Na John Gagarini, Kibaha
MKOA wa Pwani unatarajiwa kuwa moja
ya mikoa ambayo itakuwa kwa kasi kutokana na kuongezeka kwa shughuli nyingi za
uwekezaji za kiuchumi ikiwa ni pamoja na ujenzi wa bandari wilayani Bagamoyo.
Akizungumza na mwandishi wa habari
hizi mjini Kibaha mkuu wa mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo alisema kuwa
mkoa una fursa nyingi za uwekezaji na watu binafsi pamoja na makampuni
yameonyesha nia ya kuwekeza.
Ndikilo alisema kuwa uwekezaji
umeanza kuchukua nafasi yake baada ya Jiji la Dar es Salaam kuonekana kuwa
limejaa hivyo fursa iliyopo ni mkoa huo ambao uko jirani na Dar es Salaam.
“Kwa sasa tunajivunia na mojawapo ya
uwekezaji mkubwa ni ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo ambayo itaongeza pato la mkoa
huo kwani utazalisha ajira nyingi na wageni wengi wataingia kwa ajili ya
shughuli nyingi za kibiashara,” alisema Ndikilo.
Alisema uwekezaji mwingine ni pale
Kisarawe ambapo kimejengwa kiwanda cha saruji, Kibaha kuna viwanda vya Jipsam,
Nondo na uwekezaji sehemu nyingine mbalimbali za wilaya zinazounda mkoa huo.
“Tukija kwenye zao kuu la biashara la
Korosho nalo limezidi kunufaisha wakulima ambapo kwa sasa kilo ya korosho
imepanda na kwa mnada sasa inauzwa kati ya 2,600 na 2,700 kutoka chini ya
shilingi 1,000 na hii ni kutokana na mfumo wa stakabadhi ghalani,” alisema
Ndikilo.
Aidha alisema kuwa kwa kipindi kirefu
mkoa huo haukuwa na fursa nyingi hali ambayo ilisababisha uonekane kama uko
nyuma kiuchumi tofauti na ilivyo sasa fursa zimekuwa nyingi sana hivyo
mafanikio ya kiuchumi yatakuwa makubwa.
Aliwataka watu wa mkoa huo hususani
vijana kutumia fursa hizo zilizopo ambazo zimejitokeza kwa sasa ili kujikwamua
na hali ngumu ya kimaisha pia watumie fursa za kilimo ambazo ni nyingi.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
MKOA wa Pwani unaendelea na uhakiki
wa watu walioweka mashamba pori ili taarifa zipelekwe kwa Waziri husika na
baadaye kwa Rais ili kutengua umiliki wao endapo watashindwa kuyaendeleza
hususani wale walionunua kwenye kitovu cha Mji wa Kibaha.
Kwa mujibu wa Mkuu wa mkoa wa Pwani
Injinia Evarist Ndikilo alisema kuwa kuna mashamba pori mengi makubwa ambayo
hayajaendelezwa kwenye wilaya zote za mkoa huo ikiwa ni pamoja na Kibaha,
Kisarawe, Rufiji, Bagamoyo na Mkuranga.
Ndikilo alisema kuwa tayari
wameshaanza kuyafanyia kazi mashambapori hayo kwa kushirikiana na wakurugenzi
wa Halmashauri kwa mashamba yasiyoendelezwa.
“Tayari tumeshawapelekea notisi
baadhi yao ili wajieleze ni kwanini wameshindwa kuyaendeleza mashamba hayo na
kwanini wasinyanganywe kutokana na kushindwa kuyaendeleza,” alisema Ndikilo.
Kwa upande wa kitovu cha Mji wa
Kibaha ambako ndiyo makao makuu ya mkoa huo alisema kuwa wamiliki binafsi
pamoja na taasisi ambazo ni nyingi wameshapewa barua kujieleza kwanini
hawakuviendeleza viwanja hivyo.
“Tunawashangaa ni kwa nini
wameshindwa kuendeleza viwanja hivyo ambavyo endapo vingejengwa vingeweka suraa
nzuri ya mji kwani hapo ndiyo kwenye mandari ya uso wa mji,” alisema Ndikilo.
Alisema kuwa licha ya kutakiwa
kujieleza kwa nini hawakuviendeleza viwanja hivyo pia waeleze kuwa watavijenga
lini na muda watakaokubaliana hawapaswi kuupitisha tena.
“Kwa watakaoshindwa kuviendeleza
baada ya makubaliano watanyanganywa viwanja hivyo ili wapewe wengine
watakaoweza kuviendeleza kwa kujenga kwa wakati ukaoakuwa umepangwa,” alisema
Ndikilo.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
JUMUIYA ya Wazazi kupitia Chama Cha
Mapinduzi (CCM) Kibaha Mjini kimezigawia Jumuiya za Kata ardhi yenye ukubwa wa
hekari moja kwa lengo la kuziendeleza kiuchumi.
Akizungumza na mwandishi wa habari
hizi mjini Kibaha baada ya zoezi hilo la kuwagawia ardhi hiyo ambalo
lilifanyika kwenye sherehe za siku ya Uhuru, Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Kibaha
Mjini Dk Athuman Mokiwa alisema kuwa eneo hilo litakuwa kitovu cha uchumi wa
Jumuiya hiyo.
Mokiwa alisema kuwa eneo hilo lenye
ukubwa wa hekari 15 wameligawa kwa kata 14 za kichama ambapo kila kata inapaswa
kuziendeleza kwa kulima na baadaye kufanya ujenzi.
“Kipindi cha nyuma tulishindwa
kuliendeleza kutokana na kukosa fedha kwa ajili ya kulipima lakini baada ya
kulipima sasa tumegawa kila kata wawe na eneo lao kwa ajili ya shughuli za
kiuchumi,”alisema Dk Mokiwa.
Alisema kuwa shamba hilo lilikuwa
likivamiwa na watu kutokana na kutokuwa na hati za umiliki lakini kwa sasa
wameshalimiliki kisheria hivyo hakuna mtu atakayeweza kuvamia tena.
Naye katibu wa Wazazi kata ya Kibaha
lilipo shamba hilo Rehema Ally alisema kuwa wanaushukuru uongozi kwa kuwapatia
eneo ambapo wanatarajia kuliendeleza na hiyo ni rasilimali yao kiuchumi.
Ally alisema kuwa baada ya kupatikana
hati watawakaribisha wawekezaji kwa ajili ya kujenga taasisi zikiwemo za shule
au zaahanati na huduma nyingine za kijamii.
Viongozi wa Jumuiya hizo za kata
wamekubaliana kufanya usafi kila baada ya wiki mbili ikiwa ni kuunga mkono
juhudi za Rais Dk John Magufuli juu ya usafi kukabiliana na magonjwa ya
milipuko pia kuweka maeneo mbalimbali katika hali ya usafi.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
KUFUATIA dereva wa Pikipiki wa Maili
Moja wilayani Kibaha mkoani Pwani Ally Rashid (35) kuuwawa kwa kupigwa risasi
na watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi kisha kumpora pikipiki aliyokuwa
akiieendesha madereva wenzake wameomba uchunguzi wa kina ufanyike kuhusiana na
tukio hilo.
Akizungumza na mwandishi wa habari
hizi mjini Kibaha katibu wa Chama Cha Madereva Pikipiki Kibaha (CHAWAMAPIKI)
Shaban Kambi alisema tukio hilo ni la kushangaza kwa watu kutumia bunduki kwa
ajili ya kupora pikipiki likiwa ni tukio la pili.
Kambi alisema kuwa kumekuwa na
matukio ya wizi wa pikipiki lakini kwa kutumia bunduki si hali ya kawaida hivyo
tunaomba polisi wafuatilie tukio hilo la kusikitisha kwa mwenzetu kuuwawa.
“Matukio ya kutumia silaha ni matatu
ambapo mtu mmoja alivamiwa nyumbani kwake na kupigwa risasi na kufa la pili ni
mwenzetu mwingine alipigwa risasi ya mguuni na kuporwa pikipiki lakini hakufa
huku mwenzetu wa juzi naye alipigwa risasi na kufa ambapo cha kushangaza
matukio yote yametokea upande mmoja,” alisema Kambi.
Alisema matukio yote hayo yametokea
maeneo ya machinjioni hali ambayo inawapa hofu wakazi wa Maili Moja kwa kuona
kuwa maisha yao sasa yako hatarini kwa watu hao kufanya uahalifu kwa kutumia
bunduki.
“Tumesha waambia madereva pikipiki
kuwa makini kwani kuna baadhi ya maeneo kwa sasa ni hatarishi pia wakiwa na
wasiwasi wasiwabebe watu wasiowafahamu hasa nyakati za usiku hasa katika
kipindi hichi cha mwisho wa mwaka,” alisema Kambi.
Aidha alisema kuwa wao wako tayari
kushirikiana na jeshi la polisi katika kufuatilia watu wanaojihusisha na
matukio hayo ya uporaji wa pikipiki pamoja na mali za watu.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
MKOA wa Pwani unatarajia kujenga
Kituo Kikubwa cha Mabasi pamoja na Soko baada ya kupata mkopo toka Benki ya
Uwekezaji ya (TIB) na kuufanya mji wa Kibaha kuwa wakisasa.
Hayo yalisemwa na mkuu wa mkoa wa
Pwani alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mkuu wa mkoa
wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo na kusema kuwa kwa sasa taratibu zinaendelea
baina ya Halmashauri ya Mji wa Kibaha na benki hiyo.
Ndikilo alisema kuwa ujenzi huo
unatarajiwa kuanza wakati wowote kuanzia sasa mara taratibu za kitaalamu
zitakapokamilika ambapo kwa sasa bado zinaendelea.
“Tunatarajia kuwa na stendi ya kisasa
pamoja na soko hasa ikizingatiwa mkoa ulikuwa hauna soko kubwa bali lililopo ni
dogo na halina uwezo wa kuchukua bidhaa nyingi,” alisema Ndikilo.
Alisema kuwa wafanyabiashara wa mkoa
wa Pwani hususani wale wa makao makuu ya mkoa Maili Moja na vitongoji vyake
huwalazimu kwenda kununua bidhaa Kariakoo au kwenye masoko mengine Jijini Dar
es Salaam jambo ambalo linafanya bei za bidhaa kuwa juu.
“Kibaha ambako ndiyo makao makuu ya
mkoa ni kama malango wa Jiji la Dar es Salaam lakini bidhaa zimekuwa zikipita
hapa na kwenda huko kisha wafanyabiashara kwenda kununua na kuzirudisha hapa
hivyo kupandisha bei kutokana na gharama kuwa kubwa,” alisema Ndikilo.
Aidha alisema kuwa soko hilo ambalo
litajengwa sambamba na stendi litakuwa la kisasa ambapo magari yatakuwa na
uwezo wa kuingia na kushusha bidhaa na si kama ilivyo sasa ambapo kutokana na
udogo wa soko lililopo hubidi magari ya bidhaa yashindwe kuingia.
Mwisho.