Thursday, August 17, 2023

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA ARDHI, MALIASILI NA UTALII YARIDHISHWA NA UTENDAJI WA TFS


Kamati ya Kudumu ya  Ardhi, Maliasili na Utalii imeridhishwa na utendaji kazi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa kuendelea kusimamia vyema rasilimali za misitu.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Mhe. Timotheo Mnzava (Mb) ameyasema hayo leo katika kikao cha Kamati hiyo kilichofanyika ukumbi wa Utawala Annex Bungeni jijini Dodoma.

Mhe. Mnzava amewapongeza wahifadhi kwa kujitolea kufanya kazi kwa bidii.

"Tuwatie moyo hawa wapiganaji wetu kwani wameendelea kutekeleza majukumu yao vyema na kuhakikisha kila kitu kinaenda sawa, waendelee kuitumikia nchi kwa kuwa wanajitolea na sisi kama Bunge tunawaunga mkono" Mhe. Mnzava amesisitiza. 

Aidha, ameitaka Wizara ya Maliasili na Utalii kufanyia kazi mapendekezo ya wajumbe wa Kamati hiyo na kuangalia namna bora ya kuzuia ukataji wa miti kwa kuwa yapo maeneo ambayo wananchi wanaishi kwa kutegemea miti hiyo .

Naye, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) ameishukuru kamati hiyo kwa mapendekezo na kuahidi Serikali itafanyia kazi.

Pia, amefafanua kuwa Serikali inaendelea kuhamasisha wananchi kuacha kukata miti hovyo pamoja na kuacha matumizi ya nishati chafu na badala yake kutumia nishati safi.

Kikao hicho kimehudhuriwa na baadhi ya Watendaji kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii na Wakala ya Huduma za Misitu Tanzania (TFS).

Wednesday, August 16, 2023

WAGONJWA ZAIDI YA 500 WA MTOTO WA JICHO MBARALI KUFANYIWA UPASUAJI BILA MALIPO

 

Na. Majid Abdulkarim, Mbarali 

Wagonjwa zaidi ya 500 wenye matatizo ya mtoto wa jicho wanatarajiwa kupatiwa huduma ya upasuaji wa mtoto wa jicho  kutoka kwa madaktari bingwa wa macho ambao wameweka kambi ya wiki moja katika Wilaya ya  Mbarali Mkoani Mbeya.

Hayo yamebainishwa leo na Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Mhe. Kanali Dennis Mwila wakati wa uzinduzi rasmi wa kambi ya matibabu ya upasuaji wa mtoto wa jicho itakayodumu kwa muda wa siku saba Wilayani hapo.

Kambi hiyo ilianza Agosti 14 mwaka huu na inatarajiwa kumalizika Agosti 20 mwaka huu, ambapo wakazi wa Wilaya hiyo wanaendelea kupata nafasi ya kufanyiwa uchunguzi na kupatiwa matibabu ya upasuaji wa mtoto wa jicho.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kambi hiyo, Kanali Mwila amesema kulingana na taarifa ya Shirika la Afya Duniani (WHO) asilimia Moja ya watu wanapata matatizo ya macho.

Aidha, Kanali Mwila amelipongeza Shirika la Kimataifa la Helen Killer kwa kuanza kampeni ya kutokomeza magonjwa ya macho Juni 2022 ambapo wametoa vifaa vyenye thamani ya Sh: Mil. 140 kwa Mkoa wa Mbeya na walitoa mafunzo kwa watumishi wa Afya ngazi ya jamii wapatao 570.

“Juni, 2022 Shirika la Helen Killer liliweza kugundua wagonjwa 1,750 ambao walikuwa na tatizo la mtoto wa jicho  kwa awamu tatu tofauti”, ameeleza Kanali Mwila.

Amesema, katika kambi hiyo inayoendelea jumla ya watu 500 wanatarajiwa kupatiwa huduma ambapo zaidi ya kiasi cha Sh:  Mil. 110 kitatumika katika kuwapatia huduma ya upasuaji wa mtoto wa jicho.

Amesema, kwa mwaka jana (2022) wagonjwa 29,000 waliyo onwa katika Mkoa Mbeya, wagonjwa 3,406 walikuwa na tatizo la mtoto wa jicho na magonjwa mengine.

Vile vile, Kanali Mwila ameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan  kwa kuwa imara katika kuwasogezea huduma za Afya karibu.

Naye, Meneja Mpango wa Taifa wa Macho kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Bernadetha Shilio amesema kuwa mbinu inayotumika kuwapata wagonjwa  ni kupitia wahudumu ngazi ya jamii ambao wanaambatana na wataalamu wa Afya nyumba kwa nyumba na kuwabaini wagonjwa.

Dkt. Shilio amesisitiza kuwa Huduma za upasuaji katika kambi hiyo ya siku saba katika Hospitali ya Wilaya ya Mbarali zinatolewa bila malipo chini ya ufadhili wa Shilika la Kimataifa la Helen Killer.  

Kwa upande wake Mwakilishi wa Mratibu wa Macho kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Ernest Paul amesema Serikali itahakikisha inawezesha upatikanaji wa huduma za macho karibu na wananchi hususani ngazi ya msingi.

BODI YA MKONGE NCHINI IMESAMBAZA MICHE MILIONI 6.9 BURE KWA WAKULIMA WADOGO


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Samia Suluhu Hassan amedhamiria kufanya mageuzi katika kilimo cha Mkonge Kwa kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kusambaza miche 6,991,200 ya mbegu za mkonge bure kwa wakulima wadogo katika Wilaya 16 nchini.

Mageuzi hayo yamefanya Tanzania kuwa Nchi ya pili Duniani kwa kuzalisha mkonge ikitanguliwa na Brazili.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mkonge Tanzania Saddy Kambona wakati akizugumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa majukumu wa bodi hiyo na mwelekeo katika mwaka huu wa fedha 2023/24.

Kambona ametaja Wilaya zilizopatiwa mbegu hizo ni Korogwe, Muheza, Tanga, Mkinga, Handeni, Kilindi, Rorya, Bunda, Butiama, bariadi, Bagamoyo, Kisarawe, Mkuranga, Manyoni, Singida Vijijini na Mkalama.

Amesema Rais Dk.Samia ametoa fedha kwa ajili ya kununua mitambo mipya ya kuchakata Mkonge na kufufua mitambo ya kuchakata mkonge ya mashamba ya Kibaranga Wilayani Muheza, Tanga na shamba la serikali la TPL lililopo Kata ya Bwawani Wilayani Arumeru, Arusha ambalo linasimamiwa na kuendeshwa na TSB.

Aidha,Kambona amesema Serikali iliongeza lengo na kuiagiza Bodi ya Mkonge Tanzania kuhakikisha kuwa uzalishaji unaongezeka hadi kufikia tani 120,000 kwa Mwaka, ifikapo Mwaka 2025/2026.

WATAKIWA KUTUNZA MISITU KWA VIZAZI VIJAVYO

 

Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania ( TFS ) imesema kuwa uhifadhi wa rasilimali za Misitu ni manufaa ya kizazi cha Sasa na vizazi vya baadae hivyo jamii inapaswa kujiepusha kuchoma moto Misitu pamoja na uvunaji haramu.

Hayo yamesemwa Leo Agosti 16,2023 na  Kamishna wa uhifadhi wakala wa huduma za Misitu Tanzania Prof. Dos Silayo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa majukumu ya hifadhi hiyo ndani ya Miaka ya miwili ya serikali ya awamu ya sita .

Amesema kuwa sekta ya Misitu na nyiki nchini ni muhimu kutokana na mchango wake Katika ukuaji wa sekta ya Utalii, Maji , kilimo, mifugo, nishati pamoja na viwanda hivyo kutokana  na umuhimu huo Wadau wote wanapaswa kulinda rasilimali za Misitu.

Aidha amesema kuwa wakala umeendelea kutatua migogoro kati ya hifadhi za Misitu na jamii inayoizunguka ambapo jumla ya hekta 296,881 za maeneo  zimetolewa kwa wananchi kwa ajili ya makazi , kilimo na ufugaji.

Pia wakala unaendea kutoa Elimu ya uhifadhi na usimamizi wa Misitu kwa jamii sambamba na kuimarisha mipaka kwa kuisafisha , kuweka vigingi na mabango Ili kuzuia uvamizi Katika maeneo ya hifadhi.

*MADEREVA WAVUNJA SHERIA KUDHIBITIWA CHALINZE*


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Kamishina Msaidizi wa Polisi, Pius Lutumo amewataka askari wa Polisi Chalinze kutokuwa na muhali kwa madereva wanaokiuka Sheria za usalama barabarani.

Kauli hiyo imetolewa Leo Agosti 16 akiwa katika siku ya pili ya ziara ya ukaguzi katika Wilaya zilizopo Mkoa wa Pwani ambapo alizungumza na maafisa, wakaguzi na askari wa vyeo mbalimbali akiwataka  kutokuacha jukumu la ukamataji wa madereva wanaovunja Sheria kwa askari wa kikosi cha usalama barabarani pekee,badala yake nao wachukue hatua ili kuweza kutokomeza ajali za mara kwa mara zinazotokana na makosa ya kibinadamu kama vile kuyapita magari mengine bila tahadhari, mwendo kasi, matumizi ya vileo na kutokuheshimu vivuko vya watembea kwa miguu.

Hivi karibu watu wa nne wa familia moja walipoteza maisha katika ajali ya barabarani eneo la Mapatano, Kata ya Mbwembwe tukio ambalo lilivuta hisia kwa watu wengi kutokana na ajali hiyo ya barabarani.

Kamanda Lutumo amesema " Askari wote wana jukumu la kutoa taarifa kwa wenzao waliopo barabarani pindi wanapoona dereva anaendesha gari kwa kuvunja Sheria za usalama barabarani ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa".

Aidha, amewakumbusha umuhimu wa utoaji huduma bora pindi wanapowakamata madereva wanaovunja Sheria kwa kuwaeleza makosa yao kabla ya kutoa adhabu ili wajue makosa yaliyopelekea kupewa adhabu husika.

*POLISI BAGAMOYO WATAKIWA KUBADILIKA KIUTENDAJI*



Askari Polisi Wilaya ya Bagamoyo wametakiwa Kubadilika kifikra na kufanya kazi kwa weledi na kuachana na utendaji kazi wa mazoea.

Hayo yamesemwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Kamishina Msaidizi wa Polisi, Pius Lutumo  wakati wa ziara yake ya Ukaguzi wa kuangalia utendaji wa kazi Wilayani hapo  wakati akizungumza na Maafisa, wakaguzi na askari wa vyeo mbalimbali ambapo amewataka kuzingatia ufanyaji kazi kwa mujibu wa Sheria za nchi na kuacha kufanya kazi kwa mazoea na kupeleka utendaji usioridhisha.

Pia, Kamanda Lutumo amesisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa nidhamu na kuzingatia maadili ya Jeshi la Polisi kwa kujiepusha na vitendo vya mmomonyoko wa maadili vitakavyolichafua Jeshi ambavyo huweza kusababisha kufukuzwa kazi.

Kadhalika, amewataka askari kufanya kazi kwa kusimamia misingi ya utendaji bora kwa kutenda haki kwa tunao wahudumia vituoni " Wananchi hawapendi kuja kwenye vituo vyetu ila wanafika kwa kuwa wanashida zinazohitaji kusaidiwa nasi hivyo ni jukumu letu kuwapa huduma bora wanapofika kwenye vituo vyetu vya Polisi”, Alisema.

Aidha, amewakumbusha askari umuhimu wa kutunza vizuri vielelezo na kutokuwa na tamaa au kushawishika katika kuiba vielelezo hivyo viwapo kituoni. "Ni jukumu letu kulinda vielelezo vilivyopo kituoni na kuhakikisha vinatunzwa vizuri na siyo kuwa sehemu ya upotevu wa vielelezo hivyo ambavyo vitatumika kama ushahidi Mahakamani.

Polisi (M) Pwan

TAKUKURU PWANI YABAINI MIRADI KAMATI HEWA MIRADI YA HALMASHAURI

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Pwani imebaini uwepo wa kamati hewa kwenye baadhi ya miradi ya maendeleo inayosimamiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga

Hayo yalisemwa Mjini Kibaha na Mkuu wa Takukuru Mkoa huo Christopher Myava alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.

Myava alisema kuwa kutokana na kamati hewa kunasababisha mianya ya rushwa katika malipo yanayofanyika.

"Pia tumebaini kuwa jamii kutokuwa na umiliki wa miradi hiyo kutokana na kutoshirikishwa katika utekelezaji wake mfano ujenzi wa kituo cha afya Kisiju ambapo jamii haikushirikishwa kabisa,"alisema Myava.

Alisema kuwa mradi mwingine ambao ulibainika kuwa na changamoto ni mzabuni aliyechaguliwa kupeleka vifaa vya ujenzi shule ya sekondari ya kata ya Shungubweni hakuomba kazi hiyo kwenye mfumo wa serikali wa TANEPS.

"Mzabuni huyo alipewa zabuni kinyume cha utaratibu na tukafanya kikao na Halmashauri kwa lengo la kuhakikisha waombaji wa zabuni wanashindanishwa ili kuondoa dhana ya utoaji zabuni kwa upendeleo,"alisema Myava.

Alibainisha mradi mwingine ni kwenye soko la Mnarani Halmashauri ya Mji Kibaha wakusanyaji wa ushuru kutotoa risiti za mashine EFD baada ya wafanyabiashara kufanya malipo kwa kisingizio cha ubovu wa mashine.

"Sababu nyingine wanasema kuwa eti mashine haina chaji hali ambayo imesababisha wakusanyaji kutumia fedha hizo kwa matumizi yao binafsi,"alisema Myava.

Aliongeza kuwa kutokana na hali hiyo kunakosekana kumbukumbu za wafanyabiashara waliofanya malipo hivyo kusababisha upotevu wa mapato.

"Maegesho ya magari nako kuna upotevu wa mapato unaosababishwa na utendaji mdogo wa kukusanya mapato ambapo baadhi ya wakusanyaji hutoza viwango tofauti vya ushuru kwa malori yanayoegeshwa sokoni tofauti na vilivyowekwa kwenye sheria ndogo,"alisema Myava.

Mkuu huyo wa Takukuru Mkoa wa Pwani alisema kuwa baada ya kubaini hayo walifanya kikao na wadau wa soko na kuweka maazimio ikiwa ni pamoja na kudai risiti, kutoa taarifa za ubovu wa mashine na kuweka vibao vinavyoonyesha tozo.