Monday, January 12, 2026

BARBERIAN YAICHAPA TMA

TIMU ya Soka ya Barberian imefanikiwa kuifunga timu ya TMA ya Arusha kwa magoli 2-1 kwenye mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza.

Mchezo huo uliokuwa mkali umefanyika kwenye uwanja wa Filbert Bayi uliopo Mkuza Wilayani Kibaha Mkoani Pwani.

Akizungumzia juu ya mchezo huo mwalimu wa timu ya Barberian Julio Elieza amesema kuwa waliweka mpango mzuri ambao ulifuatwa na wachezaji wake hadi kuibuka na ushindi licha ya kutanguliwa na wapinzani.

Kwa upande wake nahodha wa Barberian Kasim Haruna amesema ushindi wao ulitokana na kufuata maelekezo ya mwalimu wao. 

Mwalimu wa TMA Tiko Tiko alikiri kuzidiwa na wapinzani wao na kujikuta wakiambulia kipigo hicho.

Naye nahodha wa timu hiyo Fadhil Mahimbo amesema licha ya kuongoza walicheza chini na kuwapa nafasi wapinzani wao kurudi na kupata ushindi.

Timu ya Barberian ambayo inatumia uwanja huo wa Filbert Bayi inatarajiwa kucheza tena Januari 17 kwenye uwanja huo dhidi ya timu ya Songea United ambapo wameahidi kuendeleza wimbi la ushindi.


Tuesday, January 6, 2026

KIDULI FC YAJIPANGA KUPINDUA MATOKEO ILI KUTWAA UBINGWA WA MKOA WA PWANI

TIMU ya Soka ya Kiduli Fc ya Kibaha licha ya kupoteza mchezo wa fainali ya kwanza dhidi ya Bagamoyo Sugar ya Bagamoyo kwa 1-0 imejipanga kupindua matokeo ili kutwaa ubingwa wa mkoa wa Pwani.

Kiduli inatarajia kucheza mchezo wa marudiano Januari 12 kwenye uwanja wa Mwendapole na mshindi wa jumla ndiye atakayekuwa bingwa wa ligi daraja la Tatu mkoa wa Pwani.

Akizungumza na waandishi wa habari Mwenyekiti wa timu hiyo Ally Masimike amesema wamepoteza mchezo huo kwa bahati mbaya.

Masimike amesema kuwa watarudi kwenye uwanja wa mazoezi na kufanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza kwenye mchezo wao wa kwanza.

"Lengo letu ni kupambana na kuhakikisha tunashinda ili kuwa mabingwa na kuuwakilisha Mkoa wetu kwenye michuano ya Mabingwa wa Mikoa,"amesema Masimike.

Bagamoyo Sugar iliifunga Kiduli Fc kwa goli 1-0 kwenye mchezo wa fainali ya kwanza kwenye uwanja wa Mwendapole Kibaha huku mchezo wa marudiano ukitarajiwa kupigwa kwenye uwanja huo huo ikiwa ni fainali ya pili ili kupata bingwa wa Mkoa.

Mwenyekiti wa kamati ya mashindano ya Chama Cha Soka Mkoa wa Pwani (COREFA) Nasoro Mbilinyi amesema kuwa ligi hiyo ilikuwa ni kwa wachezaji wenye umri chini ya miaka 20.


Mbilinyi amewataka wadau wa michezo kujitokeza kwa wingi kwenye fainali hiyo ambayo inatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kutokana na matokeo ya mchezo wa kwanza.


Bingwa wa ligi hiyo atapata kombe na atawakilisha Mkoa wa Pwani kwenye mashindano ya ligi ya Mabingwa wa mikoa.

PWANI YAMUUNGA MKONO RAIS KUTOA AJIRA KWA WANANCHI

KONGANI ya viwanda ya Gaini Company Limited iliyopo Kata ya Kikongo Wilaya ya Kibaha Mkoani Pwani inatarajiwa uzalisha na kutoa ajira 1,500 ifikapo Machi mwaka huu itakapoanza uzalishaji.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge alipotembekea Kongani hiyo ambapo uwekezaji huo unaendana kikamilifu na mkakati wa Serikali wa kukuza uchumi wa viwanda pamoja na kuongeza fursa za ajira kwa wananchi, hususani vijana.

Kunenge amesema kuwa Mkoa unaendelea kutekeleza vipaumbele vya Serikali kwa vitendo hususani katika eneo la uzalishaji wa ajira kwa vijana ikiwa ni sehemu ya kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan.

"Hatua hii inayochochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika Mkoa wa Pwani na kuongeza mapato ya Taifa kwa ujumla huku Mkoa ukiendelea kushirikiana na taasisi wezeshi zikiwemo TANESCO, DAWASA na TANROADS ili kuhakikisha hakuna urasimu wowote katika utekelezaji wa masuala ya uwekezaji,"amesema Kunenge.

Amesema kuwa ushirikiano na taasisi hizo ni kuwezesha upatikanaji wa mahitaji muhimu ikiwemo nishati ya umeme, maji pamoja na miundombinu ya barabara na kuwa mradi wa bomba la gesi kutoka Kinyerezi hadi Chalinze tayari umefanyiwa upembuzi yakinifu wa bilioni 2.3 na TPDC jambo litakaloongeza ufanisi wa upatikanaji wa nishati kwa viwanda mkoani humo.

Naye Meneja wa Mradi katika Kongani hiyo QS Bradley Cuthbert Muro amesema kuwa ujenzi wa viwanda viwili umefikia hatua za mwisho ambapo kiwanda cha chuma kimefikia asilimia 85 ya ujenzi huku kiwanda cha cubes kikifikia asilimia 95.

Muro amesema kuwa Kongani hiyo itakuwa na viwanda mbalimbali ikiwemo heavy duty industry, medium industry na light duty industry vikiwemo viwanda vya uzalishaji wa Nondo, Mabati, Steel Pipes, Hallow Sections (RHS) Squqre, Hallow Sections (SHS) Circular, Hallow Sections (CHS) Flat bars pamoja na Misumari.

mwisho

Saturday, December 27, 2025

VIJANA WATAKIWA KULINDA NA KUTUNZA AMANI YA NCHI

MWANADIPLOMASIA Omary Punzi amewataka Vijana kulinda na kutunza amani umoja uzalendo na mshikamano katika nyakati zote ili kuleta Maendeleo ya Taifa.

Punzi ameyasema hayo katika Bonanza la Michezo kwa Vijana liliratibiwa na Kamati ya Vijana Wazalendo Bonanza lililofanyika kwenye viwanja Soko la Ndizi vya Mabibo (Las Vegas) Jijini Dar es Salaam

Punzi ambaye pia ratibu wa Makongamano amesema kuwa lengo la Bonanza hilo ni kuhimiza amani na utulivu nchini. 

Kwa upande wake Mgeni rasmi katika Bonanza hilo Mwenyekiti wa Mtaa wa Jitegemee  Abdallah Kilema aliwaomba vijana wapende michezo na kuwakumbusha michezo ni Ajira Upendo na Afya hivyo wanamichezo wanawajibu wa kutunza amani ya Taifa.

Naye mratibu kutoka mtandao wa YAS Neema aliwaomba vijana wajitokeze kwa wingi katika fursa mbalimbali za kimaendeleo na wao kama Taasisi wataendelea kudhamini mashindano mbalimbali.

Aidha Gervas Pai alishukuru kwa maandalizi mazuri na vijana kuwa na uwezo mkubwa na kuomba walinde Amani, Umoja na Mshikamano wa Taifa na wajitokeze kwa wingi kushiriki michezo.

Kocha wa Timu ya 7 lite Zayd Rashid aliwaomba wadau wa michezo waendelee kuongeza nguvu katika kuwatafutia vijana vifaa vya michezo ambavyo ni kero kubwa na kumshukuru muaandaji wa Bonanza hilo. 

Naye mchezaji Isack Rashid mchezaji bora wa mashindano hayo anesema kuwa ndoto yake ni kuwa mchezaji mkubwa hapa Tanzania ili kuweza kusaidia nchi yake 

Kwenye Bonanza hilo michezo ya vijana chini ya miaka15 kati ya Las Vegas na 7 lite mshindi ni 7 lite 4-0 mchezo wa pili ilikuwa kati ya Las Vegas na 7 lite ambapo Las Vegas imeshinda magoli 3-2

Mshindi wa kwanza alipatiwa mipira 5 na mshindi wa pili mipira 2 kwa upande wa mchezaji bora na goli kipabora kila mmoja aliibuka na shilingi 5,000.Bonanza hilo likishirikisha timu nne za Las Vegas na 7 lite miaka 15 na Las Vegas na 7 lite chini ya miaka 20.

Monday, December 22, 2025

KIDULI YAJISAFISHIA NJIA NUSU FAINALI DARAJA LA TATU MKOA WA PWANI

TIMU ya Kiduli imejihakikishia kuingia hatua ya nusu fainali ya ligi daraja la tatu Mkoa wa Pwani kutoka kundi A baada ya kuifunga Anga kwa magoli 3-2.

Katika mchezo huo ambao ulichezwa kwenye uwanja wa Mwendapole Kibaha Kiduli ilifunga goli la kuongoza kwa bao lililofungwa na Amrani Mkumbo dakika ya 53 ya mchezo.

Kiduli waliongeza goli la pili lililofungwa na Jonathan Martin dakika ya 63 hata hivyo Anga walirudisha magoli yote ambayo yalifungwa na Elia Nduligu dakika ya 76 na Hussein Haruna alisawazisha dakika ya 85.

Huku kila mtazamaji akiamini kuwa mchezo huo utamalizika kwa sare ya magoli 2-2 Benjamin alipigilia msumari wa mwisho dakika ya 90+5 na kuamsha shangwe kwa mashabiki wa Kiduli.

Kwa matokeo hayo Kiduli inaongoza kundi hilo ikiwa imejikusanyia alama 6 huku ikiwa na mchezo mmoja mkononi na kesho itakuwa ni mchezo kati ya Bagamoyo Sugar na Nyika kutoka kundi B mchezo utakaokuwa na ushindani mkali.

Kundi A lina timu za Kiduli, Anga South Academy na Kampala huku kundi B likiwa na timu za Bagamoyo Sugar, Nyika na Kibaha Mji.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani (COREFA) Nasoro Shomvi "Mbilinyi amesema kuwa hatua ya nusu fainali itachezwa Desemba 30 na 31


Tuesday, December 9, 2025

MIAKA 64 YA UHURU "AMANI KWANZA UJENZI WA TAIFA DAIMA-TBN

Leo Desemba 9, tunapoadhimisha miaka 64 tangu Taifa letu lipate Uhuru, Tanzania Bloggers Network (TBN) inawapongeza Watanzania wote kwa kufikia hatua hii muhimu katika historia ya Taifa letu. 

Hii ni siku ya kutafakari safari tuliyotoka, mahali tulipo, na mwelekeo tunaoujenga kwa pamoja.

Waasisi wetu walituwachia zawadi kubwa—Uhuru. Lakini walituonya kuwa Uhuru hauwezi kuwa kamili bila kujitegemea. Leo tunakumbusha maneno ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliyewahi kusisitiza:

"Uhuru hauwezi kukamilika pasipo kujitegemea. Hatuwezi kuitwa huru kama tunategemea wengine kutupatia mahitaji yetu ya kimsingi."

Tujenge Taifa Letu – Tusiibomoe Tanzania

Kama mtandao wa habari za kidijitali, TBN inasisitiza kuwa mafanikio yetu kama Taifa yametokana na utulivu, umoja na mshikamano. Ili kuendelea mbele, tunahitaji kudumisha amani na maridhiano—nguzo muhimu za maendeleo.

Rais mstaafu Benjamin William Mkapa alituasa kwa busara:

"Amani si kitu cha asili; tunahitaji kuilinda na kuitunza kila siku. Bila amani, hakuna maendeleo ya kweli."

Tukikubali kuongozwa na chuki, uchochezi na vurugu, juhudi za waasisi wetu za kupambana na ujinga, umaskini na maradhi zitapotea. Tusiitumie mitandao au uhuru wa maoni kuharibu Taifa letu; tuitumie kulijenga.

Kila Zama na Kiongozi Wake – Tuunge Mkono Mageuzi

Kila kizazi kina wajibu wake. Kama alivyoeleza Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi:

"Kila utawala na zama zake. Kila kiongozi na mchango wake katika ujenzi wa Taifa hili."

Katika awamu ya sasa chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Tanzania inaendelea na mwelekeo wa 4R: Reconciliation, Resilience, Reforms, and Rebuilding. Huu ni mwaliko kwa Watanzania wote kushiriki katika kujenga Taifa lenye maridhiano, mageuzi chanya na uimara wa kiuchumi na kijamii.

Tuna nafasi ya kuzungumza—basi tuseme kwa njia inayojenga, si inayobomoa. Kuthamini Uhuru ni kufanya kazi kwa bidii, kulinda amani, na kuacha kutumiwa kuharibu misingi ya Taifa letu.

TBN Inawatakia Maadhimisho Mema ya Miaka 64 ya Uhuru!

Tanzania Kwanza — Kazi, Utu na Mshikamano. Tusonge Mbele!

Beda Msimbe

Mwenyekiti, Tanzania Bloggers Network (TBN)

TANZANIA NA MAREKANI ZASONGA MBELE KUKAMILISHA MAKUBALIANO MAKUBWA YA UWEKEZAJI


Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, leo amefanya mazungumzo na Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Andrew Lentz, katika Ikulu ya Chamwino, kujadili maeneo muhimu ya ushirikiano na kuimarisha dhamira ya pamoja ya kujenga ushirikiano wa kisasa na wenye manufaa kwa pande zote mbili.

Balozi Lentz—aliyefuatana na Mshauri wa Masuala ya Kisiasa na Uchumi—amesisitiza dhamira ya Washington kuhuisha mahusiano na kuongeza kina la ushirikiano wa kiuchumi, kisiasa na kiusalama kati ya mataifa haya mawili.

“Marekani imejitolea kujenga ushirikiano usiotegemea misaada, bali unaojengwa juu ya ustawi wa pamoja,” alisema Balozi Lentz.

Mazungumzo yamejikita katika hatua za majadiliano ya miradi mikubwa inayoongozwa na kampuni za Marekani. Pande zote mbili zimekubaliana kuwa majadiliano ya miradi miwili ya kimkakati—Mradi wa LNG na Mradi wa Tembo Nickel—yamefikia hatua za mwisho kabla ya kutiwa saini rasmi. Uwekezaji wa tatu, Mradi wa Mahenge Graphite, unaendelea kufanyiwa uchambuzi wa kiufundi.

Rais Samia ameukaribisha upya msimamo wa Marekani na kuhakikishia ujumbe huo kuwa Tanzania itaendelea kusimamia hatua zote zilizobaki ili kukamilisha taratibu na kufungua njia ya utekelezaji wa miradi hiyo.

“Kama taifa lisilofungamana na upande wowote, Tanzania iko wazi, tayari na imejitoa kufanya kazi na washirika wote wanaoheshimu uhuru wetu na kushiriki katika dira yetu ya maendeleo,” alisema Rais.

“Miradi hii ni ya umuhimu mkubwa kwa taifa, na tumejidhatiti kuikamilisha ili iweze kufungua ajira, uwekezaji, na ustawi endelevu kwa wananchi wetu.”

Rais pia alibainisha kuwa zaidi ya kampuni 400 za Marekani kwa sasa zinafanya shughuli zao nchini Tanzania—kiashiria cha uthabiti wa nchi, mazingira mazuri ya uwekezaji na historia ya muda mrefu ya ushirikiano wa kiuchumi kati ya mataifa haya mawili.

Mbali na uwekezaji, mazungumzo yamegusa maeneo mapana ya ushirikiano ikiwemo utulivu wa kisiasa, usalama wa kikanda, mageuzi ya kiuchumi, ukuaji wa sekta binafsi, ushirikiano katika afya na programu za kubadilishana uzoefu kati ya wananchi wa nchi hizi mbili.

Balozi Lentz amempongeza Rais Samia kwa maono na mipango madhubuti ya muda mrefu kupitia Vision 2050, na kusisitiza kuwa Serikali ya Marekani iko tayari kuunga mkono utekelezaji wake pamoja na kuimarisha falsafa ya 4R ya Rais—maridhiano, ustahimilivu, mageuzi na kujenga upya imani katika utawala.

Pande zote zimekubaliana kuwa mawasiliano ya karibu, ushirikiano wa mara kwa mara, na hatua za haraka katika kukamilisha makubaliano yaliyosalia ni muhimu katika kufungua uwezo kamili wa uhusiano kati ya Tanzania na Marekani.

Kikao hiki kinawakilisha hatua muhimu katika kufafanua upya na kuhuisha mahusiano kati ya Tanzania na Marekani. Dhamira ya pamoja iliyothibitishwa na serikali zote mbili inaashiria mwanzo wa ushirikiano wa kisasa, wazi, unaoongozwa na sekta binafsi—ukijengwa juu ya ustawi wa pamoja, kuheshimiana na ushirikiano wa muda mrefu wa kimkakati.

Miradi Mikuu ya Kimkakati

1. Mradi wa LNG — Thamani Inayokadiriwa: Dola Bilioni 42

Mradi mkubwa wa kugundua na kuchakata gesi asilia unaohusisha kampuni kubwa za kimataifa za nishati. Mradi huu unalenga kufungua hazina kubwa ya gesi iliyopo baharini, kuongeza mapato ya taifa, kuunda maelfu ya ajira na kuiweka Tanzania katika ramani ya dunia kama mchezaji muhimu wa LNG.

2. Mradi wa Tembo Nickel — Thamani: Dola Milioni 942

Uwekezaji mkubwa wa madini muhimu eneo la Ngara unaolenga nikeli—kiungo muhimu katika utengenezaji wa betri za magari yanayotumia umeme. Mradi huu utaimarisha minyororo ya kimataifa ya nishati safi, kuchochea viwanda na kuongeza pato la mauzo ya nje.

3. Mradi wa Mahenge Graphite — Thamani: Dola Milioni 300

Chanzo kikubwa duniani cha madini ya graphite yenye ubora wa juu, yenye umuhimu katika uzalishaji wa betri na teknolojia za nishati jadidifu. 

Mradi huu utaimarisha nafasi ya Tanzania kama mtoa huduma mkuu wa malighafi muhimu za viwanda vya kisasa vya betri.