ILI kuwa na vyama vya siasa imara na kuwa na serikali imara vyama hivyo vimetakiwa kuwa na mafunzo kwa viongozi vijana ili waendeleze maono ya waasisi wa vyama vya ukombozi Kusini mwa Afrika.
Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar Dk Mohammed Said Mohammed wakati wa akifunga Mafunzo ya 13 ya uongozi vijana kutoka vyama sita vya ukombozi Kusini mwa Afrika kuhusu masuala ya maendeleo kwenye Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere Kibaha.
Mohamed amesema kuwa kuwekeza kwenye mafunzo kwa vijana itakuwa na vyama imara ambavyo vitajenga serikali zenye uwezo.
"Historia ya vyama hivi sita ni kuwa vinamshikamano wa kweli tangu enzi hizo kujenga ukombozi wa siasa kwa maono ya waasisi hivyo vijana hawa wanapaswa kurithishwa ili wawe viongozi bora,"amesema Mohamed.
Amesema kuwa ili kuleta ufanisi wa vyama na nchi yapaswa kuwekeza elimu na mafunzo kwa vijana ili kuleta mafanikio na yanategemea kwa kuwa na maono ya waasisi wa mataifa hayo.
"Mafunzo haya ni bora kwani yamezidi kuwandaa vijana kuwa viongozi bora wa baadaye kwa mustkbali wa vyama na nchi kwa ujumla,"amesema Mohamed.
Aidha amesema kuwa wanaishukuru nchi ya China kupitia Chama Cha Kikomunisti cha CPC ambacho kimekuwa kikivisaidia vyama hivyo sita rafiki na imesaidia Afrika kwenye sekta za afya usafiri, na viwanda.
"Wahitimu muwe kigezo cha kujenga masoko ya pamoja na masoko na nchi ya China ni muhimu sana kwani ushirikiano wa kibiashara kati ya nchi hizo ni kubwa pia tunashukuru chama cha CPC kwa kufadhili wa mafunzo haya,"amesema Mohamed.
Kwa upande wake Mkuu wa Shule hiyo ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere Profesa Marcelina Chijoriga amesema kuwa mafunzo mbalimbali ya uongozi yamekuwa yakitolewa kwa vijana kupitia vyama hivyo.
Chijoriga amesema kuwa mafunzo hayo ni kuwaandaa vijana ili kuwa viongozi bora wa baadaye ambapo wanafundishwa juu ya masuala ya maendeleo na kujifunza maono ya viongozi ambao ni waasisi wa mataifa hayo kwa kushirikiana na CPC.
Mafunzo hayo siku 10 yaliwashirikisha viongozi vijana zaidi ya 100 kutoka vyama vya ANC-Afrika Kusini, CCM-Tanzania, FRELIMO-Msumbiji, MPLA-Angola, SWAPO-Namibia na ZANU-PF-Zimbabwe.
No comments:
Post a Comment