Thursday, November 3, 2022

WIZARA AFYA KUDUMISHA HUDUMA ZA AFYA


WATUMISHI KUWA WAKUTOSHA KWENYE VITUO VYA KUTOLEA HUDUMA ZA AFYA.

Dodoma,

Katibu Mkuu,Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi amesema Wizara ya Afya inaendelea kuimarisha huduma za afya kwa kuwa na watumishi wa kutosha kwenye vituo vya kutolea huduma za afya nchini.

Prof. Makubi amesema hayo leo tarehe 3 Novemba, 2020 wakati wa kikao cha Sekretarieti ya maandalizi ya Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote na Menejimenti ya Ofisi ya Rais-TAMISEMI ikiwa ni kuelezea hatua iliyofikiwa pamoja na nini kifanyike kama sekta moja endapo Muswada huo utapitishwa na Bunge na kuwa Sheria.

Aidha, Prof. Makubi amesema Wizara ya Afya inaendelea kuboresha upatikanaji wa Dawa, vifaa tiba na vipimo kwenye vituo vya kutolea huduma za afya ili huduma zinazotolewa ziwe bora.

"Afya ni kitu muhimu na ndio haki ya kwanza ambayo Mungu amempa Mwanadamu hivyo kila mmoja lazima athamini uhai wake kwa kuwa na Bima ya Afya".

Hata hivyo Katibu Mkuu huyo alisema dhana ya bima ya afya kwa wote ni kuchangiana pindi mmoja anapougua aweze kupata matibabu bila kuwa na kikwazo cha fedha.

Naye, Naibu Katibu Mkuu-Afya kutoka TAMISEMI Dkt. Grace Magembe amesisitiza utoaji wa elimu kwa wananchi ngazi zote ili waelewe zaidi dhana nzima ya Bima ya Afya kwa Wote.

HUDUMA ZA NDEGE ZAONGEZEKA NCHINI.

VIWANJA VYA NDEGE VYAONGEZA HUDUMA ZA NDEGE NCHINI.


Na Wellu Mtaki, Dodoma

JUMLA ya ndege 40,323 zilihudumiwa katika kipindi cha mwaka 2021/2022 ikilinganishwa na huduma iliyotolewa mwaka 2020/2021 sawa na ongezeko la asilimia 13. 

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Huduma za Utabiri - Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dkt. Hamza Kabelwa wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu majukumu ya Mamlaka hiyo na mwelekeo wa utekelezaji kwa mwaka wa Fedha 2022/23 katika Ukumbi wa Idara ya Habari MAELEZO Novemba 2, 2022 Jijini Dodoma.

Dkt Kabelwa amesema kuwa sekta ya usafiri wa anga inaendelea kukua kutokana na kuzingatiwa kwa mfumo wa kudhibiti ubora wa huduma na ongezeko hilo linatokana na jitihada za kuifungua nchi zinazofanywa na serikali, pamoja na kuendelea kukidhi viwango vya Kimataifa na kuihakikishia dunia usalama wa anga la Tanzania katika masuala ya hali ya hewa kwa ndege zote za kimataifa.

Amesema kuwa mamlaka hiyo katika mwaka 2021/22 iliendelea na utengenezaji wa rada mbili zitakazofungwa katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro (KIA) na cha Jiji la Dodoma ambao umefikia asilimia 45.

Ameongeza kuwa Mamlaka imeendelea kutekeleza kwa ufanisi majukumu yake iliyopewa na Shirika la Hali ya Hewa Duniani ya kuwa Kituo cha kutoa mwongozo wa utoaji wa utabiri wa hali ya hewa kwa nchi za ukanda wa Ziwa Victoria (Regional Specialized Meteorological Centre) kwa nchi zilizopo Afrika Mashariki.

Kwa upande wake Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari Maelezo Gerson Msigwa ametoa wito kwa Wananchi kujenga utaratibu wa kutumia taarifa za hali ya hewa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania.

Majukumu ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)yamegawanyika katika sehemu kuu tatu ambapo sehemu ya kwanza ni kutoa huduma za hali ya hewa; sehemu ya pili ni kudhibiti shughuli za hali ya hewa hapa nchini kwa mujibu wa Kifungu cha (14) na sehemu ya tatu ni kuratibu shughuli za hali ya hewa nchini Tanzania kulingana na Kifungu cha (5) cha Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Na.2 ya Mwaka 2019.

Mwisho

Sunday, October 30, 2022

JWT PWANI YAITA WAFANYABIASHARA KUJIUNGA NA JUMUIYA




WAFANYABIASHARA PWANI WATAKIWA KUCHANGAMKIA FURSA KWENYE JUMUIYA 

Na John Gagarini

JUMUIYA ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT) Mkoa wa Pwani imewataka wafanyabiashara kujiunga ili wanufaike na fursa mbalimbali zilizopo kwenye Jumuiya hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekekezaji wa majukumu ya taasisi hiyo pamoja na fursa zilizopo ndani ya Jumuiya hiyo katibu wa JWT Mkoa Wellu Mtaki amesema kwenye Jumuiya hiyo kuna fursa nyingi.

Mtaki amesema kuwa Jumuiya hiyo inamuwezesha mfanyabiashara kutatua changamoto zake na mfanyabiashara anauwezo wa kutoa kero maoni na mapendekezo yanayohusu biashara na taasisi ikafikisha sehemu husika kwa ajili ya utatuzi tofauti na mtu kupeleka kero yake mwenyewe.

"Lengo la Jumuiya ni kuwaunganisha kwa pamoja wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao katika eneo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuwawezesha kutoa mawazo na maoni yao kuhusu changamoto mbalimbali zinazowakabili kwa na kuziwasilisha serikalini,"amesema Mtaki

Amesema kuwa taasisi hiyo imekuwa ikishirikiana na serikali katika kutengeneza mazingira bora ya kufanya biashara nchini Tanzania na moja ya huduma ni kuwaunganisha na bima za aina tofauti ambazo zimeanza kutolewa kwa wanachama.

"Huduma za bima zinazotolewa ni pamoja na bima ya Elimu au Carrier Life Plan kupitia shirika la bima la Jubilee ambalo linamsaidia mtoto wa mwanachama kunufaika kwenye elimu, bima ya Afya ambayo ina kifurushi cha aina tatu ambacho Scare individual and Family health insurance, pamoja Afya, Jubilee Afya na huduma ya bima ya nafaka," Amesema Mtaki.

Ametoa wito kwa wafanyabiashara wote mkoani Pwani kuhakikisha wanafuata taratibu na miongozo ya Mamlaka ya Mapato Tanzania  (TRA) ili kepuka changamoto zitakazojitokeza.

Aidha amesema kuwa Jumuiya ya wafanyabiashara Tanzania haijihusishi wala kufungamana na udini, ukabila, siasa, wala ushabiki wa michezo.


RAIS SAMIA KUZINDUA MATOKEO YA SENSA


RAIS SAMIA KUTANGAZA MATOKEO YA SENSA KESHO.

Na Wellu Mtaki, Dodoma.

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi wa kutangaza matokeo ya Sensa ya watu na Makazi Oktoba 31 kwenye uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hamza Juma ameyasema hayo Jijini Dodoma alipokuwa akitoa taarifa kwenye kikao maalumu cha wajumbe wa kamati ya maandalizi ya uzinduzi wa tukio hilo.

Juma amesema kuwa maandalizi ya uzinduzi wa tukio la kutangazwa kwa matokeo ya sensa ya watu na anwani za makazi yamekamilika.

Ameeleza kuwa kazi kubwa ya kuratibu na kusimamia imefanywa na viongozi wa mkoa wa Dodoma na kilichobaki watakuwa wamekamilisha Oktoba 30.

Aidha amesema kuwa zoezi la sensa ya watu na makazi la mwaka huu limefanyika kisasa zaidi tofauti na miaka ya nyuma na litaisaidia Serikali katika kupanga mipango yake ya kiuchumi,kijamii na maendeleo. Zoezi la sensa ya watu na makazi lilifanyika hivi karibuni.

Saturday, October 29, 2022

MATRILIONI YATENGWA MIRADI YA BARABARA NCHINI


TANROADS YATENGA TRILIONI 3.8 UTEKELEZAJI MIRADI YA BARABARA 

Na Wellu Mtaki, Dodoma

WAKALA wa Barabara Nchini (TANROADS) imetenga kiasi cha shilling trilioni 3.8 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya ujenzi wa barabara na madaraja makubwa nchi nzima.

Hayo yamesemwa leo na mtendaji mkuu wa Tanrods injinia Rogatus Mativila alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma kuhusu shughuli mbalimbali zinazoendelea kufanywa na wakala.

Mativila amesema kuwa tayari wakala wa barabara imefanya usanifu wa miradi hiyo ambayo baadhi ni madaraja makubwa sita ikiwa ni pamoja na daraja la bwawa la Mtera Mkoani Dodoma , daraja la Jangwani Mkoani Dar - es- Salam, daraja la mkoa wa Simiyu, daraja la Mzinga, daraja la Mtoroni na makaravati sehemu mbalimbali nchini.

Amesema kuwa mradi mwingine mkubwa utakaotekelezwa ni ule wa ujenzi wa uwanja wa ndege wa Msalato ambapo Rais Samia Suluhu Hassan ataweka jiwe la msingi Oktoba 30 mwaka huu.

Ametoa wito kwa Watanzania hasa madereva wa magari kuitunza miradi hiyo kwa kuwa Serikali inatumia fedha nyingi kugharamia miradi hiyo.

UVCCM YAPONGEZA SHULE KUFUTA ZIRO


Na John Gagarini Kibaha

UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Kata ya Mkuza Wilaya ya Kibaha Mjini imetoa fedha na vyeti vya pongezi kwa walimu wa Shule ya Sekondari ya kutwa ya Nyumbu kwa kufanya vizuri kwenye baadhi ya masomo na kuondoa ziro kwenye shule hiyo.

Akizungumza kwenye mahafali ya 16 ya shule hiyo Mwenyekiti wa UVCCM Kata ya Mkuza Hashim Kibonge alisema kuwa wameamua kuwapa motisha walimu ili waendelee kufanya vizuri ili kuongeza ufaulu shuleni hapo.

Kibonge alisema kuwa walimu hao wametekeleza vema ilani ya CCM juu ya masuala ya Elimu ikiwa ni moja ya vipaumbele vilivyopo kwenye ilani ya chama juu ya uboreshaji wa elimu.

"Tumetoa vyeti kwa walimu wa masomo ya Kiingereza, Baiolojia na Kiswahili walimu wote wamefanya vizuri lakini masomo haya tumeona tuwapongeze hawa lakini wote wamepambana kuleta mafanikio shuleni,"alisema Kibonge.

Naye Mwenyekiti wa CCM Kata ya Mkuza Matata Ngolo alisema kuwa wamekuwa wakiifuatilia shule hiyo na kuona jinsi inavyopambana kuhakikisha watoto wanapata elimu inayostahili.

Ngolo alisema shule hiyo licha ya kuwa na wanafunzi wengi lakini imeendelea kufanya vizuri kwenye Halmashauri ya Mji wa Kibaha ambapo ufaulu kwa mwaka jana ilikuwa asilimia 99.

Naye Mgeni rasmi Naibu Kamishna wa Elimu Bahati Chikwindo alisema kuwa Wizara itasaidia shule hiyo kuhakikisha inakabili changamoto za shule hiyo ikiwemo ujenzi wa jengo la utawala.

Chikwindo alisema kuwa watasaidia pia upatikanaji wa vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano TEHAMA ili wanafunzi waweze kupata elimu hiyo ambayo ni muhimu kwa kipindi hichi cha utandawazi.

Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Juma Mrope alisema kuwa shule hiyo ndiyo shule inayoongoza kwenye Mkoa huo ambapo ina wanafunzi 2,136 huku wahitimu wa kidato cha nne walikuwa ni 460.

Mrope alisema kuwa changamoto kubwa waliyonayo ni kutokuwa na jengo la utawala hali ambayo inasababisha watumie madarasa matatu hivyo kusababisha mlundikano wa wanafunzi kwani kuna upungufu wa madarasa unaofanya wanafunzi wasome kwa awamu mbili.

Akisoma risala ya wahitimu wa kidato cha nne Ahmed Kikoto alisema kuwa wanahitaji viti na meza zaidi ya 300, wanahitaji maktaba, ukarabati wa sakafu na kuomba kujengewa ukumbi.

Kikoto alisema kuwa wanawashukuru wadau mbalimbali kwa kuwapatia miradi mbalimbali ikiwemo wa Tehama na serikali kujenga shule shikizi ya Sofu ambapo imepunguziwa wanafunzi 75.

WATANZANIA WATAKIWA KULA NYAMA


DKT. MUSHI AMEWASISITIZA WATANZANIA KUJENGA UTAMADUNI WA KULA NYAMA

Na Wellu Mtaki, Dodoma

MSAJILI wa bodi ya nyama nchini Dkt Daniel Mushi amewasisitiza Watanzania kujenga utamaduni wa kula nyama ili kukabiliana na utapiamlo.

Aidha utafiti unaonyesha Mtanzania mmoja hula kilo 15 za nyama badala ya kilo 50 kama inavyotakiwa

Ametoa kauli hiyo Jijini Dodoma alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa habari maelezo .

Dkt Mushi amesema kwamba utafiti uliofanywa na bodi hiyo umebaini baadhi ya nchi za Ulaya na nyinginezo mtu mmoja anakula kilo hadi 100 kwa mwaka.

Amepinga kauli ya watu kuwa nyama nyekundu ni hatari bali mlaji anatakiwa kuandaa nyama vizuri kuanzia katika kuipika hadi kwenye ulaji.

Katika hatua nyingine ameeleza kuwa kwa sasa wana mipango thabiti ya kutafuta masoko ya uhakika kwani mahitaji ya nyama nje ya nchi ni makubwa lakini Tanzania inasafirisha nyama kwa kiwango kidogo.