MKUU wa wilaya ya Kibaha Asumter
Mshama amesema anasikitishwa na watu wanaomsema vibaya Rais Dk John Magufuli
kwa kutothamini kile anachokifanya katika kurejesha rasilimali za umma.
Akizungumza na waandishi wa
habari ofisini kwake mjini Kibaha alisema kuwa kazi inayofanywa na Rais
inapaswa kuungwa mkono na kila Mtanzania yoyote anayeitakia mema nchi yake.
Mshama alisema kuwa kutokana na
jitihada anazozifanya wananchi wanapaswa kumuunga mkono kwa kubainisha wale
ambao hawana uzalendo na nchi yao.
“Rais kasikia kero nyingi na
sasa ameanza kutekeleza kwa vitendo mfano masuala ya usafiri, upatikanaji wa
dawa, suala la madini, reli na masuala ya viwanda iweje watu waanze kumsemea
vibaya na kumwita majina yasiyofaa jambo hili halikubaliki,” alisema Mashama.
Alisema kuwa kuna njia nzuri za
kumfikishia ujumbe hata kama unaona anakosea lakini siyo kumwambia maneno
mabaya yasiyofaa ni vema kutumia njia nzuri.
“Hata vitabu vya dini
vinatuelekeza kutii mamlaka iliyopo na mamlaka yoyote imewekwa na Mungu hivyo
lazima watu wanapaswa kuheshimu mamlaka,” alisema Mshama.
Aidha alisema anatoa pole kwa
Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lisu kwa kujeruhiwa kwa kupigwa risasi na
watu wasiojulikana hivi karibuni mkoani Dodoma.
“Tunampa pole Tundu Lisu kwa
kujeruhiwa na tunaamini watu waliohusika na tukio hilo watakamatwa tu na
wananchi ndiyo watakaojua wafanywe nini watu hao,” alisema Mshama.
Alibainisha kuwa kwa sasa nchi
imeingia kwenye matukio ambayo si ya kawaida ikiwa ni pamoja na watoto kutekwa
watu kujeruhiwa kwa silaha utamaduni ambao si Wawatanzania na haupswi kuungwa
mkono.
“Matukio kama haya na mengine ya
ukatili kama yaliyokuwa yakitokea wilaya ya Kibiti ya kuwaua watu wasio na
hatia ni mambyo mabaya na serikali imedhamiria kupambana nayo kwa nguvu zote,”
alisema Mshama.
Aliwataka Watanzania kuendelea
kuiombea nchi imani ili iendelee kuwa Kisiwa cha amani na kuachana na watu
wanaotaka kuichafua nchi ili ionekane ina matatizo.
Mwisho.
John Gagarini, Kibaha
WATUMISHI wa Umma ambao
wanaotumia vyeti vya kughushi wametakiwa kujiondoa wenyewe kwani endapo
watabainika watapelekwa kwenye vyombo vya sheria ikiwa ni pamoja na kurudisha
fedha wanazojipatia kupitia mishahara.
Hayo yalisemwa mjini Kibaha na Waziri
wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Angela
Kairuki wakati akizungumza na watumishi wa ofisi ya mkuu wa mkoa, watumishi wa
Halmashauri ya wilaya ya Kibaha na Halmashauri ya Mji Kibaha.
Kairuki alisema kuwa watumishi
wa umma nchini wanaotumia vyeti vya kughushi au visivyo vyao wajiondoe wenyewe mara
moja katika utumishi wa umma kwani wakiendelea kukaa itawagharimu na endapo
watabainika watatakiwa kurejesha mishahara ya miezi yote waliyoiibia serikali.
“Hata kwa upande wa watumishi
ambao hawajahakikiwa kwenye zoezi la uhakiki wa vyeti kwa watumishi nao
wanatakiwa wajiondoe kwani wakibainika hatua kali zitachukuliwa dhidi yao na
fedha wanazolipwa kupitia mshahara watazirudisha,” alisema Kairuki.
Alisema kuwa makatibu tawala wa
mikoa wanapaswa kuangalia na kujiridhisha na majina ya watumishi kwenye orodha
ya malipo ya mishahara ya watumishi wa umma na ya kwenye zoezi la uhakiki kama
yanafanana.
“Majina yalioonekana kwenye
zoezi la uhakiki ndiyo yanayopaswa kuonekana kwenye orodha ya ya malipo ya
mishahara na kama kuna mtumishi hajahakikiwa anatakiwa aondolewe kwenye malipo
ya mshahara,” alisema Kairuki.
Aidha alisema kuwa serikali
itaendelea na zoezi kuhakikiwa watumishi hadi itakapojiridhisha kuwa hakuna
watumishi ambao hawana sifa kwenye utumishi wa umma.
Mwisho.