Tuesday, June 27, 2023

JAMII YAASWA KUWEKEZA UJUZI KWA WATOTO



Jamii imeaswa kuwekeza zaidi kwenye  kuongeza ujuzi wa malezi makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto ili kuwa na Taifa lenye raia wenye misingi imara katika nyanja zote.

Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mwanaid Ali Khamis wakati akifungua Mafunzo  ya kitaifa ya Sayansi ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya awali ya Mtoto kwa Wadau kutoka mikoa 16 Nchini pamoja na Wizaraa za kisekta ,Mkoani Dodoma, Juni 26, 2023.

“Mafunzo haya yasiishie tu maofisini bali yafike hadi ngazi za Vijiji kwani huko watu huchelewa kupata taarifa za mambo ya msingi. Mnatakiwa mshuke kwa wananchi wa ngazi za chini kwani  Malezi ya awali ni ya muhimu sana katika makuzi ya mtoto”Alisema Mwanaidi.

Akielezea lengo la Mafunzo hayo Naibu katibu Mkuu  kutoka  Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Wakili Amon Mpanju amesema  mafunzo hayo ni muhimukwaajili  yakuwaongezea ujuzi Wataalam husika ili waweze kutekeleza Majukumu yao kama inavyostahili

“Lengo la mafunzo haya ni kuwajengea uwezo bobezi ili waweze kutekeleza inavyostahili,  kwani mafunzo haya yanatolewa na chuo cha Aga khan ambacho kina Mamlaka ya kutoa mafunzo hisika" amefafanua Mpanju

Akiongea wakati wa Mafunzo hayo Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Mtoto kutoka Wizra ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Waanwake na Makundi Maalum, Sebastian Kitiku,  amesema Wizara itaendelea kushirikiana  kwa karibu na wadau wa Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Mtoto ili kuhakikisha kuna mazingira salama ya ustawi na Maendeleo ya Watoto Nchini.

Naye mshiriki Tedson Ngwale ambaye ni Afisa Maendeleo kutokea Shinyanga ameishukuru Serikali kwa jitihada hizo za kuhakikisha inaanda mazingira salama kwa watoto kwa kutoa mafunzo hayo kwa maafisa maaendeleo na Ustawi wa Jamii.

“Tuna ahidi kuitendea haki Serikai kupitia Mafunzo haya  kwa kutekeleza kama tulivyoelekezwa na kama ilivyokusudiwa kwa kuwafikia Wananchi wa ngazi zote hasa vijijini ambako kuna changamoto zaidi”.

KAMATI YA BUNGE YAITAKA TARURA KUTIMIZA AZMA YA SERIKALI

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Dennis Londo ameutaka Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kuendelea  kuaminika na Serikali kwa  kutekeleza majukumu yake ipasavyo ya kujenga mbiundombinu ya barabara ili kuwaondolea adha ya usafiri wananchi.

Mhe. Londo ametoa kauli hiyo Juni 24, 2023 katika ziara ya kikazi ya kukagua miundombinu ya  barabara zilizojengwa chini ya usimamizi wa TARURA Wilaya ya Morogoro.

Mwenyekiti huyo amesema dhamira ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwaongezea bajeti ya sh.  Bilioni 350 kwa mwaka wa fedha 2023/24 ni kuona umuhimu wa taasisi hiyo  katika kutekeleza majukumu yake hasa katika ujenzi na marekebisho ya barabara maeneo  ya vijijini na mijini ili kuwa na miundombinu rafiki kwa wananchi.

Amesema asilimia kubwa ya watanzania shughuli yao kubwa ni kilimo hivyo TARURA wafanye kazi ili barabara  ziwe rafiki kwa watumiaji na kurahisisha maisha yao.

Mhe.Londo ameipongeza TARURA kujengwa barabara yenye kilometa 70 kwenye Wilaya ya Morogoro ambayo imerahisisha kuunganisha vijiji vinne ikiwamo cha Ngerengere na kuhimiza kutunza miundombinu ya barabara hiyo.

"Kujengwa kwa barabara hii kutawezesha kufika kwa urahisi bwawa la Kidunda ambalo ni mradi mkubwa utakaosaidia upatikanaji wa maji kwa wakazi wa Morogoro, Pwani na Dar es Salaam,"amesema.

N





aye, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Deogratius Ndejembi ameishukuru Kamati hiyo ya Bunge kwa maelekezo yake na kuiahidi TAMISEMI itaendelea kutimiza lengo la Serikali kwa kuisimamia TARURA kutoa huduma bora kwa wananchi.

Monday, June 26, 2023

SERIKALI YATAHADHARISHA WANANCHI IRINGA KUACHA KUTEMBEA USIKU KUEPUKA ATHARI ZA KUVAMIWA NA SIMBA

SERIKALI imewatahadharisha Wananchi Mkoani Iringa kuacha kutembea usiku ili kuepukana na madhara ya kuvamiwa na Simba walioingia katika makazi ya watu.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) ameyasema hayo leo jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Grace Tendega aliyetaka kujua nini mkakati wa Serikali wa kuhakikisha wananchi wananchi wa Iringa wanaishi kwa uhuru kutokana na changamoto ya Uvamizi wa Simba.

“Niendelee kutoa elimu kupitia Bunge hili kwamba wakati huu ambapo tunawasaka hawa Simba wananchi wawe na tahadhari ya kutotembea usiku lakini pia wenye mifugo wawashe mioto kuzunguka maeneo ya mifugo ili kuepusha Simba wasisogee katika maeneo yao” Mhe. Masanja amesisitiza.

Kufuatia hatua hiyo Mhe.Masanja amesema Serikali tayari imeshapeleka helikopta inayozunguka usiku na mchana kuhakikisha Simba hao wanapatikana na kurudishwa katika maeneo yao ili kuhakikisha  maisha ya Watanzania yanalindwa kwa gharama yoyote

Kuhusu mikakati ya Serikali ya kukabiliana na wanyama wakali na waharibifu, Mhe. Masanja amesema Serikali inatekeleza Mkakati wa kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu wa mwaka 2020 – 2024 ambapo Wizara inatoa elimu juu ya kujikinga na wanyamapori wakali na waharibifu; inajenga vituo vya askari wanyamapori ili kusogeza huduma karibu na wananchi; kuwafunga mikanda (GPS collars) tembo; na kuanzisha timu maalum (Rapid response Teams).

Pia, Serikali inaendelea kuwashirikisha wananchi kwa kutoa mafunzo kwa Askari wa Vijiji (VGS) ili kuongeza nguvu ya kudhibiti tembo katika maeneo ya wananchi.

Aidha, amesema Serikali imeshaweka mipango ya kujenga fensi ya umeme katika baadhi ya maeneo ili kupunguza athari ya wanyama wakali na waharibifu.

Thursday, June 22, 2023

*MAJALIWA APOKEA TAARIFA YA KAMATI MAALUM ALIYOIUNDA KUFUATILIA CHANGAMOTO ZA WAFANYABIASHARA*


WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa leo Alhamisi, Juni 21, 2023, Jijini Dodoma amepokea taarifa ya Kamati Maalum aliyoiunda kwa ajili ya kupitia, kuchambua na kutoa mapendekezo ya kutatua changamoto za wafanyabiashara nchini. 

Taarifa hiyo imekabidhiwa na Mwenyekiti wa kamati, Dkt. John Jingu ambaye pia ni Katibu Mkuu, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum.

Mkutano huo umehudhuriwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama, Waziri Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba, Waziri wa Viwanda na Uwekezaji Ashatu Kijaji, Waziri wa Nchi OR – TAMISEMI, Angela

Kairuki, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Ahmad Chande, Makatibu Wakuu, Makamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), wanakamati na wataalam kutoka sekta mbalimbali za masuala ya kodi, biashara na uwekezaji.

Akizungumza baada ya kupokea taarifa hiyo, Mheshimiwa Majaliwa amesema Kamati hiyo imefanya kazi kubwa na imeleta majibu ambayo yatatatua changamoto za wafanyabiashara nchini na ameahidi kuwa Serikali imepokeat aarifa hiyo na itayafanyia kazi mapendekezo na ushauri uliotolewa na kamati hiyo.

Kamati hiyo ambayo ilipewa siku 14, imefanya mapitio katika maeneo mbalimbali ya kikodi, bandari na maeneo ya wafanyabiashara kwenye mikoa mbalimbali nchini.

Sunday, June 18, 2023

TAASISI MWALIMU NYERERE YAFANIKISHA UPATIKANAJI DAMU









TAASISI ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Mkoa wa Pwani imefanikisha upatikanaji wa damu uniti 32 ambazo zitatumika kwenye Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha.

Akizungumza mara baada ya zoezi la uchangiaji damu lililofanywa kwa pamoja na Taasisi hiyo ya Nyerere kwa kushirikiana na Taasisi ya Chawa wa Mama Kibaha Vijijini  mgeni rasmi Yahaya Mbungulume ambaye alimwakilisha Mganga Mkuu wa Halmashauri hiyo alisema uniti hizo zitasaidia sana wagonjwa.

Mbungulume alisema kuwa zoezi hilo limekuwa na mafanikio makubwa kwani limesaidia upatikanaji wa damu ambayo itasaidia wagonjwa wakiwemo wajawazito, wagonjwa na watu wanaopata ajali.

Kwa upande wake katibu wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere Mkoa wa Pwani Omary Pumzi alisema kuwa waliamua kujitolea damu baada ya kupita kwenye Hospitali na kuona jinsi gani kuna uhitaji mkubwa wa damu.

Pumzi alisema kuwa Taasisi hiyo imeendelea kutekeleza malengo ya Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere ya kukabilana na adui wa maendeleo ambao ni maradhi ujinga na umaskini hivyo afya ni moja ya malengo kwama yalivyo kwa Rais Dk Samia Suluhu Hassan.

Naye mwenyekiti wa Chawa wa Mama Kibaha Vijijini Rehema Chuma alisema kuwa malengo ya taasisi yao ni kumsaidia Rais katika kuhakikisha nchi inapata maendeleo.

Akiongoza zoezi la uchangiaji damu Katibu Msaidizi wa Taasisi ya Mwalimu Taifa Neema Mkwachu alisema wanamuunga mkono Mwasisi wa Taifa kwa vitendo kwa kushiriki moja kwa moja.

Akielezea mafanikio ya zoezi la uchangiaji damu mratibu wa huduma za maabara Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Nabwike Mwairinga alisema kuwa wamepata uniti 32 kwenye zoezi hilo ambazo zitasaidia kwa kiasi kikubwa kwenye benki ya damu ambapo wanahitaji uniti 40 kwa kila mwezi.






Friday, June 16, 2023

MJEMA AWATAKA WANACCM WATEMBEE KIFUA MBELE

 

KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi, Itikadi na Uenezi, Ndugu Sophia Mjema, amewataka wanachama wa chama hicho na wananchi kwa ujumla kutembea kifua mbele akisema chama hicho kimenyoka na hakiyumbishwi.

Mjema ametoa kauli hiyo 15.6.2023 katika viwanja vya Mnarani mjini Mpwapwa Mkoani Dodoma akiwa katika ziara ya Katibu Mkuu wa CCM, ndugu Daniel Chongolo.

Katika mkutano huo wa hadhara, Mjema amesema Chama Cha Mapunduzi chini ya Mwenyekiti wake Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kinaendelea kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazowakabili wananchi kwa vitendo.

Amewataka wana-CCM kutoogopa kukisemea chama chao hasa kwa watu wanaotosha miradi mbalimbali ambayo inatekelezwa na chama hicho kupitia Ilani yake ya uchaguzi ya mwaka 2020-2025.

"Niwaambieni wananchi wa Mpwapwa mna chama imara sana, chama chemu ni sikivu kinasikiliza changamoto zenu na kuzitafutia ufumbuzi kupitia kwa watendaji mbalimbali wa serikali, hivyo ungeni mkono juhudi za serikali na msiwasikikize wapotoshaji.

Aidha, Mjema amesema CCM imenyooka kama rula na haiyumbishwi.

*MHE. MWINJUMA AFUNGUA MASHINDANO YA UMISSETA TABORA*

 

Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Hamis Mwinjuma leo Juni 15, 2023 mkoani Tabora amefungua mashindano ya michezo kwa Shule za Sekondari Tanzania (UMISSSETA) kitaifa katika viwanja vya Shule ya Sekondari ya Wavulana  Tabora.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mashindano hayo Mhe. Mwinjuma amesema Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya michezo nchini kwa kuanza na shule 56 za sekondari, mbili katika kila Mkoa, ili kukuza na kuendeleza vipaji vya michezo mbalimbali

‘’Ndugu viongozi na wanamichezo Serikali kwa upande wake kupitia ushirikiano wa Wizara zetu tatu (Ya kwangu  Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na TAMISEMI)  imefanya jitihada kubwa katika kuimarisha shughuli za michezo katika shule za Msingi na Sekondari”amesema Mhe. Mwinjuma.

Mashindano hayo yatafanyika kwa siku saba yakihusisha timu za michezo  mbalimbali kutoka Mikoa 32 ya Tanzania bara na Zanzibar.