Saturday, June 10, 2023

PWANI BINGWA WA VIWANDA NCHINI

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh.Dkt Samia Suluhu Hassan ameutaja Mkoa wa Pwani kuwa bingwa viwanda nchini.

Rais Dkt. Samia ametoa kauli hiyo Juni 9, 2023 wakati akiwatambulisha Wakuu wa Mikoa waliohudhuria kwenye mkutano wa 14 wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) Ikulu jijini Dar es Saalam.

Katika Mkutano huo Rais amewataka wakuu wa mikoa nchini kuweka mazingira rafiki kwa ajili ya kuvutia wawekezaji na kwamba ataandaa tuzo kwa ajili ya mkoa kinara wa ukusanyaji mapato.

Mkoa wa Pwani una jumla ya viwanda 1522 kati ya hivyo  vikubwa ni 117 na 120 vya kati.

SERIKALI YAWAGAWIA ARDHI WANANCHI


SERIKALI imewagawia wananchi sehemu ya eneo  waliolivamia kwenye Hifadhi ya Chemchem ya Maji ya Moto Wilayani Rufiji na kumaliza mgogoro baina ya wananchi na hifadhi hiyo.

Hayo yalisemwa na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge wakati akitoa tamko la kuhitimisha Mgogoro huo ikiwa ni Utekelezaji wa maazimio la Baraza la Mawaziri nane wa kisekta walioshughulikoa mgogoro huo ambapo Mkuu wa Wilaya ya Rufiji Meja Edward Gowele alisoma taarifa hiyo ya Mkuu wa Mkoa.

Kunenge alisema kufuatia wananchi hao kumegewa sehemu ya ardhi kutoka kwenye hifadhi hiyo aliwataka wananchi wanaozunguka maeneo hayo kutovamia tena eneo hilo.

"Naagiza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na Kamishna Msaidizi wa Ardhi kupima upya eneo hilo la Hifadhi na kuandaa GN mpya,"alisema Kunenge.

Aidha aliwataka TFS kuchonga Barabara kuzunguka eneo hilo ili Kuweka kinga ya mipaka kati ya wananchi na Hifadhi hiyo.

Katika hatua nyingine Mkoa umetoa taarifa ya kuhitimisha mgogoro wa ardhi kwenye eneo la Delta ya Mto Rufiji Wilayani Kibiti na kuwataka wananchi kutofanya shughuli za kibinadamu katika hifadhi ya Misitu ya Mikoko na mazalia ya samaki.

Akisoma taarifa ya Mkuu wa mkoa ambapo mkuu wa Wilaya ya Kibiti Kanali Samwel Kolombo aliisoma amepiga marufuku ukataji wa Misitu ya Mikoko kwenye hifadhi hiyo ya Delta ya Mto Rufiji.

Alimtaka Mkurugenzi wa Halmshauri ya Kibiti kutoa elimu ya uhifadhi kwa wananchi na kuwawezesha vifaa vya kuvulia samaki kwenye maji marefu.

Alisisitiza pia  kuanzisha kwa vikundi vya uhifadhi (BMU) ili kuimariasha ulinzi wa hifadhi hiyo ambayo ina mikoko mingi.

Friday, June 9, 2023

WADHAMINI WA MICHEZO WATAKIWA KUBORESHA ZAWADI ZA WASHINDI




WADHAMINI wa Michezo Mkoani Pwani wametakiwa kutoa zawadi ambazo zitakuwa kumbukumbu kwa washindi wa michezo mbalimbali ili kuleta hamasa kwa vijana kushiriki kwenye michezo.

Hayo yalisemwa Mjini Kibaha na  mdhamini wa mashindano ya Umoja wa Michezo Sanaa kwa Shule za Sekondari Tanzania (UMISSETA) Mkoa wa Pwani Musa Mansour na kwa kuwa michezo ni ajira wadhamini waangalie kwa kuboresha upande wa zawadi ili ziwe kivutio.

Mansour alisema kuwa ili vijana wafikie malengo ya kuwa wachezaji bora na kufanikiwa lazima wawe na nidhamu ambapo kwa sasa michezo inawaletea maisha mazuri wachezaji na mamlaka husika ziboreshe viwanja na kuwapatia vifaa vya michezo na kuboresha maeneo ya wazi.

Naye ofisa michezo wa mkoa huo Grace Bureta alisema kuwa jumla ya wachezaji 120 wamechaguliwa kuunda timu ya  Mkoa ambayo itashiriki mashindano ya Taifa yatakayofanyika  mkoani Tabora ambapo timu hiyo imeiingia kambini kwenye shule ya sekondari Kibaha.





HALMASHAURI ZATAKIWA KUTENGA BAJETI ZA MICHEZO


HALMASHAURI za Mkoa wa Pwani zimetakiwa kutenga bajeti kwa ajili ya shughuli za michezo ili kuinua vipaji vya vijana kwenye michezo.

Hayo yalisemwa Mjini Kibaha na Katibu Tawala wa Mkoa huo Rashid Mchata wakati akifunga mashindano Umoja wa Michezo na Sanaa kwa Shule za Sekondari Tanzania (UMISSETA) Mkoa wa Pwani.

Mchata alisema kuwa mbali ya bajeti pia Halmashauri zihakikishe kila shule inatenga eneo kwa ajili ya michezo ili wanafunzi wapate sehemu ya kucheza.

Naye ofisa michezo wa mkoa huo Grace Bureta alisema kuwa jumla ya wachezaji 120 wamechaguliwa kuunda timu ya  Mkoa ambayo itashiriki mashindano ya Taifa yatakayofanyika  mkoani Tabora ambapo timu hiyo imeiingia kambini kwenye shule ya sekondari Kibaha.

Naye mdau wa michezo Musa Mansour alisema kuwa kwa kuwa michezo ni ajira wadhamini waangalie kwa kuboresha upande wa zawadi ili ziwe kivutio kwa vijana kushiriki michezo.

Thursday, June 8, 2023

WAKAZI CHANGWAHELA WARIDHIA KUHAMA


WAKAZI wa Kitongoji Changwahela wilayani Bagamoyo wameridhia kutekeleza agizo la Serikali la kuondoka katika eneo walilolivamia na kufanya shughuli za kibinadamu na kufanya uharibifu wa mazingira.

Akizungumza na wananchi kwenye Kitongoji hicho na kutoa maagizo hayo ya serikali akiwa katika kushughulikia changamoto zinazotokana na migogoro ya ardhi Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amesema kuwa kuna uharibifu mkubwa umefanywa na wananchi hao ikiwemo ukataji wa  mikoko ambayo inatunza kingo za bahari na kuhifadhi mazingira ya fukwe na mazalia ya samaki.

Kunenge amesema kuwa maagizo hayo ni utekelezaji wa maamuzi yaliyofanywa na baraza la Mawaziri kufuatia ushauri wa timu ya mawaziri nane wa kisekta iliyoundwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan mwaka 2019/2020 ambao walishirikiana na wataalamu kushughulikia migogoro ya ardhi mkoani humo na maeneo mengi nchini.

Akiwa Wilayani Bagamoyo alifika katika Kitongoji cha Sanzale Kata ya Magomeni na aliwaelekeza wakazi waliyovamia eneo la Yusuph Kikwete kupisha ili mwenyewe aweze kuendelea na shughuli za uwekezaji au wakae nae na kukubaliana watakavyoona inafaa.

Wakati huo huo ametoa muda wa siku 90 kwa Halmashauri ya Chalinze Wilaya ya Bagamoyo kukamilisha  zoezi la urasimishaji makazi kwa ajili ya mpango wa matumizi bora ya ardhi kwa wananchi wa waliopewa eneo la hekari 5,520 za Ranchi ya Taifa ya Ruvu.

Wednesday, June 7, 2023

WANANCHI WA SANZALE WALIOSHINDWA MAHAKAMANI WAZUNGUMZE NA MMILIKI


KUFUATIA hukumu iliyotolewa na Baraza la Ardhi na Nyumba Kibaha kuwa wavamizi 86 kwenye eneo linalomilikiwa na Yusuph Kikwete waondoke Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amewataka wananchi hao kuongea na mmiliki huyo ili waangalie namna ya kuwasaidia.

Kunenge ameyasema hayo kwenye Kitongoji cha Sanzale kata ya Magomeni wilaya ya Bagamoyo kufuatia wananchi hao kumwomba ashughulikie suala hilo kwenye ziara ya kutatua kero za wananchi kwenye mkoa huo ambapo amesema suala hilo ni amri ya mahakama na ni la kisheria na limeamuliwa kwa kufuata sheria.

Amesema suala la kisheria haliwezi kuingiliwa kwani walalamikaji walipaswa kufuata taratibu za kisheria kama waliona kuwa maamuzi yaliyotolewa hawakuridhika nayo ikiwa ni pamoja na kukata rufaa ndani ya siku 45 baada ya hukumu ambapo hawakufanya hivyo njia pekee ni kukaa na mmiliki huyo ili aangalie namna ya kuwasaidia.

Aidha amesema kutokana na maamuzi hayo ya kumpa ushindi mmiliki huyo tayari dalali ameshapatikana ili kuondoa watu hao kwenye kitalu namba D kwenye viwanja namba 14 hadi 25 ambapo kumejengwa nyumba 47, nyumba ambazo hazijakamilika 13, maboma 14 na vibanda 12.




CHANGWAHELA WATAKIWA KUPISHA ENEO KWA AJILI YA HIFADHI YA MIKOKO

HALMASHAURI ya Bagamoyo imetakiwa kukaa na mwekezaji wa Sea Salt ili kutoa hekari 50 kwa wananchi wa Kitongoji cha Changwahela kata ya Mapinga wilaya ya Bagamoyo ambao wameondolewa kwenye eneo ambalo ni la uhifadhi wa Mikoko.

Akitoa taarifa ya Mawaziri nane wa kisekta ambao walitembelea eneo hilo ambalo ni la mikoko lilikuwa mgogoro wa ardhi na mwekezaji huyo alikuwa na eneo lenye ukubwa wa hekari 600 ambazo nyingine hakuziendeleza na kutakiwa azitoe kwa wananchi hao, Mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amesema nyumba 90 ndizo zitapewa hekari hizo.

Kunenge amesema maamuzi ya baraza la mawaziri lilitoa maamuzi hayo baada ya kulitembelea na kuona jinsi lilivyofanyiwa uharibifu wa mikoko ambayo ni kingo ya bahari na mazalia ya samaki hivyo Halmashauri wakae na mwekezaji wajadili kutoa hekari 50 kwa ajili ya wananchi hao ambao walijenga nyumba za makuti.

Amesema eneo hilo litasimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu TFS ambapo litabaki kwa ajili ya uhifadhi na siyo kwa ajili ya shughuli za kibinadamu.