Thursday, August 24, 2023

WAENEZI WATAKIWA KUSEMEA MIRADI UTEKELEZAJI ILANI YA CCM

WAENEZI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya za Mkoa wa Pwani wametakiwa kuisemea miradi ya maendeleo kwenye maeneo yao ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya chama.

Hayo yalisemwa Wilayani Bagamoyo na Katibu wa Siasa Itikadi na Uenezi wa CCM Mkoa wa Pwani David Mramba alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa semina elekezi kwa waenezi wa wilaya za mkoa huo.

Mramba alisema kuwa semina hiyo ililenga waenezi hao kujua majukumu yao kwa wanachama na kwa wananchi ambapo wanapaswa kuielezea miradi ya maendeleo ambayo imetekelezwa kupitia ilani ya chama ya miaka mitano.

"Waenezi wanapaswa kusemea shughuli mbalimbali za chama pamoja na utekelezaji wa ilani kupitia miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali ambayo inaongozwa na CCM,"alisema Mramba.

Alisema kuwa kuelezea miradi inayotekelezwa kwanza ni kumsaidia Rais Dk Samia Suluhu Hassan kumsemea jitihada anazozifanya kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo.

"Mambo mengi yanafanywa na serikali ya awamu ya sita lakini baadhi hayasemwi lakini mafunzo haya yawe sehemu ya kukitangaza chama na uzuri wa sera zake ili kuwavutia watu kujiunga nacho,"alisema Mramba.

Aidha alisema kuwa waenezi hao kupitia mafunzo hayo kubadilika na kwenda kisasa na kuacha kufanya kazi kwa mazoea kwani nyakati za sasa zimebadilika lazima wajitume.

Kwa upande wake Mwenezi wa Kibaha Mjini Clemence Kagaruki alisema kuwa mafunzo jayo watayashusha ngazi ya kata na matawi ili kuboresha utendaji kazi.

Kagaruki alisema kuwa pia yamewajengea uwezo wa kujiandaa kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji utakaofanyika mwakani na uchaguzi mkuu wa 2025.

Naye Mwenezi wa Wilaya ya Kibiti Juakali Kuanya alisema kuwa atakuwa kiungo muhimu katika kutoa taarifa mbalimbali kwa wananchi na umma kwa ujumla.

Kuanya alisema kuwa atatumia mafunzo hayo kuleta mabadiliko ambayo yataleta maendeleo kwa wananchi kupitia sera za chama na mipango mbalimbali ya kiwilaya na kitaifa.

Moja ya wakufunzi wa mafunzo hayo Khadija Juma alisema somo alilofundisha ni kuhusu uzalendo ambalo ni muhimu kwa kila Mtanzania kulijua ili kuitetea nchi yake.

Juma alisema kuwa ili watu waweze kutekeleza majukumu yao lazima wawe wazalendo kama ilivyokuwa kwa waasisi wa nchi ambao walitanguliza uzalendo kwanza.

Wednesday, August 23, 2023

KPC WAJADILI MAREKEBISHO YA BAADHI YA SHERIA

KITUO cha Msaada wa Sheria Kibaha (KPC) kimefurahishwa na marekebisho ya baadhi ya sheria yaliyofanyika kati ya mwaka 2019-2023 ikiwemo ya uendeshaji wa mirathi ambapo imeongeza adhabu kwa msimamizi wa mirathi anaposhindwa kutimiza wajibu wake kutoka shilingi 2,000 hadi milioni 2.

Hayo yalisemwa na Mkurugenzi wa kituo hicho Catherine Mlenga mara baada ya kufanya kikao kupitia marekebisho hayo yaliyofanyika kupitia bunge kwa mujibu wa sheria.

Mlenga alisema kuwa kwa mujibu wa sheria kifungu cha 107 (3) cha sheria ya usimamizi wa mirathi sura 352 ni kuwa msimamizi wa mirathi endapo atashindwa kupeleka taarifa za ukusanywaji na ugawaji wa mali ndani ya muda uliopangwa anaweza kuondolewa na kushtakiwa.

"Kabla ya mabadiliko adhabu ilikuwa ni kulipa shilingi 2,000 au kifungo cha miezi sita ambapo sheria hiyo imefanyiwa marekebisho ambapo faini isiyopungua milioni mbili au kifungo kisichopungua miaka miwili,"alisema Mlenga.

Tuesday, August 22, 2023

MAKAM WA RAIS DK MPANGO ATAKA WAKUU WA MIKOA KUSHIRIKIANA NA SEKTA BINAFSI





MAKAMU wa Rais wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Philip Mpango ameitaka mikoa nchini kushirikiana na sekta binafsi ikiwemo mabaraza ya biashara ya mikoa na kutowatumia wakati wa kuomba michango ya shughuli za maendeleo.

Dk Mpango aliyasema hayo jana Mjini Kibaha kwenye Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere wakati akifungua mafunzo ya uongozi kwa wakuu wa mikoa na makatibu Tawala wa mikoa Tanzania Bara.

Alisema kuwa baadhi ya sekta hiyo imeikitumika na kuwa nao karibu wanapokuwa wanahitaji michango kutoka kwao ikiwemo ya mbio za mwenge, ugeni na maadhimisho mbalimbali.

"Mnapaswa kuwa karibu na sekta binafsi na mabaraza ya biashara ya mikoa yenu kwani ni wadau muhimu wa maendeleo na wakifanya vizuri watatoa ajira kwa watu wengi hivyo lazima muwashirikishe na kuwa karibu nao kwenye mipango mbalimbali ya maendeleo,"alisema Dk Mpango.

Alisema kuwa baadhi ya wakuu wa mikoa wamekuwa na mahusiano mabaya na waliochini yao na wengine hujihusisha unyanyasaji wa kijinsia, kuwa wababe na upendeleo kwenye upandishwaji vyeo.

Kwa upande wake Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Angellah Kairuki alisema kuwa mafunzo hayo ni maelekezo ya Rais kutaka viongozi wapewe mafunzo mbalimbali ya kuwajengea uwezo ili kuboresha utendaji kazi wao.

Kairuki alisema kuwa mafunzo hayo ni kama waliofanyiwa wakuu wa Wilaya 139 huko Dodoma Machi mwaka huu, mafunzo kwa maofisa tarafa na watendaji wa kata 356 kwenye mikoa ya Songwe, Njombe, Katavi na Rukwa na yatafanywa ya wakurugenzi Septemba mwaka huu.

Naye Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Ridhiwani Kikwete aliyemwakilisha waziri George Simbachawene alisema kuwa kundi hilo ni muhimu sana kwani asilimia 70 ya viongozi hao ndiyo wanaosimamia masuala mazima ya maendeleo.

Kikwete alisema kuwa viongozi hao wanaliwakilusha Taifa kwenye sera zote za serikali kupitia mamlaka za mikoa na serikali za mitaa hivyo watahakikisha kunakuwa na tija kwenye ofisi za umma kuwa na utawala bora na maadili kwa utumishi wa umma.


Sunday, August 20, 2023

NYERERE SUPER CUP KUANZA KUTIMUA VUMBI TAREHE 23.9.2023

 


Katika kundeleza FIKRA za mwasisi wetu wa Taifa Mwalimu  Nyerere Taasisi ya kumbukumbu ya Mwalimu Julius kambarage Nyerere Mkoa wa Pwani ikiongozwa na Katibu wa Taasisi hiyo Ndugu Omary Punzi Tarehe 20.8.2023 imefanya Hitimisho la kikao Cha maandalizi ya Mashindano ya NYERERE SUPER CUP yatakaotimua vumbi Tarehe 23.9.2023 na kutamatika 12.10.2023.Mashindano hayo yatashirikisha Wilaya Mbili wilaya ya KIBITI na RUFIJI Kwa Timu 12 Timu sita kutoka kundi A (KIBITI)Timu shiriki Bungu,Jaribu,Mtawanya, Kibiti,Mchukwi,Dimani,na  upande wa kundi B Rufiji timu zinazoshiriki Ngorongo,Utete,.Mgomba, Muhoro,Umwe na Mkongo vikao hivyo vyote viwili Cha Tarehe 19.8.2023 na 20.8.2023 vilikuwa na agenda ya Kuandaa kanuni na ratiba ya kuanza Usajili wa wachezaji,wajumbe wote walikubaliana Dirisha la Usajili lifunguliwe tarehe 23.8.2023 na kuisha 13.8.2023  inatoa shukrani Kwa NSSF na Chuo Cha Afya St David college Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na wilaya ya Kibiti na Rufiji,Ofisi ya Mbunge Kibiti na Rufiji,Chama Cha Mpira KIBITI na RUFIJI

TAASISI YA KUMBUKUMBU YA MWALIMU NYERERE YATOA SHUKRANI KWA WADAU MAANDALIZI NYERERE SUPER CUP

Taasisi ya kumbukumbu ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Mkoa wa Pwani inatoa shukrani Kwa Viongozi wote mliofanikisha safari yetu ya maandalizi ya NYERERE SUPER CUP Taasisi inashukuru 1.Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani 2.ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Kibiti na Rufiji 3.Ofisi ya Mbunge Kibiti na Rufiji 4.Chama Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani COREFA 5.Chama cha Mpira wilaya Kibiti na Rufiji 6.Mdhamini Nssf na St David college Chuo Cha Afya kimara temboni,Madiwani wa Kibiti na Rufiji kuruhusu Viongozi wao kuhudhuria kikao na washiriki waliohudhuria UZALENDO NI KULIPENDA TAIFA LAKO MITANO TENA

*LYIDENGE ATAKA WAFANYAKAZI WA MIRADI KUWA NA NIDHAMU*

MKUU wa Polisi Wilaya ya Chalinze, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Sophia Lyidenge amewataka wafanyakazi wa mradi wa umeme wa serikali kuwa na nidhamu na kutokujihusisha na vitendo vya kihalifu.

Amebainisha hayo leo Agosti  20 alipotembela mradi huo wakati  akizungumza na wafanyakazi hao kuona kama wana changamoto zozote za kiusalama.

SSP Lyidenge aliwaeleza wafanyakazi hao kuwa wameaminiwa na serikali kufanya kazi hivyo wanatakiwa kuwa waadilifu na wasijihusishe na vitendo vya kihalifu ikiwemo wizi wa vitendea kazi na kuwataka wawe walinzi wa kwanza wa vifaa hivyo.

Sambamba na hayo SSP Lyidenge aliwasihi viongozi wa mradi huo kuwa na mahusiano mazuri na wafanyakazi ikiwemo lugha nzuri yenye staha ili kuongeza hamasa ya utendaji na kufikia malengo ya mradi kwa wakati uliokusudiwa.

"Niwaombe viongozi kuwatia moyo na kuwa na lugha shawishi kwa mnao wasimamia ili mradi huu uweze kukamilika kwa wakati, lugha zisizo na staha huwavunja moyo watendaji na kujikuta ikiwapunguzia morali ya kujituma". 

Sote tunatambua umuhimu wa mradi huu utakavyochochea maendeleo ya kiuchumi kwa kwa wakazi wa Chalinze, Mkoa wa Pwani na taifa kwa ujumla” alisema Lyidenge

CCM WAASWA KUFUATA UTARATIBU

 

WANACHAMA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Pwani wanaotoa misaada na kufanya shughuli za maendeleo wametakiwa kufuata utaratibu ili kuepusha mkanganyiko na viongozi waliochaguliwa na wananchi.

Hayo yalisemwa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) Taifa Hamoud Jumaa wakati wa mkutano wa tathmini baada ya ziara ya CCM Kibaha Mjini.

Jumaa alisema kuwa kukisaidia chama siyo tatizo lakini kinachotakiwa ni utaratibu kufuatwa ili kusitokee tofauti baina ya wale wanaosaidia na wale waliochaguliwa.

"Tunajua kwa sasa ni kipindi cha kuelekea uchaguzi mwakani ni wenyeviti wa Vijiji, Vitongoji na Mitaa na 2025 ni uchaguzi mkuu hivyo wanaotoa misaada ndani ya chama wafuate taratibu lakini siyo kosa kukisaidia chama,"alisema Jumaa.

Alisema chama kinasaidiwa na wanachama na wadau mbalimbali wana haki ya kufanya hivyo ili mradi wazingatie utaratibu uliowekwa na chama wa namna ya kuchangia.

"Chama kinajengwa na wanachama na wanaokichangia siyo tatizo hata mimi kwenye eneo langu nachangia lakini kwa kufuata utaratibu hivyo na wengine wafuate utaratibu wa chama,"alisema Jumaa.

Kwa upande wake mwentekiti wa CCM Kibaha Mjini Mwajuma Nyamka alisema kuwa utekelezaji wa ilani umefanyika kwa asilimia zaidi ya asilimia 90 ndani ya kipindi cha miaka miwili tu.

Nyamka alisema kuwa wanamshukuru Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia Kibaha fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya maendeleo ambapo miradi mingi inaendelea na mingine imekamilika.

Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka alisema kuwa kwa kushirikiana na serikali na wananchi wameendelea kukabili changamoto kwenye jimbo hilo.

Koka alisema utekelezaji wa ilani unaendelea vizuri na hakuna kilichokwama kila kitu kinakwenda vizuri lengo likiwa ni kuwaondolea changamoto wananchi na kutimiza malengo ya Rais.

Naye mwenekiti wa Halmashauri ya Mji Kibaha Focus Bundala alisema kuwa wanaishukuru serikali kutoa kwa kuipatia Halmashauri kiasi cha shilingi bilioni 8.

Bundala alisema kuwa baadhi ya fedha zimetumika kwenye ujenzi wa shule sita za sekondari na shule tisa za msingi na miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwa ni pamoja na barabara, maji na afya.