Friday, May 3, 2024

KPC YAENDELEA KUTOA MSAADA NA ELIMU YA KISHERIA KWA WANANCHI WA KIBAHA

KITUO cha Msaada wa Kisheria (KPC) kimeendelea na utoaji elimu na msaada wa kisheria kwa makundi mbalimbali ili kuwajengea ufahamu wa sheria wananchi wa Halmashauri ya Mji Kibaha.

Akizingumza na waandishi wa habari baada ya kutoa mafunzo kwa wanafunzi wa Shule mbalimbali Mkurugenzi wa KPC Catherine Mlenga amesema kuwa elimu hiyo ni kwa wananchi wote.

Mlenga amesema kuwa wanatoa elimu pamoja na msaada kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo serikali.

"Tunaishukuru serikali kwa kutupatia vibali ambavyo vinatuwezesha kutoa elimu na msaada wa kisheria kwa wananchi lengo likiwa ni kuwapa uelewa wa kujua sheria mbalimbali,"amesema Mlenga.

Amesema kuwa elimu ya sheria imekuwa msaada mkubwa kwa wananchi ambapo baadhi wamepata uelewa na kuweza kutoa taarifa pale wanapoona kuna uvunjwaji wa sheria.

"Elimu tunayoitoa ni kuanzia kwa wanafunzi mashuleni, majumbani, masokoni, kwenye nyumba za ibada, kwenye mikutano na mikusanyiko mbalimbali ta kijamii,"amesema Mlenga.

Aidha amesema kuwa wanatoa msaada wa kisheria bure kwa watu wasiokuwa na uwezo hususani wanawake na watoto na kuwapigania hadi kupata haki zao.

"Sheria tunazowafundisha ni zote ikiwa ni pamoja na mirathi, ndoa, ardhi, matunzo ya watoto, haki za watoto, sheria za kazi, mazingira, na nyinginezo,"amesema Mlenga.

Amewataka wananchi wa Kibaha kukitumia kituo hicho ili waweze kusaidiwa pale wanapopata changamoto za kisheria na wasifumbie vitendo vya ukatili ndani ya jamii kwa kutoa taarifa.

Wednesday, May 1, 2024

WAHITIMU JKT KUJITOLEA WATAKIWA KUTANGULIZA UZALENDO

 




Na John Gagarini, Kibaha

VIJANA wanaohitimu mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) wakujitolea wametakiwa kutumia dhana ya uzalendo katika shuguli za ujenzi wa Taifa ili kuiletea nchi maendeleo.

Hayo yalisemwa Mlandizi na Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson John wakati wa kufunga mafunzo ya (JKT) ya kujitolea Operesheni Miaka 60 ya JKT kwenye Kikosi cha Ruvu Kibaha.

John alisema kuwa Vijana hao wameandaliwa vema kulipambania Taifa hivyo wakati wa utekelezaji wa majukumu yao lazima watangulize uzalendo.

"Zingatieni mambo manne muhimu Utii, nidhamu, uhodari na uaminifu haya ndiyo mambo ya kuzingatia hapa ndipo mtakuwa mnafanya uzalendo ambayo ndiyo nguzo kuu ya mafunzo yenu,"alisema John.

Alisema kuwa pia wawe na uhodari kwenye jambo moja ambalo ni fani ili wawe mahiri kwani kuchanganya mambo mengi kwa wakati mmoja hawataweza kuwa mahiri.

Kwa upande wake mwakilishi wa Mkuu wa Majeshi Meja Jenerali Ibrahim Mhona alisema kuwa vijana hao wanapaswa kujilinda kiafya kwani suala la afya ni muhimu sana.

Mhona ambaye pia ni Mkuu wa Mafunzo na Utendaji Kivita Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) alisema kuwa mafunzo hayo ni ya kuwapatia stadi za maisha na baadaye watapata stadi za kazi ikiwa ni hatua ya pili baada ya hatua ya kwanza.

Alisema kuwa mafunzo hayo yamekuza moyo wa uzalendo ukakamavu na kutumia vizuri muda na hawajakosea kujiunga na mafunzo hayo ya kujitolea kwani maamuzi yao ni ya busara na kuwapongeza wazazi na walezi kwa kuwapeleka vijana wao kwenye mafunzo hayo.

Naye mwakilishi wa Mkuu wa JKT Kanali Robert Kessy alisema kuwa wakati wa kutekeleza majukumu yao wahakikishe wanatatua changamoto bila kuvunja sheria na kuwa na nidhamu bila kusahau uhodari kwani Taifa limewekeza sehemu sahihi.

Kessy alisema kuwa vijana wanapaswa kujitolea kulitumikia Taifa na kumuenzi Baba wa Taifa ambaye aliasisi Jeshi hilo na wahakikishe wanaonyesha uzalendo kwa vitendo na weledi na wajiulize watalifanyia nini Taifa siyo Taifa kuwafanyia nini pia wahakikishe wanasimamia viapo vyao.

Awali Mkuu wa Kikosi cha Ruvu 832 KJ Kanali Peter Mnyani alisema kuwa mafunzo hayo ya awali ya kijeshi waliyoyapata vijana hao ni pamoja na ukakamavu ujasiri ambavyo wamefanya kwa vitendo.

Mnyani alisema kuwa mafunzo hayo yalikuwa ya muda wa miezi minne kati ya miezi 24 ya mkataba wao ambapo walijifunza utimamu wa mwili, usomaji ramani, uraia,  usalama na utambuzi na kwata za silaha ndogo ndogo.

Akisoma risala ya wahitimu wa mafunzo hayo Lulu Godfrey alisema kuwa Vijana wa Kujitolea Operesheni Miaka 60 ya JKT walianza mafunzo hayo Desemba 2023.

Godfrey alisema kuwa kwenye mafunzo hayo walifundishwa mbinu mbalimbali ikiwa ni pamoja mbinu za ulinzi, ukakamavu, utii, ulinzi wa taifa ujasiri uvumilivu, na hawatatumia vibaya mafunzo hayo kinyume na malengo ya Taifa.

Jumla vijana 800 walijiunga na mafunzo hayo ambapo waliohitimu walikuwa 776 wavulana wakiwa 438 na wasichana walikuwa 338 na vijana 24 hawakumaliza mafunzo hayo na kwa kipindi cha miezi 20 watakuwa kwenye majukumu mbalimbali ikiwa ni pamoja na malezi, uzalishaji mali na ulinzi.

 Mwisho.

Tuesday, April 30, 2024

*BMH YAHUDHURIA UFUNGUZI WA MKUTANO WA 24 BARAZA LA MAWAZIRI* *SEKTA* *YA* *AFYA* *EAC*

Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) imehudhuria ufunguzi wa Mkutano wa Kawaida wa 24 wa Baraza la Mawaziri la sekta ya Afya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) jijini Dar es Dar es Salaam. 

Mkutano huo wa siku tano, ulioanza leo tarehe 29 Aprili hadi Mei 3,  unafanyika kwa njia ya mseto (video na ana kwa ana) umeanza katika ngazi ya wataalam ukilenga kufanya tathimini ya utekelezaji wa maagizo na makubaliano yaliyofikiwa katika mkutano wa 22 wa Baraza hiloa mbapo taarifa itawasilishwa katika Mkutano wa Makatibu Wakuu.

Mkutano utafuatiwa na ngazi ya Makatibu Wakuu tarehe 2 Aprili 2024, ambapo taarifa itawasilishwa, Makatibu na kuhitimishwa na Mkutano ngazi ya Mawaziri ukaofanyika Mei 3.

Mbali na kufanya tathimini ya utekelezaji wa maagizo na makubaliano yaliyofikiwa katika mkutano wa 22 wa Baraza hilo, Mkutano huo utajadili agenda nyingine zinazotarajiwa ikiwemo Mkutano taarifa za Vikundi Kazi (Technical Working Group – TWG) sita (06) vya Sekta ya Afya na mapendekezo ya Tanzania ya kuanzisha Kituo cha Umahiri cha Upandikizaji Uloto na Sayansi ya Matibabu ya Magonjwa ya Damu chini ya Hospitali ya Benjamin Mkapa. 

Akizungumza katika ufunguzi wa Mkutano huo, Mganga Mkuu wa Serikali wa Tanzania Prof. Tumaini Nagu, ametoa rai kwa wataalamu wa sekta ya Afya ya EAC kutoa michango itayosaidia Jumuiya kuimarisha miundombinu ya huduma ya afya ili kukabiliana na matishio ya kiafya kwa magonjwa yanayoambukiza na yasiyoambukiza.

“Tumekuja kujadili na kutoa suluhisho na majawabu yatakayotusaidia kukabili changamoto za kiafya katika Jumuiya yetu kwa kuzingatia ubunifu na weledi katika mifumo yetu ya afya huku tukiwa wamoja na wenye nguvu zaidi” amesema Prof. Nagu

Pro. Nagu amehimiza umuhimu wa Sekta ya Afya katika Jumuiya kuendelea kufanya kazi kwa ufanisi na umoja katika utekelezaji progamu mbalimbali za Afya ikiwemo miradi ya Sekta ya Afya na mikakati inayopangwa ili kufikia mafanikio yanayotarajiwa kwa wakati.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Sekta ya Jamii katika Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dkt. Irene Isaka, ameeleza kuwa kupitia mkutano huo nchi wanachama watapata fursa ya kusikia taarifa zitakazowasilishwa na kila nchi ili kwa pamoja kuweza kuchangia na kushauri namna bora ya kusimamia na kutekeleza programu, miradi na miundombinu ya Afya katika Jumuiya.

Ujumbe wa Tanzania katika Mkutano huo umeongozwa na Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Tumaini Nagu na wajumbe kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambapo imewakilishwa na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii Mhandisi Abdillah Mataka. 

Wengine kutoka Tanzania walioshiriki Mkutano huo ni pamoja na Wizara za Afya (Tanzania Bara na Zanzibar), Hospitali ya Benjamin Mkapa, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Kituo cha Umahiri cha Magonjwa ya Moyo na Mishipa ya Damu cha Afrika Mashariki, Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Mamlaka ya Chakula na Dawa (TMDA), Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi (NACP), Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi (MUHAS) Bohari ya Dawa (MSD), Maabara Kuu ya Taifa, Mpango wa Kitaifa wa Kudhibiti Malaria (NAMCP) na Mamlaka ya Chakula na Dawa Zanzibar (ZFDA).

Monday, April 29, 2024

MWENGE KUPITIA MIRADI YA TRILIONI 8.6

MWENGE wa Uhuru umeanza mbio zake Mkoani Pwani ukitokea Mkoani Morogoro ambapo utapitia miradi 126 ya maendeleo yenye thamani ya shilingi trilioni 8.5.

Hayo yalisemwa na Mkuu wa Mkoa huo Abubakar Kunenge alipoupokea Mwenge huo eneo la Bwawani Halmashauri ya Chalinze Wilaya ya Bagamoyo, kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Adam Malima.

Kungenge alisema kuwa kati ya miradi hiyo 18 itawekewa mawe ya msingi 22 itazinduliwa 86 itakaguliwa.

"Miradi hiyo imefanikiwa kutokana na Rais kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji na ushirikiano kati ya viongozi, wananchi na wadau wa maendeleo katika kutafuta fedha hasa ikizingatiwa Pwani ni Mkoa wa kimkakati,"alisema Kunenge.

Kwa upande wake kiongozi wa mbio za Mwenge Godfrey Eliakim Mzava alisema kuwa wanapofika kwenye miradi ya maendeleo wakute taarifa sahihi za utekelezaji wa miradi ya maendeleo pia nyaraka zote za msingi zinazoeleza utekelezaji wa miradi iliyoyopo na wataalamu watoe maelezo ya kina na vifaa vya upimaji ubora wa miradi viwepo.

Mwisho. 




Saturday, April 27, 2024

MKUU WA MKOA WA PWANI ABUBAKAR KUNENGE ATAKA SHERIA ICHUKUE MKONDO WAKE WALIOMDHALILISHA DK KAWAMBWA

MKUU wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amelitaka jeshi la Polisi Wilayani Bagamoyo kumchukulia hatua za kisheria Hassan Usinga "Wembe" kwa tuhuma za kumdhalilisha aliyewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo na Waziri wa Miundombinu Dk Shukuru Kawambwa.

Kunenge ameyasema hayo wakati wa kikao baina ya Dk Kawambwa na Wembe na baadhi ya viongozi wa Wilaya ya Bagamoyo akiwemo Mkuu wa Wilaya Halima Okash na Mkurugenzi wa Halmashauri Shauri Selenda na baadhi ya wakuu wa idara mbalimbali. 

Alisema kuwa suala hilo limesababisha kuhatarisha usalama wa Mkoa na taharuki kwa baadhi ya watu nchini kutokana na kitendo hicho cha udhalilishaji ikiwa ni pamoja na kufungwa pingu kwa kiongozi huyo mstaafu ambapo serikali haikubaliani nacho.

"Mwekezaji wa machimbo hayo ya mchanga ana vibali vyote vya umiliki na uchimbaji lakini changamoto iliyotokeza ni uharibufu wa barabara uliofanywa na malori ya yanayopita hapo yanayobeba mchanga na kuharibu barabara kutokana na uzito mkubwa na kusababisha wananchi kuifunga,"alisema Kunenge.

Naye Dk Kawambwa alisema kuwa alifungwa pingu na mtuhumiwa huyo akishirikiana na mgambo Abdala Mgeni na kusukumwa hali ambayo ilimfanya ajisikie vibaya.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Halima Okash alisema kuwa mwekezaji aliomba kibali cha shughuli za uchimbaji mchanga na baraza la madiwani likamkubalia baada ya kufuata taratibu zote kuanzia ngazi ya chini.

Meneja wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) Wilaya ya Bagamoyo Bupe Angetile alisema kuwa walizuia kutumika barabara hiyo ilifungwa kutokana na kuharibika lakini bado iliendelea kutumika kupitisha malori ya mchanga ambapo inauwezo wa kutumika na malori yenye uzito wa tani 10.

WAWILI MATATANI KUMDHALILISHA DK KAWAMBWA

JESHI la Polisi Mkoa wa Pwani limewakamata watuhumiwa wawili Hassan Usinga au Wembe na Abdallah Mgeni kwa tuhuma za kumdhalilisha aliyewahi kuwa Waziri wa Miundombinu Dk Shukuru Kawambwa.

Aidha Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani linamtaka mtu aliyechukua na kusambaza video hiyo mitandaoni ajisalimishe kituo cha Polisi Bagamoyo
mara moja.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mjini Kibaha Kamanda wa Polisi Mkoani Pwani (SACP) Pius Lutumo alisema kuwa tukio hilo lilitokea Aprili 24 saa 8 mchana huko Kitopeni Wilaya ya Bagamoyo.

Lutumo alisema kuwa tukio hilo lilionekana kupitia mitandao ya kijamii ambapo video ilionekana ikimwonyesha Waziri na Mbunge mstaafu Dk Shukuru Jumanne Kawambwa akishambuliwa kwa maneno makali na kudhalilishwa kwa kufokewa na
kutishiwa kufungwa pingu kama mhalifu na watuhumiwa hao hali ambayo iliyosababisha taharuki kubwa kwa jamii.

"Video hiyo ilionyesha Dk Shukuru Jumanne Kawambwa na mtu mwingine aitwaye Cathbert Enock Madondola walishambuliwa ambapo watuhumiwa hao baadae walipewa dhamana kwa mujibu wa sheria na watafikishwa mahakamani mara upelelezi utakapokamilika,"alisema Lutumo.

Alisema kuwa Wembe alifanya tukio hilo akiwa na askari mgambo aitwaye Abdala Mgeni ambapo chanzo cha tukio hilo ni magari ya mchanga ya mtuhumiwa kuharibu barabara na mashamba.

"Mtuhumiwa alifikia hatua hiyo baada ya magari yaliyokuwa yakienda kuchukua mchanga kwa mbali ya kuharibu barabara wakati yakipita kwenda kubeba mchanga eneo hilo hali iliyosababisha wananchi kufunga barabara kwa magogo ili kuzuia uharibifu huo wa barabara,"alisema Lutumo.

Kamanda Lutumo alisema kuwa Dk Kawambwa ni moja ya  wakazi wa eneo hilo ambapo walijaribu kuyazuia magari hayo ili kupunguza uharibifu.

Thursday, April 25, 2024

TFS YATOA MILIONI 20 KWA WANANCHI WA RUFIJI NA KIBITI WALIOKUMBWA NA MAFURIKO

WAKALA wa Misitu Tanzania (TFS) imetoa fedha kiasi cha shilingi milioni 20 kwa ajili ya wananchi wa Wilaya za Rufiji na Kibiti Mkoani Pwàni ambazo zimekumbwa na mafuriko.

Akikabidhi mfano wa hundi Meneja Uhusiano wa (TFS) Johary Kachwamba kwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amesema kuwa fedha hizo ni kusaidia mahitaji mbalimbali.

Kachwamba amesema kuwa wana misitu zaidi ya 10 yenye ukubwa wa hekari 32,000 hivyo wameona watoe pole kwa wananchi waliokumbwa na changamoto ya mafuriko.

Amesema kuwa wataendelea kushirikiana na serikali kusaidia sehemu mbalimbali zilizokumbwa na changamoto kama hizo.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Pwani ameishukuru TFS kwa kujitolea fedha hizo kwani zitaweza kusaidia wananchi hao kuweza kukabili baadhi ya mahitaji.

Kunenge amesema kuwa mbali ya kutoa fedha hizo pia wametoa eneo kwenye Kitongoji cha Chumbi B ambapo wananchi wa Muhoro watahamishiwa hapo.

Amesema wanaishukuru TFS katika jitihada za kulinda na kutoa elimu juu ya kuhifadhi mazingira na kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala.

Aidha amesema wanashauri wananchi kuondoka kwenye eneo ambalo ni mkondo wa Bonde la Mto Rufiji na wananchi wakae maeneo ambayo si hatarishi kwa mafuriko.