Akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake Mwenyekiti wa Mtaa huo Mboni Mkomwa amesema kuwa shule hiyo shule hiyo ina madarasa manne yamekamilika isipokuwa wana mahitaji ya matundu nane ili ikamilke na kuanza masomo kwa wanafunzi wanaotoka mtaa huo.
Mkomwa amesema kuwa kwa sasa anaandaa mpango wa kukutana na wadau wa maendeleo wa mtaa huo ili kufanya harambee ya kuchangia kukamilisha ujenzi wa vyoo hivyo kabla ya mwaka huu kwisha ili hadi Januari viwe vimekamilika na wanafunzi kuanza kusoma.
“Wanafunzi wanaotoka kwenye mtaa huu wanasoma shule za sekondari za Mwambisi na Miembe Saba ambako ni mbali hivyo baada ya kuona changamoto hiyo tulikaa na wananchi na kukubaliana kujenga madarasa ambapo manne yamekamilika kilichobaki ni vyoo matundu nane yakikamilika hayo shule inaanza,”amesema Mkomwa.
Amesema kuwa wanaishukuru serikali ambayo ilitoa kiasi cha shilingi milioni 50 kwa ajili ya ujenzi huo pia wananchi nao walichangia kila kaya 2,000 na kufanikisha ujenzi huo kufikia hapo na kubaki hatua ndogo ili ianze.
“Tuliomba tena fedha ila walituambia kuwa wasubiri hadi kipindi cha bajeti ambapo malengo yetu hayatafikia kwani bajeti ni katikati ya mwaka ambapo mwanzo wa mwaka tunataka wanafunzi wanaotoka kwenye mtaa wetu waanze kusoma hapo pia itasaidia maeneo ya mitaa jirani ambao nao watanufaika,”amesema Mkomwa.
Aidha amesema kuwa changamoto nyingine ambayo iko kwenye mipango yake katika kuitatua ni baadhi ya wakazi wa mtaa wake wapatao 23 hawana huduma ya maji kabisa hali ambayo inawasababisha kupata shida ya kupata maji kwa ajili ya matumizi mbalimbali ya kawaida.
“Wakazi hao waliandika barua baada ya kukaa kikao lakini wakifika Dawasa wanaambia watoe milioni mbili au wasubiri mradi upite maeneo yao jambo ambalo kwao bado ni mtihani na wanahitaji bomba kubwa la nchi sita ili wananchi waweze kuvuta maji kwa urahisi ambapo kwa sasa wanapotaka kuvuta maji kwa majirani huwabidi kuwalipa na kuilipa Daawasa hivyo kujikuta wakilipa mara mbili,”amesema Mkomwa.
Mkomwa alishinda kwenye uchaguzi wa wenyeviti uliofanyika hivi karibuni na alichaguliwa akiwa anatoka kuwa mjumbe wa mtaa huo kwa kipindi cha miaka mitano pia alikuwa mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) tawi la Bamba ambapo mtaa huo una jumla ya wananchi 7,546 yeye ni mjane akiwa na watoto watatu na alifiwa na mume wake mwaka 2015 na ni mjasiriamali.
No comments:
Post a Comment