Tuesday, August 30, 2016

MADARASA YAUNGUA MOTO

Na John Gagarini, Kibaha

MADARASA matatu na ofisi ya Mwalimu Mkuu shule ya Msingi Kongowe wilayani Kibaha mkoani Pwani zimeungua na moto ambao ulitokea juzi usiku na kusababisha hasara kubwa.

Akizungumza na Patapata mwenyekiti wa mtaa wa Kongowe Maimuna Jamhuri alisema kuwa moto huo ulitokea Agosti 28 majira ya saa nne usiku ambapo chanzo chake bado hakijafahamika mara moja.

Jamhuri alisema kuwa moto huo ulianzia kwenye ofisi hiyo ambayo ni ya mwalimu mkuu na kuenea kwenye madarasa pamoja na chumba cha kuhifadhia vitabu ambavyo navyo vimeteketea kwa moto huo ambao ulikuwa mkali.

“Moto huo ulizimwa na wananchi ambao walijitokeza kwa wingi ambapo gari la zimamoto lilifika kwa kuchelewa kutokana na kuwa kwenye harakati za kuzima moto sehemu nyingine”, alisema Jamhuri.

Kwa upande wake Diwani wa kata ya Kongowe Iddi Kanyalu alisema kuwa baada ya kutokea moto huo viongozi kadhaa walifika akiwemo mkurugenzi, Mwenyekiti na Injinia wa Halmashauri kwa ajili ya kuangalia athari za moto huo.

Kanyalu alisema kuwa kutokana na makisio ya harakaharaka zinahitajika zaidi ya milioni 50 kwa ajili ya kujenga upya madarasa hayo na ofisi kwani madarasa hayo yameharibika sana na hayafai kwa matumizi wala kufanyiwa ukarabati.

Alisema kuwa kutokana na hali hiyo leo kamati ya maenedeleo ya kata ina kaa kuangalia namna ya kukabiliana na tatizo hilo ambalo limewakumba wanafunzi 200 waliokuwa wanatumia madarasa hayo.

Naye mtendaji wa kata hiyo ya Kongowe Said Kayangu alisema kuwa mwalimu mkuu wa shule hiyo Beatus Lingumbuka alitapa athari kidogo kichwani na mikononi kwani alikuwa kwenye harakati za kujaribu kuokoa baadhi ya vitu wenye ofisi yake.

Kayangu alisema kuwa kutokana na jitihada za wananchi wameweza kuokoa madawati kwenye madarasa hayo ambayo yalikuwa hatarini kuungua lakini hata hivyo waliweza kuyatoa na hakuna dawati hata moja lililoungua

Mwisho.


WAAMUZI KIBAHA WAPATA VIONGOZI WAPYA

Na John Gagarini, Kibaha

CHAMA cha Waamuzi wa Soka Tanzania (FRAT) mkoa wa Pwani kimemchagua  Jeremia Komba kuwa mwenyekiti wa chama hicho kwa kupata kura 15 huku mpinzani wake Kassim Safisha akipata kura tano.

Uchaguzi huo ambao ulifanyika mjini Kibaha na kusimamiwa na mwamuzi mkongwe Hussein Magoti na kuwashiriki waamuzi ambao ni wanachama wa chama hicho cha waamuzi.

Komba alikuwa akichuana na mwamuzi mwenzake Kassim Safisha nakumshinda kwa tofauti ya kura tano hivyo kumfanya Komba kuwa bosi wa waamuzi wilaya ya Kibaha.

Nafasi ya makamu mwenyekiti ilikwenda kwa Sayenda Lubisa ambaye hata hivyo hakuwa na mpinzani na kujipatia kura 17 huku tatu zikiharibika.

Upande wa katibu mkuu Endrew Kayuni alikuwa mshindi kwa kupata kura 15 huku Mohamed Juaji akipata kura tano, nafasi ya katibu msaidizi ilikwenda kwa Hamis Mpangwa ambaye alijinyakulia kura 11 akimshinda Mohamed Msengi aliyepata kura tisa.

Nafasi ya mweka hazina ilikwenda kwa Kassim Naroho aliyepata kura 16 akimshinda Nickson Haule aliyepata kura nne, kwa upande wa mwakilishi wa mkutano mkuu ilikuwa na mgombea mmoja Hamad Seif ambaye alipata kura 19..

Kwa upande wa kamati ya utendaji nafasi tatu walioshinda ni Kasule Ambogo kura 18, Leah Petro kura 16, Gabriel Kinyogoli kura 15 na Sultan Singa kura nane ambapo mwenyekiti mpya Komba aliwataka waamuzi kuwa na mshikamano.

Komba alisema kuwa jambo kubwa ili waweze kufikia malengo ni kuwa nidhamu na kuzingatia sheria kwa kuzitafsiri wawapo uwanjani ili kuondoa malalamiko dhidi yao kwani baadhi wamekuwa wakienda kinyume na sheria za mchezo huo.


Mwisho.



 

ATISHIA KUWABAKA WANAFUNZI


Na John Gagarini, Chalinze

MWENYEKITI wa Halmashauri ya mji wa Chalinze wilayani Bagamoyo mkoani Pwani Said Zikatimu ameutaka uongozi wa Kitongoji Cha Msanga kata ya Talawanda uhakikisha inamkamata mtu ambaye anatishia kuwabaka wanafunzi wa shule ya Msingi Msanga.

Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Talawanda wakati wa ziara yake kuangalia shughuli za maendeleo kwenye kata ya Talawanda alisema kuwa mtu huyo hapaswi kuachwa kwani anahatarisha afya za wanafunzi hao.

Zikatimu alisema kuwa baadhi ya wanafunzi wakike wa shule hiyo tayari wameshatoa taarifa dhidi ya mtu huyo ambaye huwa anawakimbiza kwa nia ya kuwafanyia kitendo hicho na endapo hatakamatwa anaweza kutekeleza azma yake hiyo mbaya.

“Mtu huyo inasemekena yuko Kijijini hapa amekuwa akificha sura yake ili asifahamike amekuwa akijificha kwenye vichaka na kuwakimbiza wanafunzi kwa nia ya kutaka kuwabaka hivyo lazima viongozi muweke mtego ili mumkamate mtu huyo ambaye ni hatari,” alisema Zikatimu.

Alisema kuwa serikali haiwezi kukaa kimya kwa mtu wa namna hiyo ambaye ni hatari kwa wanafunzi na kuwafanya watoto wa kike wasisome kwa amani hivyo lazima hatua za haraka zichukuliwe ili kumdhibiti mapema.

“Lazima mfanye mpango wa kumkamata mtu huyo pia mnaweza kupiga kura ili kumbainisha mtu huyo ambaye baadhi ya watu wanamfahamu na wengine hawamfahamu ambapo kwa kutumia kura anaweza kufahamika kwa urahisi,” alisema Zikatimu.

Aidha alisema kuwa kamati za ulinzi na usalama ya Kijiji na Kitongoji zinapaswa kulishughulikia suala hilo na wananchi kutolifumbia macho kwani mtu huyo anaweza kufanya kweli endapo hatua hazitachukuliwa mapema.

Mwisho.

Thursday, August 11, 2016

MZEE WA BARAZA LA MAHAKAMA APANDISHWA KIZIMBANI KWA RUSHWA

Na John Gagarini, Kibaha

TAASISI ya Kuzuia na Kupamaba na Rushwa (TAKUKURU) Mkoani Pwani imemfikisha mahakamani Mzee wa Baraza la Mahakama ya Mwanzo Maili Moja Kibaha Francis Ndawanje kwa tuhuma za kuomba na kupokea Rushwa ya shilingi 100,000 ili kumsaidia mtuhumiwa kushinda kesi yake.

Mtuhumiwa alisomewa mashitaka kwenye mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha  mbele ya hakimu mkazi wa mahakama ya mkoa wa Pwani  Herieth Mwailolo ambapo kwa upande wa chini ya mwendesha mashitaka kutoka TAKUKURU Mkoa Pwani Sabina Weston.

Akisoma maelezo juu shitaka hilo Weston aliiambia Mahakama kuwa mtuhumiwa huyo anatuhumiwa kutenda makosa hayo mawili kati ya tarehe 3 na 4  Agosti mwaka huu ambapo.

Mahakama iliambiwa kuwa mtuhimwa aliomba rushwa Agosti 3 kwa Omary Hoza ili amsaidie mkewe Mariamu Hoza ambaye ana kesi namba 324 kwenye mahakama hiyo hivyo kumuomba rushwa ya shilingi 100,000.

Ikaelezwa kuwa mtuhumiwa alipokea rushwa siku iliyofuata Agosti 4 alipokea fedha hizo eneo la jirani na Kituo cha Polisi Tumbi jirani na barabara kuu ya Morogoro Maili Moja wilayani Kibaha.

Baada ya kusomwa mashtaka hayo mtuhumiwa alikana tuhuma hizo ambapo upande wa Taasisi hiyo ulisema kuwa hauna pingamizi na dhamana kwa mtuhumiwa ili mradi akamilishe masharti ya dhamana na yuko nje kwa dhamana ya shilingi 500,000 kwa wadhamini wawili kila mmoja.

Hakimu alisema kuwa wadhamini wanapaswa kuhakikisha mtuhumiwa anafika siku ya kesi hiyo ambayo imepangwa kufanyika Agosti 15 mwaka huu.

Mwisho.


MAJAMBAZI YAMUUA KWA KUMPIGA RISASI MWANAMKE ALIKWENDA DUKANI KUWEKA MUDA WA HEWANII

Na John Gagarini, Kibaha

MKAZI wa Mtaa wa Karabaka-Misugusugu kata ya Misugusugu wilayani Kibaha mkoani Pwani Zawadi Halfan (25) ameuwawa kwa kupigwa risasi na majambazi wakati akisubiri kuunganishiwa kifurushi cha muda wa maongezi kwenye simu yake.

 Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Kibaha kamanda wa Polisi mkoani humo Bonaventura Mushongi alisema kuwa marehemu alikuwa amekaa kwenye benchi kwenye kibanda cha huduma za fedha kwa mtandao mali ya Gaitano Joseph (30).

Mushongi alisema kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 9 majira ya saa 2:30 usiku kwenye mtaa huo ambapo marehemu alikuwa akisubiri huduma hiyo kabla ya mauti kumkuta.

“Marehemu hakuwa mlengwa bali walikuwa wamemlenga Yohana Koseja (24) ambaye ni mfanyakazi wa Mchungaji Raphael John ambaye ni mmiliki wa duka la M-Pesa ambapo majambazi hao baada ya kufika walimwamuru Yohana asimame baada ya kufunga duka hilo lakini alikimbia na kukaidi agizo la majambazi hayo ambayo yalikuwa matatu,” alisema Mushongi.

“Kutokana na Yohana kukimbia majambazi hayo yalianza kufyatua risasi ndipo moja ilimpata marehemu sehemu ya mgongoni upande wa mgongoni na kufariki papo hapo ambapo  walikuwa wakifyatua risasi hizo kwa Yohana wakimhisi kuwa alikimbia na fedha bada ya kufunga duka,” alisema Mushongi.

Alisema baada ya majambazi hao kutoka kwenye tukio la kwanza walivamia duka lingine la M-Pesa lililopo pamoja na duka la madawa ya binadamu linalomilikiwa na Renovatus Katabalo (29) mfanyabiashara na mkazi wa Kongowe ambapo duka lake lipo eneo hilohilo la Karabaka na kupora kiasi cha shilingi 300,000.

“Chanzo cha tukio hilo ni kuwania mali na msako unaendelea mkoa mzima ili kuwakamata watuhumiwa ili wafikishwe kwenye vyombo vya sheria kujibu tuhuma zinazowakabili za mauaji ambapo eneo la tukio maganda ya risasi aina ya SMG/SAR,” alisema Mushongi.  

Mwisho.


Monday, August 8, 2016

MWILI WAKUTWA VICHAKANI UKIWA UMEPIGWA RISASI KIDEVUNI


Na John Gagarini, Kibaha

MWILI wa mtu mmoja ambaye jina lake ambalo halikuweza kufahamika mara moja mwenye umri kati ya miaka (33) na (38) umeokotwa huku ukiwa umepigwa risasi chini ya kidevu na kutokea utosini.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mwenyekiti wa mtaa wa Lulanzi kata ya Picha ya Ndege wilayani Kibaha mkoani Pwani Thobias Shilole alisema kuwa marehemu aliuwawa na watu wasiofahamika.

Shilole alisema kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 7 majira ya saa 3 asubuhi kwenye korongo lililopo kwenye shamba linalomilikiwa na Saeed Yeslam Saeed ambapo watoto waliokuwa wakichunga mbuzi ndiyo waliogundua mwili huo na kutoa taarifa kwa wazazi wao ambao walitoa taarifa kwa balozi wao na ndiye aliyemjulisha juu ya tukio hilo.

“Mwili huo ulikuwa na jeraha la risasi chini ya kidevu na kufumua kichwa na mtu huyo anahusishwa na tukio lililofanyika siku kama tatu zilizopita kwa kumpiga risasi kwenye makalio na kumpora fedha mtu aliyetambulika kwa jina la Beno Nyoni (36) mkazi wa Picha ya Ndege ambaye alikuwa akijenga nyumba yake eneo la mtaa wa Lulanzi,” alisema Shilole.

Shilole alisema kuwa watu hao wanaosadikiwa kuwa ni majambazi baada ya kumshambulia walikimbia na kusababisha majeruhi huyo kupelekwa Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Pwani Tumbi lakini ilishindikana na kupelekwa hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu zaidi ambako hadi sasa anatibiwa baada ya kutolewa risasi iliyokuwa mwilini.

“Tunaiomba serikali kumlazimisha mmiliki kulifanyia usafi kwani pori kubwa ambalo limekuwa likitumiwa na wahalifu kwa ajili ya kujificha na kufanya wizi kisha kujificha huko kwani hata mwaka jana tulikuta mtu akiwa amejinyonga hivyo sehemu hiyo usalama wake ni mdogo hasa ikizingatiwa eneo hilo liko umbali wa kilometa 2 toka barabara kuu ya Morogoro,” alisema Shilole.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo kamanda wa polisi mkoani Pwani Bonaventura Mushongi alisema kuwa baada ya kuangaliwa marehemu alikutwa na jeraha kidevuni na kichwani huku mwili wake ukianza kuharibika.

Msuhongi alisema kuwa pembeni yake kulikutwa kofia ya kuficha sura ganda la risasi aina ya SMG/SAR na nyaraka mbalimbali ambazo ni ramani za nyumba mbili, stakabadhi za kibali cha ujenzi, hati ya hukumu ya shauri la mgogoro wa ardhi.

Alisema vitu vingine vilivyokutwa ni kadi za biashara, kadi za benki za posta, NBC, Posta na CRDB, kadi ya kupigia kura na leseni ya udereva vyote vikiwa na majina ya Nyoni ambaye ni mfanyabiashara wa Picha ya Ndege.

“Vitu hivyo ni vya Majeruhi huyo aliyofanyiwa tukio hilo la unyanganyi wa kutumia silaha na kupora mali na walifika kwenye kwenye hilo kwa lengo la kugawana mali hizo lakini inaonyesha walihitilafiana ndipo walipompiga marehemu risasi na kumuua kisha walimpekekua kwani mifuko ya suruale yake ilkuwa iko nje na hakukutwa na kitambulisho chochote na mwili umehifadhiwa hospitali ya Tumbi,” alisema Mushongi.

Naye diwani wa kata hiyo Robert Machumbe alisema kuwa shamba hilo lilikofanyika tukio hilo lina pori kubwa sana hivyo ni vema Halmashauri likafanya utaratibu kama mmiliki kashindwa litolewe kwa mtaa ili kuweza kujengwa huduma za jamii kama shule, zahanati na huduma nyingine kwani kwa sasa limekuwa hatari kwa wananchi.

Mwisho.       


  



  




WATU ZAIDI 20 WANUSURIKA KUUNGUA MOTO

Na John Gagarini, Kibaha

FAMILIA nane zenye watu zaidi ya 20 kwenye mtaa wa Mharakani kata ya Picha ya Ndege wilayani Kibaha mkoani Pwani zimenusurika kufa baada ya moto kutokea wakati wamelala.

Wakizungumza na mwandishi habari hizi wahanga wa tukio hilo la moto huo ambao ulitokea Agosti 7 usiku kuamkia Agosti 8 majira ya saa 6;30 usiku walisema kuwa watu waliokuwa jirani na nyumba yao ndiyo waliowafahamisha juu ya moto huo ambao unasadikiwa ulianzia kwenye moja ya maduka yaliyo kwenye nyumba hiyo.

Emanuel Mhina alisema kuwa wao walikuwa wamelala na ilipofika majira ya saa saba kasoro waliamshwa na watu na walipoamka walikutana na moto mkubwa ambao hawakujua ulianza saa ngapi ndipo walipoanza kujiokoa.

“Tunamshukuru mungu tumenusurika licha ya mali zetu zote kuteketea kwa moto ambao ulianzia kwenye moja ya maduka ambayo yameungana na nyumba hii ambayo tulikuwa tunaishi,” alisema Mhina.

Naye Said Juma alisema kuwa moto huo umewapa hasara kubwa kwani amepoteza vitu karibu vyote na kufanikiwa kuokoa vichache hali ambayo inamfanya aanze upya maisha.

Kwa upande wake mwenyekiti wa mtaa huo Yahaya Abdala alisema kuwa wananchi, Zimamoto pamoja Jeshi la polisi walifanikisha kuzimwa moto huo ambao ulisababisha vitu vote kuteketea lakini hakuna mtu aliyedhuriwa na moto huo zaidi.

Naye diwani wa kata ya Picha ya Ndege Robert Machumbe alisema kuwa wahanga hao hawakuweza kuokoa kitu kwani vitu vyote viliteketea kwa moto huo uliokuwa mkali.

Machumbe alisema kuwa baada ya tukio hilo walichangisha kwa majirani na kupata kiasi cha shilingi 80,000 ambazo ziligawanywa kwa wahanaga hao angalau wapate fedha kwa ajili ya chakula na wahanga hao wamehamia kwa ndugu jamaa na marafiki zao wakiangalia namna ya kutafuta nyumba nyingine.

Katika hatua nyingine mtoto mwenye umri kati ya miaka minne na nusu amenusurika kufa baada ya mama yake kumwacha kwenye nyumba huku akiwa amemfungia ndani na yeye kwenda kusikojulikana ambapo kati ya majirani waliounguliwa nyumba ambaye ni mwanajeshi wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) alijitosa na kumwokoa mtoto huyo.

Mwisho.