Saturday, October 7, 2017

CCM WILAYA YA BAGAMOYO YAPATA MWENYEKITI MPYA










Na John Gagarini, Bagamoyo

ABDUL Zahoro Sharifu amechaguliwa kuwa mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani baada ya kumshinda aliyekuwa mwenyekiti Alimasi Masukuzi.

Uchaguzi huo ambao ulifanyika Msata wilayani humo Sharifu alimshinda mpinzani wake kwa kupata kura 711 dhidi ya kura 383 za Masukuzi huku Tariq Kafuku akipata kura 185 na nafasi ya Katibu Mwenezi ilikwenda kwa John Francis maarufu kama Bolizozo aliyepata kura 112 akimshinda Hassan Sharifu aliyepata kura 4.

Kutokana na ushindi huo Sharifu amesema kuwa chama ndiyo kilichoshinda na siyo yeye na kuwataka wagombe na wanachama kuwa kitu kimoja ili kukijenga chama kwa ajili ya kuendelea kushika dola.

“Kuanzia sasa hakuna makundi makundi yamekwisha baada ya uchaguzi na kila mtu anahaki ya kuwa na mgombea anayempenda lakini kwa kuwa mshindi kashapatikana hakuna sababu ya kuwa na makundi,” alisema Sharifu.
Alisema kuwa baada ya uchaguzi kwisha malengo yake ni kujenga chama kwa kuanzisha vitega uchumi na kuachana na tabia ya kutegemea kuomba fedha kwa ajili ya kuendesha shughuli za chama.

“Furaha yangu ni kuona chama kinajitegemea chenyewe kwa kujiendesha kwani kina miradi mingi na endapo itasimamiwa vizuri itakiletea manufaa chama,” alisema Sharifu.

Kwa upande wake Bolizozo alisema kuwa kwa kutumia nafasi yake atahakikisha anashirikiana na viongozi na wanachama kuleta maenedeleo ya chama ili kiweze kwenye chaguzi kuanzia ya serikali za mitaa 2019 na uchaguzi mkuu 2020.

Mwisho.


CCM KIBAHA MJINI WACHAGUA VIONGOZI WAKE








Na John Gagarini, Kibaha

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kibaha Mjini Mkoani Pwani Maulid Bundala amefanikiwa kutetea kiti chake baada ya kushinda kwenye uchaguzi wa chama hicho.

Bundala alifanikiwa kutetea nafasi yake hiyo kwa kipindi cha awamu tatu sasa baada ya kushinda kwenye uchaguzi ambao ulifanyika kwenye shule ya sekondari ya Filbert Bayi mjini Kibaha na kuwashinda wenzake wawili.

Wajumbe wa mkutano huo mkuu wa CCM Kibaha Mjini walimpa ushindi wa kishindo Bundala kwa kumpigia kura 288 kati ya kura 489 za wajumbe wote huku kukiwa hakuna kura iliyoharibika.

Aliyemfuatia mshindi alikuwa ni Batholomew Nyalusi ambaye alipata jumla ya kura 164 akifutaiwa na Joseph Masenga ambaye alipata kura 37.

Kwa upande wa uwakilishi wa mkutano mkuu wa mkoa washindi wawili walikuwa ni Rugemalila Rutatina kura 392 na Happines Mgalula kura 201 kwa upande wa uwakilishi Halmashauri Kuu wilaya wajumbe wawili ni Kabunda Bekari kura 238 na Philemon Mabuga  kura 209.

Nafasi nne za uwakilishi toka Umoja wa Vijana (UVCCM) nafasi nne ni Makwiro selaman kura 289, magreth Mbawala kura 283, Herman Kagaruki kura 269 na Jagala Salum kura 233.

Kwa upande wa uwakilishi Jumuiya ya Wanawake (UWT) nafasi nne washindi walikuwa ni Zamda Komba kura 276, Dk Alice Karungi kura 255, Joyce Mushi 230 na Joyce Shauri kura 185.

Washindi wa nafasi tatu za uwakilishi mkutano mkuu wa Taifa ni Abdulaziz Jaad kura 355, Catherine Katere kura 336, Dk Alice Kaijage 332 ambapo katibu wa CCM Kibaha Mjini Abdala Mdimu alisema uchaguzi huo ulikwenda vizuri na hakukuwa na malalamiko yoyote kutoka kwa wagombea.


Mwisho.

WAFANYABIASHARA MKOA WA PWANI WAFANYA UTALII WA NDANI MIKUMI















Na John Gagarini, Morogoro

WAFANYABIASHARA nchini wametakiwa kuungana na Serikali katika kutangaza vivutio vya Utalii ili kuongeza idadi ya watu wanaotembelea vivutio hivyo na kuongeza pato la Taifa kupitia utalii.

Hayo yalisemwa Mikumi na Abdala Ndauka mwenyekiti wa Jumuiya ya wafanyabiashara Tanzania (JWT) mkoa wa Pwani wakati waliotembelea Mbuga ya wanyama ya Mikumi iliyopo mkoani Morogoro.

Ndauka alisema kuwa wafanyabiashara wananafasi kubwa ya kutangaza vivutio vya Utalii vilivyopo nchini ambavyo havipatikani sehemu yoyote duniani kupitia bidhaa zao wanazozalisha.

“Sisi jumuiya ya wafanyabishara mkoa wa Pwani tumeamua kufungua ukurasa kwa wafanyabiashara kutembelea vivutio vya utalii ambavyo vinavutia watalii wengi nchini na duniani,” alisema Ndauka.

Alisema kuwa ili vivutio vya utalii vitambulike wafanyabishara wana nafasi kubwa ya kuvitangaza na kuongeza watalii wa ndani na nje ya nchi.

“Kwa kuja kwetu huku kuangalia vivutioo hivi tumeweza kujifunza na kuona mengi ambayo tulikuwa tukiyasikia na kuona kupitia vyombo vya habari lakini tumeona wenyewe kwa macho yetu wanyama kama vile Simba,Tembo Swala, Twiga, Nyati, Pundamilia,Viboko na Mamba,” alisema Ndauka.

Aidha alisema kuwa watalii wa ndani wanapaswa kutapembelea vivutio mbalimbali vilivyopo nchini kwani gharama za kuingia kwa sasa zimepungua japo zinapaswa kupungua zaidi ili watu wengi waweze kutembelea.

Kwa upande wake Salugroli Masaga alisema kuwa kwa kutembelea Mbuga hiyo ya Mikumi ameweza kujifunza mambo mengi ikiwiwa ni pamoja na fursa zilizopo kwa wafanyabiashara.

Masaga alisema moja ya fursa ambazo aliziona ni wafanyabiashara kufanyabiashara mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuanzisha migahawa, uuzaji bidhaa za kitalii kama mikufu hereni na mavazi yanayotengenezwa hapa nchini.

“Mbali ya kuona wanyama tumepata fursa ya kujua tabia zao na maisha yao ambayo ni kivutio kikubwa kwani baadhi ya wanyama wanaonekana kama wana tabia tofauti ambazo ni faida kwa wengine,”  alisema Masaga.


Aliwataka wafanyabiashara, vikundi na watu mmojammoja kutembelea pia kutangaza biashara zao kwa kutangaza vivutio hivyo vya kitalii adimu duniani.

Mbuga hiyo ilianzishwa mwaka 1964 ikiwa na ukubwa wa kilometa za mraba 1,070 na iliongezwa ukubwa na kufikia kilometa za mraba 3,200 mwaka 1975 ikiwa ni ya tano kwa ukubwa kwa Mbuga za Taifa.

Mbuga inayoongoza ni Ruaha yenye ukubwa wa Kilometa za mraba 20,226, Serengeti yenya ukubwa wa Kilometa za mraba 14,763 na Mkomazi yenye ukubwa wa Kilometa za mraba 3,245 ikiwa na wanyama wakubwa aina nne kati ya tano ambao ni Simba,Tembo, Nyati na Chui

Mwisho.  

MAMIA YA WANANCHI WALILIA AJIRA WAMOMBA RC AWASAIDIE






Na John Gagarini, Kibaha

MAMIA ya wananchi wa wilaya ya Kibaha na mkoa wa Pwani wamelilia mkuu wa mkoa huo Mhandisi Evarist Ndikilo awasidie kupata ajira wazuia msafara wake kwa mabango kwenye kituo cha ujenzi wa reli ya kisasa ya Standard Gauge kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro kilichopo kwenye Kijiji cha Soga inayojengwa na kampuni ya Yapi Merkezi ya nchini Uturuki.

Wananchi hao walifikia hatua hiyo wakati mkuu wa mkoa wa Pwani akiwa na kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa ilipotembelea kujionea ujenzi huo ambao tayari umeanza na kusema kuwa watu wa mkoa huo wamekuwa wakibaguliwa na kuajiriwa watu kutoka Jijini Dar es Salaam zaidi wananchi hao.

Kwa upande wa Rukia Ally amesema kuwa wametumia gharama kubwa kujenga mabanda wanayofanyia biashara hiyo ya chakula na wamekopa mikopo kwenye taasisia za kifedha hali ambayo inawapa wasiwasi huenda wakauziwa mali zao.

Ally amesema kuwa wanahofu kuuziwa mali zao kwani watashindwa kurudisha fedha walizokopa kwa ajili ya kujenga mabanda na kunuanua bidhaa kwa ajili ya biashara hiyo hivyo kumwomba mkuu wa mkoa kuwasaidia ili kampuni hiyo iruhusu waendelee kupata huduma ya chakula nje na si ndani kwa mzabuni.

Kwa upande wake meneja mradi kutoka kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli (RAHCO) Mhandisi Maizo Mgedzi amesema kuwa wao wanaajiri kutokana na sifa za waombaji ambao wengi ni madereva na waendeshaji wa mitambo.
Kutokana na malalamiko hayo mkuu huyo wa mkoa wa Pwani ametoa siku saba kwa vyombo vya dola kufutailia suala la rushwa kama lipo na kutaka wahusika waliotajwa na wananchi hao kusimama kupisha uchunguzi.

Aidha ametaka kupelekewa majina ya watu waliajiriwa kama wanatoka mkoa wa Pwani au la kwani serikali imekuwa ikitaka wanufaika wa kwanza wawe wanaoishi kwenye eneo la mradi.

Pia ametaka utaratibu wa chakula nao uangaliwe ili akina baba na mama lishe walioko nje ya eneo hilo la mradi huo waruhusiwe kuendelea kufanyabishara badala ya kuwazuia wafanyakazi wasitoke nje baada ya kupewa mazabuni kwa ajili ya kuwapa chakula.

Naye mwakilishi wa mkandarasi wa kampuni hiyo Merz Oz alisema kuwa waliamua kuacha utaratibu wa wafanyakazi wao kula chakula nje kwa madai kuwa wanatumia muda mwingi na kufanya shughuli kushindwa kufanyika kwa wakati.

Oz alisema kuwa sababu nyingine ni kuhakikisha wafanyakazi wanapata chakula chenye ubora hasa ikizingatiwa kampuni yao ni ya kimataifa hivyo haiwezi kuwaacha wafanyakazi wao wanakula bila ya utaratibu na huwapatia bure chakula hicho jambo ambalo lilipingwa na wananchi.

Mwisho.



Wednesday, September 6, 2017

WATATU WAFA WAKITOKA BUNGENI DODOMA KUSHUHUDIA KUAPISHWA WABUNGE VITI MAALUMU CUF

Na John Gagarini, Kibaha
WATU watatu wamefariki dunia huku wengine watatu wakijeruhiwa walipokuwa wakitokea Bungeni mkoani Dodoma kushuhudia kuapishwa kwa wabunge saba wa Viti Maalumu wa Chama Cha Wananchi (CUF) baada ya gari walilokuwa wakisafiria kugongana na lori la mizigo.
Hayo yalisemwa mjini Kibaha na kamanda wa Polisi mkoani Pwani Jonathan Shana alipozungumza na waandishi wa habari na kusema kuwa watu hao walifia papo hapo.
Kamanda Shana alisema kuwa tukio hilo lilitokea Septemba 6 majira ya saa 8:30 usiku eneo la Kijiji cha Ubena Zomozi barabara ya Dar es Salaam-Morogoro wilaya ya Kipolisi Chalinze-Bagamoyo.
“Gari lililokuwa limetoka Dodoma kwenda Muheza mkoani Tanga ni aina ya Toyota Noah lenye namba za usajili T 968 CSK likiendeshwa na dereva Uled Sarumaa (32) mkazi wa Muheza liligongana na gari aina ya Scania lenye namba za usajili T 929 CBK lenye tela namba T 472 CAX lililokuwa likiendeshwa na Yasin Kanoni (35) mkazi wa Jijini Dar es Salaam na kusababisha vifo hivyo,”alisema Shana.
Aliwataja waliokufa kwenye ajali hiyo kuwa ni dereva wa Noah Sarumaa, Mary Komba (40) mkulima mkazi wa Muheza na mtu aliyetambuliwa kwa jina moja la Isaack mfanyabiashara anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka (37).
“Majeruhi wa ajali hiyo kuwa ni Juma Nindi (47) mfanyabiashara wa Muheza, Chausiku Hassan (47) mkulima wa Muheza na Ester Mafie (67) mkulima mkazi wa Muheza,” alisema Shana.
Aidha alisema kuwa miili ya marehemu imehifadhiwa kwenye Hospitali Teule ya Rufaa ya mkoa wa Pwani Tumbi kusubiri uchunguzi wa daktari na kusubiri ndugu kwa ajili ya mazishi huku majeruhi wakiwa wamelazwa kituo cha afya cha Chalinze
Alibainisha kuwa na chanzo cha ajali kinachunguzwa na alipoulizwa juu ya waliokufa kama ni viongozi wa CUF amesema kuwa bado hajapata taarifa kuhusiana na hilo pia dereva wa lori Yasin Kanoni alikimbia mara baada ya tukio hilo na kwa sasa anatafutwa.
Mwisho. 

BABA WA KAMBO AMJERUHI MTOTO KWA KUIBA MAYAI MAWILI





Mtuhumiwa Abdala Machupa akiwa kituo cha Polisi Kongowe
Na John Gagarini, Kibaha
JESHI la Polisi Mkoani Pwani linamshikilia Abdala Machupa (49) fundi ujenzi mkazi wa Kongowe kwa tuhuma za kumjeruhi kwa kumkata na kisu kichwani mwanae wa kufikia (jina limehifadhiwa) mwenye umri wa miaka (5) mwanafunzi wa shule ya awali ya Kongowe Kati kwa madai ya kuiba mayai mawili.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na kamanda wa Polisi mkoani humo Jonathan Shana alisema kuwa mtuhumiwa huyo alipata taarifa hizo mitaani za mwanae kuiba mayai hayo.
Kamanda Shana alisema kuwa  mtoto huyo alitutuhumiwa kuiba mayai kwa Bibi Baby Septemba 4 majira ya saa 2 usiku na kumfiki mama yake mzazi aliyefahamika kwa jina moja la Hadija ambaye alimkanya mwanae kwa kumchapa viboko.
“Mnamo Septemba 5 mtuhumiwa huyo alipata taarifa mtaani kuwa mtoto wake kaiba mayai alirudi nyumbani na kuanza kumchapa kwa fimbo na kama haitoshi alichukua panga lakini mwanae mwingine Hamis Abdala miaka (8) akamzuia ndipo alipochukua kisu na kumkata kichwani mara mbili,” alisema Shana.
Alisema kuwa wananchi baada ya kupata taarifa walifika na kuingilia kati ili kumwokoa mtoto huyo na wao ndipo walipomshambulia na kumjeruhi kichwani na kisogoni kisha walimfikisha polisi.
“Mtuhumiwa alipatiwa matibabu na kwa sasa bado yuko mahabusu na amekemea tabia ya vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto ambapo upelelezi umekamilika na mtuhumiwa alitarajiwa kufikishwa mahakamani jana,” alisema Shana.
Awali akizungumzia juu ya tukio hilo mwenyekiti wa mtaa wa Bamba Amri Mavalla alisema kuwa wakati mtuhumiwa huyo akimwadhibu mama mzazi wa mtoto huyo ambaye ni mjamzito alipoteza fahamu kwa hofu kwa mwanae.
Mavalla alisema kuwa aliletewa taarifa majira ya saa 6 ofisini kwake na ndipo alipokwenda kupata taarifa juu ya tukio hilo ambapo mama mzazi wa mtoto huyo alishindwa kuchukua yoyote wakati baba yake akimwadhibu kutokana na hali yake.
Alisema kuwa baada ya tukio hilo wasamaria wema walimpa huduma ya kwanza mama huyo wakati huo wakimkimbiza mtoto huyo kituo cha afya cha Kongowe kwa ajili ya matibabu ambapo anaendelea vizuri.
“Mtoto huyo alichukua mayai hayo akiwa anacheza na wenzake lakini yeye peke yake ndiye aliyeadhibiwa na wenzake hawakuchukuliwa hatua yoyote na ameshonwa nyuzi 12 utosini na nyuzi  nane karibu na sikio,” alisema Mavalla.
Aidha alisema kuwa mtuhumiwa huyo alibadilisha nguo akiwa na lengo la kutaka kukimbia na alipoulizwa kampiga mwanae na nini alisema kamchapa tu na fimbo.

Mwisho.