Thursday, December 17, 2015

MAKANDARASI WANAWAKE WATAKIWA KUJENGA VIWANJA VYA NDEGE

Na John Gagarini, Kibaha
WAKANDARASI wanawake nchini wametakiwa kuomba kandarasi kubwa zikiwemo za ujenzi wa barabara kubwa pamoja na viwanja vya ndege kupitia kampuni zao za ujenzi ili kujiongezea kipato na kuiletea nchi maendeleo.
Hayo yalisemwa jana mjini Kibaha na Mkurugenzi wa iliyokuwa Wizara Ujenzi Kegora wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo makandarasi wanawake katika maandalizi ya zabuni na manunuzi kwa kazi za ujenzi wa barabara yaliyoandaliwa na wizara ya Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano.
Kegora alisema kuwa wanawake wameonyesha uwezo mkubwa kwa kufanya kazi za ujenzi wa barabara kwa viwnago vinavyokubalika hivyo ni vema wakaomba kandarasi za ujenzi mkubwa ambao zinatarajiwa kufanyika.
“Kwa sasa ombeni kazi za ujenzi mkubwa kama vile wa viwanja vya ndege, bandari, madaraja na reli ili muonyeshe umahiri wenu katika kazi za ujenzi na mnapaswa kuacha woga kwani uwezo mnao na mmeonyesha kuwa manaweza,” alisema Kegora.
Alisema wanawake wakandarasi wanapaswa sasa kuacha kubaki nyuma kwa kujenga miradi midogo midogo ya ujenzi bali wafanye miradi mikubwa ili wapate mafanikio kama walivyofanikiwa kupitia ujenzi.
“Jiendelezeni kitaaluma mfikie madaraja ya juu ili mpate kuimarika kitaaluma muwe juu pia muongeze idadi ya wakandarasi wanawake kwani mmeonyesha kazi nzuri na ndiyo maana mnapewa mafunzo haya,” alisema Kegora.
Kwa upande wake mratibu wa mafunzo hayo Mhandisi Rehema Myeya alisema kuwa mafunzo hayo yana lengo la kuwawezesha wakandarasi hao wanawake kujua namna ya ujazaji wa zabuni na mikata wakati wa kuomba kandarasi.
Myeya alisema kuwa makandarasi wanawake wanakabiliwa na changamoto kubwa ya kushindwa kujaza vizuri zabuni hizo hivyo kusababisha kukosa kandarasi za ujenzi wa barabara hapa nchini hasa ikizingatiwa kuwa wengi wao hawana elimu kubwa.
Jumla ya wakandarasi wanawake 26 kutoka mikoa Dar es Salaam, Morogoro, Tanga, Singida, Kilimanjaro na Arusha ambapo hadi sasa tayari wamewapatia mafunzo makandarasi zaidi ya 200 kwenye mikoa yote hapa nchini.
Mwisho.

Tuesday, December 15, 2015

ASOTA NDANI MIAKA MITANO AOMBA MSAADA

Na John Gagarini, Kibaha
MARIAMU Mpembenwe (85) mkazi wa Mkoani A kata ya Tumbi wilayani Kibaha mkoani Pwani anakabiliwa na tatizo la maumivu ya viungo mbalimbali vya mwili ikiwemo mguu na mkono hali iliyomfanya ashindwe kutoka nje kwa kipindi cha miaka mitano.
Aidha anaomba kupatiwa baiskeli ya watu wenye ulemavu ili iweze kumsaidia kuweza kutembelea kwenda kupata huduma muhimu ikiwemo za matibabu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini Kibaha waliomtembelea nyumbani kwa mwanae alisema kuwa hali yake kiafya ni mbaya kutokana na kukosa matibabu pamoja na chakula kwani mwanae ambaye anamtegemea hana kipato chochote cha kujikimu zaidi ya kuomba misaada.
Mpembenwe alisema kuwa anakabiliwa na matatizo mengi ikiwa ni pamoja na kutoona huku nyumba anayoishi kuvuja kipindi cha mvua.
“Nawaomba watu mbalimbali weneye uwezo ikiwemo serikali ili niweze kukabiliana na changamoto zinazonikabili kwani sipati huduma bora za afya, chakula, hata sehemu ninayolala kitanda hakina godoro na huduma za haja napata hapa hapa mazingira ni mabaya naomba msaada wa fedha kwa ajili ya kujikimu,” alisema Mpembenwe.
Kwa upande wake mtoto wa mama huyo Iddy Mtegya (65) alisema kuwa ni kweli mama yake anakabiliwa na matatizo mengi likiwemo la kiafya licha ya kwamba amekuwa akipatiwa matibabu hapo hapo nyumbani.
Mtegya alisema kuwa ni kweli hajatoka nje kwa kipindi hicho kwani ana matatizo ya mguu wa kulia na mkono wa kulia hivyo kushindwa kutemebea na kutokana na hali yake ya unene wanashindwa kumbeba kumtoa nje au kumpeleka sehemu nyingine.
“Naomba msaada kwa watu wenye uwezo watusaidie kiti cha magurudumu ili tuweze kumsaidia mama ili tuweze kumtoa mama nje pia kumpeleka sehemu mbalimbali ikiwa ni pamoja na hospitali licha ya kwamba yeye mwenyewe hataki kwenda hospitali,” alisema Mtegya.
Naye diwani wa kata ya Tumbi Hemed Chanyika alisema kuwa suala hilo linasikitisha kwani licha ya hali aliyokuwa nayo mama huyo anapaswa kupatiwa huduma zote za kibinaadamu kwani kumnyima huduma hizo ni kumuongezea matatizo.
Chanyika alisema kuwa hata baadhi ya watendaji wa mtaa walipaswa kulieleza tukio hilo sehemu husika ili aweze kusaidiwa kupitia vitengo mbalimbali vya misaada kwani wameonekana kutoliweka wazi suala hilo kwa kipindi hicho cha miaka mitano.
Mwenyekiti wa mtaa wa Mkoani A Titus Kabora alisema kuwa wanataarifa ya mama huyo na familia hiyo ilianza kuhudumiwa kupitia mfuko wa maendeleo ya jamii TASAF lakini tatizo misaada hiyo ni midogo na haitoshelezi mahitaji.
Mwisho.  




Tuesday, December 8, 2015

TUMIENI MISITU KUJIONGTEZEA KIPATO TOKA WATALII

Na John Gagarini, Kibaha
WANANCHI wanaoishi jirani na Hifadhi ya Msitu wa Ruvu Kusini wametakiwa kuacha kufanya uharibifu wa msitu huo badala yake wautumie kama chanzo cha mapato kwa njia ya Utalii.
Hayo yalisemwa kwenye Kijiji cha Kipangege wilayani Kibaha mkoani Pwani na ofisa miradi wa Shirika lisilo la Kiserikali la Usimamizi wa Misitu ya Asili Tanzania (TFCG) Yahaya Mtonda wakati wa tamasha la Kimataifa la Utalii wa kutumia Baiskeli.
Mtonda alisema kuwa kutokana na umuhimu wa misitu ukiwemo msituo ambao unatumika kuchuja hewa safi ukiwa ni mapafu ya kupumulia hewa ya Jiji la Dar e s Salaam wananchi wanapaswa kuulinda na kuondokana na dhana kukata miti kwa ajili ya kujiongezea kipato.
“Kwa sasa tumeshaweka mazingira ya kuufanya msitu huu kuwa wakitalii tofauti na ilivyokuwa mwanzo kwani kwa sasa watalii watakuja kuutembelea na kufanya utalii kujionea miti mbalimbali ya asili ambayo inapatikana hapa Tanzania na hakuna sehemu nyingine inakopatikana hivyo ni wakati sasa wa wananchi kutumia fursa hii kujiongezea kipato kupitia utalii badala ya kukata miti kwa ajili ya mbao na kuni au mkaa,” alisema Mtonda.
Alisema kuwa endapo wananchi watatumia fursa hiyo watapata mapato huku wakienedelea kutunza msitu huo pamoja na kuhifadhi mazingira na kukabilian na changamoto ya tatizo la Tabianchi ambayo inasababisha kukosekana mvua na kusababisha hali ya hewa kuwa mbaya hususani kuwa na joto kali.
Kwa upande wake Mshauri wa Ufundi wa (TFCG) Andrew Perkin lengo la tamasha hilo ni kuwapa uelewa wananchi juu ya umuhimu wa kulinda misitu ili waweze kufurahia mazingira mazuri ambayo uoto wake wa asili unasababisha hali ya hewa kuwa safi.
Perkin alisema kuwa misitu hiyo ilikuwa ikiharibiwa sana na wananchi kutokana na kukata miti kwa ajili ya shughuli za kibinadamu zikiwa ni pamoja na uvunaji wa misitu ambapo kwa sasa tayari wameshawaondoa watu waliokuwa kwenye msitu huo na hali yake inaanza kurudi kama ilivyokuwa mwanzo.
Naye mwenyekiti wa Umoja wa Wapanda Baiskeli (UWABA) Meja Mbuya alisema kuwa wamekuwa wakihamasisha watu kupanda baiskeli kwani matumizi ya magari yamekuwa yakiharibu mazingira kutokana na moshi unaotokanan na magari hayo.
Mbuya alisema kuwa mbali ya kupanda baiskeli wamekuwa wakitoa elimu mbalimbali ya juu ya utunzaji wa misitu na kushauri matumizi ya nishati ya jua na upepo katika baadhi ya matumizi ili kutoharibu mazingira. Jumla ya watu zaidi ya 100 toka mataifa mbalimbali walishiriki tamasha hilo ambapo walitembea umbali wa kilometa 30.

Mwisho. 

Saturday, December 5, 2015

WAWILI WAFA PWANI

Na John Gagarini, Kibaha
MLINZI wa kampuni ya Ulinzi ya Optima inayolinda kwenye jengo la Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Pwani Primc Bararwirwa amekutwa amekufa jirani na na kituo kikuu cha Mabasi cha Maili Moja Wilayani Kibaha.
Tukio hilo lilitokea Desemba 4 mwaka huu majira ya asubuhi jirani na Grosari ya Kilimani ambapo mwandishi wa habari hizi aliushuhudia mwili wa marehemu ukiwa chali na kufunikwa na shuka huku ukiwa hauna viatu.
Baadhi ya watu waliomshuhudia marehemu kabla ya kifo chake walisema kuwa usiku wake walimwona marehemu akiwa na wenzake huku wakiongea lakini walishangaa asubuhi kuona akiwa amekufa na hakuwa na jeraha lolote mwilini mwake.
Polisi walifika kwenye eneo hilo na kuuchukua mwili wa marehemu kisha kuupeleka Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Pwani kwa ajili ya kuchunguza kifo chake na kusubiri ndugu kwa ajili ya taratibu za mazishi.
Kamanda wa polisi mkoani Pwnai Jafary Mohamed alithibitisha kutokea tukio hilo ambapo wanaendelea na uchunguzi kujua chanzo cha kifo hicho ambacho kimewashtua wakazi wengi wa Maili Moja waliokuwa wanamfahamu marehemu.
Katika tukio lingine mkulima wa Kijiji cha Zogowale kata ya Misugusugu Aloyce Chuma (54) amefariki dunia huku watu wengine watatu wakijeruhiwa  baada ya kupigwa na radi ambayo iliambatana na upepo mkali.
Akizungumza na gazeti hili mwenyekiti wa Mtaa wa Zogowale Rajab Mhanyige alisema kuwa tukio hilo lilitokea majira ya saa 10 jioni wakati marehemu akiwa amekaa kwenye gogo na wenzake hao waliojeruhiwa wakati wamepumzika baada ya shughuli za kilimo.
Mhanyige alisema kuwa radi hiyo ilipiga sehemu walipokuwa wamekaa watu hao na kumwua marehemu na kuwajeruhi wenzake huku yeye akifia eneo la tukio na hakuwa na jeraha lolote mwilini mwake.
“Siku hiyo ilipiga radi kali iliyoambatana na upepo mkali ambayo mimi sijawahi kusikia tangu kuzaliwa kwangu ilikuwa na kishindo kikubwa sana na niliamini kuwa itakuwa imeleta matatizo na kweli kwani baada ya muda nilletewa taarifa kuwa kuna mtu kafa kutokana na radi hiyo ambapo baadaye mvua kubwa ilinyesha,” alisema Mhanyige.  
Alisema mara baada ya tukio hilo waliuchukua mwili wa marehemu pamoja na majeruhi na kuwapeleka kwenye kituo cha Afya cha Mlandizi kwa ajili ya kuhifadhi mwili na majeruhi kwa ajili ya matibabu ambao nao hawakuwa na majeraha yoyote.
Aidha aliwataja majeruhi ambao baadaye waliruhusiwa kurudi nyumbani kuwa ni Cosmas Bandula (54), Sultan Kigumu ambaye alirushw aumbali wa mita 10 na mtu aliyetambuliwa kwa jina moja la Kamugisha (48). Polisi walithibitisha kutokea kwa tukio hilo.

Mwisho.

Sunday, November 1, 2015

Friday, October 30, 2015

RIDHIWANI KIKWETE AWASHUKURU WANACHALINZE KUMCHAGUA TENA

Na John Gagarini, Chalinze
MBUNGE Mteule wa Jimbo la Chalinze wilayani Bagamoyo mkoani Pwani Ridhiwani Kikwete amesema kuwa hana chuki kwa wale ambao hawakumpigia kura kwenye uchaguzi uliofanyika Oktoba 25 mwaka huu kwani hizo ni changamoto za uchaguzi.
Aliyasema hayo jana kwenye uwanja wa Miembe Saba Chalinze wilayani Bagamoyo wakati wa mkutano wa hadhara wa kuwashukuru Wanachalinze kwa kumchagua kuwa mbunge kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika Jumapili.
Ridhiwani alisema kuwa licha ya baadhi ya maeneo kutompigia kura za kumchagua kuwa mbunge lakini atawatumikia wananchi wote bila ya kujali kama walimpigia kura au la kwani kila mtu ana haki ya kumpigia kura mgombea yoyote anayempenda.
“Nawashukuru wananchi wote walionipigia kura na hata wale ambao hawakunipigia kura kwani hiyo ndiyo demokrasia nitahakikisha nawahudumia wananchi wote bila ya kuwabagua nitahakikisha napeleka maendeleo kwa watu wote wa jimbo hili,” alisema Ridhiwani.
Alisema kuwa kutopigiwa kura kwa wingi siyo sababu ya kuwagawa wananchi kwani hizo ni changamoto za uchaguzi ambao unakuwa na mambo yake ambapo baadhi ya maeneo walipiga kura kwa kuzingatia ukabila.
“Sitakuwa na chuki wala hasira kwa wale ambao hawakunipigia kura nitashirikiana nao katika suala la maendeleo ili kuhakikisha jimbo letu linakuw ana maendendeleo na wananchi wanaboresha maisha yao ili yasonge mbele,” alisema Ridhiwani.
Aidha alisema kuwa atahakikisha Mji wa Chalinze ambao umekuwa Halmashauri ya Mji Mdogo unajengwa kwa kuwekewa huduma muhimu ili wananchi waweze kuboresha biahara zao hasa ikizingatiwa kuwa mji huo ni wa kibiashara.
“Moja ya mambo nitakayo yafanya ni kufanya Chalinze kuwa makao makuu ya Halmashauri hiyo na baadaye kuwa wilaya kwani mchakato unaendelea na tunaamini baada ya muda tutapewa wilaya hivyo tutaweza kujitegemea na kujiimarisha kiuchumi,” alisema Ridhiwani.
Alibainisha kuwa wananchi wasiwe na wasi wasi kwani kukichagua Chama Cha Mapanduzi CCM ni kuchagua maendeleo hivyo wasubiri kuona jinsi serikali mpya itakavyofanya kazi kwani kwao ni kazi tu.
Kwa upande wake mwenyekiti wa CCM Chalinze Nasa Karama alisema kuwa mbunge huyo ameonyesha uwezo mkubwa kwani kwa kipindi alichochaguliwa cha mwaka mmoja na miezi mitatu ameweza kufanya mambo makubwa ambapo alitumia ziadi ya shilingi bilioni moja na zaidi kwa ajali ya miradi ya maendeleo.
Mwisho.  

 Ridhiwani Kikwete

Sunday, October 25, 2015

RAIS DK JAKAYA KIKWETE ASHIRIKI ZOEZI LA KUPIGA KURA MSOGA

Na John Gagarini, Chalinze
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Jakaya Kikwete amesema kuwa mara atakapostaafu nafasi hiyo Novemba 5 mwaka huu anatarajia kuanzisha taasisi ya maendeleo kwa Afrika na Dunia.
Aidha alisema kuwa atarudi Kijijini kwake Msoga Chalinze wilayani Bagamoyo mkoani Pwani ambapo mbali ya kuanzisha taasisi hiyo ya maendeleo pia ataendeleza ufugaji na kilimo cha mananasi.
Dk Kikwete aliyasema hayo jana katika Kijiji cha Msoga mara baada ya kupiga kura yake kwenye uchaguzi mkuu wa kumchagua Rais, Mbunge na Diwani na kusema kuwa amefurahi sana kuona watu wanapiga kura bila ya usumbufu wowote.
Dk Kikwete alisema kuwa mara baada ya kustaafu na baada ya Rais mpya kuapishwa Desemba 5 atajihusisha na masuala hayo kwani hawezi kukaa tu hivi bila ya kuwa na jambo la kufanya kwani ataendelea kuwa na nguvu.
“Natarajia kuwa mfugaji kwani nina shamba la mifugo pia kuwa mkulima wa mananasi huko Kijiji cha Kiwangwa na ninafurahi kupiga kura kwani nimetumia haki yangu na nanishukuru hadi sasa hatujasikia kama kuna tatizo lolote,” alisema Dk Kikwete.
“Nawaomba wananchi wajitokeze kupiga kura na ningependa na vituo vingine viwe na utulivu kama hichi cha hapa na watu washiriki uchaguzi ili baadaye wasije wakahoji kuwa hata fulani kachaguliwa wakati wao hawakupiga kura kumchagua kiongozi ambaye wanamtaka wao,” alisema Dk Kikwete.
Juu ya uchaguzi wa mwaka huu alisema kuwa chaguzi zote zinakuwa na upinzani mkali na anaomba hali ya amani iendelee hivi ili iwe nchi ya mfano kwa kufanya uchaguzi bila ya kuwa na vurugu.
Kwa Upande wake mgombea wa Ubunge wa (CCM) Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete alisema kuwa anashukuru kwani hadi sasa zoezi hilo la upigaji kura linaendelea vizuri na hakuna tatizo lolote na anaamini kuwa uchaguzi utakwenda vizuri.
Ridhiwani ambaye naye alipiga kura kwenye kituo cha Kijiji cha Msoga alisema kuwa kuna changamoto ndogondogo zilizojitokeza ikiwa ni pamoja na baadhi ya watu hawakuona majina yao licha ya kuwa walikuwa na vitambulisho vya kupigia kura huko maeneo ya Miono.
Naye mgombea Ubunge Jimbo la Chalinze kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mathayo Torongey alisema kuwa amepita kwenye vituo vingi hajaona tatizo lakini kuna baadhi ya maeoneo mawakala wao walitishwa.
Torongey alisema kuwa mawakala hao walitishwa kwenye kituo cha Kijiji cha Msoga lakini baada ya makubaliano waliweka mawakala wengine na wakaendelea na zoezi la kusimamia kwenye vituo walivyopangiwa.
Aidha mkuu wa mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo alisema kuwa hadi mchana kulikuwa hakuna tatizo lililoripotiwa licha ya kuwa baadhi ya maeneo watu walikuwa na hofu kwamba zoezi litaenda taratibu lakini hali hiyo iliondoka na utaratibu kwenda vizuri.
Ndikilo alisema kuwa eneo la Vigwaza kulikuwa na hofu ya upungufu wa karatasi kutokana na idadi kubwa ya watu lakini hali hiyo iliwekwa sawa na mambo yanakwenda vizuri na wameweka ulinzi wa kutosha.
Alibainisha kuwa suala la kukaa mita 200 kwa ajili ya kulinda kura halipo kwani sheria imeelekeza vizuri juu ya watu mara baada ya kupiga kura wanaondoka na hakuna mtu aliyebaki kulinda kura kwani wameondoka na kuendelea na shughuli zao.
Mwisho. 

 Rais Dk Jakaya Kikwete akizungumza na mkuu wa mkoa wa Pwani wapili kulia Injinia Evarist Ndikilo , wakati Rais alipokwenda kupiga kura kwenye kituo cha Kijiji cha Msoga Chalinze wilayani Bagamoyo mkoani Pwani kulia ni mkuu wa wilaya hiyo Majid Mwanga

 Rais Dk Jakaya Kikwete akihojiwa na waandishi wa habara mara baada ya kupiga kura kwenye kituo cha Kijiji cha Msoga 

 Rais Dk Jakaya Kikwete kushoto akisubiri kupewa karatasi kwa ajili ya kwenda kupiga kura


 Rais Dk Jakaya Kikwete akiwa amepanga foleni kabla ya kwenda kupiga kura hata hivyo alisimama kwa muda mfupi kabla ya kutimiza zoezi hilo


Rais Dk Jakaya Kikwete akisalimiana na mkuu wa mkoa wa Pwani Evaristi Ndikilo alipowasili kwenye kituo cha kupigia kura kwenye Kijiji cha Msoga



Baadhi ya akinamama wakiwa wanasubiri kupiga kura kwenye kituo cha Kijiji cha Msoga

 Mgombea Ubunge wa Jimbo la Chalinze kupitia CCM Ridhiwani Kikwete akichukuliwa maelezo kabla ya kupiga kura 

 Ridhiwani Kikwete akiongea na waandishi wa habari mara baada ya kupiga kura kwenye Kituo cha Kijiji cha Msoga