Saturday, May 6, 2023

WIZARA ZA ELIMU NA UTAMADUNI ZIWASAIDIE VIJANA KUMFAHAMU ZAIDI MWL. NYERERE - MAJALIWA

 

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezitaka Wizara za Elimu, Sayansi na Teknolojia na ile ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ziandae utaratibu utakaosaidia vijana kujifunza na kumfahamu zaidi hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kuanzia shule za msingi, hadi vyuo vikuu.

Ametoa wito huo leo (Jumamosi, Mei 6, 2023) alipomuwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye kongamano la kumbukizi ya miaka 101 ya hayati Mwalimu Nyerere lililofanyika katika ukumbi wa Chimwaga, Chuo Kikuu cha Dodoma.

Amesema kuwa kama lilivyo lengo la kongamano hilo ni muhimu kuwarithisha vijana wa Kitanzania fikra na falsafa za Baba wa Taifa. “Aidha, nyote mtakubaliana nami kwamba yapo mambo mengi ambayo tungetamani vijana wetu wayafahamu kuhusu urithi aliyotuachia Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.”

Mheshimiwa Majaliwa amesema baadhi ya mambo ambayo vijana wanapaswa kurithishwa ni kuyafahamu maisha ya Mwalimu Nyerere hasa baada ya kustaafu uongozi wa nchi na siasa za majukwaani, kutambua juhudi zake katika harakati za kuleta amani na kufanikisha ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika na bara la Afrika.

Ameyataja masuala mengine kuwa ni kufahamu kipaji cha Mwalimu Nyerere katika harakati zake za kupigania uhuru na kuwaunganisha Watanzania na kuwa na uwezo wa kumfahamu na kumuelezea Mwalimu Nyerere alikuwa ni nani katika historia ya Tanzania.

“Miongoni mwa urithi huo ambao tungependa kizazi chetu kiufahamu ni pamoja na kuwa na uwezo wa kumfahamu na kumuelezea Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alikuwa ni nani katika historia ya Tanzania; kuzielewa na kuzitambua juhudi za zake katika kuimarisha ustawi wa Tanzania hususan kupitia falsafa yake ya kutokomeza maadui watatu yaani ujinga, umaskini na maradhi.”

Wakati huohuo, Mheshimiwa Majaliwa amesema kumekuwa na taarifa za malalamiko kuhusu kuongezeka kwa kelele na mitetemo katika sehemu mbalimbali nchini na maeneo yaliyoongoza kwa kulalamikiwa ni za nyumba za starehe, kumbi za burudani na nyumba za ibada.

Amesema katika kudhibiti kelele na mitetemo kutoka katika kumbi za starehe, Ofisi ya Makamu wa Rais ilitoa maelekezo mahususi yaliyolenga kudhibiti mitetemo iliyopitiliza katika kumbi za starehe hapa nchini. Pia, maelekezo hayo yaliainisha jinsi uratibu unavyopaswa kufanyika katika nyumba za ibada kwa kuwaomba viongozi wa dini kupitia Kamati za Amani kujadili suala la kelele na mitetemo iliyopitiliza kutoka kwa baadhi ya nyumba za ibada ili kupata namna bora ya kuendesha shughuli za ibada.

 Hata hivyo, Mheshimiwa Majaliwa amesema, kumejitokeza taharuki kwa baadhi ya viongozi wa dini wakati Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) linashughulikia malalamiko kuhusu ongezeko la kelele na mitetemo.

“Serikali ingependa kutoa ufafanuzi kwamba shughuli za dini ziendelee kufanyika kama kawaida na suala la uratibu wa jambo hilo katika nyumba za ibada liendelee kuratibiwa na viongozi wa dini wenyewe kupitia Jumuiya ya Maridhiano na Amani.”

“Serikali itaendelea kushauriana na jumuiya ya maridhiano na amani katika kuona namna bora ya kuendesha shughuli zao kwa kuzingatia mahitaji ya jamii na kulinda afya za Watanzania,” amesema.

Tanzania, Seattle Sounders, Seahawks, Trailblazers Kushirikiana Kutangaza Utalii



Tanzania, Seattle Sounders, Seahawks, Trailblazers Kushirikiana Kutangaza Utalii

Seattle, Washington State, Marekani

 SERIKALI ya Tanzania imeeleza azma yake ya kuongeza juhudi za kutangaza utalii kupitia michezo pia kushirikiana na taasisi mbalimbali duniani ili kuongeza idadi ya watalii kutoka nje na mapato zaidi kwa Serikali.

Azma hiyo imeelezwa na Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, Mei 5, 2023, wakati wa hafla fupi iliyoandaliwa na kampuni ya Vulcan kwenye Uwanja wa Lumen jijini Marekani na kushirikisha wadau kutoka makampuni mbalimbali yaliyoko jijini Seattle ikiwemo wawakilishi kutoka Google, Starbucks, ofisi ya Meya wa Seattle, Boeing na jumuiya ya wafanyabiashara.

Taasisi ya Vulcan inamiliki hisa katika klabu kubwa za michezo mbalimbali katika ligi kuu za nchini Marekani za Seattle Sounders (mpira wa miguu); Seahawks (soka la Marekani) na Portland Trailblazers (Ligi ya NBA).

“Nimewahi kufika Tanzania, naweza kuwahakikishia kuwa kwa wale ambao hawajafika mfike ni nchi nzuri sana. Tuliwahi kwenda pia Sounders miaka ya 2000 ikacheza na Yanga, Simba na Timu ya Taifa,” alisema Bw. Adrian Hanauer, ambaye kwa sasa ni mmiliki mwenye hisa nyingi wa klabu ya Seattle Sounders akiahidi klabu hiyo na wadau wengine wako tayari kushirikiana kusukuma mbele utalii wa Tanzania.

Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) chini ya Mtendaji wake Mkuu, Damasi Mfugale, imeingia makubaliano ya awali kuelelea ishirikiano kamili na makampuni ya Vulcan.

MAKAMU WA RAIS DKT MPANGO AWASILI BURUNDI

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akiwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Melchoir Ndadaye uliopo Bujumbura nchini Burundi na kupokelewa na Makamu wa Rais wa Burundi Mheshimiwa Prosper Banzombaza leo tarehe 06 Mei 2023. 

Makamu wa Rais anamwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa 11 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi Wanachama wa Mpango wa Amani, Usalama na Ushirikiano kwaajili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Ukanda wa Maziwa Makuu unaofanyika Bujumbura nchini Burundi.

Saturday, April 29, 2023

MAPATO YA UTALII YAONGEZEKA KUPITIA ROYAL TOUR

MAPATO ya utalii yaongezeka maradufu kutokana na watalii kuongezeka nchini kutoka Dola za Marekani 1.310.34 (Sawa na Shilingi Trilioni 3.01) mwaka 2021 hadi Dola za Marekani,527.77 (sawa la Shilingi Trilioni 5.82)  ukiwa ni   matunda ya filamu  ya The Royal Tour.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt Hassan Abbasi  wakati akielezea mafanikio ya  mwaka mmoja tangu Mhe Dkt  Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alipozindua  filamu hiyo Jijini Arusha.

Amesema  filamu ya THE  ROYAL TOUR imejenga hamasa kwa watalii na wawekezaji na hamasa hiyo  imekuwa na manufaa katika sekta ya usafiri wa Anga hadi kuongeza Ruti na  Miruko ikiwemo ndege ya  kimataifa KIA imeongezeka  kwa asilimia 28 kutoka miruko 6,115 April 2021 hadi 7,850 April, 2023.

Aidha  amesema kuwa  Novemba mwaka jana huko Dallas,Texas, USA, Taasisi ya Tuzo za Afrimma ilimtangaza Rais Dkt. Samia  Suluhu Hassan kuwa Rais Mwanamke wa kwanza Afrika na Kushinda Tuzo ya Mageuzi Katika Uongozi .

Pia amesema kuwa filamu ya The Royal Tour sio ya  mwisho ni mwanzo wa kuitangaza nchi kimataifa zaidi hivyo Kamati ya mwaka mmoja sasa, imepokea na inaendelea kuchambua The royal Tours nyingine .


KIBONG’OTO KUWASILISHA MPANGO KAZI WA MATOKEO YA UTAFITI WA KIFUA KIKUU-PROF. NAGU


MGANGA Mkuu wa Serikali Prof Tumain Nagu ameitaka Hospitali ya Taifa ya Magonjwa ambukizi ya Kibongóto kwa kushirikiana na Mtandao wa Watu Waliougua Kifua Kikuu na Kupona (MTUKTA) kuhakikisha wanakuja na mpango kazi wa kufanyia kazi matokeo ya utafiti wa mwaka mmoja uliofanyika wa kuchunguza watu waliowahi kuugua kifua kikuu na kupona lakini baada ya kupona hawakufatiliwa kwa karibu.

Prof Nagu ametoa wito huo Jijini Dodoma katika ufunguzi wa kikao kazi cha usambazaji wa matokeo ya mwaka mmoja ambao umeweza kushirikisha watu waliowahi kuumwa kifua kikuu na kupona lakini baada ya kupona wakawa hawafuatiliwi kwa karibu kujua maendeleo yao.

Amesema kuwa wanatakiwa kuwasilisha mpango kazi kwa wizara kulingana na matokeo waliopata kutoka katika utafiti huo uliofanyika ili kuhakikisha wanaongeza umakini dhidi ya maambukizi ya kifuu kikuu nchini.

Naye Mkurungenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Magonjwa Ambukizi ya Kibongóto iliyopo Wilaya ya Siha Mkoa wa Kilimanjaro Dkt Leonard Subi amesema kuwa kupitia utafiti huo wameweza kupata zaidi ya watu 625 ambao walikuwa katika jamii na watu hao wamefanyiwa uchunguzi tena kuona kama hawana kifua kikuu.

“Katika watu 625 tulio wafanyia uchunguzi tumeweza kugundua asilimia 24 kati yao tayari walishaugua tena kifua kikuu na wapo katika jamii na watu 8 walikuwa ni wale walio na  kifua kikuu sugu”, ameeleza Dkt Subi.

Hivyo ametoa rai kuwa kuna umuhimu mkubwa sana wa kushirikisha jamii hususani katika kuwafuatilia kwa ukaribu watu waliougua kifua kikuu na kupona ili kujua maendeleo yao katika jamii.


Friday, April 28, 2023

NDOTO YA RAIS SAMIA YATIMIA KWENYE WIZARA YA MIFUGO NDANI YA RANCHI YA KONGWA.


SERIKALI kupitia wizara ya mifugo imeweza kuongeza vifaa vya malisho ya mifugo pamoja na Ngo'mbe 1,000 katika Ranchi ya Kongwa iliyopo Dodoma huku ikiwa na malengo ya kuhakikisha inatoa huduma Bora kwa wananchi Katika sekta ya ajira na uhuzaji wa majani ya  malisho ya mifugo.

Hayo yamesemwa  Tarehe 27 April 2023 na waziri wa mifugo na uvuvi Abdalah Ulega wakati wa uzinduzi wa vifaa vya malisho ya mifugo na ukaguzi wa Ngo'mbe 1,000 Katika eneo ilo la Narco.

Ulega amesema serikali imefanikiwa kununua Ngo'mbe hao pamoja vifaa hivyo vya malisho ikiwemo matreta manne, mower 3, Hay rake 10 pamoja na bailer 3 Ili  kuboresha maeneo ya Malisho.

Amesema mpaka Sasa nyama zinazouzwa kwenye Ranchi hiyo ni tani 12,000 na kwa muelekeo unaoelekea wataenda kuuza nyama hadi tani 50 mpaka tani 1,000.

Aidha amemtaka Mkurugezi wa Nacro kupendezesha eneo ilo kwa kuweka mipaka minzuri ya eneo Ili kunusuru mifugo isitoke ndani  eneo  ilo na kuhakikisha wafugaji ambao wamepewa kitalu kwenye eneo hilo wafuge kisasa na kutafutiwa masoko.

Awali  Mkurugezi mtendaji wa Ranchi ya taifa  ( Nacro) Prof Peter Msoffe  amesema kuwa kwa mwaka wa fedha 2022/2023 serikali ilitenga fedha kiasi cha shillingi bilioni 4.65 kwa ajili ya kuboresha na kuongeza uzalishaji katika Ranchi za Kongwa na Mzeri fedha hizo zilitengwa kwa ajili ya kununulia ng'ombe wazazi, vifaa vya shamba na uchungaji wa visima virefu.

Ikumbukwe kuwa Ranchi ya Kongwa ni miongoni mwa Ranchi kongwe za taifa iliyopo mkoani Dodoma wilaya ya Kongwa na  ndiyo ya kwanza kuanzishwa na ilianza Mwaka 1948 na eneo hilo lina ukubwa wa hekta 3,8000  zenye uwezo wa kuweka uniti za mifugo 25,000.



Wednesday, April 26, 2023

MILIONI 2.9 HUPOTEZA MAISHA



TAKWIMU za kidunia zilizotolewa na Shirika la Kazi Duniani mwaka 2022 zinaonesha kwamba zaidi ya watu milioni 2.9 hupoteza maisha kutokana na ajali na magonjwa yatokanayo na kazi.

Aidha zaidi ya wafanyakazi milioni 402 huumia wakiwa kazini na hivyo kushindwa kutekeleza majukumu yao kwa kipindi chote wanachopatiwa matibabu hadi hapo watakapopona.

Akizungumza  na Waandishi wa habari Tarehe 26 April 2023 Jijini Dodoma kuelekea maadhimisho ya siku kuelekea kilele cha maadhimisho ya siku ya kimataifa ya usalama na afya mahali pa kazi Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi,Vijana,Ajira, na Wenye Ulemavu Prof Joyce Ndalichako amesema Kwa upande wa Tanzania jumla ya ajali na magonjwa yaliyoripotiwa katika Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi kuanzia Julai 2019 hadi Juni 2021 ni ajali 4,993 na magonjwa 249. Katika ajali hizo vifo vilikuwa 217.

Prof Ndalichako amesema kuwa maadhimisho hayo yatafanyika kitaifa Mkoani Morogoro katika viwanja vya Tumbaku Aprili 28,2023 na lengo kubwa la maadhimisho hayo ni kuendeleza kampeni za kuhamasisha na kuweka mazingira salama katika sehemu za kazi miongoni mwa wadau kupitia kauli mbiu mbali mbali ambazo hutolewa na Shirika la Kazi Duniani ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ni: “Mazingira Salama na Afya kazini ni Kanuni na Haki ya Msingi Mahali pa Kazi” (A Safe and Health Working Environment is a Fundamental Principle and Right at Work).

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda amesema kuwa moja kati ya eneo ambalo ajali nyingi zinaripotiwa ni katika sekta ya Uzalishaji ambapo imeajiri vijana wengi huku wengine wakiwa hawana ujuzi wa kutosha katika nafasi wanazofanyia kazi.

Mwenda amesema kuwa OSHA imejipanga vyema kuelekea maadhimisho hayo ya 19 ambapo washiriki wote watapatiwa Mafunzo ya Usalama na Afya miongoni mwa makundi mbali mbali wakiwemo wajasiriamali wadogo, wafanyakazi wa viwandani, wachimbaji wadogo pamoja na watu wenye ulemavu.

Siku ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi Duniani ilianza mwaka1996 Nchini Marekekani Katika Jiji la New York, ambapo waathirika wa watu walioumia na kupoteza maisha wakiwa kazini hukumbukwa. Maadhimisho hayo yalikuwa yakifanywa na Chama Cha Wafanyakazi Duniani. Ilipofika mwaka 2001,Shirika la Kazi Duniani liliona kuwa ni busara kubadilisha madhumuni ya siku hiyo na kuiita “Siku ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi Duniani


Mwisho.