MKUU wa Mkoa wa Pwani Stanslaus Nyongo amezitaka taasisi wezeshi zisiwe adui badala yake zitoe elimu kwa wadau wake ili kuondoa hali yakuonekana kama ni maadui kwa wawekezaji.
Nyongo aliyasema hayo kwenye semina ya Viwanda kupitia Chemba ya Taifa ya Biashara (TNCC) Mkoa wa Pwani.
Alisema kuwa taasisi hizo zinapaswa kuweka mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara na wawekezaji badala ya kuonekana wao kama ni maadui wa biashara.
"Taasisi wezeshi zinapaswa kuwa daraja kati yao na serikali hivyo zinapaswa kutoa elimu juu ya utendaji kazi wao ili kuwa na ushirikiano kwani lengo ni kuboresha mazingira ya utendaji kazi,"alisema Nyongo.
Alisema kuwa kazi yao kubwa ni kujenga uelewa juu ya kazi zao na kutatua changamoto za wawekezaji na wafanyabiashara ili mazingira yawe bora.
"Sekta wezeshi pia zisikilize hoja zisionekane kama kazi yao ni kukusanya tu mapato bali wajue changamoto zao na kuzitatua na serikali inasikiliza maoni na kuyafanyia kazi,"alisema Nyongo.
Aidha alisema kuwa changamoto ya miundombinu mibovu ya barabara ya kwenda viwandani inafanyiwa kazi kwani kuna mkakati maalum kutenga fedha kiasi cha shilingi bilioni 28.
"Kwa sasa mkoa una viwanda 1,768 vikubwa vikiwa ni 503 vya kati 248 vidogo 1,017 na vimetoa ajira rasmi kwa watu zaidi ya 23,000 na zisizo rasmi zaidi ya 62,000,"alisema Nyongo.
Kwa upanda wake Rais wa TNCC Vicent Minja alisema kuwa serikali imeipa sekta binafsi kutekeleza kwa zaidi ya asilimia 70 ya kufikia dira ya maendeleo wamejipanga kufikia lengo hilo.
Minja alisema kuwa kwakuwa serikali imewaamini wasilalamike bali watoe mapendekezo kwani wameona mabadiliko kwa baadhi ya sheria ambazo zimebadilishwa na bunge.
Naye Mwenyekiti wa TNCC Mkoa wa Pwani Said Mfinanga alisema kuwa sekta wezeshi zinapaswa kuwa wawezeshaji na siyo wakwamishaji wa uwekezaji.
Mfinanga alisema kuwa majukwaa kama hayo yamekuwa yakiwaweka kwa pamoja na sekta wezeshi ili kujadili kwa pamoja na kukabili changamoto.





