MJUMBE wa Kituo cha Msaada wa Kisheria Kibaha (KPC) Lydia Mgaya amekitaka kituo hicho kufuatilia baadhi ya matukio ya Ukatili kwa watoto na wanawake kwenye jamii ili wahusika wachukuliwe hatua.
Friday, June 30, 2023
KPC YATAKIWA KUPAMBANA NA VITENDO VYA UKATILI KWENYE JAMII
SERIKALI YATAKIWA KUDHIBITI MABANDA YA VIDEO KWA WATOTO
KITUO cha Msaada wa Kisheria Kibaha (KPC) kimeishauri serikali kudhibiti vibanda vinavyoonyesha video maarufu kama vibanda umiza ambapo baadhi ya watoto chini ya miaka 18 kufanyiwa vitendo vya ukatili.
Wednesday, June 28, 2023
VITUO MAALUMU 175 KWAAJILI YA HUDUMA MAHUTUTI KWA WATOTO WACHANGA VYAONGEZWA
NAIBU Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amesema, Serikali imeongeza vituo vyenye vyumba maalumu kwa ajili ya kutoa huduma kwa watoto wachanga wenye umri kati ya sifuri mpaka mitano wenye hali mahututi (Neonatal Care Unit), kutoka 18 mwaka 2017 kufikia 175 mwaka 2023.
Amesema leo Juni 28 wakati akijibu swali la Mbunge wa viti maalumu Mhe. Zaytun Seif Swai katika kikao cha kumi na mbili, Bungeni Jijini Dodoma.
"Serikali kupitia wizara ya Afya imeweka mipango ya kupunguza vifo vya watoto wenye umri 0 hadi 1 kwa kuongeza vituo vyenye vyumba maalumu kwa ajili ya kutoa huduma kwa watoto wachanga wenye hali mahututi (Neonatal Care Unit), kutoka 18 mwaka 2017 kufikia 175 mwaka 2023." Amesema
Ameendelea kusema, Serikali kupitia Wizara ya Afya imeendelea kutoa mafunzo kwa watoa huduma juu ya namna ya kutoa huduma jumuishi kwa watoto wachanga na watoto wakubwa (Intergrated Management of Childhood Illness-IMCI) ili kuokoa vifo vya watoto hao vinavyoweza kuepukika.
Amesema, Serikali imeendelea kuimarisha huduma za kukinga na kuzuia magonjwa yanayozuilika kwa Chanjo kama vile Surua, Nimonia, kuharisha, donda koo, kifaduro, pepo punda na polio kwa kuongeza utoaji wa chanjo za Watoto chini ya Mwaka mmoja kufikia kiwango cha zaidi ya asilimia 98 ya utoaji wa chanjo ya Penta 3.
Aidha, Dkt. Mollel amesema, Serikali imeongeza vituo vinavyotoa huduma kwa watoto waliozaliwa wakiwa na uzito pungufu (Kangaroo Mother Care) ambapo kwa sasa vituo 72 na Hospitali 175 zinatoa huduma hizi, huku akiweka wazi kuwa, kwa mwaka 2023/2024 Serikali imepanga kuongeza vituo 100 ili kufikia vituo 275 ifikapo mwezi Juni 2024 vitavyosaidia kuongeza huduma hizo nchini.
Sambamba na hilo Dkt. Mollel amesema Serikali imeendelea kuongeza vifaa na vifaa tiba ikiwemo CT-SCAN zimeongezeka kutoka 3 mpaka sasa zipo zaidi ya 50, MRI zilikuwa 2 lakini mpaka sasa zipo zaidi ya 19, hivyo kumtoa kuwaondoa hofu Wabunge kuwa hata vifaa vya huduma hizo vitaenda kuwekwa kwenye vituo vyote 100 vitavyojengwa nchini.
Kwa upande mwingine Dkt. Mollel amesema, ili kukabiliana na changamoto ya gharama za matibabu kwa wazee, Wizara inaendelea kuhamasisha Wabunge na viongozi wengine pamoja na wananchi kuunga mkono Bima ya afya kwa wote ili kila mwananchi aweze kunufaika na huduma bora bila gharama kuanzia ngazi ya Zahanati mpaka hospitali ya Taifa.
Tuesday, June 27, 2023
WAFANYABIASHARA WA MAZAO YA MISITU WATAKIWA KUFUATA SHERIA, KANUNI NA TARATIBU ZA UVUNAJI
Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imesema haijazuia biashara ya mazao ya Misitu huku ikiwataka wafanyabiashara wa mazao ya misitu kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu zilizowekwa ili kuhakikisha kuna kuwa na usawa katika biashara hiyo pamoja na matumizi endelevu ya rasilimali hiyo.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) ameyasema hayo leo Bungeni jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Kibaha Vijijini Mhe. Michael Costantino Mwakamo, aliyetaka kujua kauli ya Serikali juu ya Wafanyabiashara wa mazao ya misitu wanaozuiwa kufanya biashara na Wakala ya Huduma za Misitu Tanzania (TFS).
”Natoa rai kwa wafanyabiashara wote wenye nia njema ya kuvuna au kufanya biashara ya mazao ya Misitu wafuate Sheria, Kanuni na taratibu zilizowekwa” Mhe. Masanja amesisitiza.
Amesema Sheria ya Misitu Sura ya 323 na Kanuni zake za mwaka 2004 zimeelekeza utaratibu unaopaswa kufuatwa ili kuvuna, kusafirisha na kuuza mazao ya misitu kwa kuzingatia umiliki wa misitu/miti ambao ni ya watu binafsi, Serikali za vijiji, Serikali za mitaa au Serikali Kuu.
Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum,Mhe. Agnes Mathew Marwa, kuhusu Serikali kuwatafutia eneo mbadala Wananchi wa Vijiji vya Kata ya Nyantwari – Bunda wanaofanyiwa uthamini kupitisha uhifadhi Mhe. Masanja amesema kuwa zoezi la uthamini lipo katika hatua za mwisho na baada ya hapo Wananchi watalipwa fidia kwa mujibu wa sheria itakayohusisha gharama za thamani ya ardhi, mazao, majengo, posho ya kujikimu, usafiri na posho ya usumbufu.
Mhe. Masanja amesema kuwa Serikali kupitia Halmashauri ya Mji wa Bunda imetenga na kupima viwanja 350 katika eneo la Virian-Kata ya Stoo ambapo Wananchi watakaohama kutoka Kata ya Nyantwari watapewa kipaumbele wakati wa uuzaji wa viwanja hivyo.
Aidha, Halmashauri ya Mji wa Bunda imeandaa mpango wa kutwaa na kulipa fidia maeneo mbadala ya makazi yenye ukubwa wa ekari 1,625 katika maeneo ya Manyamanyama/Bitaraguru; Butakale; na Guta/Nyabehu. Maeneo yote hayo yatapimwa na kupewa kipaumbele kwa wananchi wanaotoka Kata ya Nyantwari.
JAMII YAASWA KUWEKEZA UJUZI KWA WATOTO
Jamii imeaswa kuwekeza zaidi kwenye kuongeza ujuzi wa malezi makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto ili kuwa na Taifa lenye raia wenye misingi imara katika nyanja zote.
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mwanaid Ali Khamis wakati akifungua Mafunzo ya kitaifa ya Sayansi ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya awali ya Mtoto kwa Wadau kutoka mikoa 16 Nchini pamoja na Wizaraa za kisekta ,Mkoani Dodoma, Juni 26, 2023.
“Mafunzo haya yasiishie tu maofisini bali yafike hadi ngazi za Vijiji kwani huko watu huchelewa kupata taarifa za mambo ya msingi. Mnatakiwa mshuke kwa wananchi wa ngazi za chini kwani Malezi ya awali ni ya muhimu sana katika makuzi ya mtoto”Alisema Mwanaidi.
Akielezea lengo la Mafunzo hayo Naibu katibu Mkuu kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Wakili Amon Mpanju amesema mafunzo hayo ni muhimukwaajili yakuwaongezea ujuzi Wataalam husika ili waweze kutekeleza Majukumu yao kama inavyostahili
“Lengo la mafunzo haya ni kuwajengea uwezo bobezi ili waweze kutekeleza inavyostahili, kwani mafunzo haya yanatolewa na chuo cha Aga khan ambacho kina Mamlaka ya kutoa mafunzo hisika" amefafanua Mpanju
Akiongea wakati wa Mafunzo hayo Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Mtoto kutoka Wizra ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Waanwake na Makundi Maalum, Sebastian Kitiku, amesema Wizara itaendelea kushirikiana kwa karibu na wadau wa Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Mtoto ili kuhakikisha kuna mazingira salama ya ustawi na Maendeleo ya Watoto Nchini.
Naye mshiriki Tedson Ngwale ambaye ni Afisa Maendeleo kutokea Shinyanga ameishukuru Serikali kwa jitihada hizo za kuhakikisha inaanda mazingira salama kwa watoto kwa kutoa mafunzo hayo kwa maafisa maaendeleo na Ustawi wa Jamii.
“Tuna ahidi kuitendea haki Serikai kupitia Mafunzo haya kwa kutekeleza kama tulivyoelekezwa na kama ilivyokusudiwa kwa kuwafikia Wananchi wa ngazi zote hasa vijijini ambako kuna changamoto zaidi”.
KAMATI YA BUNGE YAITAKA TARURA KUTIMIZA AZMA YA SERIKALI
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Dennis Londo ameutaka Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kuendelea kuaminika na Serikali kwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo ya kujenga mbiundombinu ya barabara ili kuwaondolea adha ya usafiri wananchi.
Mhe. Londo ametoa kauli hiyo Juni 24, 2023 katika ziara ya kikazi ya kukagua miundombinu ya barabara zilizojengwa chini ya usimamizi wa TARURA Wilaya ya Morogoro.
Mwenyekiti huyo amesema dhamira ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwaongezea bajeti ya sh. Bilioni 350 kwa mwaka wa fedha 2023/24 ni kuona umuhimu wa taasisi hiyo katika kutekeleza majukumu yake hasa katika ujenzi na marekebisho ya barabara maeneo ya vijijini na mijini ili kuwa na miundombinu rafiki kwa wananchi.
Amesema asilimia kubwa ya watanzania shughuli yao kubwa ni kilimo hivyo TARURA wafanye kazi ili barabara ziwe rafiki kwa watumiaji na kurahisisha maisha yao.
Mhe.Londo ameipongeza TARURA kujengwa barabara yenye kilometa 70 kwenye Wilaya ya Morogoro ambayo imerahisisha kuunganisha vijiji vinne ikiwamo cha Ngerengere na kuhimiza kutunza miundombinu ya barabara hiyo.
"Kujengwa kwa barabara hii kutawezesha kufika kwa urahisi bwawa la Kidunda ambalo ni mradi mkubwa utakaosaidia upatikanaji wa maji kwa wakazi wa Morogoro, Pwani na Dar es Salaam,"amesema.
N
aye, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Deogratius Ndejembi ameishukuru Kamati hiyo ya Bunge kwa maelekezo yake na kuiahidi TAMISEMI itaendelea kutimiza lengo la Serikali kwa kuisimamia TARURA kutoa huduma bora kwa wananchi.
Monday, June 26, 2023
SERIKALI YATAHADHARISHA WANANCHI IRINGA KUACHA KUTEMBEA USIKU KUEPUKA ATHARI ZA KUVAMIWA NA SIMBA
SERIKALI imewatahadharisha Wananchi Mkoani Iringa kuacha kutembea usiku ili kuepukana na madhara ya kuvamiwa na Simba walioingia katika makazi ya watu.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) ameyasema hayo leo jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Grace Tendega aliyetaka kujua nini mkakati wa Serikali wa kuhakikisha wananchi wananchi wa Iringa wanaishi kwa uhuru kutokana na changamoto ya Uvamizi wa Simba.
“Niendelee kutoa elimu kupitia Bunge hili kwamba wakati huu ambapo tunawasaka hawa Simba wananchi wawe na tahadhari ya kutotembea usiku lakini pia wenye mifugo wawashe mioto kuzunguka maeneo ya mifugo ili kuepusha Simba wasisogee katika maeneo yao” Mhe. Masanja amesisitiza.
Kufuatia hatua hiyo Mhe.Masanja amesema Serikali tayari imeshapeleka helikopta inayozunguka usiku na mchana kuhakikisha Simba hao wanapatikana na kurudishwa katika maeneo yao ili kuhakikisha maisha ya Watanzania yanalindwa kwa gharama yoyote
Kuhusu mikakati ya Serikali ya kukabiliana na wanyama wakali na waharibifu, Mhe. Masanja amesema Serikali inatekeleza Mkakati wa kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu wa mwaka 2020 – 2024 ambapo Wizara inatoa elimu juu ya kujikinga na wanyamapori wakali na waharibifu; inajenga vituo vya askari wanyamapori ili kusogeza huduma karibu na wananchi; kuwafunga mikanda (GPS collars) tembo; na kuanzisha timu maalum (Rapid response Teams).
Pia, Serikali inaendelea kuwashirikisha wananchi kwa kutoa mafunzo kwa Askari wa Vijiji (VGS) ili kuongeza nguvu ya kudhibiti tembo katika maeneo ya wananchi.
Aidha, amesema Serikali imeshaweka mipango ya kujenga fensi ya umeme katika baadhi ya maeneo ili kupunguza athari ya wanyama wakali na waharibifu.
Thursday, June 22, 2023
*MAJALIWA APOKEA TAARIFA YA KAMATI MAALUM ALIYOIUNDA KUFUATILIA CHANGAMOTO ZA WAFANYABIASHARA*
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa leo Alhamisi, Juni 21, 2023, Jijini Dodoma amepokea taarifa ya Kamati Maalum aliyoiunda kwa ajili ya kupitia, kuchambua na kutoa mapendekezo ya kutatua changamoto za wafanyabiashara nchini.
Taarifa hiyo imekabidhiwa na Mwenyekiti wa kamati, Dkt. John Jingu ambaye pia ni Katibu Mkuu, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum.
Mkutano huo umehudhuriwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama, Waziri Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba, Waziri wa Viwanda na Uwekezaji Ashatu Kijaji, Waziri wa Nchi OR – TAMISEMI, Angela
Kairuki, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Ahmad Chande, Makatibu Wakuu, Makamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), wanakamati na wataalam kutoka sekta mbalimbali za masuala ya kodi, biashara na uwekezaji.
Akizungumza baada ya kupokea taarifa hiyo, Mheshimiwa Majaliwa amesema Kamati hiyo imefanya kazi kubwa na imeleta majibu ambayo yatatatua changamoto za wafanyabiashara nchini na ameahidi kuwa Serikali imepokeat aarifa hiyo na itayafanyia kazi mapendekezo na ushauri uliotolewa na kamati hiyo.
Kamati hiyo ambayo ilipewa siku 14, imefanya mapitio katika maeneo mbalimbali ya kikodi, bandari na maeneo ya wafanyabiashara kwenye mikoa mbalimbali nchini.
Sunday, June 18, 2023
TAASISI MWALIMU NYERERE YAFANIKISHA UPATIKANAJI DAMU
TAASISI ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Mkoa wa Pwani imefanikisha upatikanaji wa damu uniti 32 ambazo zitatumika kwenye Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha.
Friday, June 16, 2023
MJEMA AWATAKA WANACCM WATEMBEE KIFUA MBELE
KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi, Itikadi na Uenezi, Ndugu Sophia Mjema, amewataka wanachama wa chama hicho na wananchi kwa ujumla kutembea kifua mbele akisema chama hicho kimenyoka na hakiyumbishwi.
Mjema ametoa kauli hiyo 15.6.2023 katika viwanja vya Mnarani mjini Mpwapwa Mkoani Dodoma akiwa katika ziara ya Katibu Mkuu wa CCM, ndugu Daniel Chongolo.
Katika mkutano huo wa hadhara, Mjema amesema Chama Cha Mapunduzi chini ya Mwenyekiti wake Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kinaendelea kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazowakabili wananchi kwa vitendo.
Amewataka wana-CCM kutoogopa kukisemea chama chao hasa kwa watu wanaotosha miradi mbalimbali ambayo inatekelezwa na chama hicho kupitia Ilani yake ya uchaguzi ya mwaka 2020-2025.
"Niwaambieni wananchi wa Mpwapwa mna chama imara sana, chama chemu ni sikivu kinasikiliza changamoto zenu na kuzitafutia ufumbuzi kupitia kwa watendaji mbalimbali wa serikali, hivyo ungeni mkono juhudi za serikali na msiwasikikize wapotoshaji.
Aidha, Mjema amesema CCM imenyooka kama rula na haiyumbishwi.
*MHE. MWINJUMA AFUNGUA MASHINDANO YA UMISSETA TABORA*
Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Hamis Mwinjuma leo Juni 15, 2023 mkoani Tabora amefungua mashindano ya michezo kwa Shule za Sekondari Tanzania (UMISSSETA) kitaifa katika viwanja vya Shule ya Sekondari ya Wavulana Tabora.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mashindano hayo Mhe. Mwinjuma amesema Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya michezo nchini kwa kuanza na shule 56 za sekondari, mbili katika kila Mkoa, ili kukuza na kuendeleza vipaji vya michezo mbalimbali
‘’Ndugu viongozi na wanamichezo Serikali kwa upande wake kupitia ushirikiano wa Wizara zetu tatu (Ya kwangu Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na TAMISEMI) imefanya jitihada kubwa katika kuimarisha shughuli za michezo katika shule za Msingi na Sekondari”amesema Mhe. Mwinjuma.
Mashindano hayo yatafanyika kwa siku saba yakihusisha timu za michezo mbalimbali kutoka Mikoa 32 ya Tanzania bara na Zanzibar.
DK JAFO NCHI KUKABILI MABADILIKO TABIANCHI
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amesema ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi wananchi hawana budi kushiriki katika zoezi la upandaji wa miti.
Amesema hayo leo Juni 15, 2023 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu maswali ya wabunge wa Viti Maalumu Mhe. Mariamu Kisangi na Mhe. Jacqueline Msongozi waliouliza mikakati ya Serikali ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Dkt. Jafo amesema kuwa kwa mujibu wa wataalamu wa hali ya hewa kiwango cha mvua kimeshuka kutokana na changamoto hiyo na kusababisha ukame katika baadhi ya maeneo yakiwemo mikoa ya Arusha na Manyara.
Hivyo, Serikali imeelekeza kila halmashauri kupanda miti milioni 1.5 kila mwaka na kuitunza ikiwa ni hatua ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Awali Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis amesema amewahamasisha wananchi kuacha shughuli zinazochangia uharibifu wa mazingira ambazo husababisha mabadiliko ya tabianchi.
Amewaasa wananchi kuacha kukata miti ovyo, kuepuka kilimo kisicho endelevu katika vyanzo vya maji, kuepuka ufugaji unaoharibu mazingira pamoja na uvuvi haramu.
Naibu Waziri Khamis amesema kuwa Serikali inachukua hatua kwa kuanzisha na kutekeleza miradi ya kuzuia madhara ya mabadiliko ya tabianchi katika jamii.
Aidha, amesema kuwa Serikali imeandaa Sera, Mikakati na Mipango ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi ambayo inatoa elimu na namna bora ya kukabiliana na athari hizo kwa wadau wote muhimu wakiwemo wananchi katika maeneo yote nchini
Thursday, June 15, 2023
𝗦𝗜𝗠𝗕𝗔𝗖𝗛𝗔𝗪𝗘𝗡𝗘 𝗔𝗜𝗣𝗢𝗡𝗚𝗘𝗭𝗔 𝗲-𝗚𝗔 𝗨𝗦𝗜𝗠𝗔𝗠𝗜𝗭𝗜 𝗪𝗔 𝗧𝗘𝗛𝗔𝗠𝗔 𝗦𝗘𝗥𝗜𝗞𝗔𝗟𝗜𝗡𝗜
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene, ameipongeza Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kwa jitihada kubwa inazozifanya katika kukuza na kuimarisha Serikali Mtandao nchini.
Mhe. Simbachawene alitoa pongezi hizo jana, alipofanya ziara ya kikazi katika Ofisi za Mamlaka ya Serikali Mtandao zilizopo Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma, kwa lengo la kukagua utekelezaji wa majukumu ya e-GA katika usimamizi wa matumizi ya TEHAMA kwenye taasisi za umma.
Alisema kuwa, kuimarika kwa matumizi ya TEHAMA katika taasisi za umma, kunatokana na usimamizi mzuri wa e-GA katika kuimarisha jitihada za serikali mtandao, hali ambayo imesaidia kuongezeka kwa ufanisi wa utendaji kazi wa shughuli za serikali pamoja na utoaji huduma kwa wananchi.
“Bila Serikali Mtandao mambo mengi yangekuwa hayaendi sawa, e-GA mmetumia teknolojia kurahisisha na kufanikisha shughuli nyingi za Serikali kufanyika kwa wakati pamoja na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi, nawapongeza sana”, alisema.
Pamoja na pongezi hizo, pia Waziri aliitaka e-GA kuimarisha Kituo cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Serikali Mtandao (eGovRIDC) ili kutengeneza vijana wengi zaidi ambao watabuni mifumo inayotatua changamoto zilizopo.
“Ni muhimu kuimarisha kituo cha utafiti na ubunifu ili kuandaa na kutengeza vijana mahiri katika masuala ya teknolojia kwa maslahi mapana ya taifa, na sisi upande wa Wizara tutahakikisha tunatoa msaada wa kutosha pale mtakapohitaji”, alisema.
Aidha, aliitaka e-GA kuendelea kuwajengea uwezo watumishi wake kwa kuhakikisha wanapata mafunzo ya muda mfupi na mrefu kutoka ndani na nje ya nchi, ili kuwaongeza ujuzi wa kukabiliana na mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia katika usanifu wa mifumo, miundombinu pamoja na miradi ya TEHAMA yenye tija kwa taifa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu e-GA Eng. Benedict Ndomba, alimshukuru Waziri kwa kufanya ziara hiyo pamoja na ushirikiano mkubwa anaoupata kutoka Wizarani katika utekelezaji wa majukumu ya taasisi.
Alisema kuwa e-GA itaendelea kuimarisha kituo cha utafiti na ubunifu pamoja na kutoa elimu kwa Taasisi za Umma katika usimamizi na uzingatiaji wa Sheria, kanuni, viwango na miongozo ya Serikali Mtandao ili kuhakikisha mifumo na miradi yote ya TEHAMA katika taasisi za umma inakuwa na tija kwa taifa.
SERIKALI NA MAPAMBANO DHIDI YA MAGUGU MAJI
RC KUNENGE AZINDUA M-MAMA
MKUU wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge leo Juni 15, 2023 amezindua Mpango wa Usafiri wa Dharura kwa Mama Wajawazito, Wanawake waliojifungua na Watoto Wachanga ujulikanao kama M-Mama.
Akizindua Mpango huo katika Ukumbi wa Baraza la wakunga na uuguzi Kibaha, Hafla iliyohudhuriwa na Viongozi wote wa Mkoa huo Kunenge amesema:- M -Mama ni Mpango ambao Mhe Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameanzisha ili kuokoa maisha ya Mama na Mtoto. Hivyo amewataka Viongozi wote wa Mkoa Kuweka kipaumbele na kuhakisha inafanikiwa.
Ameeleza mpango huo unaendea sambamba na lishe, Kuhudhuria kliniki na wakati wa kujifungua kuwahi kituo cha afya kwa wamama Wajawazito na Watoto."Mpango huo ni mnyororo wa thamani wa uzazi" Ameeleza Kunenge.
Amewataka Viongozi wote wa Mkoa wa kuhakikisha M Mama inafanikiwa. "Suala hili liingizwe kwenye viashiria vya upimaji utendaji kazi wa Watumishi kila mmoja kwenye eneo lake ambapo kila mtu atapimwa navyo" amesema Kunenge.
DKT.JAFFO ATOA KONGOLE KWA WADAU WA MAZINGIRA
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amepongeza wadau kwa juhudi za kuhifadhi mazingira na kuonesha nia ya kufanya Biashara ya Kaboni nchini.
Amesema hayo alipokutana na Meneja wa Shirika linalohudumia wakimbizi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) la Denmark Bi. Jo Povey katika kikao kilichofanyika jijini Dodoma leo Juni 14, 2023.
Dkt. Jafo amesema Serikali inatambua juhudi za wadau hao ambao wanafanya shughuli za kuhifadhi mazingira kwa kupanda miti katika kambi za wakimbizi zilizopo mkoani Kigoma na wananchi wanaozunguka kambi hizo.
Amesema kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Raia sasa inaendelea kuzifanyia kazi Kanuni na Mwongozo wa Biashara ya Kaboni ili wananchi wanufaike na biashara hiyo.
Waziri Jafo amesema changamoto ya ukataji miti kwa ajili ya kuni na mkaa ni ni kubwa katika maeneo mbalimbali hapa nchini hali inayochangia uharibifu wa mazingira na ukame na kusababisha upungufu wa maji na chakula.
Hivyo, amewashukuru wadau hao kwa kuonesha nia ya kuwekeza katika nishati mbadala ambayo kwa kiasi kikubwa itasaidia kupunguza kasi ya ukataji wa miti kwa ajili ya kuni na mkaa.
“Tunafurahi tunapoona wadau kama ninyi mnashiriki kikamilifu katika kulinda mazingira na tunaona juhudi zenu zE kupanda miti, kutuletea nishati mbadala na kuona namna ya kusaidia katika uwekezaji wa hewa ya ukaa na kwqa upande wetu kama Serikali tunaendelea kuhamisha wananchi wahifadhi mazingira,"amesema.
Kwa upande wake Meneja wa shirika hilo Bi. Jo amesema kipaumbele chao tangu mwaka 2021 ni kushirikiana na Serikali katika suala la upandaji wa miti ili kuhifadhi mazingira.
Amesema kwa kushirikiana na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) pamoja na Halmashauri ya Kibondo mkoani Kigoma wanapanda miti katika kambi za wakimbizi na maeneo ya jirani ili kurudisha hali ya mazingira iliyokuwepo awali.
“Kukiwa na mkusanyiko wa watu hususan wakimbizi wakikaa katika eneo moja lazima wawe na mahitaji kama ya kupikia na lazima wakate miti kwa ajili ya kuni kwa hiyo ni lazima kupanda tena miti, hivyo tumeona tufanye uhifadhi,“ amesema Bi. Jo
Naye Meneja wa masuala ya uchumi wa shiriki hilo Bw. Alfred Magehema amesema kuwa kwa sasa wanatekelekeza mradi wa mkaa mbadala ambao unasambazwa katika kambi za wakimbizi.
Amesema katika kambi ya Nduta zinazalilishwa tani zaidi ya mbili kwa siku ambazo zinasaidia matumizi ya kila siku ya wakimbizi hivyo kusaidia kupunguza ukataji ovyo wa miti.
Pia, amepongeza Serikali ya Tanzania kwa kulipa uzito suala la Biashara ya Kaboni hatua ambayo inasaidia kupunguza uharibifu wa mazingira huku akisema shirika linatoa hamasa ya kuhifadhi misitu.
BMH YAPANDIKIZA UUME KWA MARA YA KWANZA NCHINI
HOSPITALI ya Benjamin Mkapa (BMH)kwa kushirikiana na chama cha madaktari bingwa wa upasuaji wa mfumo wa mkojo nchini (TAUS) pamoja na dkt. Bingwa kutoka Ufaransa kwa mara ya kwanza wamefanya upasuaji wa kupandikiza uume kwa watu wawili ambao uume ulishindwa kufanya kazi kutokana na magonjwa mbalimbali.
Akizungumza baada ya kukamilisha upasuaji Dkt. Remidius Rugakingira daktari bingwa wa magonjwa ya mfumo wa mkojo na wanaume kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa amesema kuwa upasuaji huu umefanyika kwa mara ya kwanza nchini.
“Hii ni mara ya kwanza kwa Tanzania kufanya upasuaji wa aina hii kilichofanyika hapa ni kuweka vipandikizi maalumu vitakavyo wezesha uume kurudi katika hali yake upasuaji huu tumeshirikiana na chama cha madaktari bingwa wa upasuaji wa mfumo wa mkojo pamoja na daktari bingwa wa mfumo wa mkojo kutoka Ufaransa na tumefanikiwa katika hilo,” alieleza Dkt. Rugakingira
Dkt. Rugakingira aliendelea kwa kusema kuwa huu ni wito kwamba Hospitali ya Benjamin Mkapa inajali afya ya wanaume na upasuaji kama huu unaweza kufanyika Tanzania.
Kwa upande wake Dkt. Liuba Nyamsogolo ambae ni kiongozi wa chama cha madaktari bingwa wa upasuaji wa mfumo wa mkojo (TAUS) amesema kuwa wamefikia hatua hii kutokana na uwepo wa watu wengi wenye matatizo ya nguvu za kiume nchini na Afrika kwa ujumla.
“Moja wapo ya dhumuni ya TAUS ni kuendeleza wataalam nchini kwa kushirikiana ma wataalam kutoka nje ili kuleta teknolojia inayopatikana duniani nchini Tanzania na kutibu magonjwa kama haya kwa wale wenye matatizo,” alisema Dkt. Nyamsogolo.
Msemaji wa BMH Bw. Jeremiah Mbwambo ameeleza "Hospitali ya BMH imekua Hospitali ya kwanza nchini kufanya upasuaji wa kuweka vipandikizi kwenye uume kwa wagonjwa wenye matatizo ya nguvu za kiume, serikali ya awamu ya sita imeendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika Hospitali ya Benjamin Mkapa kwa kuiwezesha teknolojia za kisasa za matibabu ili kuwapatia matibabu thabiti wananchi"
Wednesday, June 14, 2023
*DKT. BITEKO ASISITIZA JENGO JIPYA MADINI KUKAMILIKA KWA WAKATI*
MKANDARASI wa Jengo Jipya la Wizara ya Madini Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ametakiwa kuongeza kasi ili kukamilisha jengo hilo kwa wakati.
Rai hiyo, imetolewa leo Juni 13, 2023 na Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko wakati wa ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo linaloendelea kujengwa katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.
Hadi kukamilika kwake Jengo hilo litagharimu shilingi bilioni 22.8 na linatarajiwa kukabidhiwa ifikapo mwezi Septemba, 2023.
Wengine walioshiriki katika ziara hiyo ni pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya Madini Kheri Mahimbali, Naibu Katibu Mkuu Msafiri Mbibo, Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania ( GST) Dkt. Mussa Budeba, Kaimu Katibu Mtendaji wa TEITI Joseph Kumburu na watumishi wa Wizara ya Madini.
Tuesday, June 13, 2023
SENYAMULE AAGIZA CHEMBA KUJIPANGA UPYA
MKUU wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule amesema hajaridhishwa na kasi ya ujenzi wa Shule Mpya ya Msingi katika Kijiji cha Magungu Kata ya Mpendo Wilaya ya Chemba na kukemea vikali uongozi wa Kijiji kukusanya fedha kwa wananchi bila kufuata utaratibu.
Senyamule ameyasema hayo leo tarehe 13/06/2023 mara baada ya kufanya ziara yakukagua utekelezaji wa miradi ya boost katika Wilaya ya Chemba.
"Sijaona dhamira ya dhati katika ukamilishaji wa mradi huu kwa muda tuliokubaliana wa tarehe 30/6/2023, tumekubaliana sote kuwa miradi hii ikamilike kwa wakati lakini leo nimesikitishwa sana hatua hii ya ujenzi ambao uko katika hatua za awali" Senyamule amefafanua
Amesema hayuko tayari kuona dhamira njema ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwaletea wananchi maendeleo hususan katika nyanja ya elimu haifikiwi kutokana na watu wachache kutotimiza wajibu wao.
"Katika mradi huu Chemba hamjafika hata asilimia 20 na mna siku 18 zimesalia, fedha zilitolewa kwa wakati mmoja nchi nzima, Wilaya nyingine za Mkoa wa Dodoma wako katika hatua za upauji, siko tayati kumuangusha Mhe. Rais, ujenzi ufanyike mchana na usiku" Senyamule ameagiza.
Katika hatua nyingine Mhe. Senyamule amekemea vikali utaratibu unaotumiwa na Mwenyekiti wa Kijiji cha Magungu Bw. Bernard Kapaya kuchangisha fedha wananchi bila kibali cha Mkuu wa Wilaya.
“Naomba kuwakumbusha kuwa Serikali imetoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa Shule mpya, vyumba vya madarasa ya awali na msingi, nyumba za walimu na ujenzi wa Vyoo. Wananchi wasishurutishwe kuchangia fedha, wachangie kwa hiari yao wenyewe na utaratibu ufuatwe ikiwa ni pamoja na kuambatanisha muhtasari wa mkutano wa Serikali ya Kijiji na barua iliyopitishwa kwa Mkurugenzi kwenda kwa Mkuu wa Wilaya. Ni kinyume kuchangisha fedha bila kufuata utaratibu huo” Senyamule ameonya
Awali, Mkuu wa Wilaya ya Chemba Bw. Gerald Mongella amesema kumekuwa na ucheweshaji kutokana na kusuasua kwa mchango wa nguvu za wananchi hali iliyopelekea ucheleweshaji wa upatikanaji wa madini.
Mkoa wa Dodoma kupitia mradi wa Boost umepokea kiasi cha Shilingi Bilioni 10.6 kwa ajili ujenzi wa Shule mpya 16, vyumba vya madarasa ya msingi 163, madarasa ya awali 16, ujenzi wa vyoo 106, nyumba za walimu 03 na darasa 01 la elimu maalumu. Wilaya ya Chemba imepokea kiasi cha shilingi Bilioni 1.3.
Katika ziara yake Mhe. Senyamule amekagua maendeleo ya ujenzi wa Shule mpya ya Magungu, Ujenzi madarasa katika Shule ya Msingi Birise, ujenzi wa madarasa Lahoda na Ujenzi wa shule mpya Handa ‘B’.
Saturday, June 10, 2023
PWANI BINGWA VIWANDA
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh.Dkt Samia Suluhu Hassan ameutaja Mkoa wa Pwani kuwa bingwa viwanda nchini.
Rais Dkt. Samia ametoa kauli hiyo Juni 9, 2023 wakati akiwatambulisha Wakuu wa Mikoa waliohudhuria kwenye mkutano wa 14 wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) Ikulu jijini Dar es Saalam.
Katika Mkutano huo Rais amewataka wakuu wa mikoa nchini kuweka mazingira rafiki kwa ajili ya kuvutia wawekezaji na kwamba ataandaa tuzo kwa ajili ya mkoa kinara wa ukusanyaji mapato.
Mkoa wa Pwani una jumla ya viwanda 1522 kati ya hivyo vikubwa ni 117 na 120 vya kati.
PWANI BINGWA WA VIWANDA NCHINI
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh.Dkt Samia Suluhu Hassan ameutaja Mkoa wa Pwani kuwa bingwa viwanda nchini.
Rais Dkt. Samia ametoa kauli hiyo Juni 9, 2023 wakati akiwatambulisha Wakuu wa Mikoa waliohudhuria kwenye mkutano wa 14 wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) Ikulu jijini Dar es Saalam.
Katika Mkutano huo Rais amewataka wakuu wa mikoa nchini kuweka mazingira rafiki kwa ajili ya kuvutia wawekezaji na kwamba ataandaa tuzo kwa ajili ya mkoa kinara wa ukusanyaji mapato.
Mkoa wa Pwani una jumla ya viwanda 1522 kati ya hivyo vikubwa ni 117 na 120 vya kati.
SERIKALI YAWAGAWIA ARDHI WANANCHI
Friday, June 9, 2023
WADHAMINI WA MICHEZO WATAKIWA KUBORESHA ZAWADI ZA WASHINDI
WADHAMINI wa Michezo Mkoani Pwani wametakiwa kutoa zawadi ambazo zitakuwa kumbukumbu kwa washindi wa michezo mbalimbali ili kuleta hamasa kwa vijana kushiriki kwenye michezo.
Hayo yalisemwa Mjini Kibaha na mdhamini wa mashindano ya Umoja wa Michezo Sanaa kwa Shule za Sekondari Tanzania (UMISSETA) Mkoa wa Pwani Musa Mansour na kwa kuwa michezo ni ajira wadhamini waangalie kwa kuboresha upande wa zawadi ili ziwe kivutio.
HALMASHAURI ZATAKIWA KUTENGA BAJETI ZA MICHEZO
Thursday, June 8, 2023
WAKAZI CHANGWAHELA WARIDHIA KUHAMA
WAKAZI wa Kitongoji Changwahela wilayani Bagamoyo wameridhia kutekeleza agizo la Serikali la kuondoka katika eneo walilolivamia na kufanya shughuli za kibinadamu na kufanya uharibifu wa mazingira.
Wednesday, June 7, 2023
WANANCHI WA SANZALE WALIOSHINDWA MAHAKAMANI WAZUNGUMZE NA MMILIKI
KUFUATIA hukumu iliyotolewa na Baraza la Ardhi na Nyumba Kibaha kuwa wavamizi 86 kwenye eneo linalomilikiwa na Yusuph Kikwete waondoke Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amewataka wananchi hao kuongea na mmiliki huyo ili waangalie namna ya kuwasaidia.
CHANGWAHELA WATAKIWA KUPISHA ENEO KWA AJILI YA HIFADHI YA MIKOKO
HALMASHAURI ya Bagamoyo imetakiwa kukaa na mwekezaji wa Sea Salt ili kutoa hekari 50 kwa wananchi wa Kitongoji cha Changwahela kata ya Mapinga wilaya ya Bagamoyo ambao wameondolewa kwenye eneo ambalo ni la uhifadhi wa Mikoko.
SERIKALI YATOA MAAMUZI UENDESHAJI MAGOFU YA KAOLE BAGAMOYO
KUNENGE akiwa Bagamoyo alimuagiza Kamishna Msaidizi wa Ardhi kufuta hati ya upimaji eneo la Mji Mkongwe uliofanyika ndani ya eneo la hifadhi kwa kuwa zilitolewa ndani ya GN namba 1983 na kutatua mgogoro wa ardhi eneo la magofu ya Kaole na familia ya Omary Sherdel.
Alimtaka kamishna msaidizi wa ardhi wa mkoa kukamilisha ufuatiliajj kwenye mamlaka husika juu ya sheria namba 64 na 10 na maboresho ya mwaka 1976.
"Kumekuwa na uvamizi kwenye magofu na malikale na watu hawafuati utaratibu ambapo kumekuwa na mgogoro wa magofu ya Kaole na kuna marekebisho ya sheria namba 10 ya mwaka 1964 na maboresho namba 20 ya mwaka 1979 na kanuni zake kuweka ulazima wa majengo yote yenye zaidi ya miaka 100 yawe chini ya umiliki wa serikali badala ya mtu binafsi,"alisema Kunenge.
Aliongeza kuwa TFS ikusanye mapato ya mali kale kwenye mahoteli au nyumba za kulala wageni na marekebisho ya Gn namba 49 ya mwakab1973 baada ya kumega eneo la hekari 24.7 lililotolewa kwa wananchi.
KITONGOJI CHA KAJANJO KIJIJI CHA SAADANI CHATENGEWA HEKARI 50
Alisema eneo hilo la hekari 50 wamepewa wakazi wa kitongoji hicho ambapo kimevunjwa ambapo kuna kaya 17 ambazo zilikuwa hapo na kuongezeka na kufika 120 pia makambi ya muda 72 ambayo wanajihusisha na uvunaji mikoko waondoke kwenye hifadhi ya mikoko.
"Hifadhi ya Saadani SANAPA ilipe kiasi cha shilingi milioni 287 kwa ajili ya mashamba na maendelezo kwa kaya 17 pia kamishna msaidizi wa ardhi abadilishe hati ya eneo la Sea Salt kwa kupunguziwa hekari 50 na mmiliki huyo alinde mipaka yake na watu wasiingie tena kwenye eneo hilo,"alisema Kunenge.
Alimtaka Kamshna Msaidizi wa Ardhi kufuta hati ya mmiliki wa sasa wa East Africa Resort kwa kuwa zipo ndani ya hifadhi na haijaendelezwa na kumtaka Mkurugenzi wa Halmshauri ya Chalinze kufuta kitongoji cha Kajanjo na kuhakisha wananchi wanahamishiwa kwenye hekari hizo 50.
WALIOVAMIA RAZABA WATAKIWA KUONDOKA
Hayo yalisemwa na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge wakati wa ziara yake kwenye maeneo ya Saadani, (RAZABA) na Mji Mkongwe Bagamoyo na kutoa matamko ya utekelezaji wa maamuzi ya Baraza la Mawaziri kuhusu Migogoro ya matumizi ya Ardhi Mkoani Pwani.
Kunenge alisema kuwa maamuzi ya kuwaondoa wananchi hao yametokana na serikali baada ys kushughulikia migogoro ya ardhi ambapo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliunda timu ya Mawaziri nane wa kisekta iliyoshirikiana na timu ya wataalam na kufika katika maeneno mbalimbali likiwemo la RAZABA na kutoa mapendekezo ambayo yaliridhiwa na baraza la Mawaziri kwa utekelezaji.
"Shamba hilo lilikuwa ranchi ya Mifugo ambayo ilitolewa na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, eneo hili lilikuwa na ukubwa wa hekari 28,097 ambazo ziligawanywa katika shamba namba 364,365/1 na 365/2 Makurunge,"alisema Kunenge.
Alisema kufuatia maagizo hayo aliwataka wananchi waliovamia eneo hilo la RAZABA kuondoka kwa sababu ni mali ya serikali na kuanzia sasa eneo hilo litakuwa chini ya usimamizi wa Wakala wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (TFS).
Tuesday, June 6, 2023
SERIKALI YATATUA MIGOGORO SUGU YA ARDHI MKOANI PWANI
SERIKALI imewaagiza wananchi zaidi ya 5,000 waliyovamia na kuishi katika Ranchi ya Zanzibar Bagamoyo (RAZABA) kuondoka na kuikabidhi Wakala wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (TFS) kulisimamia eneo hilo.
Agizo hilo limetolewa leo Juni 6, 2023 na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge wakati wa Ziara yake eneo la Saadani na (RAZABA) na Mji Mkongwe Bagamoyo ya kutoa matamko ya Utekelezaji wa Maamuzi ya Baraza la Mawaziri kuhusu Migogoro ya Matumizi ya Ardhi Mkoani Pwani.
Kunenge amesema maamuzi ya kuwaondoa wananchi hao yametokana na serikali kushughulikia migogoro ya ardhi ambapo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliunda timu ya Mawaziri wanane wa kisekta iliyoshirikiana na timu ya wataalam na kufika katika maeneno mbalimbali likiwemo la RAZABA na kutoa mapendekezo ambayo yaliridhiwa na baraza la Mawaziri kwa utekelezaji.
"Shamba hilo lilikuwa ranchi ya Mifugo ambayo ilitolewa na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, eneo hili lilikuwa na ukubwa wa hekari 28,097 ambazo ziligawanywa katika shamba namba 364,365/1 na 365/2 Makurunge,"amesema Kunenge.
“Naagiza wananchi wa eneo hili la RAZABA kuondoka mara moja kwa sababu ni mali ya serikali na kuanzia sasa lipo chini ya usimamizi wa Wakala wa Usimamizi wa Misitu Tanzania TFS,” amesema Kunenge.
Katika hatua nyingine akiwa Kijiji cha Saadani Kunenge ameagiza leseni ya kampuni ya Sea Salt kupunguza eneo la hekari 50 kati ya 2,000 zinazomilikiwa na kampuni hiyo ambalo litagawiwa kwa ajili ya wananchi wa Kitongoji cha Kajanjo.
Amemtaka Kamshna Msaidizi wa Ardhi kufuta hati ya mmiliki wa sasa wa East Africa Resort kwa kuwa zipo ndani ya hifadhi na hakijaendelezwa.
Aidha amemtaka Mkurugenzi wa Halmshauri ya Chalinze kufuta kitongoji cha Kajanjo na kuhakisha Wananchi wanahamishiwa kwenye hekari hizo 50.
Pia amemuagiza Kamishna Msaidizi wa Ardhi, kufuta hati ya upimaji eneo la Mji Mkongwe, uliofanyika ndani ya eneo la hifadhi kwa kuwa zilitolewa ndani ya GN namba 1983 na kutatua mgogoro wa ardhi eneo la magofu ya Kaole na Familia ya Omary Sherdel.
Sunday, June 4, 2023
WAFANYABIASHARA HALMASHAURI YA WILAYA YA KIBAHA WATAKIWA KUUNGANA
WAFANYABIASHARA wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Mkoani Pwani wametakiwa kuungana ili waweze kupata fursa mbalimbali za kiuchumi zilizopo kwenye Wilaya hiyo.
Hayo yalisemwa Mlandizi Wilayani Kibaha na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT) Mkoa wa Pwani Abdala Ndauka wakati wa mkutano na wafanyabiashara wa Mlandizi.
Ndauka alisema kuwa serikali au wadau wanashindwa kuwafikia wafanyabiashara kutokana na kutokuwa na umoja lakini wakijiunga kwenye umoja ni rahisi kunufaika.
"Serikali haifanyi kazi na mtu mmoja bali inawapa fursa watu kutokana na makundi hivyo ili wafanyabiashara wa Halmashauri hiyo wanufaike na fursa hizo lazima waungane,"alisema Ndauka.
Alisema kuwa Jumuiya ya wafanyabiashara Halmashauri hiyo ilikuwepo lakini ilivunjika hivyo wafanyabiashara walikosa fursa nyingi lakini nia waliyoionesha ya kurudi itawasaidia sana.
"Mnapoungana mnakuwa na sauti moja hivyo ni rahisi kusikilizwa tofauti na mfanyabiashara anapolalamika peke yake pia inasaidia kupata haki zao na kupunguza vitendo vya rushwa na serikali kupata mapato,"alisema Ndauka.
Aidha alisema kuwa na wafanyabiashara hao hawapaswi kuchanganya siasa na biashara kwani inasababisha mgawanyiko baina yao na siasa wawaachie wanasiasa.
Kwa upande wake mratibu wa mkutano huo Majuto Ngozi alisema kuwa wanamshukuru mwenyekiti wa kutoa elimu kwa wafanyabiashara juu ya umuhimu wa kuungana.
Ngozi alisema wataendelea na mchakato ili kuunda Jumuiya yao kwa kutoa elimu kwa wafanyabiashara wengi zaidi ili kuwa na utaratibu mzuri na kufanya uchaguzi wa viongozi ili kupata uongozi imara.
Naye moja ya wafanyabiashara Fihiri Msangi ambaye ni moja ya wanachana wa Jumuiya hiyo alisema kuwa amepata manufaa makubwa ikiwa ni pamoja na kupata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali ya kibiashara.
Msangi alisema kuwa ameweza kupata pasi ya kusafiria kupitia Jumuiya hivyo kuwa na urahisi wa kwenda nje ya nchi kwa ajili ya kutafuta fursa nje ya nchi.
Katika mkutano huo wafanyabiashara hao walikubaliana kuunda Jumuiya hiyo lakini wapewe elimu juu ya faida za Jumuiya ili wapate uelewa wa pamoja ambapo waliomba wapewe katiba ili waone miongozo ya Jumuiya hiyo.