Thursday, October 2, 2014

KIBAKA AUWAWA KWA KUCHOMWA MOTO KWA WIZI WA PIKPIKI

Na John Gagarini, Kibaha
KIJANA mwenye umri kati ya miaka (25) na (30) anayedahaniwa kuwa ni kibaka ambaye jina lake halikuweza kufahamika ameuwawa kwa kuchomwa moto na wananchi wenye hasira kwa tuhuma za kuiba pikipiki.
Wananchi hao walifikia hatua hiyo baada ya kubaini kuwa mtuhumiwa huyo akiwa na mwenzake waliiba pikipiki hiyo huko Gairo mkoani Morogoro na kutaka kuiuza Chalinze wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo kaimu kamanda wa Polisi mkoani humo Athuman Mwambalaswa alisema kuwa tukio hilo lilitokea Septemba 25 mwaka huu majira ya saa 1 asubuhi eneo la Pera Chalinze wilaya ya Bagamoyo.
Kamanda Mwambalaswa alisema kuwa watuhumiwa hao wawili walikuwa na pikipiki ainaya ya Toyo yenye namba za usajili T 336 BZC ambayo inadhaniwa kuwa waliiba huko Gairo na walifika Chalinze kwa lengo la kutaka kuiuza.
“Vijana hao ambao ni wa kabila la Kimasai walifika hapo huku wakitafuta wateja wa pikipiki hiyo na wananchi hao walipowauliza uthibitisho wa pikipiki hiyo yaani kadi walishindwa kuonyesha na ndipo walipoanza kuwapiga na mmoja alifanikiwa kukimbia huku mwingine akipigwa kisha kuchomwa moto,” alisema Kamanda Mwambalaswa.
Alisema kuwa mwili wa marehemu ulikutwa mashambani ukiwa umechomwa moto na kuharibika vibaya sehemu mbalimbali za mwili.
Aidha aliwataka wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi kwani ni kinyume cha sheria na kuwataka kuwapeleka kwenye vyombo vya sheria ikiwa ni pamoja na polisi ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.
Mwisho.


SHERIA ZA USHIRIKA ZIMEPITWA NA WAKATI, UMRI WA URAIS UPUNGUZWE

Na John Gagarini, Mkuranga
MKUU wa mkoa wa Pwani Mwantumu Mahiza amesema kuwa sheria za Ushirika  zimepitwa na wakati hali ambayo inasababisha baadhi ya watu kutumia mwanya kuwadhulumu wakulima wa zao hilo hapa nchini.
Kutokana na fedha nyingi kutumiwa kwa matumizi binafsi na baadhi ya viongozi wa vyama vya ushirika kumesababisha chama kikuu cha ushirika cha mkoa CORECU kuwa na madeni makubwa ambapo mabenki yamekataa kukikopesha fedha kwa ajili ya ununuzi wa zao la korosho.
Aliyasema hayo wilayani Mkuranga wakati wa mkutano wa mfuko wa wakfu wa kuendeleza zao la korosho (CIDTF) kwa wakulima  na wataalamu wa mkoa wa Pwani na bodi ya zao la korosho nchini juu ya msimu mpya wa uuuzaji na ununuzi wa zao hilo.
Mahiza alisema kuwa baadhi ya viongozi wa vyama vya ushirika vya zao la korosho mkoani humo wamewadhulumu wakulima malipo ya korosho walizo wauzia wanunuzi hali iliyosababisha hasara kubwa kwa mkoa.
“Mfano mkoa wa Pwani ulikidhamini chama kikukuu cha ushirika cha mkoa (CORECU) kupata mikopo toka kwenye mabenki ambapo CRDB ilitoa bilioni 6 na NMB ilitoa biloni 3 lakini fedha hizo zimeshindwa kurejeshwa hali ilioyosababisha chama hicho kishindwe kukopeshwa tena,” alisema Mahiza.
Alisema kuwa kila wanapojaribu kuwachukulia hatua viongozi hao inashindikana kutokana na sheria zilizopo za ushirika ambazo zinaonekana zinawalinda viongozi hao hivyo kushindwa kuadhibiwa huku wakulima wakiendelea kudai fedha zao.
“Ukiwashitaki kwa makosa ya jinai ushirika unasema huwezi kuwashitaki kwa kosa la jinai lakini baada ya kufuata taratibu za kisheria tayari tunaweza kuchukua hatua ambazo ni stahiki kwa viongozi hao ambao baadhi yao wamezitumia fedha hizo kwa manufaa binafsi,” alisema Mahiza.
Aidha alisema kuwa sheria hizo si nzuri kwani zinawaumiza wakulima lakini kwa sasa mkoa umefikia hatua nzuri za kuweza kuwashtaki waliohusika na kula fedha za wakulima kwani ushirika sio kudhulumu watu bali ni kuboresha maslahi ya wakulima.
Kwa upande wake mwenyekiti wa mfuko wa kuendeleza zao la korosho Athuman Nkinde alisema kuwa maandalizi ya msimu wa kilimo kwa zao hilo tayari zimeanza na mkoa wa Pwani utapatiwa pembejeo za dawa za kupulizia pamoja na miche bora ya zao hilo ipatayo 70,000.
Nkinde alisema kuwa matarajio ni mkoa huo kuzalisha zao hilo kwa wingi ili kuboresha kipato cha wakulima kwani zao hilo ni utajiri endapo wakulima na wataalamu watawaelekeza kilimo bora cha zao hilo.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
MWENYEKITI wa Umoja wa Vijana (UVCCM) Taifa Sadifa Juma ameomba suala la umri wa kugombea Uspika na Urais liangaliwe ili kuwapa nafasi vijana kuweza kugombea nafasi hizo kwa kupunguza umri wa sasa wa miaka 40 na kuwa 30.
Aliyasema hayo wakati wa akiwahutubia vijana wa umoja huo kutoka Jimbo la Kibaha Mjini, alipokuwa akifunga kambi ya mafunzo ya vijana ya siku 10 ambayo yalifunguliwa na katibu mkuu wa Abdulrahman Kinana Septemba 19.
Sadifa alisema kuwa kwenye Ubunge unaruhusu umri wa kuanzia miaka 21 lakini kwenye nafasi hizo umri ni kuanzia miaka 40 jambo ambalo ameona kuwa vijana hawatendewi haki.
“Kama ubunge ni miaka 21 na Uspika pamoja na Urais angalau iwe kuanzia miaka 30 na kuendelea kwani kwa umri huo bado kijana ana nguvu na anaweza kutekeleza vema majukumu yake tofuati na kumchagua Rais mwenye umri mkubwa,” alisema Sadifa.
Alisema kuwa mambo yanabadilika ifike wakati sasa vijana nao wapate nafasi kutokana na uwezo wake kwani vijana ndiyo wenye nguvu na wanauwezo mkubwa wa kutekeleza majuku yao ikiwa ni pamoja na kuongoza.
“Nchi kama Kongo na Korea Marais wao ni vijana lakini wanaongoza vizuri hivyo hakuna sababu ya kuwawekea mazingira magumu ya kugombea nafasi hizo za juu wapewe nafasi kama watafanikiwa kuchaguliwa basi wachaguliwe kwani kiongozi siyo umri bali ni uwezo wa kuongoza,” alisema Sadifa.
Kw upande wake kamanda wa Vijana wa Kibaha Mjini Silvestry Koka alitoa sare 50 kwa makamanda wa umoja huo Green (Guard) zenye thamani ya shilingi milioni 2.5 na kuwataka vijana hao kuyatumia mafunzo hayo kukiimarisha chama.
 Awali akisoma risala ya kambi hiyo ya vijana katibu wa Umoja wa Vijana wa CCM Kibaha Mjini Khalid King alisema kuwa kambi hiyo iliwafundisha vijana 101 juu ya masuala mbalimbali yakiwemo ya itikadi za chama, ujasiriamali, uongozi na masuala mbalimbali ya kisiasa.
Mwisho.



WATOTO WANUNUA SIMU KUWASILIANA NA WAPENZI WAO

Na John Gagarini, Kibaha
IMEBAINIKA kuwa baadhi ya watoto wanaojishughulisha na biashara ndogondogo wilayani Kibaha mkoani Pwani wamejiingiza kwenye mahusiano ya kimapenzi ambapo fedha wanazopata wananunulia simu za mkononi ili kuwasiliana na wapenzi wao.
Watoto hao licha ya kuwa na umri mdogo lakini tayari wanajiingiza kwenye masuala ya mapenzi jambo ambalo ni hatari na linalosababisha kuingia kwenye ngono wakiwa na umri mdogo hivyo kuongeza vitendo vya ubakajiani ndani ya jamii.
Akizungumza mjini Kibaha wakati wa mafunzo ya kupinga vitendo vya ukatili kwa watoto kwa timu za kuzuia vitendo hivyo ndani ya jamii kwenye kata ya Kibaha wilayani humo mwenyekiti wa mafunzo hayo Alkhas Katopola alisema kuwa baadhi ya watoto wanamiliki simu ambazo wanazitumia kwa ajili ya mawasiliano na wapenzi.
“Inashangaza sana kuona watoto wadogo wanamiliki simu za mkononi na kikubwa wanachokifanya na hizo simu ni masuala ya mapenzi hivyo kutokana na umri wao kuwa mdogo ni kama vile wanabakwa kwa sasabu wengi wana mahusiano ya kimapenzi na watu wazima,” alisema Katopolo.
Katopola alisema kuwa wengi wa watoto hao ni wale ambao hawakupata nafasi ya kwenda au kuacha shule kutokana na sababu mbalimbali za kimaisha au wenyewe kukataa kuendelea na masomo.
“Pia baadhi ya watoto hawa wanategemewa na familia zao kwa ajili ya mahitaji ya nyumbani hivyo wazazi au walezi wanashindwa kuwadhibiti mara wafanyapo vitendo visivyofaa ikiwa ni pamoja na kujihusisha kwenye masuala ya mahusiano ya kimapenzi,” alisema Katopola.
Kwa upande wake mratibu wa shirika lisilo la kiserikali la (KICODET) la Kibaha lililoandaa mafunzo hayo Dk Rose Mkonyi alisema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kukabiliana na vitendo vya ukatili kwa watoto kwenye Halmashauri ya Mji wa Kibaha.
“Vitendo vya ukatili kwa watoto ni vingi na ndiyo sababu ya kuandaa mafunzo hayo ili jamii iweze kujua namna ya kutoa taarifa kwenye vyombo vya sheria na si kuvifumbia macho kama baadhi ya familia zinavyofanya kwani baadhi ya wanaofanya vitendo vya ukatili ni ndugu hivyo kuhofia mahusiano kuvunjika,” alisema Dk Mkonyi.
Dk Mkonyi alisema kuwa mafunzo hayo ambayo yatatumika kuunda timu za ufuatiliaji wa matukio mbalimbali ya ukatili kwa watoto yamewajengea uwezo wa kuweza kuwa na mtandao baina yao na vyombo vya sheria kama vile viongozi wa mitaa, waalimu, jeshi la polisi, mahakimu na wadau wengine wanaohusika kukabiliana na vitendo hivyo.
Kwa upande wake mwezeshaji wa mafunzo hayo Faustina Kayombo ambaye ni ofisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha alisema kuwa tatizo kubwa ni usiri unaofanywa na umaskini imekuwa ni vyanzo chanzo vikuu vya kuendela kwa vitendo hivyo.
Mradi huo ni wa miaka miwili ambapo mafunzo hayo yamefadhiliwa na Plan International, UNICEF, Save the Children na Jumuiya ya Ulaya na serikali kwa kushirikiana na shirika hilo la KICODET.
Mwisho.

  


MABANDA UMIZA YAONGEZA VITENDO VYA UBAKAJI

Na John Gagarini, Kibaha
BAADHI ya wadau wa watoto wilayani Kibaha mkoani Pwani wameiomba serikali kuyafutia usajili mabanda ya video ambayo yamekuwa chanzo kikuu cha watoto wadogo kufanyiwa vitendo vya ubakaji.
Mabanda hayo yamekuwa yakitumiwa na baadhi ya watu wazima ambao wanawafanyia watoto hao vitendo hivyo baada ya kuwarubuni kuwaingiza kwenye mabanda hayo kisha kuwapakata na kuwaingilia watoto hao ikiwa ni pamoja na kinyume cha maumbile.
Hayo yalisemwa mjini Kibaha na mratibu wa shirika lisilo la kiserikali la (KICODET) Dk Rose Mkonyi wakati wa mafunzo ya kupinga vitendo vya ukatili kwa watoto kwa wadau mbalimbali kwenye kata ya Kibaha wilayani humo  alisema moja ya vyanzo vya ongezeko la vitendo vya ubakaji watoto ni mabanda hayo.
“Vitendo vya ubakaji watoto ambapo ni moja ya ukatili vimekithiri na kuongezeka wilayani Kibaha na moja ya sababu ni mabanda hayo ambayo yanaonyesha video chafu za ngono bila ya kujali umri,” alisema Dk Mkonyi.
Dk Mkonyi alisema kuwa mabanda hayo yamejaa kwenye mitaa na vijiji hayajali umri licha ya sheria kutaka watoto wenye umri chini ya miaka 18 kutoingia lakini wamiliki wamekuwa wakiwaruhusu watoto hao ambao ni wanafunzi kuingia pia kufunguliwa muda wa kazi ambapo wanafunzi hao wamekuwa wakiishia humo na kuacha kwenda shule.
Kwa upande wake mwezeshaji wa mafunzo hayo Faustina Kayombo ambaye ni ofisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha alisema kuwa tatizo kubwa ni usiri unaofanywa na umaskini imekuwa ni chanzo kikuu cha kuendela kwa vitendo hivyo.
Naye mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo ambaye ni mwenyekiti wa mafunzo hayo Alkhas Katopola alisema kuwa mafunzo hayo yamtawafanya waweze kujua namna ya kukabilina na vitendo hivyo ndani ya jamii ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa kwenye vyombo vya sheria.
Katopolo alisema kuwa baadhi ya matukio hayo yamekuwa yakiendelea kutokana na wanafamilia kuficha kuogopa mahusiano mabaya au kurubunia kwa kupewa fedha ili wasitoe taarifa za vitendo hivyo.
Mradi huo ni wa miaka miwili ambapo mafunzo hayo yamefadhiliwa na Plan International, UNICEF, Save the Children na Jumuiya ya Ulaya na serikali kwa kushirikiana na shirika hilo la KICODET.
Mwisho.

   



WANAFUNZI KIDATO CHA SITA WAZAWADIWA FEDHA


Na John Gagarini, Kibaha
SHIRIKA lisilo la Kiserikali la Piniel Medical Mission la Jijini Dar es Salaam limewapa fedha wanafunzi wanne wa shule ya sekondari Kilangalanga ambao wamefaulu daraja la kwanza kwenye mtihani wa Taifa wa kidato cha sita.
Waliozawadiwa fedha hizo ni pamoja na Peter Didas, Ally Makutubu, Obote Juma na Venance Peter ambao kila mmoja alikabidhiwa kiasi cha shilingi 100,000 kila mmoja.
Akiwakabidhi fedha hizo mgeni rasmi kwenye makabidhiano hayo ambayo yalifanyika shuleni hapo Mlandizi Kibaha mwakilishi wa ofisa elimu wilaya ya Kibaha Blandina Mwenura aliwapongeza wanafunzi hao na kuwataka wanafunzi watakaofanya mitihani hiyo kutoogopa masomo ya sayansi.
Mwenura alisema kuwa wanafunzi wengi wamekuwa wakifanya vibaya kutokana na kuyaogopa masomo hayo ambayo ndiyo masomo muhimu katika kupata wataalamu mbalimbali.
“Nalipongeza shirika hili kwa kujitolea kuhamasisha masomo haya ambayo wanafunzi wamekuwa wakiyakimbia na kukimbilia masomo ya Sanaa wakidhani kuwa ndiyo rahisi,” alisema Mwenura.
Aidha aliwataka wadau wengine kujitokeza zaidi kuwatia moyo wanafunzi wanaosoma masomo hayo ili kujenga nchi yenye wataalamu wenye uwezo mzuri kwani watafanya kazi kwa mapenzi kwa kile walichokisomea.
Kwa upande wake kaimu mkurugenzi wa shirika hilo Jaqline Ngoma alisema kuwa walitoa ahadi kwa wanafunzi wa shule hiyo kuwa endapo mwanafunzi wa kidato cha sita atapata daraja la kwanza watampatia kiasi hicho cha fedha na huo ndiyo utekelezaji wa ahadi hiyo.
“Lengo letu ni kuwatia moyo wanafunzi wanaosoma masomo ya sayansi wawe na ujasiri na kuondoa woga kwani wataalamu kwa sasa wanapungua mfano wataalamu wa afya hivyo lazima tutumie njia ya kuwahamasisha ili wengi wajiunge na masomo hayo,” alisema Ngoma.
Shule hiyo ya serikali ni ya kutwa ni ya wavulana na wasichana na bweni kwa wanafunzi wa kidato cha tano na sita wavulana wanaochukua masomo ya mchepuo wa Sayansi.
Mwisho.

Friday, September 26, 2014

WEZI WAVAMIA WAPORA MMOJA AKAMATWA

Na John Gagarini, Kibaha
HUKU ikiwa imepita wiki moja ya tukio ambalo lilisababisha kifo cha mfanyabiashara wa Jijini Dar es Salaam  Mahoro Mlelwa kupigwa risasi na majambazi na kufa eneo la Maili Moja wilayani Kibaha watu wanaodhaniwa kuwa ni wezi wakiwa na silaha za jadi wamevamia maduka na kupora.
Watu hao walivamia maduka hayo baada ya kupiga baruti kwa lengo la kuwatisha watu ili waweze kufanikisha wizi huo.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana mjini Kibaha kaimu kamanda wa Polisi mkoani Pwani, Athuman Mwambalaswa alisema kuwa tukio hilo lilitokea Septemba 26 mwaka huu majira ya saa 2 usiku.
Kamanda Mwambalaswa alisema kuwa mawili yaliyopo eneo la Kwa Mathias wilayani Kibaha na kufanikiwa kupora fedha taslimu kiasi cha shilingi 200,000 pamoja na simu 4 pamoja na vocha za simu zenye thamani ya shilingi 200,000.
“Katika tukio hilo watu hao walivamia kwa Godfrey Lunyelele (32) na kumwibia simu nne na fedha taslimu kiasi cha shilingi 100,000 na kwa Hassan Mkuwili (42) waliiba vocha za simu zenye thamani ya shilingi 200,000 na fedha taslimu shilingi 100,000,” alisema Kamanda Mwambalaswa.
Aidha alisema Lunyelele alipata ujasiri baada ya kubaini silaha hizo hazina madhara na kumpiga kwa tofali kichwani mwizi mmoja kati ya watatu, na alipoanguka chini walimkamata na anashikiliwa na jeshi hilo kuhusiana na tukio hilo.
“Mtu tuliyemkamata jina linahifadhiwa ili uchunguzi usiharibike na tunaendelea kumshikilia ili atupe taarifa za wenzake ambao walifanikiwa kukimbia,” alisema Kamanda Mwambalaswa.
Alibainisha kuwa kutokana na tukio hilo wamefanya kikao na maofisa wa jeshi hilo na kuamua kufanya doria ya nguvu ya miguu pamoja na magari ili kuhakikisha wanafanikiwa kudhibiti matukio hayo na kuwataka wananchi kutoa taarifa ya watu wanaowadhania kuwa ni majambazi.
Mwisho. 

Sunday, September 21, 2014

johngagariniblog: KINANA AIBUA MAKUBWA KIBAHA

johngagariniblog: KINANA AIBUA MAKUBWA KIBAHA: Na John Gagarini, Kibaha KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Abdulrahman Kinana amezishauri Halmashauri nchini kulipatia Shirika la ...