Sunday, July 20, 2014

MGOMO WA WACHINJAJI NGOMBE WAISHA



Na John Gagarini, Kibaha
HATIMAYE ule mgomo wa wachinjaji ngombe na wamiliki wa mabucha wilayani Kibaha mkoani Pwani umekwisha baada ya pande mbili zilizokuwa zikitofautia Halmashauri ya Mji wa Kibaha na wamiliki wa mabucha hayo chini ya mkuu wa wilaya ya Kibaha Halima Kihemba kukaa meza moja na kumaliza mgomo huo uliodumu kwa muda wa siku mbili kuanzia Julai 18 hadi 19.
Mgomo huo ambao uliendeshwa na wamiliki hao wa mabucha ambao ndiyo wachinjaji wa ng’ombe kupitia Umoja wa wafanyabiashara wa nyama na mazao yake wilayani Kibaha  (UWABINK) walifanya mgomo wa kuuza nyama kwa mji wa Kibaha na vitongoji vyake kwa madai kuwa machinjio mpya ya Mtakuja waliohamishiwa haina huduma muhimu ikiwemo maji huku wakitaka kutumia ile ya zamani ya Maili Moja.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jana mjini Kibaha kwa njia ya simu mkuu wa wilaya ya Kibaha Kihemba alisema kuwa kulitokea tofauti baina ya pande hizo mbili hali iliyosababisha mgomo huo ambao uliathiri walaji wa nyama wa mji huo na maeneo ya wilaya ya Kinondoni Jijini Dar es Salaam.
Kihemba alisema kuwa suala la maji pande hizo zimekubaliana Halmashauri watanunua maji kwa kipindi cha wiki moja na UWABINK nao watanunua wiki moja hivyo watapeana zamu ya kununua maji hadi suala hilo litakapopatiwa ufumbuzi ambapo halmashauri imetenga kiasi cha shilingi milioni 19 kwa ajili ya kuchimba kisima kirefu cha maji Septemba mwaka huu.
“Muafaka ni kwamba waendelee kuchinja kwenye machinjio ya zamani kwa muda wa siku tatu kuanzia Julai 20 hadi Julai 22 kisha wahamie kule, kwani kwa kipindi hicho taayari marekebisho yatakuwa yamefanywa na maji watashirikiana kununua,” alisema Kihemba.
Aidha alisema kuwa baada ya siku tatu watatakiwa hamie huko machinjio mpya na ile ya zamani itabomolewa ili kupisha shughuli nyingine kwenye eneo hilo hivyo anaamini muafaka huo utaondoa msuguano uliojitokeza.
“Kuhusu zizi walikuwa hawajajenga hivyo wajenge zizi hilo katika kipindi hicho walichokubaliana ambapo waliingia mkataba wa uendeshaji ambapo wao wanachinja halmashauri wao ni wa miliki wa miuondombinu na wao hulipa ushuru kwa kila mwezi ni zaidi ya shilingi milioni moja,” alisema Kihemba.
Kwa upande wake msemaji wa umoja huo Athumani Mkanga alisema waliamua kufanya mgomo huo kupinga kuhamishiwa kwenye machinji hayo ya Mtakuja kutoka yale ya Maili Moja kwani yalikuwa hayajakamilika na hayakuwa na huduma muhimu ikiwemo maji na umeme ambapo ule wa jua hautakidhi mahitaji yao.
Mkanga alisema kuwa walikaa meza moja na halmashauri chini ya mkuu wa wilaya ambaye alikuwa mwenyekiti na kukubaliana kuwa watashirikiana katika masuala mbalimbali kwenye machinjio hayo mapya.
“Tumekubaliana baadhi ya mambo ikiwemo sula la maji ambapo tutayanunua kwa zamu wakati wao wanaendelea na utaratibu wa kuchimba kisima kirefu ili kukabiliana na tatizo la maji na masuala mengine,” alisema Mkanga.
Alibainisha kuwa wamekubaliana na marekebisho hayo lakini wanachokitaka ni kuboreshwa kwa huduma ili waweze kufanya shughuli zao bila ya kikwazo chochote lengo likiwa ni kutoa huduma bora kwa walaji.
Mwisho.

Picha zikionyesha machinjio mpya ya Mtakuja iliyopo kata ya Pangani wilayani Kibaha mkoani Pwani ambayo wachinjaji na wamiliki wa mabucha mjini Kibaha waliigomea wakidai kuwa baadhi ya miundombinu yake haijakamilika ikiwemo maji.

Friday, July 18, 2014

RIDHIWANI ATOA MSAADA POLISI



Na John Gagarini, Chalinze

KATIKA kuhakikisha Jeshi la Polisi linafanya kazi kwa teknolojia ya kisasa Mbunge wa jimbo la Chalinze wilayani Bagamoyo mkoani Pwani  Ridhiwani Kikwete ametoa msaada wa kompyuta na mashine za kutolea kopi zenye thamani ya shilingi milioni 11 kwa kanda maalumu ya kipolisi ya Wilaya ya Chalinze.

Msaada huo wa kompyuta, na mashine ya kutolea kopi utasaidia kuhifadhi nyaraka za kipolisi na pia kuachana na usumbufu wa kutumia steshenari zilizopo nje ya ofisi yao.

Akikabidhi msaada huo wa kompyuta pamoja na fedha taslimu kwa kamanda wa polisi wa mkoa wa Pwani Ulrich Matei, Ridhiwani alisema lengo ni uboreshaji wa vituo vya polisi katika jimbo hilo.

“Kwa kuwa kituo hichi cha polisi Chalinze kimepandishwa hadhi na kuwa cha wilaya bado kinakabiliwa na changamoto ya uwepo wa ofisi ndogo ambayo haikidhi mahitaji na kusababisha kutumia kontena kufanyia kazi nyingine za kiofisi nimetoa kwa ajili ya siri za kiofisi badala ya kufanyia kazi nje ya kituo,” alisema Ridhiwani.

Ridhiwani alisema kuwa siri nyingi za ofisi zilikuwa zikivuja kutokana na kazi kufanyiwa nje ya ofisi jambo ambalo lilikuwa likisababisha uvujaji wa taarifa hivyo kushindwa kufanikiwa kudhibiti uhalifu kikamilifu.

Kwa upande wake  Kamanda Matei  alimshukuru mbunge huyo na kusema kuwa kituo cha Chalinze ambacho kimepandishwa hadhi na kuwa cha kiwilaya kwasasa ni kipya na
hivyo kinahitaji maboresho mengi ambapo aliahidi kudumisha ushirikiano ili kusaidiana katika kutatua changamoto nyingine za vituo hivyo.

Naye Diwani wa kata ya Bwilingu Nasa Karama alimueleza mbunge huyo kuwa  tangu kituo hicho kipandishwe hadhi na kuwa cha wilaya, shughuli nyingi zimeongezeka na hivyo kuwa na kazi kubw aya kuzuia uhalifu

“Tunashukuru kwa msaada huu pia tunaomba msaada wa kujengewa nyumba kwa ajili askari kwani wengi wa kituo hicho hawana nyumba za kuishi na hivyo kulazimika kupanga uraiani na kusababisha utendaji kazi kupungua.

Misaada iliyokabidhiwa kwa jeshi hilo ni pamoja na shilingi Milioni
tatu kwa ajili ya kituo cha polisi Mbwewe, mifuko ya saruji 20 na
shilingi 350,000 kwa ajili ya kuharakisha ujenzi wa kituo cha polisi
Kiwangwa pamoja na kompyuta na mashine ya kutolea kopi kwa ajili ya
kituo cha Chalinze.

Mwisho.


Wednesday, July 16, 2014

SHERIA KANDAMIZI KWA WANAWAKE KIKWAZO KUPATA HAKI



Na John Gagarini, Kibaha
IMEELEZWA kuwa ucheleweshaji wa ubadilishaji wa sheria kandamizi kwa wanawake na watoto hapa nchini kumechangia kiasi kikubwa kuendelea vitendo vya unyanyasaji wa makundi hayo ndani ya jamii.
Sheria hizo ambazo zilitungwa miaka ya nyuma zinaonekana kuyakandamiza makundi hayo ambayo yanaonekana ni manyonge ndani ya jamii kwani watu wameendeleza kuyakandamiza hasa katika mgawanyo wa mali.
Hayo yalisemwa jana mjini Kibaha na Jane Mgaigita mwezeshaji wa mafunzo ya siku mbili yaliyoandaliwa na kituo cha msaada wa Kisheria kwa wanawake (WLAC) kwa wadau wa kituo hicho wakiwemo maakimu, watendaji wa mitaa na kata pamoja na polisi, wilaya ya Kibaha mkoani Pwani juu ya haki za wanawake.
Magigita alisema kuwa baadhi ya sheria ni kandamizi ambazo inapaswa zibadilishwe ili makundi hayo yaweze kupata haki zao hasa pale inapofikia wakati wa mgawanyo wa mali.
“Wanawake wengi na watoto wamekuwa wakikandamizwa na sheria hizo zikiwemo zile za ndoa na masula ya mirathi ambazo bado zinatumiwa na Mahakama zikiwemo zile za mwanzo hivyo ni vema zikarekebishwa ili kuondoa unyanyasaji ndani ya jamii,” alisema Magigita.
Alisema kuwa wao kama wanaharakati wamekuwa wakipeleka mapendekezo ya mabadiliko ya sheria hizo kandamizi ili zibadilishwe lakini zimekuwa hazifanyiwe marekebisho na kuwafanya wanajamii hao kuzidi kukandamizwa kutokana na hali hiyo.
“Baadhi ya sheria za masuala mengine zimekuwa zikirekebishwa harakaharaka  lakini hizi za wanawake hazipewi nafasi kabisa na kufumbiwa macho hivyo kuendeleza unyanyasaji, ” alisema Magigita.
Kwa upande wake hakimu mkazi mfawidhi wa mkoa wa Pwani Salome Mshasha alisema kuwa mbali ya changamoto hiyo ya sheria pia baadhi ya wanawake wamekuwa wakikata tamaa na kuacha kutoa taarifa juu ya haki zao.
“Baadhi ya wanawake wamekuwa wakijirudisha nyuma kwenye suala la kudai haki zao jambo ambalo linawafanya wasipate haki na kuwaacha wanaume wakijinufaisha,” alisema Mshasha.
Naye mwenyekiti wa baraza la Ardhi la wilaya ya Kibaha Maketa Bigambo alisema kuwa wao kama wadau wa utoaji haki watahakikisha kila kundi linapata haki yake ili kuondoa malalamiko hayo.
Bigambo alisema jambo ambalo linatakiwa ni pamoja na wanake kutokata tamaa kufuatilia haki zao kwenye vyombo vinavyohusika ili kukabiliana na ukandamizaji unaofanywa na baadhi ya wanafamilia.
Mwisho.     


Thursday, July 10, 2014

AMLAWITI KIKONGWE AMWUA KWA KUMNYONGA



Na John Gagarini, Kibaha
JESHI la Polisi mkoani Pwani linamshikilia Fikiri Mwinyimvua (35) mkazi wa Mfuru Kivukoni kata ya Marumbo Tarafa ya Maneromango wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani kwa tuhuma za kumlawiti bibi kizee mwenye umri wa miaka (60) kisha kumwua kwa kumnyonga shingo.
Kabla ya kumwua mtuhumiwa alikuwa akinywa pombe za kienyeji  na marehemu lakini aliwahi kuondoka eneo la kinywaji kisha kumvizi marehemu na kumfanyia vitendo hivyo ambavyo vilisababisha kifo chake.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo kamanda wa Polisi mkoani Pwani, kamanda mwandamizi msaidizi wa jeshi la polisi (SACP) Ulrich Matei alisema kuwa tukio hilo limetokea Kijiji cha Mfuru Kivukoni wilayani humo.
Kamanda Matei alisema kuwa tukio hilo Julai 10 mwaka huu majira ya saa 1:30 usiku Kijijini hapo ambapo mtuhumiwa alimvizia marehemu kwenye eneo la kichaka kisha kufanya unyama huo.
Katika tukio lingine Nuran Hamis (31) kwa tuhuma ya kusafirisha bangi kilo 12 akiwa kwenye basi dogo la abiria aina ya Toyota Coaster lenye namba za usajili namba T 618 CMU.
Kamanda Matei alisema kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa jana majira ya saa 2:00 usiku kwenye kizuizi cha Maliasili cha Kibiti kata na Tarafa ya Kibiti wilayani Rufiji.
Aidha watu watano wakazi wa Kidongo Chekundu kata ya Magomeni Tarafa ya Mwambao wilaya ya Bagamoyo wanshikiliwa na jeshi hilo kwa tuhuma za kukutwa na pombe ya Moshi maarufu kama Gongo lita 21 kwenye matukio tofauti.
Aliwataja wathumiwa hao kuwa ni Hadija Shaban (37), Rajabu Michael (37), Msafiri Ramadhan (38), Seif Omary (35), Asha Ramadhan (40) pia wakazi watatu wa Ikwiriri wilayani Rufiji nao walikamatw awakiwa na lita 4 za pombe hiyo ambao ni Tabia Salehe (31), Hamis Rwambo (27) na Abdul Rwambo (40).
Mwisho.

Sunday, July 6, 2014

WANANCHI WAPATA OFA YA MAJI MRADI MKUBWA KUONDOA KERO YA MAJI KIBAHA

Na John Gagarini, Kibaha
WAKAZI wa Mitaa ya Vikawe, Vikawe Shuleni, Vikawe Bondeni na Vikawe wilayani Kibaha mkoani Pwani wamepatiwa ofa ya kutumia maji bure kwa miezi mitatu baada ya huduma hiyo kuanza kupatikana ambapo mitaa hiyo haikuwa na maji ya bomba tangu kuanzishwa kwake.
Maji hayo tayari yameshaanza kutoka yanatokana na chanzo cha maji cha Ruvu Juu baada ya mitaa hiyo kutokuwa na maji kabisa ambapo awali walikuwa wakitumia maji ya visima na mto .
Akizungumza na mabalozi, makatibu na viongozi wa Jumuiya za Chama Cha Mapinduzi (CCM) kata ya Mkuza wilayani Kibaha wakati wa semina ya viongozi hao iliyofanyika jana mjini Kibaha, Mbunge wa Jimbo la Kibaha Silvestry Koka alisema kuwa maji yameanza kutoka kwenye mitaa hiyo hivi karibuni.
“Wananchi hao wamepata ofa hiyo ya kutumia maji bure lakini baada ya miezi mitatu wataanza kuyalipia maji hayo baada ya kukosa maji ya bomba kwani kulikuwa hakuna maji kabisa na walikuwa wakichota maji kwenye visima na mto ambapo baadhi walipoteza maisha kwa kukamatwa na mamba walipokuwa wakichota maji mtoni,” alisema Koka.
Katika hatua nyingine Koka alisema kuwa mji wa Kibaha utaondokana na tatizo kubwa la ukosefu wa maji baada ya mradi wa bomba kubwa kutoka chanzo cha mto Ruvu kuanza.
Koka alisema kuwa kwa muda mrefu wa mji huo umekuwa ukikabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa maji huku wakati mwingine maji yakiwa yanatoka kwa mgao kutokana na chanzo kilichopo kutokuwa na uwezo wa kutoa maji ya kutosha.
“Mradi huu kwa sasa uko kwenye hatua nzuri ambapo uchimbaji wa mtaro utaanza muda wowote kuanzia sasa kwani taratibu zingine zimekamilika na bomba litakalopitishwa litakuwa ni kubwa ambalo litapitisha maji mengi,” alisema Koka.
Kwa upande wake katibu wa (CCM) Kibaha Mjini Abdala Mdimu alisema kuwa utekelezaji wa miradi hiyo ni utekelezaji wa ilani ya chama  ambayo ni ahadi kwa wananchi ili kuboresha utoaji huduma.
Mdimu alisema kuwa chama kupitia kwa viongozi wake kitahakikisha ahadi zote zinatekelezwa kwa wakati uliopangwa ili wananchi waondokane na kero za huduma muhimu.
Mwisho.