Monday, July 3, 2023

WAZIRI DKT. GWAJIMA ASEMA JUMUIYA ZA WANAWAKE ZINA NAFASI KUTOKOMEZA UKATILI.




WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amefungua Warsha ya Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA) ambapo ametoa wito kwa taasisi hiyo kushirikiana na Serikali katika kuwainua wanawake kiuchumi na  kutokomeza ukatili wa kijinsia katika jamii.

Dkt. Gwajima ameyasema hayo, Julai 03, 2023 wakati akifungua warsha ya Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani (WUCWO) ukumbi wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) Dar es Salaam ambapo wajumbe kutoka nchi mbalimbali za Afrika wameshiriki ufunguzi huo.

"Warsha hii imelenga kukuza usawa wa kijinsia na kutokomeza ukatili na unyanyasaji kwa wanawake na inawapa nafasi kubwa ya kujifunza na kushirikishana mbinu za kukabiliana na changamoto hizo kwa kuwa na sauti ya pamoja.

"Jambo hili ni jema kwani siku zote umoja unaleta matunda chanya na ya haraka zaidi." amesema Dkt. Gwajima.

Dkt. Dorothy Gwajima ameongeza kuwa,  amefarijika kwakuwa WAWATA pia ina lengo la kumfanya mwanamke ajitambue kuwa yeye ni muhimu ndani ya Jamii na maendeleo ya kiroho na kimwili.

Kwa upande wake Rais wa  Umoja wa Wanawake Wakatoliki Afrika, World Union of Catholic Women Organization (WUCWO) na Mwenyekiti wa WAWATA, Eveline Ntenga amesema, kwenye vipaumbele nane vya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa bajeti ya mwaka 2023/24 vipo vipaumbele viwili vinavyoendana na Mradi wa World Women Observatory (WWO) ambavyo ni kuratibu hatua za kukuza usawa wa kijinsia, uwezeshaji wanawake kiuchumi na kiungozi, kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake, Watoto na wazee na kuratibu utoaji wa huduma za msingi kwa watu wenye mahitaji maalum.

Aidha Eveline ameiomba Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii kuweka mkazo juu ya suala la kuwataka wazazi waone umuhimu wa watoto wa kike kupata elimu kwanza badala ya kufikiria kuwaozesha mapema.

Aidha Rais huyo ameiomba Wizara iwasaidie kuendelea kuweka utaratibu sahihi na wa haraka kuanzia ngazi ya Msingi  ili kufikisha taarifa za unyanyasaji na ukatili zinazofanywa na jamii kwa makundi yote katika vyombo husika.

“Tunaomba zichukuliwe hatua kali na kwa haraka kwa wale wote wanaohusika na vitendo vya ukatili kwa makundi yote “ amesema Bi. Aveline. 

Kwa upande wake Katibu Mkuu Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) Pd. Dkt. Charles Kitima, amesema katika kufikia maendeleo halisi kama ilivyolengwa kwenye ajenda ya maendeleo ya Dunia (Suistainable Development Goals)  ya mwaka 2030, Kanisa linawaona  wamama kama watendaji wakuu, na wakishikwa mkono na kanisa na Serikali wanaweza wakaifanya Dunia kuwa imara. 

Dkt. Kitima amesema,  jina la Wizara  Wizara ya Maendeleo ya Jamii linasawidi  mambo mengi yanayohusu utu wa mwanadamu ambapo ndipo Mungu Muumba anatukuka, Utukufu wa Mungu uko katika Utu wa mwanadamu, kwani wizara inashughulikia mambo ya Watoto, makundi yaliyotengwa, na akina mama hii ni heshima kubwa kwamba Waziri wa Wizara hii ni mama.

MUNIS ACHAGULIWA MENYEKITI KIBAFA

CHAMA Cha Soka Wilaya ya Kibaha (KIBAFA) kimefanya uchaguzi wake Mkuu na kupata viongozi watakaokiongoza chama hicho kwa kipindi cha miaka minne ambapo Robert Munis amechaguliwa kuwa mwenyekiti.

Munis alishinda uchaguzi huo uliofanyika Mjini Kibaha ambapo hakuwa na mpinzani, kwa kupata kura 30 na kura moja ya hapana kati ya wapiga kura 31.

Nafasi ya makamu mwenyekiti ilichukuliwa na David Mramba aliyepata kura 27 nafasi ya katibu ilikwenda kwa Daud Mhina aliyepata kura 29 na katibu msaidizi ni Omary Pumzi aliyepata kura 28.

Nafasi ya mweka hazina ilikwenda kwa Laurent Shirima aliyepata kura 28, nafasi ya mjumbe wa mkutano mkuu kwenda Corefa ni Japhet Mbogo aliyepata kura 30, Mwakilishi wa vilabu Mohamed Mwenda aliyepata kura 28.

Mwakilishi wanawake ni Jesca Siha aliyepata kura 28 huku kamati ya utendaji ni Method Mselewa, Nasoro Shomvi na Emanuel Mbunda.

Akizungumzia mikakati yake katika kipindi cha miaka minne Munis alisema kuwa moja ya mikakati yake ni kuhakikisha Kibaha inakuwa na timu ya ligi kuu ambapo ataweka mikakati Ruvu Shooting irudi kwenye ligi hiyo baada ya kushuka daraja.

Munis alisema kuwa atahakikisha mpira wa miguu unachezwa na kupata viwanja vizuri ili kukuza vipaji vya vijana kwenye soka ili waje kuwa hazina kwa timu za mkoa na taifa kwa ujumla.

Naye Katibu wa chama cha soka Mkoa wa Pwani COREFA Mohamed Masenga alisema kuwa kwa vyama ambavyo havijafanya chaguzi vifanye hivyo ili kwendana na kalenda ya vyama vikuu vya soka.

Masenga alisema anapongeza uongozi uliochaguliwa na kuwataka kuzingatia mipango na taratibu zilizopo ili soka la mkoa wa Pwani lisonge mbele.

Kwa upande wake ofisa michezo wa Halmashauri ya Mji Kibaha Burhan Tulusubya alisema kuwa uchaguzi huo ulienda vizuri kwa kuzingatia taratibu za chama hicho na sheria kwani ulikuwa wa kisheria.

Tulusubya alisema kuwa viongozi hao wasimamie maneno yao kwa kutafsiri kwa vitendo na wahamasishe vilabu navyo vifanye chaguzi ili wawe kisheria. Uchaguzi huo ulisimamiwa na makamu mwenyekiti wa uchaguzi wa KIBAFA Mabel Nasua.

WAANDISHI WA HABARI WAULA UCHAGUZI WA SOKA WILAYA YA KIBAHA (KIBAFA)



WAANDISHI wa habari waula baada ya kuchaguliwa kwenye uchaguzi wa Chama Cha Soka Wilaya ya Kibaha (KIBAFA) ambapo Hassan Mtengefu amechaguliwa kuwa meneja wa habari wa chama hicho.
Chama hicho kimewateua waandishi hao ikiwa ni sehemu ya uundaji wa kamati mara baada ya uchaguzi mkuu wa chama hicho uliofanyika jana Mjini Kibaha.

Waandishi hao wameteuliwa kwenye kamati mbili ikiwemo ya nidhamu na maadili na kamati ya habari uhamasishaji na zawadi.

Ukiachilia mbali Mtengefu wengine ni Gustaph Haule aliyeteuliwa kwenye kamati ya nidhamu na maadili.

Wengine ni Mariam Songoro ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya habari uhamasishaji na zawadi huku wengine wakiwa ni Margareth Malisa, Ben Komba na John Gagarini ambao ni wajumbe.

Saturday, July 1, 2023

MHE.MASANJA ACHANGISHA MILIONI 95 ZA UJENZI WA KANISA LA WAADVENTISTA WASABATO SDA PASIANSI MWANZA

 





Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mwanza na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja  ameongoza harambee ya kuchangia ujenzi wa nyumba ya ibada ya Kanisa la Waadventista Wasabato SDA Pasiansi kwenye Jimbo Kuu la Nyanza Kusini leo mkoani Mwanza na kupata kiasi cha shilingi milioni 95. 2 ambapo  fedha taslimu zilikuwa shilingi milioni 47.3 na ahadi shilingi milioni 47.8.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Masanja amelipongeza kanisa la SDA Pasiansi kwa kuanza ujenzi wa kanisa hilo jipya ambalo ujenzi wake ulianza mwaka 2022 huku waumini wa kanisa hilo wakiwa wameshafanikiwa kuchangia shilingi milioni 56 za ujenzi.

"Serikali inatambua mchango wa kanisa hili katika sekta ya Elimu na Afya. Ujenzi wa kanisa hili ni wito na wajibu wa kila mmoja wetu"  amesema Mhe. Masanja

Amesema lengo kuu la kufanya harambee hiyo ni kutafuta fedha za ujenzi wa kanisa na fedha zinazohitajika ni zaidi ya milioni 200. 

Amewaomba waumini wa kanisa hilo waendelee kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan katika kuleta maendeleo na pia kuendelea kuiombea Tanzania iendelee kuwa na  amani, umoja na upendo.

Naye, Mchungaji wa Kanisa la SDA Pasiansi Harun Kuyenga amesema mradi huo wa ujenzi la kanisa ulianza mwaka 2022 na unatarajia kukamilika mwaka 2024 na mara baada ya kukamilika kwake kanisa  litakuwa na uwezo wa kubeba waumini 3000 ambapo  kanisa la sasa lina uwezo wa kubeba waumini 800.

Ameongeza kuwa  wameamua kujenga kanisa hilo jipya  kutokana na ongezeko la waumini kutoka maeneo tofauti tofauti huku akisisitiza kuwa kwa sasa kiasi cha fedha shilingi milioni 200 zinahitajika ili kukamilisha ujenzi wa Kanisa hilo.

Katika Harambee hiyo, Mhe.Masanja pamoja na familia yake na marafiki zake walifanikiwa kuchangia ujenzi wa kanisa hilo kiasi cha shilingi milioni 51,050,000 ambapo fedha taslimu ilikuwa ni shilingi milioni 30,550,000 na ahadi shilingi milioni 20,500,000.

MHE.MARY MASANJA ATEMBELEA OFISI ZA CCM MKOANI MWANZA

 


Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mwanza na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja leo ametembelea Ofisi za Chama cha Mapinduzi jijini Mwanza na kufanya mazungumzo na Katibu wa  CCM, Mkoa wa Mwanza Ndugu Omary Mtuwa.

Pia, alipata nafasi ya kuzungumza na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza Ndugu Sixbert Reuben Jichabu.

Mhe. Masanja anatarajia kushiriki katika Harambee ya Kuchangia ujenzi wa Nyumba ya Ibada ya Kanisa la Pasiansi SDA jijini humo tarehe 1 Julai,2023.

Friday, June 30, 2023

KPC YATAKIWA KUPAMBANA NA VITENDO VYA UKATILI KWENYE JAMII



MJUMBE wa Kituo cha Msaada wa Kisheria Kibaha (KPC) Lydia Mgaya amekitaka kituo hicho kufuatilia baadhi ya matukio ya Ukatili kwa watoto na wanawake kwenye jamii ili wahusika wachukuliwe hatua.

Ameyasema hayo kwenye ofisi za KPC zilizopo Mjini Kibaha baada ya kuteuliwa kwenye nafasi hiyo ambapo amesema baadhi ya matukio yamekuwa yanashindwa kuendelea kutokana na kutokuwa na kutofuatiliwa.

Mgaya ambaye pia ni diwani wa viti maalumu amesema baadhi ya matukio likiwemo la binti mmoja ambaye ni mwanafunzi wa shule ya sekondari kubakwa na baba yake wa kambo tangu mwezi wa Aprili mwaka huu lakini haliendi kwa haraka hali inayoweza kusababisha kutofanikiwa.

"Nashukuru kwa kuniteua kwenye nafasi hii nawapongeza kwani kuna tukio nilileta kwenu sasa liko mahakamani nataka na hili lifuatiliwe ili liende kwenye utaratibu ili muhusika achukuliwe hatua na mtoto apate haki yake,"alisema Mgaya.

Alisema kuwa tukio lingine ni mtoto kupigwa na mjomba wake baba kampiga na kumjeruhi mwanae hivyo kituo hicho kina nafasi kubwa ya kuzifuatilia kesi hizo ili ziende kwa utaratibu mzuri kwani wanaofanyiwa hawana sauti.

Naye meneja wa kituo hicho Dismas Chihwalo amesema kuwa katika kuhakikisha vitendo vya ukatili vinapungua ndani ya jamii wanatoa elimu na msaada wa sheria kwa viongozi wa kata, mitaa, wanafunzi na wananchi.

Chihwalo amesema kwa sasa mwamko wa jamii kuripoti matukio umekuwa ni mkubwa tofauti na zamani baada ya kupatiwa elimu ya sheria na msaada wa sheria ambapo watu walikuwa hawatoi taarifa yanaporokea matukio ya ukatili kwenye jamii.

SERIKALI YATAKIWA KUDHIBITI MABANDA YA VIDEO KWA WATOTO

KITUO cha Msaada wa Kisheria Kibaha (KPC) kimeishauri serikali kudhibiti vibanda vinavyoonyesha video maarufu kama vibanda umiza ambapo baadhi ya watoto chini ya miaka 18 kufanyiwa vitendo vya ukatili.

Aidha kimeshauri wazazi kuwa makini na kuwapatia watoto wao simu ambapo baadhi wamekuwa wakizitumia vibaya kujifunza mambo yasiyofaa.

Akifundisha somo la Ndoa kwa viongozi wa Mita na Kata ya Visiga mwezeshaji kutoka (KPC) Humphrey Munuo alisema kuwa baadhi ya mabanda hayo yamekuwa yakionyesha video mbaya ambazo zinasababisha watoto kujifunza vitendo viovu vikiwemo vya ngono.

Alisema kuwa baadhi ya watu wakubwa wamekuwa wakiwarubuni watoto hao kwa kuwalipia kuingia kwenye mabanda hayo na kuwafanyia vitendo vya ubakaji.

"Serikali ifanye ufuatiliaji wa mabanda hayo picha zinazoonyeshwa na pia iwafuatilie baadhi ya watu wanaowafanyia watoto vitendo vya ubakaji ambapo vitendo hivyo hufanyika kupitia mabanda hayo,"alisema Munuo.

Aliongeza kuwa pia iangalie maudhui yanayoonyeshwa kwenye mabanda hayo kwani inavyoonekana baadhi ya tabia watoto wanajifunza kupitia kwenye mabanda hayo pamoja na Play Station.

"Juu ya Tehama wazazi wawe makini kwa watoto wao ambao ni wanafunzi kuwapatia simu kwani baaadhi ya picha au video hazina maadili mazuri hali inayosababisha mmomonyoko wa maadili",alisema Munuo.

Alibainisha kuwa digitali ni nzuri lakini lazima wazazi wawe makini na matumizi hayo kwa watoto wao ili wasijiingize kwenye vitendo vibaya na kuharibu maisha yao.