MWAJUMA Makuka ni jina maarufu kwenye Mtaa wa Msangani ambalo limetokana na uongozi wake thabiti akiwa ni mwanamke wa shoka kutokana na jinsi anavyopambana kuwaletea maendeleo wananchi anaowaongoza.
Ubora wake unatokana na umahiri wake wa kutekeleza majukumu yake kikamilifu bila ya kujali jinsi yake na kufanya baadhi ya mambo ambayo watangulizi wake ambao ni wanaume walishindwa katika uongozi wao.
Makuka ni mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Msangani Mtaa ulio jirani na kambi ya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) Msangani kata ya Msangani Wilaya ya Kibaha Mkoani Pwani.
"Moja ya vitu vilivyokuwa vikiniumiza kama kiongozi ni kutokuwa na huduma ya uzalishaji mama wajawazito kwenye zahanati yetu ya Kata ya Msangani ambayo iko kwenye mtaa wa Msangani lakini changamoto hiyo iko mbioni kwisha kwani tayari vitanda viwili kwa ajili ya kuzalishia akinamama wajawazito kimepatikana",amesema Makuka.
“Kwa kuanzia nyumba ya Mganga iko tayari ambapo kwa sasa imepauliwa baada ya serikali kutoa kiasi cha shilingi milioni 22 kinachosubiriwa ni kumalizia na mganga akiwepo huduma zitatolewa kwa saa 24 kwani kwa sasa huduma hutolewa muda wa kazi lakini baada ya hapo hufungwa hivyo endapo ikitokea changamoto ya mgonjwa huwabidi kumpeleka Tumbi au kituo cha afya Mkoani,”amesema Makuka.
Alisema kwa sasa huduma zote za vipimo zinatolewa lakini huduma za uzalishaji hazifanyiki hapo kutokana na kutokuwa na vifaa vya uzalishaji lakini kwa sasa huduma hizo zitatolewa hapo hali ambayo itawakomboa wanawake wakati wa kujifungua kwani huduma zitakuwa karibu na kupunguza changamoto za uzazi.
Alisema kuwa kutokana na huduma za afya kuwa karibu wanawake amabao wengi wanajishughulisha na shughuli za kiuchumi watakuwa na muda mwingi wa kufanya shughuli zao kwani wanwake wao ndiyo wanaotumia zaidi huduma za afya ambapo wao wakiumwa au watoto wao wakiumwa wao ndiyo huwapeleka watoto hospiatali tofauti na wanaume.
Mbali ya mafanikio ya ujenzi wa zahanati ambayo aliikuta kwenye hatua za awali vitu vingine ambavyo amefanikiwa na anajivunia ni pamoja na ujenzi wa madarasa mawali ya shule ya Msingi Msanagani, ofisi ya serikali ya mtaa ambayo ni ya kisasa ambayo ina vyumba vitatu na wanatafuta fedha kuongeza ili kupata ukumbi.
"Huduma ya maji nayo yalikuwa hayajasambaa kipindi naingia madarakani lakini kwa sasa sehemu kubwa ya mtaa ina huduma ya maji safi ambapo maeneo mawili tu ya Kiembeni na Mwanyundo ndiyo hayana maji pia aliwahi kuwapatia viti mwendo vinne watu wenye ulemavu katika mtaa wake,"amesema Makuka.
Akizungumzia kuhusu masuala ya uongozi amesema kuwa Wazee wa Mtaa huo ndiyo walimwambia watampigania hivyo hakukutana na masuala ya ubaguzi kwani wazee hao walihakikisha hakuna anayeweza kutumia mila au desturi kumkwamisha katika harakati zake za kuwa kiongozi wanamheshimu sana hakuna mtu ambaye anaongelea masuala ya mapenzi.
“Nashukuru sana kwani kabla ya kuwa mwenyekiti wa mtaa nilikuwa katibu wa Kijiji na katibu wa ccm Msangani wakati huo hivyo sikukumbana na changamoto ya kubaguliwa au kunyanyaswa kijinsia kwani wazee wa kiume ndiyo waliopendekeza niwanie nafasi hiyo,’alisema Makuka.
Alisema kuwa aliingia kwenye uchaguzi wa ndani ya chama akiwa na washindani wenzake wanne wanaume na yeye mwanamke pekee lakini aliwashinda na kuwaacha mbali na yeye kuwa mgombea kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuwashinda wanaume ambapo hata hivyo hakukuwa na uchaguzi wa vyama vingine baada ya vyama vya upinzani kujitoa kwenye uchaguzi wa serikali za mtaa mwaka 2021.
Je mume wake alimsaidia vipi anasema alikuwa msaada mkubwa kwake kwani alikuwa akimsaidia na hakuwa na wivu naye na wakati akifanya shughuli za kisiasa alikuwa msaada kwake na alimuwezesha masuala mengi ili kuhakikisha shughuli zake zinakwenda vizuri bila ya kukwama na alikuwa msaada na anamkumbuka sana ambaye kwa sasa ni marehemu alikuwa ni mwelewa na hakuwa na wivu kwani alikuwa akitambua kazi za viongozi.
"Nilikuwa nashirikiana naye vizuri kwenye baadhi ya majukumu ya kifamilia ili mimi niweze kutekeleza majukumu yangu ya kisiasa ambapo nikiwa sipo nyumbani mume wangu alikuwa akinisaidia kuhudumia familia kwani tuna watoto ambao walikuwa wakitakiwa kupata huduma mbalimbali,"amesema Makuka.
Pia hutenga muda kwa ajili ya kutekeleza majukumu yake ya kifamilia na uongozi kwani huwa anatenga muda wake kwa ajili ya kuhudumia familia pale anapomaliza anahudumia wananchi wa mtaa wake na siasa haimfanyi ashindwe kuhudumia familia yake.
Anaelezea kuhusu changamoto ambayo wakati mwingine ni kikwazo kwa wanawake kwenye kuwania nafasi za uongozi ni rushwa ya ngono hakukumbana nayo kwa sababu wazee maarufu ndiyo walimshauri awanie nafasi hiyo hivyo hakukumbana na kikwzo cha kuombwa rushwa ya ngono kwa hilo anamshukuru Mungu kwani hakuna aliyeweza kumtamkia kuhusu masuala ya ngono japokuwa mambo hayo yapo na upande wa mila na desturi ambazo zilikuwa zikiwakandamiza wanawake kadri muda unavyokwenda zinapungua.
Alisema anawashukuru wananchi wakiwemo wanaume ambapo hawa mbezi kwa kusema kauli au misemo mbalimbali kwani anawaongoza anashirikiana nao vizuri kwenye masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na shughuli za kujitolea na wanawake ndiyo wanaojitokeza kwa wingi kwenye shughuli mbalimbali za kimaendeleo.
Aliongeza kuwa ushauri wake kwa viongozi wanwake na wale wanaotarajia kugombea jambo kubwa wanalotakiwa kulifanya ni kuwa na ujasiri na kutokuwa na woga japo yeye alipoambiwa agombee uenyekiti alikuwa na woga lakini alijipa moyo na kukabili changamoto za uongozi.
Moja ya wakazi wa mtaa huo Ahmed Majengo alisema mwenyekiti wao ni shupavu licha ya kuwa ni mwanamke kwani anapambana sana katika kuhakikisha analeta maendeleo kwenye mtaa wake na pia anakabili changamoto ikiwa ni pamoja na dawa za kulevya na biashara ya wanawake kujiuza ambayo inaongezeka.
Majengo alisema kuwa kitu kinachomsaidia ni mtiifu na anayependa ukweli ambapo hupenda kukemea bilaya kuogopa ambapo matukio hata ya wizi yanapungua na uhalifu kwa ujumla siyo wa kutisha kutokana na hatua anazochukua kwani akijua kuna kijana analeta shida na akijiridhisha anamkamata na kumchukulia hatua.
Naye Amina Matima alisema kuwa mwenyekiti wao anafanyakazi haijalishi kuwa ni usiku au muda gani yeye anafanyakazi bila ya woga na hata ikifika hatua ya kuchangia mfano ujenzi wowote anachangia bila ya shida yoyote.
Salum Abdala anasema kuwa anajua changamoto nyingi na anazikabili licha ya kuwa yeye ni mwanamke haimfanyi kushindwa kuongoza na anasimamia miradi mingi ya maendeleo imefanikiwa kutokana na misimamo yake kwani hakubali kuyumbishwa na mtu yoyote.
Abdala anasema kuwa hawajutuii kumchagua kwani hata kubeba tofali anabeba kufukia mashimo barabarani anafanya kazi zote kama mwanaume kwake hakuna mfumo dume kwani anapambana bila ya hofu yoyote.
Makuka alianza siasa miaka ya 90 ambapo kabla ya kushika nafasi hiyo ya uenyekiti, katibu mwenezi wa kata hiyo kwa kipindi cha miaka mitatu kuwa makamu mwenyekiti wa chama cha ushirika cha msingi cha Msangani, pia aliwahi kuwa mwenyekiti wa kamati ya shule ya Msingi Msangani na ana watoto watatu ambao wote hakuna anayefuata nyayo zake.
No comments:
Post a Comment