Tuesday, July 26, 2016

PWANI YATAKIWA KUMALIZA ZOEZI LA WATUMISHI HEWA


Na John Gagarini, Kibaha
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Angella Kairuki ameutaka uongozi wa mkoa wa Pwani kuhakikisha unamaliza kushughulikia tatizo la watumishi hewa haraka.
Mkoa huo una jumla ya watumishi hewa 272 ambao wamebainika na kuitia serikali hasara ya shilingi bilioni 1.4 kufuatia zoezi la uhakiki wa watumishi hewa kufanyika kutokana na agizo la Rais Dk John Magufuli.
Kairuki aliyasema hayo juzi mjini Kibaha wakati wa mkutano wake na uongozi wa mkoa huo, wakurugenzi wa Halmashauri na Miji za mkoa huo pamoja na watumishi wa ofisi ya mkuu wa mkoa ili kujua changamoto zinazowakabili watumishi wa Umma.
Alisema kuwa kwa kuwa tayari agizo la Rais lilishatoka tangu mwezi Machi mwaka huu kinachotakiwa ni kuwachukulia hatua wahusika baada ya kuwabaini na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria kujibu tuhuma zinazowakabili na si kuwaacha tu.
“Rais alitoa maagizo kubainisha watumishi hewa na baada ya kubainika wanapaswa kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kuwafikisha mahakamani kwani wamefanya makosa ya kuiibia serikali hivyo hakuna sababu ya kutowachukulia hatua stahiki,” alisema Kairuki.
Aidha alisema kuwa hatua stahiki zichukuliwe mapema ikiwa ni pamoja na kurekebisha taarifa za watumishi hao ikiwa ni pamoja na kusitisha mishahara yao kabla ya malipo yamwezi Agosti ili tatizo hilo lisije likaendelelea.
“Pia nataka kusiwe na data chafu ambazo Halmashauri ziliweka kwa watumishi hao ambazo ni pamoja na kutopandishwa madaraja, malipo kwa watu ambao wana umri zaidi ya miaka 60 na watumishi kutokuwepo kwenye vituo vyao vya kazi huku wakiendelea kulipwa,” alisema Kairuki.
Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo alisema kuwa mkoa huo una watumishi 16,156 huku ukiwa na upungufu wa watumishi 3,306 na watumishi hewa waliobainika ni 272 kwenye Halmashauri saba za mkoa huo ambazo ni Kibaha Mjini, Kibaha, Mafia, Rufiji, Mkuranga, Kisarawe na Bagamoyo.
Ndikilo alisema kuwa mkoa unalishughulikia suala la watumishi hewa ambapo wanashirikiana na Jeshi la Polisi pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa na kusema kuwa zoezi hilo ni gumu hivyo inabidi walifanye kwa umakini ili lisije likaleta matatizo na watalikamilisha mapema.

Mwisho.

OFISI YA MKUU WA MKOA INAKABILIWA NA UHABA WA MAGARI


Na John Gagarini, Kibaha
MKUU wa mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo amesema kuwa mkoa wake unakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa magari hali ambayo inawafanya kuazima magari kwenye wilaya katika shughuli za kikazi katika mkoa huo.    
Aliyasema hayo juzi mjini Kibaha wakati wa mkutano wake na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Angella Kairuki alipokuwa akizungumza na watumishi wa ofisi ya mkuu wa mkoa na wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya na Miji za mkoa huo.
Ndikilo alisema kuwa changamoto hiyo kwa wataalamu wa mkoa ni kubwa hali ambayo inawafanya wafanye kazi kwenye mazingira magumu hasa kwenye maeneo ya mbali ikiwa ni pamoja na kwenye Halmashauri za mkoa huo.
“Waziri mkoa una changamoto kubwa ya ukosefu wa magari ikiwemo ofisi yangu na wataalamu wangu inapofika hatua ya kwenda kwenye maeneo ya mbali inakuwa mtihani mkubwa kwani inatubidi tuazime magari ya kwenye wilaya kwa ajili ya kufika baadhi ya maeneo,” alisema Ndikilo.
Alisema kuwa hata mkuu wa wilaya ya Kibaha gari alilonalo ni bovu ambapo hivi karibuni alipata ajali ya kuligonga gari jingine kutokana na breki kugoma naye mkuu wa wilaya ya Mkuranga naye gari lake siyo zuri sana, wilaya Mpya ya Kibiti yenyewe haina gari kabisa.
“Usafiri kwa mkoa wetu ni changamoto kubwa hivyo tunaomba mtusaidie ili katika bajeti ijayo mtufikirie kwa kutupatia usafiri ili tuweze kutekeleza majukumu yetu vizuri ili kukabiliana na changamoto hii ambayo inatupa wakati mgumu inapofikia suala la usafiri,” alisema Ndikilo.
Aidha alisema kuwa changamoto nyingine ni ukomo wa bajeti ambayo kwa mwaka 2014-2015 ulishuka kwa asilimia 40 ikilinganishwa na bajeti iliyopita, fedha za maendeleo kuchelewa, madeni ambayo yamefikia milioni 152, watumishi kuhama kutafuta maslahi mazuri, vitendea kazi na upandishwaji wa madaraja.
Akijibu baadhi ya hoja Waziri Kairuki alisema kuwa Wizara inazifanyia kazi changamoto hizo na pale fedha zitakapopatikana itaboresha mazingira ya watumishi ili wafanye kazi vizuri kwani serikali inawathamini wafanyakazi na haitaki wafanye kazi katika mazingira magumu.
Kairuki alisema kuwa juu ya maofisa utumishi waliokuwa wakilipa mshahara watumishi hewa itabidi wawajibike ambapo kwa sasa inawsafuatilia kwani inaonekana nao walichangia kulipa mishahara kwa watumishi ambao hawakustahili.

Mwisho.

VIONGOZI WAKATAA KUKABIDHI OFISI ZA SOKO


Na John Gagarini, Kibaha
UONGOZI wa zamani wa soko la mkoa la Maili Moja wamegoma kuwakabidhi ofisi uongozi mpya uliochaguliwa mbele ya mkuu wa wilaya ya Kibaha Asumter Mshama wakidai kuwa taratibu za uchaguzi huo zilikiukwa.
Makabidhiano ya ofisi ambayo yalikuwa yakisimamiwa na diwani wa kata ya Maili Moja Theodory Joseph, ofisa mtendaji wa mtaa wa Maili Moja John Dotto, mwenyekiti mpya wa soko Ramadhan Maulid na katibu Elias Kisandu yalishindikana kutokana na uongozi wa zamani kutoridhia jinsi walivyoondolewa madarakani
Akizungumza baada ya makabidhiano ya soko hilo kushindikana katibu wa zamani wa soko hilo Muhsin Yusuph alisema kuwa hawawezi kukabidhi mali za soko hilo bila ya taratibu kwani soko hilo lilikuwa liko kwenye mfumo wa ushirika.
Yusuph alisema kuwa taratibu za ushirika zinafahamika hivyo sisi hatuwezi kuwakabidhi uongozi mpya bila ya taratibu ikiwa ni pamoja na kufanya uchaguzi chini ya mrajisi wa vyama vya ushirika.
“Huu ni ushirika na ushirika una taratibu zake sasa sisi hatuwezi kuukabidhi uongozi mpya bila ya kufuata utaratibu kwani uchaguzi haukufanyika kwa kufuata katiba ya ushirika ambapo mrajisi ndiye aliyetakiwa kuwa msimamizi,” alisema Yusuph.
Alisema kuwa siku walipochaguliwa viongozi wapya ilikuwa ni mkutano na mkuu wa wilaya kujua changamoto zinazotukabili lakini haukuwa mkutano wa uchaguzi ambao unakuwa ni maalumu na unasimamiwa na mrajisi wa vyama vya ushirika.
Mwenyekiti wa kamati ya makabidhiano diwani Theodory Joseph alisema kuwa wao walikuwa wakikamilisha taratibu kwani uchaguzi ulifanyika na uongozi huo wa zamani kushindwa na kutakiwa kuwakabidhi ofisi viongozi wapya.
Joseph alisema kwa kuwa wamekataa watawasiliana na ngazi zinazohusiaka kwa taratibu zaidi lakini wao hawana la zaidi kwani kila kitu kilikuwa kinajulikana hivyo watasubiri taratibu zingine.
Kwa upande wake mwenyekiti mpya Ramadhan Maulid alisema kuwa kwa kuwa uongozi uliopita umegoma kukabidhi ofisi watawasiliana na mkuu wa wilaya ili kujua nini cha kufanya juu ya hatua hiyo.
Soko hilo lilikuwa likiendeshwa kwa taratibu za ushirika ambapo kuna zaidi ya wafanyabiashara zaidi ya 500 ambapo baadhi ni wanachama wa ushirika na wengine si wanachama wa ushirika ambapo mkuu wa wilaya alishauri ni vema uongozi ukawa tofauti kati ya ule wa ushirika na soko ili kuondoa muingiliano wa majukumu.

Mwisho.  

RC AKATAA KUSIKIA HALMASHAURI IMEPATA HATI CHAFU

Na John Gagarini, Kibaha
MKUU wa Mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo Ndikilo amesema kuwa kuanzia sasa hataki kusikia Halmashauri za Miji au wilaya za mkoa huo kuwa zimepata hati chafu.
Sambamba na hilo amezitaka Halmashauri hizo kuwatumia wakaguzi wa hesabu wa ndani ili kuweka mambo yao katika mpangilio mzuri ili kuondokana na hati chafu ambazo zimekuwa zikiziandama baadhi ya Halmashauri hizo.
Ndikilo aliyasema hayo wakati wa kikao na Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya na Miji za Mikoa hiyo ambao waliapishwa hivi karibuni baada ya kuteuliwa na Rais Dk John Magufuli.   
Alisema kuwa taarifa za hesabu za kila Halmashauri zinapaswa kupelekwa kwa wakati kulingana na utartibu uliowekwa na serikali pia hoja za mkaguzi mkuu wa serikali (CAG) zijibiwe mapema.
“Kuanzia sasa sitaki kusikia Halmashauri imepata hati chafu kutokana na uzembe kwani wakati mwingine inatokana na kushindwa kuonyesha risiti ambazo ni za manunuzi jambo ambalo liko ndani ya uwezo wenu hakuna sababu ya kuharibu sifa za utendaji kazi wenu kwa mambo madogomadogo,” alisema Ndikilo.
Aidha alisema kuwa jambo jingine ambalo wakurugenzi wa halmashauri tisa za mkoa huo wanapaswa kulizingatia ni kutekeleza miradi kwa thamani halisi ya fedha na si kutekeleza miradi hiyo chini ya kiwango.
“Mnapaswa kutekeleza miradi ya maendeleo ya wananchi kwa wakati na kama mnaona kuna mtendaji ambaye anafanya vibaya hakuna sababu ya kumuonea haya dawa ni kumwondoa,” alisema Ndikilo.
Mkuu huyo wa mkoa wa Pwani alisema kuwa wakurugenzi hao wanapaswa kukuisanya mapato kwa nguvu kwani makusanyo makubwa ndiyo yatakayoifanya Halmashauri kuweza kuendesha shughuli zake ikiwa ni pamoja na kuchangia uchumi wa wananchi na Taifa.
“Watu wanaohusika na vyanzo vya mapato wanapaswa kuwa wabunifu wa kuanzisha vyanzo vipya na siyo kuwa na vyanzo vilevile miaka yote pia wavifanyie uchambuzi ili kutokusanya mapato chini kutokana na taarifa za wazabuni ambao wamekuwa wakiidanganya Halmashauri juu ya mapato huku mengine yakiingia mifukoni mwao,” alisema Ndikilo.
Kwa upande wake mkurugenziwa Halmashauri ya Mji wa Kibaha Jenifa Omolo alisema kuwa amejipanga vyema kutekeleza majukumu ya serikali kama walivyokula kiapo ili kuboresha utoaji huduma kwa wananchi pamoja na ukusanyaji wa mapato.
Naye Tatu Seleman mkurugenzi wa Halmashauri ya Kibaha alisema kuwa atahakikisha anashirikiana na wananchi katika kutekeleza majukumu ya Halmashauri kwani ushirikishwaji utasaidia kupatikana kwa maendeleo hasa kupitia kwenye huduma za kiajamii.

Mwisho.

JAKAYA AKARIBISHWA KISHUJAA BAGAMOYO

Na John Gagarini, Bagamoyo

RAIS Mstaafu wa Awamu ya Nne Dk Jakaya Kikwete amesema kuwa hakuna kitu kilichokuwa kikimpa wakati mgumu kama kushindwa katika uongozi wake wa miaka 10 iliyopita.

Aliyasema hayo juzi mjini Bagamoyo wakati wa sherehe iliyofanyika kwenye ukumbi wa Chuo cha Sanaa Bagamoyo (TASUBA) ya kumkaribisha nyumbani baada ya kukabidhi uongozi kwa mwenyekiti mpya wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dk John Magufuli mjini Dodoma hivi karibuni.

Dk Kikwete alisema kuwa hali ya kushindwa ilikuwa ikimpa wakati mgumu na kujiona kuwa kama endapo angeshindwa basi ange waangusha Wanabagamoyo na Pwani nzima.

“Kila nilipokuwa nikifikiria kushindwa kwenye jambo lolote la uongozi wangu kwa nchi au kwenye Chama lakini namshukuru Mungu kwani tulifanikiwa sana katika suala la maendeleo kwa nchi nzima kwani huwezi ukapendelea sehemu uliyotoka au ukawanyima maendeleo ni kitu ambacho hakiwezekani,” alisema Dk Kikwete.

Alisema kuwa wakati fulani alikuwa akilalamikiwa na baadhi ya wabunge kuwa anapendelea Bagamoyo jambo ambalo si la kweli ambapo walidai kuwa amehamisha fedha za ujenzi wa barabara na kuzihamishia kwenye ujenzi wa barabara ya Msata Bagamoyo.

“Hali kama hiyo Ilikuwa inanipa wakati mgumu kwnai kila sehemu inataka maendeleo na nisingeweza kutofanya maendeleo kwa watu wa Bagamoyo kwani hata wao wanahitaji maendeleo kama sehemu nyingine,” alisema Dk Kikwete.

Aidha alisema kuna wakati ilibidi ahamishe fedha kutoka Bagamoyo na kufanya ujenzi kwenye maeneo ya Geita-Sengerema hadi Usagara wakati huo waziri wa Ujenzi alikuwa Basil Mramba lakini hawakuliona lakini anasema alishukuru Mungu kwani ujenzi kwenye barabara hizo ulifanyika vizuri.

“Namshukuru Mungu katika uongozi wangu tulifanya kazi na kuleta maendeleo makubwa na tumeiacha nchi mahali pazuri na salama kwnai imetulia licha ya mwaka 2015 wakati wa uchaguzi ambapo baadhi ya watu walisema kuwa Rais gani hata hafanyi mpango wa kubadilisha katiba ili aendelee kukaa madarakani kwani watu walishindana lakini hawakupigana wala kumwaga damu na uchaguzi ulipokwisha maisha yaliendelea salama kabisa,” alisema Dk Kikwete.

Alibainisha kuwa Watanzania wanapaswa kumuombea Rais Dk John Magufuli ili aweze kuleta maendeleo kwani ni mpenda maendeleo hivyo lazima asaidiwe aweze kuleta maendeleo ya watu.

Akizungumzia kuhusu Chama alisema kuwa kiko vizuri na hakuna kinachoiweza CCM kwani anajua hakuna chama cha kuweza kukishinda kwani havina uwezo ikizingatiwa ni chama kikubwa na viongozi wake ni imara.

Kwa upande wake mwenyekiti wa CCM wilaya ya Bagamoyo Maskuzi alisema kuwa katika uongozi wake alifanikiwa kuleta maendeleo makubwa kuanzia kwenye elimu na mpango wa shule za kata sasa umeonyesha mafanikio ambapo shule hizo kwa mwaka huu zimeongoza kwenye matokeo.

Maskuzi alisema kuwa umeme ni moja ya mafanikio ambapo kwa sasa umefika hadi vijijini kupitia mpango wa Umeme Vijijini REA, ujenzi wa barabara na masuala mengine ya kimaendeleo kwenye nchi ambayo ni ya kujivunia.

Katika sherehe hiyo ambayo ilihudhuriwa na familia ya Dk Kikwete alipewa zawadi mbalimbali ikiwa ni pamoja na mifugo kama vile ngombe, mbuzi, kuku, bata, mavazi ya jadi na vitu mbalimbali ambavyo vilitolewa na wananchi wa mkoa wa Pwani.


Mwisho.

BAGAMOYO YAGUNDUA WTUMISHI HEWA ZAIDI 83 WAGUNDULIKA

 Na John Gagarini, Bagamoyo

WILAYA ya Bagamoyo mkoani Pwani imebaini uwepo wa watumishi hewa 83 na kuifanya wilaya hiyo kwa sasa kuwa na watumishi hewa 91 ambapo wakati zoezi hilo linaanza lilibaini watumishi hewa nane tu.

Akizungumza wakati wa zoezi la kuzindua madawati 300 yaliyotengenezwa na wadau mbalimbali na kuzinduliwa na mkuu wa mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo, mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Majid Mwanga alisema kuwa watumishi hao wamebainika baada ya kuundwa kikosi kazi kuchunguza watumishi hao.

Mwanga alisema kuwa awali baada ya agizo lililotolewa na Rais Dk John Magufuli kulibainika watumishi hewa nane lakini sasa idadi hiyo imeongezeka baada ya kufanywa kwa kina.

Alisema kuwa kikosi kazi kilichoundwa na watu sita wanaoundwa na kamati ya ulinzi na usalama na kugundua watumishi hewa wengi ni kutoka idara ya elimu hasa kwenye shule za msingi na sekondari.

“Watumishi wengi ni walimu ambao wengi wamekwenda masomoni bila ya kuaga na hawana ruhusa na baadhi walishaacha kazi lakini cha kushingaza mishahara yao ilikuwa inaingizwa kama kawaida jambo ambalo ni kinyume cha taratibu,” alisema Mwanga.

Aidha alisema kuwa tatizo kubwa linaonyesha ni idara ya elimu kushindwa kutoa maamuzi ya haraka mara walimu wanapoomba kwenda masomoni hivyo huamua kuondoka kienyeji.

“Watumishi wengine walibainika kuwa hawana vielelezo vyo vyote vya vya juu ya ajira zao na tunaomba hatua kali zichukuliwe kwa watumishi hao ambao ni hewa na wamekuwa wakilipwa mishahara huku hawafanyi kazi wanachukua mishahara ya bure,” alisema Mwanga.

Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo alisema kuwa kutokana na kubainika watumishi hao 83 hewa wilayani Bagamoyo kwa sasa mkoa wamefikia watumishi hewa 272.

Ndikilo alisema kuwa zoezi hilo bado linaendelea na kukipongeza kikosi kazi cha wilaya hiyo kuweza kuwabaini watumishi hao hewa na itaendelea kuchunguza hadi kuondoa kabisa suala hilo.


Mwisho.

Tuesday, July 5, 2016

WAFUGAJI WATAKA WASIONDOLEWE CHAURU

Na John Gagarini,Bagamoyo

WAFUGAJI wanaoishi kwenye Kitongoji cha Msigala Kijiji cha Visezi kata ya Ruvu wilayani Bagamoyo mkoani Pwani wamepinga kupelekwa Kitongoji cha Mnanyama kutokana na kutokuwa na huduma za kijamii.

Wakizungumza na waandishi wa habari Kijijini hapo wamesema kuwa eneo walilopangiwa halina huduma hizo ndiyo sababu ya wao kuendelea kukaa hapo walipo sasa.

Akizungumzia juu ya hali hiyo Lupina Kirayo alisema kuwa chanzo cha wao kutakiwa kuondoka ni kutokana na madai ya wakulima wa shamba la Chama Cha Ushirika wa Umwagiliaji Ruvu (CHAURU) kuwa ngombe wao wamekuwa wakiingia kwenye mashamba na kuharibu mazao.

Kirayo alisema kuwa wao wako hapo kwa muda mrefu lakini wanashangaa kutakiwa kuondoka na kwenda Mnanyama ambako hakuna huduma hyoyote ya Kijamii.

“Zamani kijiji hicho kiliweka njia kwa ajili ya ngombe kupita kwenda kunywa maji mtoni lakini wakulima walifunga njia ya kupita ngombe na ndiyo chanzo cha migogoro ya wakulima na wafugaji ilipoanza,” alisema Kirayo.

Alisema kuwa tatizo kubwa linatokana na baadhi ya wafugaji wanaoleta mifugo toka maeneo ya mbali kwa ajili ya kwenda kuuza ngombe kwenye mnada wa Ruvu ndiyo wamekuwa wakiingiza mifugo kwenye shamba hilo la ushirika wakitafuta maji.

Aidha alisema kuwa wao kama wenyeji wa Kitongoji hicho wako makini na mifugo yao ambapo wakati mwingine wachungaji wao wamekuwa wakishindwa kuwadhibiti ngombe na kuingia kwenye shamba hilo ambapo wamekuwa wakiwafukuza wachungaji wazembe ili kuondoa migongano na kuomba radhi na kutaka kuwe na maridhiano na kuangalia njia nzuri ya kudhibiti mifugo isiingie kwenye shamba hilo lakini siyo kuwaondoa hapo.

Naye Elizabeth Meja amesema kuwa yeye alizaliwa hapo na kipindi cha nyuma wamekuwa wakiishi vizuri lakini kwa sasa wanaambiwa waondoke ambako kule huduma ya afya hakuna ambapo kwa akinamama hasa pale wanapokuwa wajawazito huhitaji kupata huduma za mara kwa mara.

Meja alisema kuwa sehemu wanayotaka kuhamishiwa kuna umbali wa km 20 hadi kufika kwenye huduma za afya na hata watoto wanapozaliwa hupaswa kupelekwa kliniki lakini kutokana na umbali huo itakuwa ni matatizo pia watoto wao kwa sasa licha ya kutumia masaa zaidi ya mawili kwenda shule ni karibu tofauti na wakienda kule hatapata fursa ya kusoma kutokana na umbali huo.

“Hata suala la maji ni tatizo kwani hapa tunatumia maji ya shilingi 20,000 kwa siku lakini kule tunakotakiwa twende maji hakuna kabisa hivyo ni vema wakaweka miundombinu kwanza ili huduma kama hizo zipatikane,” alisema Meja.

Naye mwenyekiti wa kitongoji hicho cha Msigala Otiniel Mbura alisema kuwa tayari serikali iliamua wafugaji hao kwenda huko ili kuondoa migogoro inayojitokeza kila wakati.

Mbura alisema kuwa ni vema wafugaji hao wakenda kwanza na serikali itawapelekea huduma kuliko hivi sasa wanavyokataa kwenda huko walikopangiwa.