Thursday, July 27, 2017

WAZIRI WA AFYA ARIDHIA MLANDIZI HOSPITALI WILAYA





                                       Na John Gagarini, Kibaha

WAZIRI wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Ummy Mwalimu amekubali maombi ya Kituo cha Afya cha Mlandizi wilayani Kibaha mkoani Pwani kuwa Hospitali ya wilaya.

Alitoa tamko hilo kwenye uwanja wa Mtongani Mlandizi wilayani Kibahya wakati akipokea Magari mawili ya kubeba wagonjwa na vitanda vitatu vya kuzalishia mama wajawazito kutoka kwa Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini Hamoud Jumaa na gari moja kutoka kwa Rais Dk John Magufuli.

Alisema kuwa ombi lililotolewa na Mbunge huyo kwa viongozi wa ngazi za juu na kwake amelikubali hivyo mganga mkuu wa wilaya anapaswa kuandika barua na kuzipeleka sehemu husika kisha zifikishwe wizarani kwa ajili ya utekelezaji.

“Mbunge wenu amekuwa akipigania kituo hichi kwa muda mrefu kama alivyosema hivyo naona hakuna kipingamizi ili mradi tu taratibu zifuatwe ili kufikia hatua hiyo lengo kubwa ni kuboresha huduma kwa wananchi,” alisema Mwalimu.

Awali mbunge wa Jimbo hilo Hamoud Jumaa lisema kuwa maombi hayo alishayatoa kwa viongozi mbalimbali ikiwemo kwa Rais wa Awamu ya nne Dk Jakaya Kikwete na Rais Dk John Magufuli.
Jumaa alisema kuwa kituo hicho kwa sasa kinahudumia watu wengi tofauti na ilivyokuwa zamani ambapo kwa sasa wanakaribia watu 100,000 hivyo kuna haja kabisa ya kuwa hospitali ya wilaya.

“Tuliambiwa tufanye maboresho mbalimbali ikiwa ni pamoja na kujenga jengo la upasuaji, chumba cha kuhifadhia maiti pamoja na kuweka uzio vitu vyote hivyo tayari tumevifanya hivyo ombi letu hilo tunaomba ulifanyie kazi kwani tunaamini huduma zitaboreka,” alisema Ummy.

Kwa upande wake kaimu mkurugenzi wa Halmashauri ya Kibaha Beda Mmbaga alisema kuwa watahakikisha wanaboresha mahitaji yote yanayotakiwa ili kutoa huduma za ubora kwa wananchi wanaokwenda kuhudumiwa hapo.


Mwisho.   

Wednesday, June 28, 2017

WAWILI WAUWAWA KWA RISASI KIBITI

Na John Gagarini, Pwani

WATU wasiofahamika wameendelea kufanya mauaji wilayani Kibiti ambapo wamewaua viongozi wawili wa Kijiji cha Mangwi kata ya Mchukwi kwa kuwapiga.

Viongozi waliouwawa ni pamoja na Michael Nicholaus Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mangwi na mtendaji wa Kijiji hicho Shamte Makawa.

Taarifa kutoka eneo la tukio zinasema kuwa tukio hilo lilitokea Juni 27 majira ya usiku kwenye Kijiji hicho na watu hao baada ya kufanya tukio hilo walichoma nyumba moto kisha kutoweka.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo kamanda wa polisi mkoani Pwani Onesmo Lyanga alipoulizwa juu ya tukio hilo alikiri kutokea na kusema kuwa bado wanaendelea kufuatilia ili kuwabaini wahusika wa matukio hayo.    

Mwisho.
      

Tuesday, June 20, 2017

DK MAGUFULI AWATAKA VIONGOZI WASIOWAJIBIKA WAJIONDOE



Na John Gagarini, Kibaha

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk John Magufuli amewataka viongozi mbalimbali ambao wanashindwa kwenda na kasi ya awamu ya tano wajitathmini kwa kujiondoa wenyewe endapo watashindwa kuwajibika.

Aliyasema hayo mjini Kibaha wakati akihutubia wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Bwawani wilayani Kibaha mkoani Pwani.

Dk Magufuli alisema kuwa kiongozi ambaye ndani ya miezi kadhaa hadi mwaka hajui alichokifanya ni vema akajiondoa mwenyewe na asisubiri kuondolewa.

“Serikali ya awamu huu ni ya uwajibikaji na si kutaka kufaidi ukubwa kufanya kazi lengo kubwa likiwa ni kuwatumikia wananchi hasa wale wanyonge ambao wanahitaji huduma zetu kwa kuwatumikia,” alisema Dk Magufuli.

Alisema kuwa kwa sasa tumeweka utaratibu wa kupeleka fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya maendeleo na si matumboni bali ziguse maslahi ya wananchi wengi.

“Fedha hizo si matumboni, semina wala posho au safari za nje ambapo nimepata mialiko zaidi ya 50 ya nje ya nchi lakini nimekataa kwenda nataka kwanza tunyooshane wenyewe kwanza maana nikitoka watajisahau,” alisema Dk Magufuli.

Aidha alisema kuwa baadhi ya viongozi waliotumia vibaya rasilimali atapambana nao kwani Tanzania haiwezi kuwa nchi maskini kwani ni nchi ya pili duniani baada ya Barazili kwa nchi zenye rasilimali nyingi duniani.

“Tunakila aina ya madini, wanyama, maji, maziwa na mlima mrefu Afrika haiwezekani kuwa wasindikizaji wa matarajiri na sisi ni matajiri haiwezekani watu wale mlo mmoja, wanakosa dawa na huduma nyingine hii haiwezekani tutahakikisha wananchi wanaishi maisha yanayoendana na hali halisi ya mali zetu naombeni mniombee,” alisema Dk Magufuli.

Alisema ataendelea kutumbua ambapo kwa sasa wachache wanalalamika na kulia ni wale  waliokuwa wakijinufaisha huku wengi wakiumia huku wengine wakijinufaisha.


Alisema kuwa baadhi ya viongozi walishiriki kuhujumu nchi kwa kuingia mikataba mibovu hasa kwenye upande wa umeme ambapo baadhi ya walidiriki kusaini mikataba mibovu.

“Kwa sasa tuna mipango ya umeme wa uhakika ambapo nilipokwenda Ethiopia nilikutana na waziri mkuu nilimuuliza anafanyaje kupata umeme wa uhakika na kuuza nje tuliongea mengi na sasa wataalamu wake watakaja kwa ajili ya kuweka mazingira ya upatikanaji wa umeme wa uhakika,” alisema Dk Magufuli.

Akizungumzia kuhusiana na mauaji yanayoendelea wilaya za Kibiti na Rufiji alisema kuwa serikali ya awamu hii si ya kuchezea kwani wanaohusika wataona moto kwani watashughulikiwa kikamilifu.

“Tutawanyoosha na tayari tumeanza kuwanyoosha wanafikiri watapita hawatapita kikubwa kinachotakiwa ni wananchi kutoa ushirikiano kwa kuwafichua watu hao kwani baadhi ni ndugu jamaa na marafiki na kuendelea kuwaficha ni kujicheleweshea maendeleo ambapo kwa sasa wilaya hizo hazina viwanda kutokana na mauaji hayo,” alaisema Dk Magufuli.

Alibainisha kuwa mafanikio yaliyopatikana kwenye uongozi wake ni pamoja na makusanyo kuongezeka kutoka bilioni 880 na kufikia kiasi cha shilingi trilioni 1.3 kwa mwezi ambapo fedha hizo zimeweza kulipa elimu bure, pensheni ambazo hazikulipwa tangu mwaka 2010.
“Tumeweza kulipa madeni ambayo yalifikia kiasi cha shilingi trilioni 1.3 sasa yaliyobaki ni bilioni mbili ambapo tutaendelea kulipa madeni hayo kwa watu mbalimbali wanaodai halali na siyo madeni hewa,” alisema Dk Magufuli.

Alibainisha kuwa kutokana na makusanyo hayo serikali imeweza kufuta ada kwenye shule za msingi na sekondari ambapo kwa sasa zinatolewa kiasi cha shilingi bilioni 81.7 kwa ajili ya uendeshaji wa shule.

“Kutokana na elimu bure idadi ya wanafunzi wa darsa la kwanza wanaoandikishwa kwenye shule ya msingi wamefikia milioni mbili toka milioni moja na wanaojiunga na shule za sekondari wamefikia asilimia 27 huku mikopo ya elimu ya juu ikiongezeka toka watu 95,000 hadi 125,000 na bajeti kwa sasa ni bilioni 483,” alisema Dk Magufuli.

Aliupongeza mkoa wa Pwani kuwa na viwanda vingi ambapo na kuwa moja ya mikoa ambayo imetekeleza agizo la kuwa na viwanda ili kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda na kuvutia uwekezaji.

Awali akimkaribisha Rais Dk Magufuli mkuu wa mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo alisema kuwa kwa sasa mkoa una viwanda 371 huku zaidi ya 80 vikiwa ni vikubwa na vya kati na vidogo 260.

Ndikilo alisema hata hivyo pamoja na mafanikio hayo changamoto kubwa ni upungufu wa umeme ambapo mahitaji ni megawati 60 lakini zinazopatikana ni 40, maji yasiyo na uhakika, baadhi ya maeneo kutokuwa na nishati ya gesi na baadhi ya barabara kutokuwa na lami.

Mwisho.











Monday, April 3, 2017

WATUHUMIWA UHALIFU WALIOVALIA HIJABU WAUWAWA NA POLISI

Na John Gagarini, Kibaha
WATU watatu waliokuwa wamepakizana kwenye pikipiki moja wanaodhaniwa kuwa ni wahalifu wakiwa wamevalia hijabu wameuwawa kwa kupigwa risasi na polisi baada ya kukaidi amri ya kutakiwa kusimama.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Kibaha Kamanda wa Polisi mkoani Pwani Onesmo Lyanga alisema kuwa pikipiki nyingine mbili zilifanikiwa kukimbia.
Lyanga akielezea juu ya tukio hilo alisema kuwa lilitokea Aprili 2 mwaka huu majira ya saa 12:00 mchana eneo la kizuizi cha Mwembe Muhoro wilaya ya Rufiji mkoani Pwani barabara kuu ya Dar es Salaam Lindi.
“Siku ya tukio askari walipata taarifa kuwa kulikuwa na pikipiki tatu zikitokea Kibiti kwenda mikoa ya Kusini zikiwa zimebeba watu watatu kila moja huku miongoni mwa pikipiki hizo kati yake mbili wamebebwa watu waliovaa hijabu,” alisema Lyanga.
Alisema kuwa askari wa barabarani walipewa taarifa katika kizuizi cha Mparange na kuwasimamisha ili wawahoji lakini walikataa na kupita ambapo waliwajulisha wenzao kwenye kizuizi cha Ikwiriri lakini walikaidi kusimama.
“Baada ya hapo walifika kizuizi cha Ikwiriri lakini bado walikaidi kusimama na kuendelea kukimbia ndipo walipofika kituo cha Muhoro hata hivyo hawakusimama na askari waliokuwa doria wakiwa kwenye gari waliwafuatilia wakijaribu kuwafuatilia na wakavuka daraja la Mkapa na waliwapa onyo kwa kupiga risasi hewani,” alisema Lyanga.
Aidha alisema kuwa baada ya hapo watu hao waliruka kwenye pikipiki na kuanza kukimbilia msituni na ndipo askari walipowapiga risasi za miguu na kiunoni na kufanikiwa kuwakamata.
“Majeruhi hao walijulikana ni wanaume hata hivyo majina yao hayakuweza kufahamika na walikuwa kwenye pikipiki yenye namba za usajili MC 272 BLW aina ya Boxer yenye rangi nyeusi ambapo watu hao wanaodhaniwa kuwa ni wahalifu kwa mwonekano wao walijaribu kuwawahisha Hospitali ya Misheni ya Mchukwi,” alisema Lyanga.
Lyanga alisema kuwa walipofikishwa hospitali daktari alithibitisha kuwa watu hao wamefariki dunia ambapo hata hivyo majina yao hayakuweza kufahamika huku pikipiki nyingine mbili zilitoroka na kuelekea mkoa wa Lindi na taarifa zimetolewa polisi ili wawakamate.
Aliwataka wananchi kuwa watulivu pale wanaposimamishwa na askari polisi badala ya kujaribu kutoroka na kwa sasa jeshi hilo limeimarisha doria katika kukabiliana na uhalifu.
Mwisho.

Tuesday, March 28, 2017

MBUNGE AZINDUA UJENZI WA UZIO WA KITUO CHA AFYA



 Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini Hamoud Jumaa akionyesha shehena na saruji mifuko 500 kwa ajili ya uzio wa Kituo cha Afya cha Mlandizi wilayani Kibaha mkoani Pwani

 Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini Hamoud Jumaa akiwa amebeba saruji ambayo itatumika kwenye ujenzi wa uzio wa kituo cha afya cha Mlandizi wilayani Kibaha mkoani Pwani 







 Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini Hamoud Jumaa akizindua ujenzi wa uzio wa Kituo cha afya cha Mlandizi wilayani Kibaha mkoani Pwani


Na John Gagarini, Kibaha

KITUO cha Afya cha Mlandizi kimeanza mchakato wa kuelekea kuwa Hospitali ya wilaya kwa kuanza ujenzi wa uzio ambapo Mbunge wa Jimbo la Kibaha 
Vijijini wilayani Kibaha mkoani Pwani Hamoud Jumaa amewataka wafadhili mbalimbali kujitokeza kusaidia ujenzi wa uzio huo ambao utagharimu kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 200.

Akizungumza na waandishi wa habari Mlandizi wakati akizindua ujenzi huo mbunge huyo alisema kuwa wameanza kuboresha huduma zinazotolewa kituoni hapo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa uzio huo ikiwa ni moja ya vigezo vinavyotakiwa kufikia hadhi hiyo.

Jumaa alisema kuwa Kituo hicho cha afya ni tegemeo kubwa kwa wakazi wa Jimbo hilo ambalo kwa sasa lina wakazi 70,000 na wilaya jirani za Bagamoyo na miji ya Chalinze na Kibaha wanapata huduma hapo.

“Mpango huu nimeuanzisha kwa jitihada zangu binafsi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ambapo hadi sasa nimepata mifuko 500 ya saruji, kokoto lori saba mchanga, mchanga na tani moja ya nondo ambavyo vitasaidia katika ujenzi wa uzio huu tunaomba wadau wengine waendelee kutusaidia,” alisema Jumaa.

Alisema kuwa kutokana na kituo hicho cha afya kuwa tegemeo kubwa kwa wameona kuna haja ya kuwa Hospitali ya Wilaya ili waweze kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi watakaokuwa wanapata huduma hapo.

“Tumekubaliana vitongoji 26 na madiwani sita watoe 240,000 huku mfuko wa jimbo ukitoa kiasi cha shilingi milioni 4 kwa ajili ya tofali za uzio ambao utasaidia kuondoa uingiaji holela wa watu bila ya sababu za msingi ndani ya eneo la Kituo cha afya,” alisema Jumaa.

Kwa upande wake Diwani wa kata ya Mlandizi Eufrasia Kadala alisema kuwa wataungana na Mbunge huyo kuhakikisha wanafanikisha ujenzi huo ili kuboresha kituo hicho cha afya.

Kadala alisema kuwa kutokana na kutokuwa na uzio kumekuwa na mwingiliano wa watu kuingia kiholela hasa kutokana na kituo hicho kuwa jirani na makazi ya watu. 

Naye mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Mdogo wa Mlandizi Tatu Jalala alisema kuwa waliupokea mkono mpango huo na kuupeleka kwa jamii kwa lengo la kumuunga mkono mbunge wao.

Jalala alisema kuwa wanaendelea kuihamasisha jamii ili iweze kuchangia ujenzi huo wa uzio ukamilike kwa wakati lengo likiwa ni kufanikisha harakati za kuwa Hosptali ya wilaya.

Mwisho. 

Thursday, March 23, 2017

MWENYEKITI ANUSURIKA KIFO RISASI ZAMJERUHI

Na John Gagarini, Rufiji

MWENYEKITI wa Kitongoji cha Mpalange Kijiji cha Ikwiriri Kaskazini wilayani Rufiji mkoani Pwani Bakari Mpawane amenusurika kifo baada ya kupigwa risasi na watu wasiofahamika.

Mpawane alisema kuwa tukio hilo lilitokea Machi 19 mwaka huu majira ya saa 2 usiku akiwa dukani kwake ambapo alipigwa risasi mkononi na tumboni.

Alisema kuwa mtu aliyempiga alikuwa amepakizwa kwenye pikpiki akampiga kisha wakatokomea kusikujulikana kwa kutumia pikpiki hiyo ambayo namba zake hazikuweza kutambulika mara moja.

“Watu hao ambao walikuwa wamepakizana kwenye pikipiki walifika hapo na mmoja wao kumwita jina lake mara nikashtukia napigwa risasi ambazo hata hivyo namshukuru Mungu ziliniparaza tu na hazikuweza kuniletea madhara makubwa ambayo yangehatarisha uhai wangu,” alisema Mpawane.

Aidha alisema kuwa anamshukuru Mungu na sasa anaendelea na matibabu na hali yake inaendelea vizuri hata hivyo ana hofu na anafikiria atakaporudi kwake baada ya matibabu ataishije baada ya kunusurika kwenye tukio kubwa na la uuaji kama hilo.

“Naomba serikali na jeshi la polisi liweke mikakati kabambe ili kuvunja ngome za kiuhalifu na mtandao unaomaliza hasa viongozi bila kujua chanzo ni masuala ya kisiasa ama nini,”alisema Mpawane.

Akizungumza mara baada ya kwenda kumtembelea mwenyekiti huyo katika kituo cha afya cha Mchukwi anapopatiwa matibabu Mkuu wa mkoa wa Pwani Mhandisi  Evarist Ndikilo alisema kuwa hilo ni tukio la tatu kwa mwezi mmoja likiwemo lililotokea machi 13 mwaka huu kwa mwenyekiti wa kitongoji cha Kazamoyo wilayani hapa, Hemed Njiwa (45) kuuwawa kwa kupigwa risasi akiwa nyumbani na tukio lililohusisha kifo cha OCCID.

Ndikilo alisema kuwa wanaendelea kuwasaka watu hao usiku na mchana hadi kuhakikisha wanawakamata ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria kuhusiana na tukio hilo.

“Tutawasaka na hatafanikiwa  kwa mipango yao waliojiwekea tumejidhatiti na tutahakikisha tunategua mipango yao na kurejesha amani kwa wananchi,”alisema Ndikilo.

Aidha aliwashukuru wahudumu wa afya katika kituo cha afya cha Mchukwi kwa kuokoa maisha ya mwenyekiti huyo pamoja na kutoa huduma nzuri kwa majeruhi na wagonjwa wengine wanaofikishwa hapo kupata matibabu.

Naye Kamanda wa polisi mkoani Pwani,Onesmo Lyanga,aliomba ushirikiano wa wananchi kutoa taarifa polisi mara wanapopata wasiwasi wa watu wanaoingia kwenye maeneo yao.

Kamanda Lyanga alisema ameletwa mkoa wa Pwani kutoka Simiyu kwa ajili ya kufanya kazi na jambo kubwa analohitaji ni ushirikiano na jamii ili waweze kupunguza matukio yanayotikisa ikiwemo la kuuwa wa wenyeviti wa vitongoji,watendaji na wenyeviti wa vijiji.


Mwisho 

MADEREVA SABA WAPORA FEDHA NA SIMU WAJERUHIWA

Na John Gagarini, Kibaha

MADEREVA saba wamejeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili kisha kuwapora fedha kiasi cha shilingi 920,000 baada ya watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi kufunga barabara ya Kilwa kwa kutumia magogo.

Aidha watu hao licha ya kuwajeruhi na kuwapora fedha pia waliwaibia madereva hao simu saba na kutoweka kusikojulikana.

Kwa Mujibu wa taarifa zilizotolewa mjini Kibaha na kamanda wa Polisi mkoani Pwani Onesmo Lyanga amesema kuwa tukio hilo lilitokea Machi 22 majira ya saa saba usiku katika kijiji cha Kitembo kata ya Mchukwi wilaya ya Kibiti.

Kamanda Lyanga amesema kuwa watu hao sita wanaotuhumiwa kuwa ni majambazi walikuwa na silaha za jadi ikiwa ni pamoja na mapanga na marungu na walizitumia kuwajeruhi madereva hao.

Amesema kuwa hadi sasa hakuna mtu aliyekamatwa kuhusina na tukio hilo na wanaendelea na msako kuhakikisha watu hao wanakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria waweze kujibu tuhuma hizo.

Aidha amewataja madereva waliojeruhiwa kwa mapanga kuwa ni Issa Juma (26) mkazi wa Jijini Dar es Salaam aliyejeruhiwa shavu la kulia, Badru Uwesu (31) mkazi wa Kisemvule Mkuranga aliyejeruhiwa shavu la kulia na mgongoni, Edward Safari (37) mkazi wa Morogoro.

Amewataja wengine kuwa ni Ramadhan Ally (34), Nasoro Mohamed (26), Kassimu Omary (36), Khalifa Mohamed wote wakazi wa Mbagala Jijini Dar es Salaam ambapo majeruhi wote walitibiwa kwenye Hospitali ya Misheni ya Mchukwi na kuruhusiwa kuondoka.

Katika tukio lingine ngombe 102 wamekufa baada ya kunywa maji ambayo yanasadikiwa kuwa hayafai kutumika kwa matumizi yoyote kwenye machimbo ya kokoto.

Kamanda Lyanga amesema kuwa tukio hilo lilitokea Machi 22 mwaka huu majira ya saa 9 alasiri kwenye Kijiji cha Pongwe Msungura Chalinze wilayani Bagamoyo.

Mwisho.