Na John Gagarini, Kisarawe
SHIRIKA la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO) mkoa wa Pwani kupitia mradi
wa umeme vijijini (REA) unatarajia kusambaza umeme kwa wananchi 11,000 wenye
thamani ya shilingi bilioni 30 kwenye vijiji 109 vya mkoa huo .
Kwa mujibu wa Mhandisi mkuu wa Mradi huo wa REA mkoa wa Pwani Leo
Mwakatobe alisema mradi huo wa awamu ya pili utakamilika mwishoni mwa mwezi wa
sita mwaka huu.
Mwakatobe alisema
kuwa lengo kubwa kwa sasa ni kutekeleza agizo lililotolewa na serikali la
kuhakikisha miradi hiyo ya umemem vijijini inawafiki wananchi wengi na kwa
wakati uliopangwa.
“Tumeshaanza katika kutekeleza
miradi hiyo katika maeneo ya Chalinze, Kisarawe na tutaendelea katika sehemu
mbali mbali za Mkoa wetu wa Pwani na tunatarajia kufikia vijiji vipatavyo 109
vilivyopo katika Mkoa wetu,” alisema Madulu.
Alisema kuwa kuwa mbali ya kuendelea kukutekeleza miradi hiyo hata hivyo
wanakumbana na changamoto nyingi katika utekelezaji wa wakati wanapotaka kupitisha miundomibu katika
makazi ya watu.
“Baadhi ya watu wamekuwa hawataki kuridhia umeme kupita kwenye maeneo
yao au kutaka fidia kubwa hali ambayo inasababisha kuwa na changamoto za hapa
na pale lakini hata hivyo tunajitahidi kuwaelewe umuhimu wa miradi hiyo na
kupata nishati hiyo ya umeme,” alisema Mwakatobe.
Kwa upande wake Meneja wa TANESCO Mkoa wa Pwani Martin Madulu
alisema kuwa kwa sasa wanatekeleza agizo lililotolewa na serikali
kuhakikisha wanawafikia wateja wao wote hususani wale wa vijijini kwa
lengo kuweza kuwaunganishia umeme kwa bei nafuu.
Madulu alisema kuwa watahakikisha wanafanya jitihada ili kuwafikia
wateja wao ili waweze kuwa na nishati ya umeme katika maeneo mbai mbali hususan
kwa wananchi wanaoishi katika maeneo ya vijijini.
Wakati huo huo wakazi zaidi wa 100 katika kijiji cha
Nyeburu Wilayani Kisarawe waliokuwa na tatizo la upatikanaji
wa nishati ya umeme na kuishi katika giza kwa kipindi cha muda
mrefu kwa sasa wamenufaika baada ya kuunganishiwa umeme kutokana na
kukamilika kwa mradi wa umeme vijijini (REA) awamu wa pili.
Baadhi ya wakazi hao walisema kwamba kukamilika kwa mradi huo kutaweza
kuleta chachu kubwa ya kimaendeleo katika kijiji hicho kwani mwanzoni walikuwa wanashindwa tutimiza malengo
yao waliyojiwekea kutokana na kutokuwa na nishati hiyo ya umeme.
Mwisho.