Monday, May 23, 2016

VIJANA WAILILIA SERIKALI KUWAINUA KIUCHUMI

Na John Gagarini, Kisarawe

SERIKALI imeombwa kusaidia vikundi vya vijana vinavyopata mafunzo mbalimbali ya kuwainua kiuchumi ili waweze kujiajiri wakiwa Vijijini badala ya kukimbilia Mijini.

Akisoma risala ya wahitimu mbele ya mgeni rasmi ambaye ni kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa George Mbijima kwenye Kijiji cha Kibuta wilayani Kisarawe, Mariam Christopher alisema kuwa mafunzo hayo yatawawezesha kuweza kukabili mazingira wanayoishi huko huko waliko kuliko kukimbilia mjini kutafuta ajira.

Christopher alisema kuwa masomo waliyojifunza ni ya ufundi kwa vijana wa kata ya Kurui kupitia mradi wa kuwajengea uwezo vijana (YEE) unaosimamiwa na shirika lisilokuwa la kiserikali Plan International wilaya ya Kisarawe.

“Tunashukuru wafadhili wetu kwani tumeweza kujifunza mambo mengi ya ufundi tunaamini yatatusaidia tukiwa huku huku bali kikubwa ni Halmashauri kutuwekea mazingira mazuri ya kufanya kazi ili tuisaidie jamii ya Kijijini hasa ikizingatiwa nako kuna hitaji maendeleo,” alisema Christopher.

Alisema kuwa mafunzo hayo wameyapata kwa kina katika fani mbalimbali za upambaji, mapishi, udereva, ushonaji na utengenezaji wa mapambo na wanatarajia kuboresha shughuli hizo Vijijini ili kuleta maendeleo kwa familia zao na wao binafsi.

Aidha alisema kuwa mafunzo hayo yanafadhiliwa na Eu, Vso, Uhiki, Veta na Plan International wilayani humo na yanatekelezwa kwenye kata Sita za Kibuta, Kisarawe, Manerumango, Msimbu, Kurui na Marumbo na yanatarajiwa kuwafikia vijana 1,000 kwa kipindi cha miaka mitatu.

Kwa upande wa kiongozi wa mbio za mwenge Kitaifa George Mbijima alisema kuwa Halmashauri inapaswa kuwatengenea vijana asilimia tano ya mapato yao kwa ajili ya kuwakopesha vijana kwani suala hilo liko kisheria na wanapaswa kutekeleza ili kuwajenga vijana kiuchumi, Mwenge huo leo unatarajiwa kukimbizwa wilaya ya Rufiji.

Mwisho. 





SERIKALI KUWAWEKEA MAZINGIRA MAZURI WAWEKEZAJI

Na John Gagarini, Kisarawe
SERIKALI itaendelea kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji wa ndani na nje ambao watafuata taratibu za nchi ili kuongeza pato la taifa kupitia sekta ya uwekezaji ambayo kwa sasa inakuwa kwa kasi kwenye mikoa mbalimbali.
Hayo yalisemwa na kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa George Mbijima alipokuwa akiweka jiwe la msingi kwenye Bandari ya Nchi Kavu inayojengwa kwenye Kijiji cha Kazimzumbwi wilayani Kisarawe mkoani Pwani.
Mbijima alisema kuwa nchi kwa sasa iko kwenye kipindi cha utekelezaji  kwa vitendo sera ya uwekezaji ili iweze kuleta manufaa kwa wananchi pamoja na serikali ili iweze kuwaletea maendeleo wananchi kupitia uwekezaji.
“Serikali inathamini mchango wa wawekezaji kwani wana nafasi kubwa ya kuleta maendeleo kwa wananchi pamoja na nchi lakini kikubwa ni kuwa wazi wakati wa kufanya taratibu za uwekezaji ili kuondoa malumbano yanayojitokeza baina ya wananchi na wawekezaji,” alisema Mbijima.
Alisema kuwa baadhi ya wawekezaji wamekuwa wakikiuka taratibu za uwekezaji kwa kutokuwa wazi wakati wakufanya michakato ya uwekezaji kwani wanapaswa kuwa wazi kwa pande zinazohusika ili kuondoa mikanganyiko.
“”Wawekezaji wanapaswa kufuata sheria za nchi zilizowekwa ili faida inayopatikana iweze kuleta manufaa kwa wananchi wanaozunguka maeneo ya uwekezaji hivyo wanapaswa kushirikiana na wananchi ili kuondoa migogoro isiyo na tija kwa uwekezaji”,  alisema Mbijima.
Aidha alisema kuwa serikali inatoa ushirikiano na wawekezaji kwnai mbali ya kutoa ajira kwa wananchi pia serikali inapata mapato yake kupitia sekta hiyo ili iweze kuendesha shughuli zake kupitia kodi na ushuru mbalimbali.
Kwa upande wake mkurugenzi wa Kampuni ya DSM Corridor Group  Sada Shaban alisema kuwa ujenzi huo wa Bandari kavu ulianza 2013 na kukamilika mwaka huu kwa baadhi ya vitengo ukiwa umegharimu kiasi cha shilingi bilioni 7.5 ambapo gharama iliyobakia ni kiasi cha shilingi bilioni 38 hadi kukamilika kwake.
Shaban alisema kuwa eneo hilo litakuwa ni hifadhi ya bidhaa mbalimbali ikiwa ni pamoja na maghala ya mazao mbalimbali, madini na mizigo ya kila aina na itasaidia kupunguza msongamano barabarani kwani ikitoka hapo inapakizwa kwenye treni ambayo iko jirani na bandari hiyo. Mwenge huo ukiwa wilayani Kisarawe ulizindua na kuweka mawe ya msingi kwenye miradi yenye thamani ya shilingi bilioni 6.5 leo mwenge unakimbizwa wilayani Rufiji.
Mwisho.





Friday, May 20, 2016

WANANCHI KUEPUKANA NA ADHA YA UKOSEFU WA MAJI

Na John Gagarini, Kibaha
WANANCHI wa Mitaa ya Viziwaziwa na Sagale wilayani Kibaha mkoani Pwani wataondokana na adha ya ukosefu wa Maji baada ya mradi mkubwa wa maji wenye thamani ya shilingi 517,110,110 kuzinduliwa na kiongozi wa mbio za Mwenge Kitaifa George Mbijima.
Mradi huo utakaohudumia wakazi 1,482 umekamilika baada ya Halmashauri kuomba maji kwenye bomba kuu la Mamlaka ya Maji Safi na Maji taka Dar es Salaam (DAWASCO) la Ruvu Juu baada ya majaribio ya kuchimba visima vya ardhini ambavyo havikupata maji.
Akielezea juu ya mradi huo katibu wa Jumuiya ya Watumiaji Maji wa Ziwaziwa na Sagale (SAVI) Abdulrahman Mango alisema kuwa mradi huo ni moja ya miradi ya Maji na Usafi wa Mazingira ni moja wapo ya mitaa minne iliyopo kwenye kata ya Viziwaziwa ambako katika Halmashauri kwenye miradi hiyo kuna jumla ya mitaa 13.
“Kabla ya kuwa na mradi huu tulikuwa tunategemea maji ya visima vya asili ambavyo ni vya msimu ambapo maji tuliyokuwa tukiyatumia yalikuwa siyo safi wala salama na inapofikia wakati wa kiangazi tunakwenda kuchota maji kwenye mtaa jirani wa Kwa Mfipa uliopo kilomita saba na kuwachukulia wananchi muda mwingi kutafuta maji badala ya kufanya shughuli za maendeleo,” alisema Mango.
Mango alisema kuwa mradi huo una husisha ujenzi wa tanki la chini lenye ujazo wa lita 50,000, ujenzi wa chumba kwa ajili ya kuweka pampu, uchimbaji wa mitaro na ulazaji wa mabomba, tanki la juu lenye ujazo wa lita 50,000, ujenzi wa vituo 10 vya kuchotea maji na ujenzi wa mifumo matanki ya uvunaji wa maji ya mvua.
“Ujenzi wa miundombinu ya umekamilika na kwa sasa vituo tisa kati ya 10 vinatoa huduma ya maji kwa mgao wa DAWASCO siku mbili kwa wiki na unasimamiwa na SAVI na jamii huchangia shilingi 100 kwa ndoo ya lita 20 ambapo fedha hupelekwa benki na hadi sasa kuna akiba ya shilingi 950,000 na fedha zinazopatikana hutumika kwa ajili ya kulipia bila ya umeme, kufanya ukarabati mdogomdogo, uendeshaji wa ofisi na kulipa bili ya DAWASCO,” alisema Mango.
Aidha alisema kuwa mradi huo umechangiwa na wananchi kiasi cha shilingi milioni 12 kwa kutoa maeneo yao na kupitisha mabomba na kujenga vituo vya maji vya jamii na kutekeleza azma ya Rais Dk John Magufuli ya kumtua mama ndoo kichwani.
Kwa upande wake kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa Mbijima alisema kuwa azma ya serikali ni kuwapunguzia kero wananchi kwa kupata huduma za kijamii karibu ili wapate muda mwingi wa kufanya shughuli za maendeleo na si kutumia muda mwingi kutafuta huduma.  

Mwisho.

MWENGE HAUNA ITIKADI

Na John Gagarini, Kibaha
IMEELEZWA kuwa dhana ya Mwenge wa Uhuru si itikadi ya chama au watu wa aina fulani bali ni kuhamasisha maendeleo ya wananchi kupitia miradi ambayo imetokana na nguvu zao.
Hayo yalisemwa wilayani Kibaha na kiongozi wa mbio za Mwenge Kitaifa George Mbijima alipokuwa akizindua bweni la wasichana kwenye Shule ya Sekondari ya Zogowale wakati mwenge huo ukikimbizwa wilayani humo.
Mbijima alisema kuwa Mwenge wa Uhuru ni alama ya maendeleo katika nchi ambapo mwasisi wake Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliutumia kama ishara ya maendeleo.
“Mwenge ni alama muhimu katika maendeleo ya nchi kwani kila mahali ulipopita umeacha alama ya maendeleo na lengo lake ni kuhamasisha watu kuwa wanapaswa kuwajibika ili kuleta mafanikio kwa mtu mmoja mmoja na jamii nzima kwa jumla,” alisema Mbijima.
Alisema kuwa watu wanaobeza Mwenge hawajui historia ya nchi na umuhimu wa mwenge ambacho umezindua na kufungua miradi mingi ya maendeleo ambayo imewaletea watu mafanikio.
“Sehemu yoyote ambayo mwenge umepita umeleta mafanikio kutokana na miradi iliyopo na kufunguliwa au kuzinduliwa na mbio hizi ambazo hufanyika kila mwaka,” alisema Mbijima.
Aliwaasa wanafunzi kuzingatia masomo na kuacha kujiingiza kwenye mambo ambayo yatawaharibia masomo yao ikiwa ni pamoja na matumizi ya dawa za kulevya au kushiriki kwenye vitendo vya ngono ambavyo mwisho wake ni kupata maambukizi ya magonjwa mbalimbali ukiwemo ukimwi.
Awali akisoma risala kwa mgeni rasmi mwalimu mkuu wa shule hiyo tatu Mwambala alisema kuwa ujenzi huo ulianza mwaka 2015 na kukamilika mwaka mwaka huo huo na kugharimu kiasi cha shilingi milioni 230,814,608.
Mwambala alisema kuwa lengo la ujenzi huo ni kuweka mazingira rafiki ya kujifunza na kujifunzia kwa wanafunzi wa kidato cha tano na sita ili kuongeza ufaulu ambapo bweni hilo lina uwezo wa kulaza wanafunzi 86 na lina miundombinu yote. Shule hiyo ilianzishwa mwaka 2007 na ilipata kibali cha kuanzisha kidato cha tano na sita mwaka 2014 na ina wanafunzi 408.
Mwenge huo ukiwa wilayani Kibaha ulitembelea miradi mbalimbali yenye tahamani ya shilingi zaidi ya bilioni nne leo unakimbizwa wilayani Mkuranga kuendelea na mbio zake.

Mwisho.          

ASKARI POLISI AUWAWA KWA RISASI

Na John Gagarini, Kibaha

ASKARI wa jeshi la  polisi kikosi cha usalama barabarani mwenye namba F.1839 sajent (SGT) Ally Salum maarufu Kinyogori ameuwawa kwa kupigwa risasi na watu wasiofahamika akiwa nyumbani  kwake.
>
> Tukio hilo limetokea may 19,majira ya saa 1.30 usiku huko katika kijiji cha Chatembo kata ya Mwandege wilayani Mkuranga mkoani Pwani.
>
> Kamanda wa polisi mkoani hapo,Boniventure Mushongi,amesema katika hali isiyo ya kawaida watu wawili wakiwa wamevalia makoti meusi na nyuso zao wakiwa wamezificha kwa mask walifanya mauaji hayo na kutokomea.
>
> Amesema watu hao waliingia ndani ya uzio wa nyumba ya askari huyo wakitumia usafiri wa pikipiki aina ya boxer na baada ya kushuka kwenye pikipiki waliingia ndani na kumfyatulia risasi askari huyo kichwani pamoja na ubavuni na kumpotezea maisha yake.
>
> Kamanda Mushongi amesema katika tukio hilo wauaji hao hawakuchukua  kitu chochote zaidi ya funguo wa gari la  marehemu ambapo waliondoka nalo.
>
> Amesema msako mkali wa kuwasaka waliohusika  na tukio unaendelea  na ameomba  ushirikiano kutoka kwa wananchi kwa wale wenye taarifa zitakazosaidia kuwapata  wahusika hao.
>
> Mwili  wa marehemu umehifadhiwa  katika hospital ya Temeke na utakabidhiwa  kwa ndugu zao kwa ajili ya mazishi mara  baada ya kufanyiwa uchunguzi .
>
> Mwisho

Thursday, May 19, 2016

MKURANGA MBIONI KUMALIZA TATIZO LA MADAWATI

Na John Gagarini, Kibaha
WILAYA ya Mkuranga mkoani Pwani limechonga madawati 5,043 ili kukabiliana na tatizo la upungufu wa madawati kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.
Mkuu wa wilaya ya Mkuranga Abdala Kihato akisoma taarifa ya wilaya hiyo kwa mkuu wa mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo wakati wa ziara yake kutembelea wilaya hiyo kukagua shughuli za maendeleo.
Kihato alisema kuwa wilaya hiyo ilikuwa na upungufu wa madawati 5,131 hivyo kubakiwa na upungufu wa madawati 500 ambayo wanatarajia kukamilisha utengenezaji muda mfupi ujao.
“Tatizo la upungufu wa madawati kwa wanafunzi wa shule za Sekondari tatizo hilo hakuna ila tatizo kubwa liko kwa wanafunzi wa shule za Msingi kutokana na uwingi wao na hata wale wa darasa la kwanza ambapo kwa mwaka huu walioandikishwa ni wengi sana,” alisema Kihato.
Alisema kuwa hawana wasiwasi kwani hadi ule muda uliowekwa wa Juni 30 kwa wilaya zote kuondoa tatizo la wanafunzi kukaa chini litakuwa limekwisha kabisa kwani wanashirikiana na wadau mbalimbali kutengeneza madawati.
“Tunawahimiza watendaji wa vijiji na kata kuhakikisha wanakamilisha zoezi hilo ili kuwaondolea adha wanafunzi kukaa chini na kuwafanya washindwe kujifunza vizuri masomo yao,” alisema Kihato.
Aidha aliwaomba wadau wa maendeleo ndani ya wilaya hiyo kuwaunga mkono katika kufanikisha zoezi hilo la uchongaji wa madawati kwa wanafunzi kwenye wilaya hiyo.
Naye mkuu wa mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo alisema kuwa anaipongeza wilaya hiyo kwa kuweza kufanikisha kuchonga madawati hayo ambayo sasa yanaenda kuondoa tatizo hilo la upungiufu wa madawati.
Ndikilo alisema kuwa mkoa huo ulikuwa una upungufu wa madawati 43,047 kwa shule za msingi lakini kwa jitihada hizo zitakuwa zimepunguza kwa kiasi kikubwa upungufu huo.

Mwisho.

MKURANGA YAZUIA MALIPO YA MISHAHARA YA WATUMISHI 15

Na John Gagarini, Mkuranga
WILAYA ya Mkuranga mkoani Pwani imewasimamishia malipo watumishi 15 ambao wameondoka kwenye vituo vyao vya kazi bila ya taarifa kwa mwajiri wake ambaye ni Halmashauri.
Hayo yalisema na mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Abdala Kihato alipokuwa akisoma taarifa ya wilaya wakati wa ziara ya mkuu wa mkoa wa Pwani kutembelea shughuli za maendeleo kwenye wilaya hiyo.
Kihato alisema kuwa mishahara hiyo ilizuiliwa kutokana na watumishi hao kutotoa taarifa walipoondoka kwenye vituo vyao vya kazi wakati wa uhakiki watumishi katika zoezi la kutambua watumishi hewa.
“Tulifanya uhakiki wa watumishi 179 na kubaini kuwa watumishi 85 walikuwa ni watoro ambapo 51 wamehamia kwenye vituo vingine vya kazi 10 hawakujitokeza na 15 ndiyo walioondoka kwenye vituo vya kazi bila ya taarifa na watano ni watoro kabisa,” alisema Kihato.
Alisema kuwa zoezi hilo ni endelevu na linaendelea kwani linaoneka lina changamoto nyingi katika kubainisha watumishi hewa na wale ambao wako kisheria.
“Hatua tuliyoichukua kwa wale ambao waliondoka kwenye vituo vyao vya kazi bila ya taarifa ni kusimamisha mishahara yao ili wasije wakwa wanachukua fedha pasipo kufanya kazi,” alisema Kihato.
Kwa upande wake Ndikilo alisema kuwa maofisa utumishi wanapaswa kutoa ushirikiano kwa serikali katika kuhakikisha watumishi hewa wanapatikana na itawachukulia hatua kali wale watakaowaficha watumishi hewa.
Ndikilo alisema kuwa zoezi hilo litakapokamilika mkoa utatoa taarifa juu ya zoezi hilo ambalo lina lengo la kuondoa watumishi hewa ambao wamekuwa wakijipatia fedha pasipo kufanya kazi.

Mwisho.