanatoa elimu kwa wananchi juu ya mafanikio ya Serikali kuhusu Utekelezaji wa Miradi mbalimbali ili kuhakikisha Chama kinapata ushindi katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaokuja. 

"Sasa tunaenda kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa tusilale wakinamama sisi ni wenye kura sisi ndio wa kuzitafuta kura usiku na mchana kuhakikisha chama chetu kinaibuka kinara" Mhe. Masanja ameongeza.

Amesema ni lazima kutembea kifua mbele kutokana  na miradi iliyotekelezwa na Rais Samia Suluhu Hassan na kusisitiza kwamba anastahili kupewa maua yake.

Katika kuunga mkono juhudi za Rais Samia za kutangaza utalii,Mhe. Masanja wajumbe wataanza kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii hapa nchini.

Mhe. Masanja anaendelea na ziara yake jijini Mwanza kwa ajili  ya kukutana na makundi mbalimbali ya kijamii yenye uhitaji maalum  ambayo yanajihusisha na biashara mbalimbali.

WIZARA YA MALIASILI NA UTALII YAZIDI KUJIZATITI KUTOA ELIMU YA UHIFADHI KWA JAMII

Wizara ya Maliasili na Utalii inaendelea na jitihada za kuelimisha jamii ikiwa ni pamoja na kutembelea Ofisi za Vyama katika kila Mkoa na kuelezea juu ya umuhimu wa uhifadhi na utunzaji wa rasilimali za Taifa pamoja na fursa zitokanazo na Sekta ya Maliasili na Utalii kwa lengo la kukuza uchumi kwa wananchi. 

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) ameyasema hayo leo katika mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa uliofanyika leo  jijini Mwanza.

"Moja ya maelekezo tuliyoyapata kutoka kwa Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Mohamed Mchengerwa ni wahifadhi kushuka kwenda kila mkoa kuzungumza na chama kuelezea fursa zilizopo katika maeneo yote ya hifadhi tunayoyasimamia na changamoto tunazozipata" Mhe. Masanja amesema.

Amefafanua kuwa lengo la uelimishaji huo ni kuelezea shughuli zinazofanywa na Taasisi za Uhifadhi, kufafanua kuhusu namna ya kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika maeneo ya  pamoja na namna ya kutumia fursa mbalimbali za uwekezaji katika Utalii.

Amesema endapo elimu ya uhifadhi na fursa za utalii ikielezewa kwa ufasaha vijana wataweza kujiajiri wenyewe na hivyo  kuchangia  uchumi wao binafsi na wa Taifa kwa ujumla. 

Amezitaja mojawapo ya  fursa zilizopo kuwa ni pamoja na upandaji miti na uanzishwaji wa mashamba ya miti ambapo Wakala ya Huduma za Misitu Tanzania ( TFS)  imekuwa ikigawa miche hiyo  ya miti kwa watu binafsi.

Amesema kupitia shughuli za upandaji miti wananchi wanaweza kujiongezea kipato na pia kuchangia kwenye uchumi wa Taifa.

WAZIRI KAIRUKI AKABIDHI MAGARI 43 KWA TARURA NA MAKATIBU TAWALA MIUNDOMBINU.

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Mhe. Angellah Kairuki amekabidhi magari 43 kwa Watendaji wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) katika ngazi ya Makao Makuu, Mikoa na Makatibu Tawala Wasaidizi wanaoshughulika na Miuondombinu katika ngazi za Mikoa.

Makabidhiano hayo yamefanyika Julai 05, 2023 Makao Makuu ya TARURA - Mtumba Dodoma kwa watendaji hao kwa ajili ya kuwawezesha kuboresha utendaji kazi wao.

Waziri Kairuki amesema magari 30 kati ya 43 ni kwa ajili ya matumizi ya Ofisi za Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) makao makuu na mikoa na magari 13 ni kwa ajili ya ofisi za wakuu wa mikoa kwa ajili ya usimamizi wa kazi za miundombinu.

Amesema lengo kuu kukabidhi magari haya kwa TARURA na mikoa ni kuwawezesha kuboresha utendaji kazi, hususan katika utekelezaji wa majukumu ya usimamizi wa ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya barabara." 

“Serikali ya Awamu ya Sita katika kuendelea kuhakikisha kuwa inatoa huduma bora kwa wananchi, imeendelea kuwezesha taasisi za umma, hususan Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini, kwa kuwapatia fedha kwa ajili ya ununuzi wa magari ili kuimarisha utendaji kazi na usimamizi wa miradi”

Aidha, Waziri Kairuki amesema hadi sasa wakala imefanya manunuzi ya magari 270, ambapo magari hayo yamekuwa yakiwasili kwa vipindi tofauti, na kukabidhiwa kwa wahusika na hivyo kufanya magari yaliyokabidhiwa kuwa 241, tangu wakala ulipoanza ununuzi wa magari Julai 2017 hadi Juni 2023.

Amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuwezesha wananchi kuwa kitovu cha maendeleo na kuimarisha ubia baina ya wananchi na Serikali.

“magari haya yatasaidia kurahisisha huduma ya usafiri kwa watendaji wa TARURA na makatibu tawala wasaidizi sehemu ya miundombinu katika kusimamia, kuratibu na kufuatilia shughuli ujenzi  katika mikoa” amesema Waziri Kairuki

Kadhalika, Waziri Kairuki amesema magari hayo yatagawiwa kwenye Ofisi za TARURA na Ofisi za Sekretatieti za Mikoa zenye changamoto na uhitaji zaidi wa magari kwa sasa, na zenye maeneo makubwa ya kusimamia. 

Amesema Sekretarieti za mikoa zitakazopata magari awamu hii ni Mtwara, Ruvuma, Mbeya, Songwe, Rukwa, Katavi, Kigoma, Kagera, Mara, Lindi, Dodoma, Tabora na Tanga. 

Ameagiza magari yatumike kwa kuzingatia miongozo na taratibu za Serikali, ili yalete tija katika kuboresha huduma kwa wananchi ikiwemo kuongeza ushiriki wa wananchi katika shughuli za kijamii na kiuchumi, kutokana na kuwa na miundombinu bora, na sio kutumika katika matumizi binafsi kinyume na taratibu.

𝗪𝗔𝗭𝗜𝗥𝗜 𝗕𝗔𝗦𝗛𝗘 𝗔𝗭𝗜𝗡𝗗𝗨𝗔 𝗠𝗙𝗨𝗠𝗢 𝗪𝗔 𝗨𝗦𝗜𝗠𝗔𝗠𝗜𝗭𝗜 𝗪𝗔 𝗩𝗬𝗔𝗠𝗔 𝗩𝗬𝗔 𝗨𝗦𝗛𝗜𝗥𝗜𝗞𝗔 (𝗠𝗨𝗩𝗨)

Waziri wa Kilimo Mhe.Hussein Bashe, amezindua Mfumo wa kielektroniki wa Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (MUVU) unaowezesha na kurahisisha uhamasishaji, usimamizi na uendeshaji wa Vyama vya Ushirika kidijitali.

Uzinduzi huo ulifanyika hivi karibuni wakati wa kilele cha maadhisho ya siku ya ushirika duniani yaliyofanyika katika viwanja vya Nanenane Ipuli Mjini Tabora, na kushuhudiwa na viongozi mbalimbali wa serikali, wananchi pamoja na waandishi wa habari.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mhe.Bashe alisema mfumo wa MUVU utasaidia kutatua changamoto mbalimbali zilizokuwa zikiikabili sekta ya Ushirika kwa muda mrefu ikiwemo changamoto ya soko la mazao ya wakulima.

“Kupitia mfumo huu, wakulima hawatadhulumiwa tena mazao yao kwakuwa mkulima atapata taarifa ya kila hatua kupitia simu yake ya kiganjani na kumuwezesha kujua masoko ya mazao yake”, alisema Mhe.Bashe. 

Vilevile, Mhe.Bashe aliipongeza Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kwa kushirikiana kikamilifu na Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC) katika kujenga na kusanifu mfumo huo kuanzia hatua ya awali mpaka kukamilika pamoja na usimamizi wa mfumo huo.

Aidha, alisisitiza mfumo huo kutumika katika mazao yote ikiwemo  zao la pamba na tumbaku na kuitaka e-GA kuhakikisha mfumo huo unawasiliana na  mfumo wa kusajili wakulima wa nchi nzima, sambamba na kuwa na mfumo mmoja ambao utamsajili mkulima na kuonesha miamala yake ya kila siku.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu e-GA, Mkurugenzi wa Huduma za TEHAMA e-GA, Bw. Ricco Boma alisema katika mwaka wa fedha 2023/24 e-GA imejipanga kujenga Mfumo mkuu wa sekta ya kilimo wenye dirisha moja tu kwa Mkulima, msambazaji wa pembejeo na mfanyabishara wa Kilimo yaani ‘Agriculture Single Window’, mifumo mingine itakuwa ni mifumo saidizi yaani ‘backend supporting systems’ itakayokuwa inazungumza na mfumo mkuu wa Kilimo.

‘’Mfumo huu utakuwa umebeba mnyororo mzima wa thamani wa kilimo, hivyo basi ninaomba kutoa wito kwa wadau wa sekta ya kilimo kuunga mkono juhudi hizi  na kutoa ushirikiano ili Mamlaka ya Serikali Mtandao iweze kutekeleza agizo la Mhe Rais na Sheria ya Serikali Mtandao inayoitaka Mamlaka kutengeneza mifumo michache inayowasiliana’’ Alisema Bw.Ricco

Naye Mrajisi wa Vyama vya Ushirika Tanzania Dkt. Benson Ndiege, alisema zoezi la utengenezaji wa mfumo limekamilika na tayari vyama vya ushirika vinaendelea na usajili, na kuanzia sasa vyama vyote vya Ushirika vitahitajika kutoa taarifa zake kupitia mfumo wa MUVU.

WAZIRI MKUU AWATAKA MADAS KUZINGATIA MIIKO NA MAADILI YA UONGOZI WA UMMA.

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Makatibu Tawala wa Wilaya zote Tanzania Bara watekeleze majukumu yao kwa kuzingatia utawala bora, miiko na maadili ya viongozi wa umma.

“Kila mmoja akazingatie utumishi wa umma unaongozwa kwa misingi ya sheria, kanuni, taratibu na miongozo mbalimbali ya Serikali. Misingi hiyo, ndio chachu ya ujenzi wa taswira nzuri ya Serikali ya Awamu ya Sita.”

Ametoa maagizo hayo leo (Jumanne, Julai 04, 2023) wakati akifungua semina elekezi kwa Makatibu Tawala wa Wilaya katika ukumbi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Dodoma.

Pia, Waziri Mkuu amewasisitiza viongozi hao wahakikishe wanadhibiti matumizi mabaya ya fedha za umma katika maeneo yao na wanapobaini kuwepo kwa ubadhirifu wasisite kuchukua hatua.

Waziri Mkuu amesema ili viongozi hao waweze kutekeleza  majukumu yao ipasavyo wanatakiwa waweke mikakati namba ambavyo wilaya zao ya  zitakavyoweza wilaya kubeba na kusimamia vizuri ajenda za kitaifa.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene amesema lengo ya mafunzo hayo ni kuwaongezea weledi viongozi hao ili kuimarisha utawala bora.

Naye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, Angela Kairuki amewataka viongozi hao watimize majukumu yao ipasavyo na wahakikishe wanasimamia utekelezaji wa maagizo ya viongozi katika maeneo yao ya kazi.

Awali, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete alitoa wito kwa  viongozi hao wahakikishe mafunzo wanayopatiwa wanakwenda kuyafanyia kazi katika maeneo yao.

Mafunzo hayo ya siku tatu yameandaliwa na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa kushirikiana na Taasisi ya Ungozi yamehusisha Makatibu Tawala wa Wilaya 135 za Tanzania Bara.

Tuesday, July 4, 2023

WAKAZI WA DODOMA WATAKIWA KUJITOKEZA KWA WINGI MAONYESHO YA MIAKA 60 YA JKT


Wakazi wa Mkoa wa Dodoma na Mikoa ya jirani wametakiwa  kujitokeza kwa wingi katika maonyesho ya Jeshi la kujenga Taifa (JKT) yanayoendelea katika viwanja vya Jengo la SUMA JKT Medeli Mashariki ikiwa ni wiki ya maadhimisho ya miaka 60 tangu kuanzishwa  kwake.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule leo  Julai 4, 2023 wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Jengo la Mkapa Jijini Dodoma. 

Mhe. Senyamule amesema kuwa Maonyesho hayo  yameanza  Julai 1 hadi 9 ndio itakuwa ni kilele chake na yanatarajiwa  kufanyika katika viwanja vya Jamhuri Mkoani Dodoma.

"Niko hapa kutoa rai kwa wakazi wa Dodoma na watanzania wa mikoa ya jirani kutenga muda wao kutembelea maonesho hayo kwa lengo la kujifunza mambo mbalimbali yaliyofanywa na Jeshi letu”, amesisitiza Mhe. Senyamule

Vile vile amesema katika maonyesho hayo kuna teknolojia mbalimbali kuhusu masuala ya kilimo, uvuvi, useremala na kadha wa kadha.

Aidha, Mhe. Senyamule ametoa wito kwa vijana kujitokeza kwa wingi kushiriki maonyesho hayo ili kupata fursa mbalimbali zilizopo katika maonyesho hayo. 

"Ni fursa kubwa sana kwa jamii  hususan vijana kutembelea eneo hilo la maonesho kwa lengo la kujifunza namna ya kujiajiri kwa kutumia fursa zilizopo hapa nchini" amebainisha Mhe. Senyamule 

Hata hivyo,   ameendelea kutoa wito kwa wananchi wote kwa ujumla wa Mkoa huo kujitokeza kwa wingi siku ya kilele ya maadhimisho hayo katika  Viwanja vya Jamhuri na kusisitiza kuwa viwanja vitakuwa wazi kuanzia saa 12 asubuhi.