Monday, October 19, 2015

WAOMBWA KULIPWA FIDIA UPANUZI WA BARABARA


Na John Gagarini, Chalinze

 

WAKAZI wa Kijiji cha Misani kata ya Kiwangwa wilayani Bagamoyo mkoani Pwani wameiomba serikali kuibana kampuni Eco Energy kuwalipa fidia ya mali zao ili kupisha upanuzi wa barabara ya kuelekea kwenye mradi wa umwagiliaji.

 

Wakizungumza kwenye mkutano wa hadhara wa mgombea Ubunge Jimbo la Chalinze kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ridhiwani Kikwete ambapo wakazi wa Kijiji hicho walisema kuwa tathmini ya upanuzi huo haukuwashirikisha wananchi na utaathiri mali zao.

 

Mkazi wa Kijiji hicho aliyejitambulisha kwa jina la Ally Hemed alisema kuwa mradi huo ambao ni wa kampuni hiyo ambapo imeweka alama za kupita barabara hiyo na kusema kuwa hakutakuwa na fidia yoyote itakayotolewa kwa uharibifu wa mali zao.

 

“Wamekuja hapa kijijini na kuweka alama za kuonyesha barabara itapita wapi ambapo katika maeneo hayo kuna mali zetu zitaathiriwa ikiwa ni pamoja na nyumba, mazao ya nanasi, miti na vitu vingine ambapo tumeambiwa kuwa hatutalipwa chochote jambo ambalo tunaona kuwa hatutatendewa haki mara zoezi hilo litakapoanza,” alisema Hemed.

 

Alisema kuwa kutokana na kutolipwa wao hawako tayari kuruhusu greda la kuchonga barabara kupita kwenye maeneo yao hadi watakapolipwa fidia za mali zao.

 

“Hatuna tataizo na kuchongwa barabara yetu lakini tunachoomba tulipwe kwanza fidia ndipo upanuzi ufanyike kama unavyoona mananasi yetu karibu yatakomaa na nyumba zetu zinaonekana zipo kwenye eneo la upanuzi wao watulipe kwanza ndipo wafanye upanuzi huo,” alisema Hemed.

 

Kwa upande wake mgombea udiwani kata ya Kiwangwa Malota Kwaga alisema kuwa jambo hilo limekuwa ni kero kubwa kwa wakazi hao hivyo ni vema suala lao likaangaliwa kabla ya utekelezaji wake.

 

Kwaga alisema kuwa wananchi wametoa malalamiko yao kwa wahusika lakini hawajaonesha nia ya kutoa fidia kwa watu ambao wataathiriwa na zoezi hilo.

 

Naye Ridhiwani alisema kuwa wahusika hao wanapswa kulipa fidia kabla ya kutekeleza mradi huo kwani haipendezi watu kuharibiwa mali zao bila ya kulipwa fidia.

 

Ridhiwani alisema kuwa tayari amewasiliana na wahusika na kuwaambia kuwa walipe kwanza fidia kabla ya kuanza upanuzi huo wa barabara hiyo inayoelekea kwenye mradi huo.

 

 “Sheria haisemi hivyo lazima unapofanya suala la maendeleo kwenye ardhi lazima ulipe fidia kwenye maeneo ambayo unayaendeleza,” alisema Ridhiwani.

 

Aidha alisema kuwa jambo hilo ni la maendeleo lakini pia liangalie haki za wananchi ambao mali zao zitaathiriwa na maendeleo hayo hivyo kwa sasa hakutafanyika chochote hadi malipo yatakapofanyika.

 

Mwisho.

 

Sunday, October 18, 2015

HABARI MOTO MOTO ZA KAMPENI ZA UCHAGUZI UCHAGUZI JIMBO LA CHALINZE

Na John GagariniChalinze

MGOMBEA Ubunge Jimbo la Chalinze wilayani Bagamoyo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCMRidhiwani Kikwete amekanusha kumtuma mgombea wa Chama Cha (SAUShaban Maulid kugombea Udiwani Kata ya Talawanda.

Akizungumza kwenye mikutano ya kampeni iliyofanyika kwenye Vijiji vya KisangaVundumu na Talawanda kwenye kata hiyo alisema kuwa yeye hajamtuma mtu huyo wala hajawahi kukutana naye.

Ridhiwani alisema kuwa yeye hawezi kumtuma mtu kwenda kugombea na kama ni kumtaka mtu basi angependekeza kutoka chama chake na si chama kingine kwani hakuna ushirikiano na vyama vingine.

“Huyo mtu kwanza na mshangaa kwani sijawahi kumuona wala sijawahi kukutana naye wala sijawahi kumtuma mtu namshangaa unajua wagombea wengine hawana sera hivyo wanatumia majina ya watu kujipatia umaarufu,” alisema Ridhiwani.

Alisema kuwa huo ni uzushi na wananchi hawapaswi kumsikiliza mtu huyo kwani chama chake hakina uhusiano na CCM wala na yeye na hajawahi hata kukutana naye.

“Achaneni na maneno ya kutuvuruga kwani kwa sasa sisi tunafanya kampeni ili kuhakikisha chama cehtu kinashinda kwenye nafasi zote ikiwemo UraisUbunge na Udiwani hivyo wasituvurge wakati huu wa kampeni kama hawana sera wakae pembeni,” alisema Ridhiwani.

Kwa upande wake meneja wa kampeni Jimbo la Chalinze Alhaj Amir Mkangata alisema kuwa anamshangaa mgombea huyo kwani hakuna muungano baina ya CCM na SAU kama ilivyo kwa muungano wa vyama vya upinzani vinavyounda UKAWA.

Alhaj Mkangata alisema kuwa wagombea kama hao hawana uwezo hivyo wanatafuta njia ya kujipenedekeza ili kuonyesha kuwa wametumwa kugombea.

“CCM haijaungana na chama kingine sasa mgombea huyo anavyojitapa kuwa ametumwa na CCM atuambie umoja huo unaitwaje atuambie hapa na tunamshangaa aache kabisa kutengeneza maneno ya uongo,” alisema Mkangata.

Kwa upande wake mgombea udiwani kata ya Talawanda Said Zikatimu alisema kuwa endapo atachaguliwa atahakikisha kuwa changamoto zilizopo kwenye kata hiyo zikiwemo za Afya, Elimu na Maji.

Mwisho.

Na John Gagarini, Chalinze

WAKULIMA na Wafugaji kwenye Kijiji cha Lulenge Jimbo la Chalinze wilayani Bagamoyo mkoani Pwani wametakiwa kuheshimiana ili kuepusha migogoro inayoweza kujitokeza na kusababisha vurugu zinazopelekea kuvunja amani baina ya wananchi.

Hayo yalisemwa na mgombea Ubunge Jimbo la Chalinze kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ridhiwani Kikwete wakati wa mkutano wa kampeni kwenye kijiji cha Lulenge kata ya Ubena.

Ridhiwani alisema kuwa tatizo kubwa la migogoro linatokana na pande mbili hizo kutoheshimu mipaka yao kwani kuna baadhi ya maeneo yametengwa kwa jamii hizo mbili.

“Mnaweza kuepusha migogoro kwa kuheshimiana na kuheshimu mipaka iliyopo kwani kila mmoja akimweshimu mwenzake migogoro haitakuwepo na watu wataishi kwa Amani na upendo,” alisema Ridhiwani.

Alisema kuwa serikali inajitahidi kuhakikisha inaondoa migogoro ikiwa ni pamoja na kutenga maoeneo kwa ajili ya mipango ya matumizi bora ya ardhi wakulima na wafugaji kwa baadhi ya maeneo huku mengine yakiwa yanaandaliwa kufanywa hivyo.

“Nyie ni ndugu hakuna sababu ya kugombana na kuingia kwenye migogoro isiyokuwa ya lazima kwani mtashindwa kufanya shughuli za maendeleo kutokana na migogoro hiyo,” alisema Ridhiwani.

Naye mgombea udiwani kupitia chama hicho Nicholaus Myuwa alisema kuwa atatumia taaluma yake ya kuwa Mwanasheria kuikabili migogoro hiyo kwa kuziweka pamoja jamii hizo.
Myuwa alisema kuwa endapo atachaguliwa kuwa diwani watahakikisha changamoto za maji, zahanati na barabara zinatatuliwa kwa kuwashirikisha wananchi.

Mwisho.

Na John Gagarini, Chalinze

WANANCHI wa Jimbo la Chalinze wametakiwa kutowachagua wagombea wa vyama vya upinzani kwani wengi wao ni viongozi wa msimu ambao wanajitokeza nyakati za uchaguzi.

Hayo yalisemwa na meneja wa kampeni wa Jimbo hilo Alhaj Amir Mkangata wakati wa mikutano ya kampeni ya mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ridhiwani Kikwete kwenye kata ya Miono.

Alhaj Mkangata alisema kuwa chama chenye uwezo wa kuwaletea maendeleo wananchi ni CCM na vyama vingine viongozi wao hawana uwezo hivyo ni vema wakaendelea kukiamini chama.

“Msiwachague wapinzani kwani wengi wao wanajitokeza wakati wa uchaguzi lakini uchaguzi ukishaisha hawaonekani hivyo mkiwachagua hamtawapata kwani wengine hawajulikani hata wanapoishi lakini wa CCM wanafahamika na wanatambulika,” alisema Alhaj Mkangata.

Alisema kuwa CCM imechagua wagombea wenye uwezo na wanasifa za kuongoza lakini wagombea wa upinzani hawana uwezo wa kuongoza hivyo hakuna sababu ya kuwachagua.

“CCM imefanya kazi kubwa ya kuwaletea wananchi maendeleo hivyo hakuna sababu ya kuchagua chama kingine kutawala hivyo msihadaike na wapinzani ambao wanaongopa kuwa wataleta maendeleo msikubali kudanganyika,” alisema Alhaj Mkangata.

Aidha alisema kuwa kwa mwaka huu chama kimejipanga kuhakikisha kinapata ushindi wa kishindo ili kiweze kuongoza na kuleta maendeleo kwa wananchi.

Aliwataka wananchi kuichagua CCM kwani ina uwezo wa kuongoza na wagombea walioingia kwenye kinyanganyiro cha ugombea kwenye ngazi mbalimbali wana uwezo kwani wamechaguliwa kwa uwezo wao.

Mwisho.

Na John Gagarini, Chalinze

KIJIJI cha Lulenge kata ya Ubena Jimbo la Chalinze wilayani Bagamoyo kinatarajia kuanza ujenzi wa zahanati Desemba mwaka huu ili kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa huduma za afya.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mwenyekiti wa Kijiji hicho Lucas Sultan alisema kuwa ujenzi huo utaanza baada ya kukamilika michango ya kila kaya.

Sultan alisema kuwa walikubaliana kwenye mkutano wa Kijiji kila kaya itoe kiasi cha shilingi 20,000 kwa ajili ya kujenga zahanati kwa ajili ya kuwapatia huduma ya afya.

“Tayari tuna eneo la ukubwa wa hekari tano kwa ajili ya kufanya ujenzi huo kwani ndani ya miezi michache ijayo tutakuwa tumekamilisha michango hiyo ili kuanza ujenzi,” alisema Sultan.

Alisema kuwa kwa kaya itakayoshindwa kutoa mchango huo atapaswa kufanya shughuli za kijamii kama sehemu ya mchango wake ili kila mtu atoe jasho lake kwenye kijiji.

Alisema kuwa kwa sasa wanapata huduma ya afya kwenye zahanati binafsi ambako ni mbali kwani usafiri uliopo ni wa pikipiki ambapo gharama yake ni shilingi 8,000 kwenda na kurudi.

“Gharama za kwenda kupata matibabu ni kubwa sana hivyo ndiyo maana tuliona kuwa kuna haja ya kweza kuanzisha ujenzi wa zahanati ili kukabiliana na changamoto hiyo,” alisema Sultan.

Aidha alisema kuwa changamoto nyingine ni kwamba sehemu kubwa ya kijiji iko kwenye hifadhi ya Wami Mbiki hivyo kushindwa kufanya shughuli za kimaendeleo.

“Suala la Kijiji kuwa kwenye hifadhi linafanyiwa kazi na tunaamini tutapata majibu mazuri na tunaamini mipaka itatengenezwa na tutaishi kwa utaratibu mzuri,” alisema Sultan.

Alisema kuwa Kijiji hicho kina jumla ya wakazi wapatao 2,700 huku kukiwa na mifugo mbalimbali ngombe wakiwa 17,000, mbuzi 4,000 na mbuzi 2,000 ambapo wakazi wake ni wakulima na wafugaji.

Mwisho.

Na John Gagarini, Chalinze

MGOMBEA Ubunge Jimbo la Chalinze kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ridhiwani Kikwete amesema kuwa endapo atafanikiwa kuwa mbunge atahakikisha anasimamia upelekwaji wa fedha pensheni za wazee kwa wakati.

Aliyasema hayo katika kijiji cha Tukamisasa kata ya Ubena na kusema kuwa wazee wanapaswa kuheshimiwa na kupewa stahiki zao kwani wamefanya kazi kubwa ya kuifanya nchi ifikie hapa ilipo.

Ridhiwani alisema kuwa kwa kuwa sera ya chama inaonyesha kuwa kuanzia mwaka 2016 wazee watakuwa wanapata pensheni zao kwa ajili ya kuwasaidia katika maisha yao.

“Wazee wetu wamefanya kazi kubwa hivyo kuna haja ya kuhakikisha wanapata stahiki zao kwani walifanya kazi kubwa kuikomboa nchi na kuifanya iwe kama ilivyo sasa moja ya vitu nitakavyovisimamia ni kuhakikisha fedha zao zinakuja kwa wakati,” alisema Ridhiwani.

Alisema kuwa wazee wanakabiliwa na changamoto nyingi hivyo wakipata pensheni zao zitawasaidia kuweza kujikimu na kumudu mambo madogomadogo tofauti na ilivyo sasa.

“Wazee wakilipwa pensheni zao zitawasaidia kumudu maisha yao kwani walikuwa wakiishi kwenye hali ngumu kutokana na kukosa fedha hata za kununua vitu vidogovidogo ambavyo vingewasaidia kumudu maisha,” alisema Ridhiwani.

Aidha wazee wamehudumia nchi ya Tanzania na kutumia nguvu zao na jasho lao hivyo ni haki yao sasa kupata pensheni ambayo itawafanya wajisaidie kwenye maisha yao.

“Mbali ya kusimamia malipo hayo pia nitahakikisha wanapata huduma mbalimbali ambao ni fursa kwao ikiwa ni pamoja na matibabu pamoja na mikopo ambayo itawasaidia kwenye ujasiriamali,” alisema Ridhiwani.

Mwisho.

Wednesday, October 14, 2015

RIDHIWANI AMWAGIA SIFA DK MAGUFULI

Na John Gagarini, Chalinze
MGOMBEA Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dk John Magufuli amepongezwa kwa kuuachia mkoa wa Pwani hususani wilaya ya Bagamoyo miradi mikubwa ambayo itakapokamilika itasaidia kuinua kipato cha wakazi wa mkoa huo.
Miradi hiyo ambayo inatoka kwenye Wizara Ujenzi na Miundombinu aliyokuwa akioongoza Dk Magufuli kabla ya kuteuliwa na chama chake kuwa mgombea Urais kwenye kinyanganyiro kitakachofanyika Oktoba 25 mwaka huu.
Pongezi hizo zimetolewa na mgombea Ubunge wa Jimbo la Chalinze kupitia chama hicho Ridhiwani Kikwete, wakati wa mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye Kijiji cha Miono wilayani Bagamoyo na kusema kuwa mgombea huyo kila mkoa ameupatia miradi ambayo itachochea maendeleo.
Ridhiwani alisema kuwa Dk Magufuli ni kiongozi ambaye anastahili kuongoza nchi hii kwani wakati akiwa waziri alihakikisha kila mkoa unatumia rasilimali zake viuzuri ili kujiletea maendeleo hali ambayo imesababisha nchi kupiga hatua.
“Sisi wakazi wa wilaya ya Bagamoyo tunamshukuru kwani ametuachia miradi mikubwa ikiwa ni pamoja na ule wa Barabara ya Afrika Mashariki itakayoanzia Bagamoyo,  Makuruge,  Saadani hadi mkoa wa Tanga hadi Mombasa nchini Kenya,” alisema Ridhiwani.
Alisema kuwa mradi mwingine ni ule wa Bandari ambayo itakuwa ni kubwa ambao utaanza wakati wowote kuanzia sasa kwani mipango tayari imekamilika huku mradi wa barabara tatu zitakazoanzia Jijini Dar es Salaam hadi mkoani Morogoro pia mzaini wa kisasa uliopo Vigwaza ambao tayari unafanya kazi.
“Mradi mwingine ni ule wa upanuzi wa Daraja la Mto Wami ili kupunguza ajali zinazotokea kwenye daraja hilo ambapo kwa sasa magari hayawezi kupishana, hakika miradi hii ni mikubwa na itafungua fursa za maendeleo kwa kukuza uchumi wao kutumia fursa zilizopo na zitakazokuwepo kwenye miradi hiyo,” alisema Ridhiwani.
Aidha alisema Dk Magufuli ni kiongozi ambaye hana kashfa yoyote na ameonyesha kuwa anafaa kuliongoza Taifa la Tanzania kutokana na uchapa kazi wake pamoja na uadilifu aliokuwa nao ukilinganisha na viongozi wengine wanaowania nafasi hiyo.
Aliwataka watanzania kumchagua kwa kumpiga kura nyingi za kishindo ili awe Rais wa awamu ya tano na anaamini kuwa uwezo wa kuongoza nchi anao akiwa chini ya CCM ambao kwa wakati huu imechagua viongozi wenye sifa na wanaopendwa na wananchi.

Mwisho.
 Meneja kampeni wa Jimbo la Chalinze Alhaj Amiri Mkangata kushoto akimtambulisha mgombea Ubunge Jimbo la Chalinze kupitia Chama Cha Mapinduzi CCM Ridhiwani Kikwete kwenye Kijiji cha Kikwazu wilayani Bagamoyo

Mgombea Ubunge Jimbo la Chalinze kupitia CCM Ridhiwani Kikwete akizindua  huku akiwa amekaa kwenye kigoda tawi la vijana wa Boda boda kwenye Kijiji cha Pongwemnazi 


Mgombea Ubunge Jimbo la Chalinze kupitia CCM Ridhiwani Kikwete akizindua tawi kwa kupandisha bendera kwenye moja ya matawi wakati wa kampeni kuwania kiti hicho.

 Mgombea Udiwani kata ya Kimange kwa tiketi ya CCM Husein Hadingoka akiwahutubia wananchi wa Kijiji cha Kikwazu wakati wa mkutano wa kampeni

 Mama Mwenye ulemavu ambaye jina lake halikuweza kufahamika mara moja akiwa kwenye mkutano wa kampeni wa Mgombea wa CCM Ridhiwani Kikwete kwenye Kijiji cha Pongwemnazi kata ya Kimange.

Baadhi ya wananchi waliojitokeza kwenye mkutano wa kampeni wa mgombea wa CCM Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete kwenye kijiji cha pongwekiona kata kimange wilayani bagamoyo 

 wananchi wa kijiji cha pongwekiona wakiwa wanamsikiliza mgombea ubunge jimbo la chalinze ridhiwani kikwete hayupo pichani wakati wa mkutano wa kampeni

 Mwigizaji aitwaye Puto akitoa burudani kwa wananchi waliohudhuria mkutano wa kampeni kwenye kijiji cha Pongwemnazi kata ya Kimange wilayani Bagamoyo

 Mwimbaji Sam wa Ukweli akiimba na moja ya wananchi kwenye mkutano wa kampeni wa CCM kwenye kijiji cha Pongwemnazi 

 Wagombea Ridhiwani Kikwete kushoto akicheza na mgombea Udiwani kata ya Kimange Hussein Hadingoka wakati wa uzinduzi wa kampeni za udiwani kwenye kijiji cha Pongwekiona

 Mgombea Ubunge Jimbo la Chalinze kupitia Chama Cha Mapinduzi CCM Ridhiwani Kikwete kushoto akimkabidhi ilani mgombea udiwani wa kata ya Kimange Hussein Hadingoka wakati wa uzinduzi wa kampeni za udiwani kwenye Kijiji cha Pongwekiona

 Mgombea Ubunge Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete kupitia CCM akimkabidhi ilani ya uchaguzi ya mwaka 2015-2020, diwani wa Viti maalumu Nuru Mpwimbwi wakati wa uzinduzi wa kampeni za udiwani kata ya kimange kwenye Kijiji cha Pongwekiona 

 Mgombea Ubunge wa CCM Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete akimkabidhi moja ya wanachama wapya kwenye Kijiji cha Pongwekiona

Friday, October 9, 2015

DK MAGUFULI AFUNIKA BAGAMOYO

 Baadhi ya wakazi wa wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani wakimskiliza mgomea Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi CCM John Magufuli kwenye uwanja wa shule ya msingi Majengo Bagamyo.

 Mkuu wa mkoa wa Tanga mwenye miwani Mwantumu Mahiza akielekeza jambo wakati wa kumsubiri mgombea Urais kwa tiketi ya CCM Dk John Magufuli kwenye kijiji cha Mbwewe wilayani Bagamoyo

 Mgombea Ubunge Jimbo la Chalinze  wilayani Bagamoyo Ridhiwani Kikwete akifurahia jambo na wananchi wa Kijiji cha Mbwewe wilayani Bagamoyo mkoani Pwani wakati wa kumsubiria mgombea Urais kwa Tiketi ya CCM Dk John Magufuli

 Baadhi ya wananchi wakiwa na mabango

 Mgombe urais wa CCM Dk John Magufuli kulia akitete jambo na Waziri wa Elimu na Mafunzo ambaye pia ni mgombe Ubunge Jimbo la Bagamoyo Dk Shukuru Kawambwa 
Aliyekuwa mgombea Ubunge kura za maoni wa CCM Jimbo la Bagamoyo Abdul Sharif kulia akiwa amepozi kushoto ni Dk zainab Gama katibu mwenezi wa CCM mkoa wa Pwani

 Abdala Bulembo mjumbe wa kampeni wa CCM Taifa akionyesha mfano wa fomu ya kupigia kura

 Mgombea Urais wa CCM Dk John Mgafuli akiongea na wananchi wa Bagamoyo waliojitokeza kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye uwanja wa shule ya msingi Majengo

 Wananchi wakiinua mikono juu kumuunga mkono mgombea Urais kwa tiketi ya CCM Dk John Magufuli

 Wananchi wakimshangilia mgombea Urais Dk John Magufuli

 Mgombea Urasi CCM Dk John Magufuli katikati akisisistiza jambo kushoto ni Waziri wa Elimu na Mafunzo na mgombea Ubunge Jimbo la Bagamoyo mkoani Pwani Dk Shukuru Kawambwa kushoto na Ridhiwani Kikwete Mgombea Ubunge Jimbo la Chalinze


 Mgombea Urasi Dk John Magufuli kushoto akimnadi mgombea Ubunge Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika bagamoyo

 Dk John Magafuli kulia mgombea Urais CCM akimtambulisha mgombea Ubunge Jimbo la Bagamoyo Dk Shukuru Kawambwa

 Baadhi ya madiwani wa wilaya ya Bagamoyo

 Mgombea Ubunge kupitia Umoja wa Wanawake UWT mkoa wa Pwani Subira Mgalu kulia akitambulishw ana mgombea Urais CCM Dk John Magufuli wakati wa mkutano wa kampeni uliofanyika Bagamoyo.

Wednesday, October 7, 2015

WAOMBA KUONDOLEWA 100,000 KWA AJILI YA GARI LA WAGONJWA

Na John Gagarini, Chalinze
WAKAZI wa Kijiji cha Kwaruhombo Jimbo la Chalinze wilayani Bagamoyo wametoa kilio chao kwa kuomba viongozi watakaochaguliwa kwenye uchaguzi mkuu kuwaondolea changamoto ya kutozwa kiasi cha shilingi 100,000 kwa ajili ya mafuta ya kuweka kwenye gari la wagonjwa wanaopata rufaa toka kwenye kituo cha afya cha Kwaruhombo.
Akizungumza Kijijini hapo mara baada ya mkutano wa kampeni wa mgombea ubunge jimbo hilo Ridhiwani Kikwete, Ally Rashid alisema kuwa hali hiyo inawapa wakati mgumu kutokana na hali halisi ya kipato chao kidogo.
Rashid alisema kuwa changamoto hiyo ni kubwa kwani wao kupata fedha hizo mzigo mkubwa ikizingatiwa maisha ya Kijijini ni magumu na hawana vyanzo vikubwa vya mapato zaidi ya kilimo ambacho nacho kimekuwa si cha uhakika kutokana na mvua kutokuwa za uhakika.
“Tunaomba viongozi watakaochaguliwa wahakikishe wanashughulikia kero hii kwani kwa sasa ni muda mrefu na tumekuwa tukilalamika lakini hakuna hatua zinazochukuliwa pia tunaomba Halmashauri itenge bajeti kwa ajili ya mafuta ya gari hilo la wagonjwa,” alisema Rashid.
Naye mgombea Udiwani wa kata ya Kwaruhombo ramadhan mahamba alisema kuwa kero hiyo ni kubwa kwa wanakijiji na kumwomba mgombea huyo wa ubunge kuhakikisha nawasemea huko halmashauri ili gari hilo liwe na bajeti ya mafuta.
Mahamba alisema kuwa mbali ya kero hiyo ya wananchi kutakiwa kutoa kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya kuwekea mafuta ya kuwasafirisha wagonjwa wanapopata rufaa kwenda hospitali kubwa pia kuna tatizo la upungufu wa wahuduma wa afya.
Kwa upande wake Ridhiwani Kikwete alisema kuwa kero hiyo ameisikia na mara atakapochaguliwa atahakikisha anashinikiza kutenga fedha za mafuta kwa ajili ya vituo vya afya ili kuwaondolea mzigo wananchi.
Ridhiwani alisema kuwa utaratibu umewekwa na Halmashauri wa bajeti ya mafuta ya magari hayo hivyo akichaguliwa hiyo ni moja ya vitu atakavyovifuatilia kwa karibu ili kuhakikisha mafuta yanapatikana kwenye gari hilo.
Mwisho.
NA John Gagarini, Chalinze
KIJIJI ch Kwaruhombo Jimbo la Chalinze wilayani Bagamoyo kinakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa maji hali inayowafanya wakazi wake kuchota maji ya visima vya kienyeji ambavyo viko chini ya ardhi huku vingine vikiwa na urefu wa futi 12.
Mbali ya visima hivyo kuwa na urefu mkubwa ambapo huwabidi wachotaji wengi wao wakiwa ni wakinamama kushuka kwa kutumia ngazi pia kumekuwa na foleni kubw ahali ambayo inawafanya wakeshe wakisubiri maji ambayo yamekauka kutokana na hali ya kiangazi.
Moja ya wanakijiji aliyejitambulisha kwa jina la Hadija Yusufu alisema kuwa maji ni changamoto kubwa kwao kwani wamekuwa wakitumia muda mrefu wa kusubiria maji hasa kipindi hichi cha kiangazi pia ni hatari kwa maisha yao kutokana na urefu wa visima hivyo.
“Tunaiomba serikali kutusaidia kupatikana maji ili kutuondolea adha hii kwani tumeletewa maji ambapo kuna vioski kwa ajili ya kuchota maji lakini havitoi maji hatujui kuna tatizo gani linalosababisha maji yasitoke hivyo tumebaki tunategemea maji ya visima hivyo vya kienyeji ambavyo navyo ni hatari kweteu,” alisema Yusufu.
Kwa upande wake mgombea udiwani kwa tiketi ya CCM Ramadhan Mahamba alisema kuwa endapo atachaguliwa atahakikisha anafuatilia suala hilo ili maji yaweze kupatikana kwa kutatua changamoto iliyopo ili maji yapatikane na kuwaondolea kero wananchi.
Naye mgombe ubunge wa Jimbo hilo Ridhiwani Kikwete alisema kuwa tatizo la ukosefu wa maji ni kutokana na miundombinu iliyowekwa kuwa ya zamani hivyo kushindwa kuhimili kasi ya maji na kupasuka.
Ridhiwani alisema kuwa endapo atachaguliwa atahakikisha miundombinu mipya ambayo ni mabomba inapatikana ili kuondoa kero hiyo inayowanyima usingizi wananchi hao ambao hicho ni kilio chao kikubwa.
Mwisho.

Tuesday, October 6, 2015

DIWANIA AHIDI KUNUA GARI LA WAGONJWA

Na John Gagarini, Chalinze
MGOMBEA Udiwani kata ya Vigwaza Jimbo la Chalinze kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Muhsin Bharwan amesema kuwa endapo atafanikiwa kuchaguliwa atanunua gari la kubeba wagonjwandani ya kipindi cha miezi sita kwa ajili ya kuwapeleka wagonjwa wanaopata rufaa kwenda hospitali kubwa.
Aliyasema hayo kwenya mkutano wa kampeni ya kumnadi mgombea Ubunge wa Jimbo hilo Ridhiwani Kikwete kwenye Kijiji cha Buyuni kwenye kata hiyo na kusema kuwa gari hilo litatumika kwenye vijiji vya kata hiyo ya Vigwaza.
Bharwan alisema kuwa kutokana na kata hiyo kutokuwa na gari la wagonjwa wakazi  hao wamekuwa wakipata taabu kuwapeleka wagonjwa wao wanaopata rufaa kwenda kwenye hospitali kubwa kama vile Tumbi au Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
“Endapo nitafanikiwa kuchaguliwa kwenye nafasi hii ya Udiwani ndani ya miezi sita nitahakikisha nimenunua gari la kubeba wagonjwa, tutamwomba mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo kupata msamaha wa kodi toka serikalini ili kufanikisha kupatikana gari hilo,” alisema Bharwan.
Alisema kuwa kwa kushirikiana na Wanakijiji hao atahakikisha ujenzi wa zahanati unakamilika ili waanze kupata huduma za afya kijijini hapo badala ya kupata huduma hiyo mbali kwani kwa sasa hakuna huduma hiyo kutokana na kukosa zahanati.
“Sera inasema kila Kijiji lazima kiwe na zahanati na kata inakuwa na kituo cha afya hivyo tutahakikisha tunatimiza hilo ili kusogeza huduma za afya kwa wananchi,” alisema Bharwan.
Kwa upande wake Ridhiwani Kikwete alisema kuwa moja ya vipaumbele vyake ni pmaoja na upatikanaji wa huduma za afya ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wahudumu wa afya wanapatikana.
Ridhiwani alisema kuwa pia upatikanaji wa madawa, vifaatiba, pamoja na ujenzi wa nyumba za wahudumu wa afya ili waishi kwenye vituo vyao vya kazi kwa lengo la kutoa huduma kwa urahisi.
Naye mkazi wa Kijiji hicho Pamilasi Sambana alisema kuwa huduma hizo za kiafya zikipatikana itawasaidia kukabiliana na matatizo yanayotokana na umbali wa upatikanaji wa huduma hizo.
Sambana alisema kuwa huduma za afya ni moja ya vilio vya wananchi na mara anapotokea mgonjwa inakuwa ni taabu sana hivyo wanawaomba wagombea hao kutimiza ahadi zao ili kuwapunguzia adha ya kupata huduma hizo.
Mwisho.

Na John Gagarini, Chalinze
UTUNGWAJI wa sheria ndogondogo kwenye Kijiji cha Malivundo kata ya Pera kwenye Jimbo la Chalinze kumesaidia kupunguza migogoro baina ya wakulima na wafugaji ambayo ilikuwa imekithiri katika Kijiji hicho.
Akizungumza na waandishi wa habari moja ya wanakamati ya maridhiano baina ya wakulima na wafugaji ya Kijiji hicho Charles Antony alisema kuwa tangu kuundwa kamati hiyo miezi minne iliyopita migogoro imepungua kwa kiasi kikubwa.
Antony alisema kuwa mkutano wa Kijiji ulipitisha sheria ya kumtoza mfugaji gunia nane za mahindi kwa hekari moja  endapo ataingiza mifugo kwenye shamba la mkulima ambalo lina mazao na kwa shamba ambalo limeandaliwa halina mazao atatozwa kiasi cha shilingi 50,000 kwa hekari moja  na 40,000 kwa shamba ambalo limevunwa mazao.
“Sheria hii iliridhiwa na wakulima na wafugaji licha ya kuwa tatizo kubwa lipo kwa wafugaji ambao wamekuwa wakilisha mifugo kwenye mashamba ya wakulima hali ambayo ilikuwa inasababisha migogoro ya mara kwa mara lakini toka sheria hii imepitishwa na Kijiji matatizo hayo yamepungua,” alisema Antony.
Alisema kuwa endapo mlalamikiwa anakataa kutekeleza agizo la kamati suala hilo linapelekwa ngazi ya kata ambako nao husisitiza mlalamikiwa kulipa faini hiyo mara baada ya kamati kupita kwenye eneo ambalo limefanyiwa uharibifu.
“Kamati hii inaundwa na watu 10 wakulima watano na wafugaji watano ambao huangalia ukubwa wa tatizo kisha hutoa maamuzi juu ya uharibifu uliofanywa lakini pia pande mbili zinazohusika nazo huruhusiwa kukaa na kuangalia namna ya kutatua tatizo hilo,” alisema Antony.
Ashura Ramadhan alisema kuwa kwa sasa angalau mazao yao yanaweza kukua bila ya tatizo lolote tofauti na ilivyokuwa awali ilikuwa ni ugomvi mkubwa kati ya wakulima na wafugaji lakini kwa sasa angalau amani inapatikana kutokana na sheria hizo.
Kwa upande wake mgombea udiwani  kata ya Pera kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM)Lekope Laini alisema kuwa endapo atachaguliwa atahakikisha anatumia taaluma yake ya sheria kukabili migogoro ya wakulima na wafugaji pia kuwaunganisha ili waishi kama ndugu.
Naye mgombea Ubunge Jimbo la Chalinze kupitia CCM Ridhiwani Kikwete alisema kuwa endapo atachaguliwa atahakikisha mpango wa matumizi bora ya ardhi unawekewa mkazo ili kuwe na maeneo ya wakulima na wafugaji kupunguza migogoro hiyo.
Mwisho.
Na John Gagarini, Chalinze
WAKINAMAMA wa Jamii ya wafugaji kwenye Kijiji cha Wafugaji cha Chamakweza wameiomba serikali kuwapatia matenki makubw aya kuhifadhia maziwa pamoja na soko la uhakika la kuuza maziwa yao.
Akizungumza kwenye mkutano wa kampeni wa mgombea Ubunge Jimbo la Chalinze kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ridhiwani Kikwete Anastazia Masaka alisema kuwa maziwa wanayozalisha ni mengi lakini hawana sehemu ya kuhifadhia pamoja na soko la uhakika.
Masaka alisema kuwa wanaiomba serikali kuwapatia matenki hayo ili waweze kuhifadhi maziwa yao ili yasiweze kuharibika wakati yakisubiri kusafirishwa au kuwasubiri wanunuzi wa maziwa hayo ambayo yanapatikana kwa wingi kwenye kijiji chao ambacho ni cha wafugaji.
“Maziwa ni mengi lakini tunataabika na soko pamoja na sehemu ya kuhifadhia hivyo tunaiomba serikali kupitia mgombea Ubunge kutusaidia kupata matenki ya kuhifadhia pamoja na soko la uhakika kwani soko likiwa kubwa vijana wetu watapata ajira kupitia maziwa,” alisema Masaka.
Alisema kuwa wakipata ufumbuzi wa masuala hayo basi itakuwa ni ufumbuzi wa changamoto wa namna ya kuhifadhi pamoja na soko la kuuza bidha hiyo ambayo inapendwa na watu kutokana na umuhimu wake kiafya.
Kwa upande wake Ridhiwani Kikwete alisema kuwa endapo atafanikiwa kuchaguliwa kwenye nafasi hiyo atahakikisha soko pamoja na matenki hayo vinapatikana ili kuwaondolea adha ya kuhifadhi maziwa yao pamoja na soko.
Ridhiwani alisema kuwa kwa kupitia umoja wao wa wauzaji maziwa atahakikisha anawaletea wanunuzi wa maziwa pia wanawezeshwa kuptia fedha ambazo zitatolewa kwa kila Kijiji kiasi cha shilingi milioni 50.
Naye mgombea Udiwani Lekope Laini alisema kuwa endapo atachaguliwa atahakikisha anakabiliana na changamoto za akinamama wa kifugaji ili nao waweze kujikwamua kiuchumi kwa kuwatengenezea mazingira mazuri ya kufanya shughuli zao.
Mwisho.

Na John Gagarini, Bagamoyo

KATIKA kuhakikisha kurahisisha utendaji kazi hasa katika kipindi hichi cha uchaguzi CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Bagamoyo mkoa wa Pwani kimetoa pikipiki 12 kwa makatibu kata kwenye Jimbo la Bagamoyo ili kuwaondolea tatizo la usafiri wakati wakutimiza majukumu yao.


 Akikabidhi pikipiki hizo mwenyekiti wa CCM wilayani hapo Maskuzi alisema walikuwa wakikabiliwa na changamoto ya ukosefu wa usafiri kwa makatibu hao hivyo kushindwa kutekeleza kikamilifu shughuli za chama.

Maskuzi alisema kuwa lengo lingine ni kuwawezesha makatibu kata hao kuweza kusimamia majukumu yao kikamilifu pamoja na uhai wa chama na kurahisisha shughuli hasa katika kipindi hichi cha uchaguzi.

“Utoaji wa pikipiki hizi zenye thamani ya  shilingi milioni 24 kwa makatibu wa kata ni muendelezo  ambapo awali kwenye awamu ya kwanza tulitoa pikipiki 15 katika Jimbo la Chalinze na sasa kumalizia na jimbo la Bagamoyo,” alisema Maskuzi.

Alisema kuwa kwasasa anaamini watendaji hao watafanya kazi zao pasipo usumbufu kwani tatizo kubwa lilikuwa ni ukosefu wa usafiri wa uhakika wakutembelea maeneo mbalimbali ya kazi.

“Pikipiki hizi tunazitoa sio kwa shughuli nyingine ila ni kwa ajili ya kutekeleza shughuli za kichama kwa kutembelea matawi,kusimamia uhai wa chama na kutekeleza majukumu yatakayotakiwa kufuatilia wakati huu wa kuelekea kwenye uchaguzi mkuu”alisema Masukuzi.

Kata zilizopatiwa pikipiki hizo ni pamoja na Mapinga, Kerege, Zinga, Kilomo, Yombo, Dunda, Magomeni, Kisutu na Nianjema, Makurunge na Fukayosi na pikipiki moja itakuwa kwa ajili ya mtendaji mkuu CCM wilayani hapo.
                            
Kwa upande wake katibu wa CCM kata ya Kisutu Buruhani Setebe alisema amepokea pikipiki na amekishukuru chama kwa kutambua changamoto yao hivyo atahakikisha anaitunza pikipiki hiyo.

Naye katibu wa CCM kata ya Mapinga ,Muhdin Mipango alisema awali walikuwa wakipata shida katika utendaji wa kazi zao ikiwa ni pamoja na kutembelea kwa miguu ama kukodi pikipiki ili kwenda kutembelea matawi.

                                          Mwisho.




Sunday, October 4, 2015

MCH MTIKILA AFARIKI AJALINI

Na John Gagarini, Chalinze
 
MWANASIASA Mkongwe hapa nchini ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama ChaDemocratic Party (DP) Mchungaji Christopher Mtikila (62) amefariki dunia na watu wengine watatu kujeruhiwa baada ya gari walilokuwa wakisafiria kuacha njia na kupinduka.
 
Kwa mujibu wa kamanda wa Polisi mkoani Pwani Jafary Mohamed alisema kuwa tukio hilo lilitokea huko Msolwa Barabara Kuu ya Dar es Salaam Morogoro wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani.
 
Kamanda Mohamed alisema kuwa ajali hiyo ilitokea saa 11:45 Alfajiri wakitokea mkoani Njombe wakiwa na gari aina ya Toyota Corola lenye namba za usajili T189 AGM lililokuwa likiendeshwa na dereva aitwaye George Steven (31) maarufu Ponera mkazi wa Mbezi Jijini Dar es Salaam.
 
"Gari hilo likiwa na abiria watatuakiwemo marehemu mkazi wa Mikocheni B, lilikuwa kwenye mwendo wa kasi liliacha njia na kuserereka pembeni mwa barabara kasha kupinduka ambapo marehemu alirushwa nje ya gari na kupoteza maisha papo hapo,"alisema Kamanda Mohamed.
 
Aliwataja waliojeruhiwa kuwa ni pamoja na dereva wa gari hio, Mchungaji Patrick Mgaya (57) na Ally Mohamed (42) wote wakazi wa Jijini Dar es Salaam ambao wote walikimbizwa kweye hospitali ya Rufaa ya mkoa ya Tumbi pamoja na kuhifadhi mwili wa marehemu.
 
"Chanzo caha ajali hiyo ni mwendo wa kasi wa dereva huyo ambao ulisababisha ashindwe kulimudu gari hilo na kuserereka pembeni ya barabara kasha kupinduka na kupelekea kifo hico cha kusikitisha cha mwanasiasa huyo," alisema Kamanda Mohamed.
 
Hata hivyo taarifa kutoka eneo la tukio zilisemakuwa mara baada ya ajali hiyo wahanga hao hawakuweza kupata msaada kwani eneo hilo halina makazi ya watu.
 
mwisho.