Friday, May 3, 2024

KPC YAENDELEA KUTOA MSAADA NA ELIMU YA KISHERIA KWA WANANCHI WA KIBAHA

KITUO cha Msaada wa Kisheria (KPC) kimeendelea na utoaji elimu na msaada wa kisheria kwa makundi mbalimbali ili kuwajengea ufahamu wa sheria wananchi wa Halmashauri ya Mji Kibaha.

Akizingumza na waandishi wa habari baada ya kutoa mafunzo kwa wanafunzi wa Shule mbalimbali Mkurugenzi wa KPC Catherine Mlenga amesema kuwa elimu hiyo ni kwa wananchi wote.

Mlenga amesema kuwa wanatoa elimu pamoja na msaada kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo serikali.

"Tunaishukuru serikali kwa kutupatia vibali ambavyo vinatuwezesha kutoa elimu na msaada wa kisheria kwa wananchi lengo likiwa ni kuwapa uelewa wa kujua sheria mbalimbali,"amesema Mlenga.

Amesema kuwa elimu ya sheria imekuwa msaada mkubwa kwa wananchi ambapo baadhi wamepata uelewa na kuweza kutoa taarifa pale wanapoona kuna uvunjwaji wa sheria.

"Elimu tunayoitoa ni kuanzia kwa wanafunzi mashuleni, majumbani, masokoni, kwenye nyumba za ibada, kwenye mikutano na mikusanyiko mbalimbali ta kijamii,"amesema Mlenga.

Aidha amesema kuwa wanatoa msaada wa kisheria bure kwa watu wasiokuwa na uwezo hususani wanawake na watoto na kuwapigania hadi kupata haki zao.

"Sheria tunazowafundisha ni zote ikiwa ni pamoja na mirathi, ndoa, ardhi, matunzo ya watoto, haki za watoto, sheria za kazi, mazingira, na nyinginezo,"amesema Mlenga.

Amewataka wananchi wa Kibaha kukitumia kituo hicho ili waweze kusaidiwa pale wanapopata changamoto za kisheria na wasifumbie vitendo vya ukatili ndani ya jamii kwa kutoa taarifa.

No comments:

Post a Comment