Sunday, June 9, 2024

375 WAFAULU BUNDIKANI SEC YAFUTA ZIRO

SHULE ya Sekondari ya Kata ya Maili Moja Bundikani Halmashauri ya Mji Kibaha imefanikiwa kufaulisha wanafunzi wote wa kidato cha nne 375 kufaulu na kuondoa daraja sifuri.

Hayo yalisemwa Mjini Kibaha na mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Bernard Muyenjwa alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake.

Muyenjwa alisema kuwa ufaulu huo ni asilimia 100 ya wanafunzi waliofanya mtihani wa kidato cha nne waliofanya mitihani yao mwaka jana.

"Wanafunzi 234 wamefaulu kwenda kidato cha tano na vyuo mbalimbali vya kati ambapi ufaulu huo ni sawa na asilimia 65 huku wengine wakisubiri uteuzi wa awamu ya pili,"alisema Muyenjwa.

Alisema kuwa jumla ya wanafunzi waliofanya mtihani walikuwa 375 wasichana wakiwa 218 wavulana 157 ambapo daraja la kwanza walikuwa 22 wasichana tisa wavulana 13.

"Daraja la pili 79 wasichana 53 wavulana 26 daraja la tatu 144 wasichana 73 wavulana 71 na daraja la nne ni 130 wasichana 83 wavulana 47 huku daraja sifuri kukiwa hakuna hata mmoja,"alisema Muyenjwa.

Aidha alisema kuwa mafanikio hayo yalitokana na mshikamano walionao walimu na kujitolea, kusimamia vizuri mipango iliyowekwa ya kufikia ufaulu.

"Ushirikiano kati ya shule, wazazi na bodi, kusimamia nidhamu kwa wanafunzi na kuhimiza walimu kufundisha kwa kasi na mazoezi ya mara kwa mara na ufuatiliaji, ufanyaji wa mitihani kila Jumamosi,"alisema Muyenjwa.

Aliongeza kuwa upande wa nidhamu ni kuweka uzio na walinzi ili kudhiti wanafunzi kutoka bila ya sababu zisizokuwa na msingi bali iwe ya msingi ndipo atoke au muda wa kuingia shuleni.

"Malengo ni kuhakikisha tunapunguza wanafunzi wanaopata daraja la nne na kuongeza ufaulu wa daraja la kwanza wafikie angala 60 au 70 na hilo linawezekana,"alisema Muyenjwa.

Alibainisha kuwa shule yao ambayo ni kinara kwa shule za Kata kwa kufaulisha kwenye Halmashauri ya Mji Kibaha ikiwa inazidiwa na shule ya Tumbi na Kibaha wasichana ambazo ziko chini ya Shirika la Elimu Kibaha.

"Tunaishukuru Serikali kwa kutoa kiasi cha shilingi milioni 120 kwa ujenzi wa vyumba vya madarasa vinne na changamoto zilizopo ni ndogondogo ambazo ziko ndani ya uwezo wetu walimu wapo wa kutosha zaidi ya 100,"alisema Muyenjwa.

Aliwaomba wazazi na wadau kuendelea kutoa ushirikiano ili shule hiyo iendelee kufanya vizuri kwenye matokeo ya kidato cha nne na kufikia malengo ya kuwa na kidato cha tano na sita.

Saturday, June 8, 2024

LAMI KUWEKWA SHELI MAILI MOJA






WANANCHI wanaopitiwa na mradi wa ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami ya BP Sheli-Maili Moja yenye urefu wa kilometa nne wametakiwa watoe ushirikiano ili kufanikisha ujenzi huo.
Hayo yamesemwa na Diwani wa Kata ya Maili Moja Ramadhan Lutambi alipokuwa akizungumza na wananchi wakati wa utoaji elimu juu ya mradi huo ambao kwa sasa uko kwenye hatua ya usanifu.

Lutambi amesema kuwa mradi huo unatekelezwa na benki ya dunia umeanza kwa kufanya usanifu hivyo wananchi wasiweke vikwazo ili hatua hiyo ambayo ni ya miezi nane iweze kwenda vizuri bila ya kikwazo chochote.

"Tunawaomba wananchi muonyeshe ushirikiano kwani kujengwa lami kwa barabara hii ni mkombozi kwa Kata yetu na italeta maendeleo na kurahisisha shughuli mbalimbali hasa za usafirishaji,"amesema Lutambi.

Amesema kuwa katika kutekeleza mradi huo hakutakuwa na fidia kwa sehemu ambazo nyumba zimejengwa barabarani itakapopita barabara hiyo ambayo inaanzia barabara kuu ya Dar es Salaam-Morogoro.

"Tusije tukakwamisha mradi ukikwama mradi utahamishiwa sehemu nyingine hivyo hii ni fursa kwetu tusiiache kwani kukwamisha ni kushindwa kujiletea maendekeo kwani barabara ni maendeleo na fursa zitajitokeza kwa wingi kupitia barabara,"amesema Lutambi. 

Kwa upande wake mwakilishi wa Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini TARURA Mhandisi Fredrick Nzogela amesema kuwa hatua ya usanifu itakamilika mwezi wa tisa ambapo mkandarasi atakabidhi taarifa ambayo itaonyesha baadhi ya maeneo yatakayo athirika.

Nzogela amesema kuwa barabara hiyo itakuwa na upana wa mita 8.5 na itakuwa na mitaro pande zote pamoja na kuwekwa taa na alama mbalimbali na matuta sehemu ambazo ni hatarishi hususani kwenye eneo la shule.

Kaimu Mtendaji wa Kata ya Maili Moja  Mwanawetu Said amewataka wananchi wasiwe na hofu kwani athari hazitakuwa kubwa kama wanavyofikiri na sehemu zitakazo athirika ni kidogo sana.

Said amesema kuwa sehemu zitakazo athirika wahusika wasikwamishe kufanyika kwa ujenzi huo kwani kuukwamisha ni kuyakataa maendeleo ndani ya maeneo yao.

Naye Mhandisi Kiza Mwesigwa ambaye anasimamia ujenzi wa barabara hiyo kwa ujenzi wa changarawe kabla ya kuwekwa lami amesema ujenzi wake utakuwa kuchonga na kuweka kifusi na kushindilia itakuwa na urrefu wa kilometa .

Mwesigwa amesema kuwa mradi huo utaanza mwezi huu kuanzia wiki ijayo na utakuwa wa miezi sita hadi mwezi Novemba itakuwa na urefu wa kilometa moja na mita 800.

Nao baadhi ya wananchi waliohudhuria mkutano huo wa elimu juu ya mradi huo waliitaka Halmashauri kutoa elimu ya kutosha juu ya utekelezaji mradi huo.

Wamesema wako tayari kutoa ushirikiano ili kufanikisha ujenzi wa barabara hiyo na kuwaweka wazi ili wajue maeneo ambayo yameonekana kuzidi ili waweze kuhamisha vitu vyao mapema.





Monday, June 3, 2024

WANAWAKE WA NDUMBWI WAASWA KUWAENZI WANAWAKE VINARA WAZALENDO







Ndugu Omary Abdul Punzi Afisa Mahusino wa Mradi wa Mazingira wa RAMATA (Rafiki wa Mazingira Tanzania) kutoka GBCF nchini Tanzania Tarehe 1.6.2024 awafunda wakina mama wa UWT tawi la Ndumbwi Mbezi Juu Kata ya Mbezi juu Wilaya ya Ubungo Jijini  Dar es Salaam.

Ndugu Omary Punzi aliwaelekeza kuwa Taifa hili limejengwa katika Misingi ya Kizalendo na walioitengeneza hii nchi ni wakina mama mfano Mwenyekiti wa kwanza Taifa wa Uwt  Sofia Kawawa na  Mwanasiasa Mashuhuri Bibi Titi Mohammed aliyejitoa kuchangia Mchango wake katika nchi hii.

Aliwaomba wanawake wamuunge mkono Mhe Dr Samia Suluhu Hassani Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika sekta ya kutunza Mazingira na sekta nyingine za Kiuchumi.

Kwa kuzifuata hizi Falsa za TA TE TI TO TU
TA = Tangaza nchi yako bila uoga
TE= Tetea nchi yako bila uoga tusikubali idhalilike
TI= Timiza wajibu wako kwa kila hali
TO= Toa Ushauri kwa hali na Mali
TU= Tubu pale unapokosea

Pia aliwakumbisha sifa kuu ya kiongozi ni Kulalamikiwa na kuwa na Kiherehere chenye Manufaa kwa nchi yake

Naye Wakili msomi Godfrey Kizito Chambi alitoa mada ya Umuhimu wa wanawake katika kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mtaa wa mwaka 2024 na wasisite kwenda kujiandikisha katika Daftari la kudumu la kupiga kula  zoezi hilo  la kupata kitambulisho kwa ajili ya uchaguzi litakalo anza tarehe 1.7.2024 alisisitiza kuwa wasijitokeze kupokea au kutoa rushwa katika mchakato wa Uchaguzi utarudisha nyuma na kuwapata wagombea siyo sahihi na aliendelea kuwakumbusha wanawake hao juu ya Umuhimu wa kutunza Mazingira kwa kutumia rasilimali rafiki ili mazingira yetu yawe rafiki alisema shughuli za binadamu zinaongoza kuchochea kuharibu Mazingira.

Kwa upande Rehema Muya Mwenyekiti wa UWT Kata ambaye alikuwa Mgeni Rasmi katika Mkutano huo alimwaga sifa kwa Mwenyekiti  na katibu wa tawi la ndumbwi kwa kufanya jambo kubwa la kuandaa mada hizo na kuwakusanya Wanawake wa UWT hii inaonesha kuwa sasa CCM inakwenda kupata Ushindi wa Kishindo kwa Mhe Dkt Samia Suluhu Hassani Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katika uchaguzi wa 2024 na 2025

Naye Mhe Anna lukindo Diwani wa kata ya Mbezi Juu alisema kuwa Serikali Mhe Dk  Samia Suluhu Hassani imewasaidia wananchi wa Mbezi Juu kujenga Daraja Mito Miwili lengo kutatua kero ya muda mrefu ya kupita hapo Daraja  hilo likikamilika litakuwa chachu ya Maendeleo kutokana na Kasi inayofanywa na Mhe Josephat Gwajima na Timu nzima ya Viongozi wa Kinondoni sambamba na hilo alivutiwa na Mada za mkutano huo.

Katibu wa Tawi la Ndumbwi ndugu Witnes Ngowi alisema kuwa UWT katika Tawi hilo wamejipanga na kuhakikisha kuwa watashinda kwa kishindo katika Uchaguzi wa 2024 na  2025.

Kwa upande wa Catherine Mpangala Mwenyekiti wa Tawi la Ndumbwi alisema wameanda Mkutano huo   kwa lengo la kutekeleza ilani ya Chama cha Mapinduzi na kuwakumbusha watanzania kuwa mwaka 2024 kutakuwa na Uchaguzi wa serikali ya Mitaa hivyo wasisite kujitokeza kwa wingi katika zoezi la kujiandikisha katia Daftari la Kupiga kula litakalo anza Julai Mosi.

Aliwashukuru Bank ya NMB kuja kutoa Elimu ya Mikopo kwa wakina mama na na watoa mada ya Ujasiliamali kutoka kwa Estar Muhanga ,Mada Itifaki na Uzalendo iliyotolewa na ndugu Omary Punzi  na ile mada ya Utunzaji wa Mazingira na Umuhimu wa kushiriki Uchaguzi wa serikali za mita iliyotolewa na wakili Msomi Geoffrey Kizito 

Ndugu Catherine aliwawapongeza wanachama wa UWT kufika kwa wingi Sambamba na viongozi wa Chama kutoka Wilaya na kata kuja kushiriki Mkutano huo.

Sunday, June 2, 2024

CHAURU YACHAGUA VIONGOZI WAKE








CHAMA Cha Ushirika wa Umwagiliaji Mpunga Ruvu (CHAURU) cha Halmashauri ya Chalinze Wilayani Bagamoyo Mkoani Pwani kimefanikiwa kumchagua Mchujuko Mchujuko kuwa mwenyekiti atakayeongoza kwa kipindi cha miaka mitano.

Kwenye uchaguzi huo ambao ulisimamiwa na Ofisa Ushirika Halmashauri ya Chalinze alimtangaza Mchujuko aliyepata jumla ya kura 214 sawa na asilimia 91.8 kati ya kura 1,165 halali zikiwa 1,162 na kura zilizoharibika ni tatu ambapo mshindi alipaswa kupata angalau asilimia 50 ya kura.

Akitangaza washindi wa uchaguzi huo msimamizi huyo Raphael Kajale amemtangaza makamu wa mwenyekiti ni Otnel Mbura aliyepata kura 186 sawa na asilimia 79.8.

Kajale amewataja wagombea wengine kuwa ni Sade Mwakitalu alipata kura 173 sawa na asilimia 74, Renatha Mwaipopo alipata kura 171 sawa na asilimia 73.3 na Shea Bilali aliyepata kura 154 sawa na asilimia 67 hawa wote wataunda bodi ya ushirika huo.

Amewataja wajumbe wa kamati ya maadili waliochaguliwa ni Moses Polepole, Rajab Mfyome, Theresia Shayo, James Ole Njolay na Zuhura Matimbwa.

Akiwashukuru wajumbe wa mkutano huo mkuu wa uchaguzi uliompa ushindi mwenyekiti mpya Mchujuko amesema kuwa kikubwa atakachokifanya ni kuhakikisha wanaongeza uzalishaji kutoka tani tano za sasa hadi saba mpaka 10 na kukarabati miundombinu.

Awali mwenyekiti aliyemaliza muda wake Chacha Sadala akishukuru amesema pia wamefanikiwa kununua trekta na jembe lake ukarabati wa pampu nne kukarabati mashine mbili za kukoboa mpunga na tayari hekari 800 zimepandwa kati ya hekari 1,800 na hadi itakapofika Juni 30 wakulima wote watakuwa wamepanda mashamba yao.

Sunday, May 26, 2024

TAASISI ZINAZAZOUNGA MKONO CCM ZIKITUMIKIE CHAMA SIYO KUSUBIRI UTEUZI


WANACHAMA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Pwani wametakiwa wasizitumie taasisi mbalimbali zinazomuunga Mkono Rais na chama kama sehemu ya kupata teuzi za kuwa viongozi.

Aidha zimetakiwa zisitembee mifukoni na baadhi ya watu wanaotaka kuwania nafasi za uongozi bali wawaache waliopo madarakani wamalize muda wao wa uongozi.

Hayo yamesemwa Mjini Kibaha na Katibu wa Siasa na Uenezi Mkoa wa Pwani David Mramba wakati wa mkutano na taasisi hizo.

Mramba amesema kuwa baadhi wanajiunga na taasisi hizo ili waonekane wachaguliwe kwenye nafasi mbalimbali za uongozi kwenye chama na serikali.

Kwa upande wake Katibu Mwenezi wa CCM mkoa wa Ruvuma John Haule alizitaka taasisi hizo kuitumia vizuri mitandao ya kijamii kwa kuelezea mambo mazuri yanayofanywa na awamu ya sita.

Naye Katibu Mwenezi wa CCM mkoa wa Morogoro Zangina Zangina amesema kuwa taasisi hizo zihamasishe wale wenye sifa wajiandae kugombea wakati utakapofika.

Thursday, May 23, 2024

CHONGELA AAPISHWA KUWA DIWANI

DIWANI wa Kata ya Msangani kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Gunze Chongela ameapishwa baada ya kushinda uchaguzi mdogo uliofanyika hivi karibuni kufuatia kifo cha aliyekuwa diwani wa kata hiyo Leonard Mlowe .

Chongela alikula kiapo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Hamis Ally wakati wa kikao cha baraza la madiwani wa Halmashauri ya Mji Kibaha.

Gunze ameahidi kuwatumikia wananchi wa kata hiyo kwa kusimamia miradi ya maendeleo kupitia ilani ya CCM.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Kibaha Mussa Ndomba amemtaka diwani huyo kuebdeleza mazuri yaliyoachwa na mtangulizi wake ili kuleta maendeleo kwenye kata hiyo.

Wednesday, May 22, 2024

KILONGA CUP MBIONI KUTIMUA VUMBI

MAANDALIZI ya michuano ya soka ya Kilonga Cup msimu wa tano yameanza ambapo timu zimealikwa kushiriki michuano hiyo ambayo inayotarajia kutimua vumbi huko Bagamoyo Mkoani Pwani.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Mjini Kibaha katibu wa mashindano hayo Idd Mpingo amesema kuwa michuano hiyo inatarajia kuanza mwezi Juni kwenye uwanja wa Mwanakalenge.

Mpingo amesema kuwa maandalizi yanaendelea vizuri ambapo kwa sasa ni usajili wa timu zitakazoshiriki michuano hiyo ambapo timu ya Kiduli imethibitisha kushiriki michuano hiyo.

Amesema kuwa zawadi kwa mshindi mwaka huu zitakuwa nzuri ikilinganishwa na mwaka jana ambapo mwaka jana mshindi alijinyakulia milioni 3 na mshindi wa pili alijinyakulia milioni 1.5.

Kiingilio cha ushiriki kwa timu ni shilingi 150,000 ambapo pia zawadi zitatolewa kwa mchezaji bora, mfungaji bora na kipa bora lengo likiwa ni kuongeza hamasa kwa wachezaji.

Ametoa wito kwa vilabu ndani na nje ya Mkoa wa Pwani kujitokeza kushiriki michuano hiyo na wanawakaribisha wadhamini kujitokeza kudhamini michuano hiyo.

Ameishukuru serikali na vyama vya soka na waamuzi kwa ushirikiano wanaoutoa kwao katika kufanikisha michuano ambayo imeibua vipaji vingi vinavyotamba kwenye ligi mbalimbali nchini.