WAJUMBE wa Bodi ya Barabara ya Mkoa wa Pwani wameiomba serikali kuhakikisha uboreshaji wa Barabara ya Morogoro ili kupunguza msongamano uliopo kwa sasa ambapo asilimia 85 ya magari kwenda nje ya Dar es Salaam yanapita barabara hiyo.
Wakizungumza kwenye kikao cha bodi ya barabara
kilichofanyika Mjini Kibaha Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka alisema
kuwa kwa sasa kuemkuwa na foleni kubwa sana ambayo imekuwa ni changamoto kubwa
kwa magari yanayotumia barabara hiyo.
Koka alisema kuwa mipango inayotarajiwa kufanywa ifanyike
kwa haraka ili kukabiliana na hali hiyo ambayo imekuwa ni kero kubwa kwa
watumiaji kwani foleni imekuw ani kubwa sana na kusababisha watu kushindwa
kwenda kwa wakati kwenye shughuli zao.
“Tunashauri mpango wa uboreshaji uendane na ukuaji wa Mji wa
Pangani na eneo la Shirika la Elimu (KEC) ni maeneo ambayo yatakuwa na
uboreshaji mkubwa hivyo uboreshaji huo uzingatie maeneo hayo kupitia mpango
endelevu wa uboreshaji barabara,”alisema Koka.
Alisema kuwa katika mpango endelevu huo wa uboreshaji
barabara pia uangalie kwa kuwa na barabara za juu na vivuko au madaraja kwa
ajili ya watu kuvuka na eneo ambalo linapaswa kufanyiwa kazi ni kuanzia Mizani
ya zamani hadi Kwamathias.
“Pale Picha ya Ndege na Mkuza nako ni kipaumbele kwa kuwa
ndiyo kwenye maungio napo papewe kipaumbele wakati wa mpango endelevu wa
uboreshaji wa barabara zetu kwani mji wetu kwa sasa umekuwa na magari ni mengi
sana,”alisema Koka.
Naye Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo Muharami Mkenge alisema
kuwa barabara hiyo ya Morogoro ni changamoto kubwa sana hivyo inapaswa
iangaliwe kwa ukaribu ili kupunguza kero hiyo ya msongamano wa magari ili
wasafiri waweze kwenda safari zao kwa wakati.
Mkenge alisema kuwa kutokana na changamoto hiyo hivyo kuna
haja ya kuboresha barabara zingine ikiwa ni pamoja na ile ya Makofia Wilayani
Bagamoyo hadi Mlandizi Wilayani Kibaha yenye urefu wa kilometa 35 itasaidia
kupunguza msongamano kwani magari yanaweza kupita huko kama barabara ya
Morogoro kuna foleni kubwa.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge
alisema kuwa kuwe na maombi maalumu ambayo yatakuwa ni vipaumbele kwa ajili ya
kuwaondolea kero ya wananchi kwani barabara ni kiungo muhimu cha maendeleo.
Kunenge alisema kuwa mahitaji ya barabara kwa Mkoa ni
makubwa lakini changamoto iliyopo ni upatikanaji wa fedha hivyo ni vema kukawa
na vipaumbele ili vianze na baadaye kufuatiwa na mahitaji mengine.
Kwa upande wake meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Pwani Mhandisi Baraka Mwambage amesema mpango uliopo ni uboreshaji wa barabara za zamani na upanuzi wa maeneo yenye msongamano wa magari.
Mwambage amesema kuwa kwa upande wa barabara ya zamani ya kuanzia Sheli mpaka DAWASA wamefanya kazi za matengenezo kwa kuchonga barabara, kuweka kifusi cha udongo na changarawe,upanuzi wa maingilio yote mwanzo na mwisho ikiwa ni pamoja na kuongeza urefu wa makalavati yaliyopo, kujenga mitaro ya zege na kuchimba mitaro ya kawaida.
Amesema katika kipande cha Picha ya Ndege-Msufini kazi zilizofanyika ni pamoja na kuchonga barabara, kuweka kifusi cha changarawe na kujenga makalavati.
Aidha ukarabati wa Barabara ya zamani ya Morogoro umefanyika kuanzia Mlandizi-Ruvu JKT, TRC Relini-Mzunguko wa Vigwaza na upanuzi wa maeneo ya miji kwa Barabara kuu ya Morogoro umefanyika eneo la Kwa Mwarabu mita 350, TANESCO mita 290 na Chalinze mita 850 ili kupunguza msongamano kwa eneo la kuingia mji wa Chalinze.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment